Na
Mwandishi Maalum
Umoja
wa Mataifa umeishukuru Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, kwa kutoa eneo la ujenzi wa majengo mapya ya Kimataifa yatakayotumika kushughulikia Mashauri Masalia ya Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya Jinai Tawi la Arusha. ( International Residual Mechanism)
Majengo hayo ambayo ujenzi wake utagharamiwa na Umoja wa
Mataifa, yatajengwa katika eneo la Laki Laki katika Jiji la Arusha. Yatahusisha pia uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu zote muhimu zinazohusiana na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimabari ya Rwanda ( ICTR).
Shukrani hizo zimetolewa mwishoni mwa wiki,na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Kitengo cha Bajeti cha Umoja wa Mataifa, Bw. Johannes Huisman, wakati alipokuwa
akiwasilisha mbele ya wajumbe wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, taarifa ya Katibu Mkuu ,
kuhusu mchakato wa ujenzi wa
majengo hayo mapya ya Kimataifa.
Kamati
ya Tano ndiyo Kamati inayoshughulikia
masuala yote yanayohusu na Utawala na Bajeti katika Umoja wa Mataifa.
“
Ninanayo furaha ya
kuiwasilisha kwenu taarifa ya Katibu Mkuu, kama taratibu zinavyoagiza. Lakini kwanza ninapenda kuchukua fursa hii
kuishukuru Tanzania kwa kutupatia eneo hilo na vile vile kwa
ushirikiano ambao serikali inaendelea
kutupatia hadi sasa katika maandalizi ya
utekelezaji wa mradi huu” akasema Bw. Huisman.
Kwa mujibu kwa Mkurugenzi huyo,
tayari Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, limekwisha kutenga kiasi cha dola za kimarekani 3 milioni za kuanzia ujenzi huo unaotarajiwa kugharimu
dola za kimarekani 8.79 milioni
Bw.
Johannes Huisman akafafanua zaidi kwa kusema kumekuwa na
maendeleo kadhaa kuhusiana na utekelezaji wa mradi tangu kuwasilishwa kwa taarifa ya mwisho ya Katibu Mkuu iliyotolewa mwaka jana.
Akazitaja
baadhi ya kazi ambazo zimekwisha kufanyika kuwa ni pamoja na mambo mengine,
kupatikana kwa eneo la ujenzi , maandalizi ya michoro ya majengo, upembuzi yakinifu wa gharama za mradi pamoja na ratiba ya ujenzi hadi kukamilika kwa mradi huo.
“Ninapenda
kueleza kwamba katika mambo yaliyofanyika ni pamoja na hili la kupunguza
muda wa ujenzi wa mradi kutoka makadirio ya awali ya miaka mitano na miezi mitatu hadi miaka minne,
matarajio ni kwa mradi huo ukamilike mwishoni mwa mwaka 2015.” Akaeleza.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri kuhusu masuala ya Utawala
na Bajeti ( ACBQ), Bw. Richard Moon akiwasilisha
maoni ya kamati yake kuhusu mradi huo alieleza kwamba, kamati yake imeridhishwa
na kwanza, kupunguzwa kwa muda wa utekelezaji wa maradi
na pili uamuzi wa kutumia uzoefu uliopo katika
uandaaji wa michoro ya majengo hayo.
Aidha
akaeleza kwamba pamoja na kuridhika na maelezo yote kuhusu mradi huo
lakini Kamati imegundua kwamba gharama
za ujenzi huo zilikuwa hazijahusisha gharama za
ununuzi wa samani za majengo hayo.
Na kwa sababu hiyo alibainisha kwamba kamati
itahitaji ufafanuzi kuhusiana na walakini huo pamoja na swala la
kutoingizwa kiasi cha dola za kimarekani 1.5 milioni katika taarifa hiyo ya Katibu Mkuu
Aidha akizungumza kwa
niaba ya Kundi la Nchi 77 na
China ( G77), Bw. Sainivalati Navoti,
aliunga mkono hoja ya kutaka maelezo ya kwa nini kiasi hicho cha dola za kimarakani 1.5 milioni zilikuwa hazijaainishwa katika ripoti hiyo.
Kundi hilo la G77
pia limeunga mkono punguzo la
muda wa ujenzi wa mradi na
likaenda mbali zaidi kwa kushauri kwamba hata miaka hiyo minne bado ni
mingi na ikiwezekana ipunguzwe hadi miaka mitatu lakini bila
kuathiri ubora na viwango vya mradi huo.
Bw. Brouz Coffi akizungumza kwa niaba ya kundi la nchi
za Afrika, alisema Kundi la nchi za Afrika linaunga mkono utekelezaji wa mradi
huo nchini Tanzania na kwamba hamu ya kundi hilo nikuona unatekelezwa kwa
wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Akaishukuru
Serikali ya Tanzania kwa kutoa
eneo la Ujenzi, na kusisitiza kwamba Umoja wa Mataifa uendelee
kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu na Mamlaka za Tanzania na kusisitiza zaidi kwamba badiliko lolote litakalogusa mradi huo lazima
lijadiliwe na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kama taratibu zinavyotaka..
Mwaka 2010, Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,
lilipitisha Azimio namba 1966 la
kuanzisha Mfumo wa Kimataifa wa kushughulikia umalizaji wa mashauri ya masalia
ya mahakama za kimataifa za mauaji ya halaiki ya
iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani,
(ICTY) na mauaji ya kimbari ya
Rwanda( ICTR.)
Kwa upande wa ICTY
tawi la mahakama hiyo litakuwa
The Hague, Uholanzi na ICTR iliamuliwa
tawi lake litakuwa Arusha, Tanzania.
Mfumo huo wa kimataifa wa kushughulikia mashauri masalia utakuwa na haki
, stahili na wajibu kama ilivyo kwa mahakama hizo ambazo zinatarajiwa kukamilisha
kazi zake si zaidi ya Desemba 31, 2014.
No comments:
Post a Comment