Wednesday, March 27, 2013

Mazingira ya uwekezaji kuendelea kuboreshwa zaidi - Dkt. Nagu


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwezeshaji na Uwekezaji DKT. Mary Nagu (katikati) akifurahia jambo na viongozi wa makampuni ya china (kushoto) ni Mkuu wa chama cha ushirikiano cha China Bw. Charles Li wakiwa wanaonyesha bango lenye maandishi ya lugha ya China kuonyesha ushirikiano kati ya China na Tanzania (kulia) ni Mwenyekiti wa Bodi wa WCUGA International Group Bw. Tiger Liang.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) Bw. Raymond Mbilinyi (kushoto) akiwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji, DKT. Mary Nagu wakielekea katika ukumbi wa kivukoni katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam juzi jioni kuonana na ujumbe wa wawekezaji wa china kwa ajili ya kujadili namna ya kuangalia fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini. Ujumbe huo wa makampuni kumi na tano toka nchini China uliongozwa na Mkuu wa chama cha ushirikiano cha China Bw. Charles Li.

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Serikali Imesema itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ikiwa ni sehemu ya kutanua wigo wa huduma za jamii na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji na Uwezeshaji , Dkt. Mary Nagu aliuambia ujumbe wa makampuni kumi na tano kutoka nchini China, uliokuja kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini kuwa serikali ina mkakati kabambe wa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji.

“Serikali na bajeti yake haitoshi kuwapa watanzania mahitaji yao ya ajira na huduma za jamii, pale ambapo kuna mradi unaleta faida kwa mwekezaji lazima tuhakikishe tunawachia wawekezaji ili fedha za bajeti ya serikali ziende kwenye huduma nyingine za jamii kama elimu” alisema Waziri Nagu katika chakula cha jioni kilichoandaliwa kwa wawekezaji hao jijini Dar es Salaam juzi usiku.

Alisisitiza kuwa kama kuna fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya barabara na hapo hapo kuna mwekezaji anataka kuwekeza katika sekta hiyo ni bora wawekezaji wapewe hiyo fursa ili serikali ielekeze nguvu katika sekta nyingine ambazo zinahitaji uwekezaji katika kusaidia wananchi.

Akizungumzia ujumbe wa makampuni kumi na tano ya kutoka nchini china, Waziri Nagu alisema wamepata moyo wakuja kuangalia fursa mbalimbali za kiuwekezaji kutokana na agizo la Rais wa nchi yao Bw. Xi Jin Ping kutembelea hapa nchini.

“Kutokana na maagizo ya Rais wa China kwamba wamewekeza katika nchi nyingine, sasa wakati umefika kuwekeza katika bara la Afrika hasa kwa nchi ya Tanzania, hivyo ni fursa ya kipekee kwa watanzania kutoa ushirikiano katika kufanya kazi na watu wa china”, alisisitiza DKT. Nagu.

Aliongeza kuwa lililo muhimu kwa sasa ni wawekezaji kuelekezwa kwenye faida, na ndio maana ameonana na ujumbe wa makampuni hayo na kuwaambia kuwa kuna fursa mbalimbali hapa nchini ambazo wakiwekeza watapata faida na nchi pia ifaidike kutokana na rasilimali zake.

“Naomba nichukue nafasi hii kuwakaribisha wawekezaji hawa kutoka china waone fursa hizi na fursa zipo wazi, kazi ya Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) ni kuwezesha wawekezaji waweze kuwekeza na kuona Tanzania inapata manufaa ya ajira, kodi itaongezeka na uchumi utakuwa”, aliongeza.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Raymond Mbilinyi, alisema mara baada ya kukutana na makampuni hayo yapatayo kumi na tano, tayari yameonyesha nia ya kuja kuwekeza katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

“Baada ya kukutana na taasisi za serikali na zile za binafsi makampuni haya yameonyesha nia ya dhati kuwekeza katika maeneo ya Elimu, Umeme, miundo mbinu, kilimo na afya” alisema Mbilinyi.

Aliongeza kuwa China ni moja ya nchi ambazo zinaongoza kwa uwekezaji hapa nchini, ikiwa ni nchi ya nne katika kuwekeza, huku akisisitiza kuwa baada ya muda mfupi inaweza kuwa nchi ya kwanza kutokana na juhudi kubwa inazofanya katika eskta hiyo.

“Sisi TIC inatupa moyo sana na hii ni kutokana na viongozi wetu wawili Rais Jakaya Kikwete na Rais wa China Xi Ji Ping kuonyesha njia na nia ya dhati, hivyo sekta binafsi kutoka China na Tanzania zitaweza kuwekeza kwa kasi katika Taifa letu”, aliongeza Kaimu Mkurugenzi huyo wa (TIC).

No comments: