Wednesday, February 20, 2013

WITO KWA MABLOGA WETU KUWA WABUNIFU BADALA YA KUIBA AU KUNUKUU TU KAZI NA PICHA ZA WENZAO BILA IDHIN

-Imeandikwa na Freddy Macha Ukingoni mwa Ziwa Nyasa- Revo Meza 
Ukingoni mwa Ziwa Tanganyika- picha ya Revocatus Meza, Desemba 2012. Wimbi la “blogging” liliikumba dunia kati ya 1995 hadi 1998 na kuanza kumea kwetu Tanzania kupitia mwanahabari Ndesanjo Macha miaka kumi iliyopita. Wakati Ndesanjo anaanza kublogu si wengi tuliomwelewa. Nakumbuka alivyokua akiniongelea juu ya fani hii kwa hamasa kwenye 2002. Baadaye kidogo aliendesha Jikomboe, blogu lililokua na taswira ya majani mabichi ya ukoka. Enzi hizo hakukua na hata senti 
moja aliyoichuma.  
Ndesanjo MachaNdesanjo Macha- mwasisi wa blogu Tanzania Ndesanjo alikua akisema blogu ni dunia ya kesho ya mawasiliano. Wakati huo vyombo vikubwa vya habari nchi zilizoendelea vilianza kuona umuhimu wa blogu vikaanza kuunda idara pembezoni mwa tovuti zake mama. Kwetu wenye magazeti wengi hawakupenda wanablogu;waliwaona washindani. Mwaka ambapo wanablogu wetu walianza kuchomoza ilikua 2006 baada ya kifo cha wapenzi wawili wa Kitanzania waliouliwa kinyama Marekani. Blogu la Michuzi (ambalo halikua maarufu kama leo) na Radio Butiama (inayojulikana kwa jina Podcast) zilisimama dede kutangaza habari hizo. Hapo ndipo miye binafsi nilipoanza kuona namna wanablogu walivyokuwa na mwendo mkali - zaidi ya vyombo vya habari vya kijadi. Niliingia rasmi uwanjani mwaka 2007- nikisaidiwa na Ndesanjo na wanabloga wengine walionitangulia; akina Simon Kitururu, Jeff Msangi (Bongo Celebrity) mathalan. Nilichogundua siku za mwanzo ni kwamba Blogaz husaidiana sana. “Ukiwa mbinafsi huendelei kama Bloga” alisisitiza Ndesanjo. Goats feeding on rubbish 
Mbuzi wetu Bongo wakila kila aina ya takataka mitaani. Nyama yake tamu. Lakini je, ina nini kinachotudhuru tusichokijua? Nilipiga picha hii, Zanzibar, mwaka 2011. Leo Jikomboe na ule ukoka havipo tena. Ndesanjo, mwasisi wa blog za Kiswahili duniani, anafanya kazi shirika la habari- Global Voices. Kati ya mamia ya waandishi wa shirika hilo la kimataifa, Mtanzania huyu anaongoza kwa habari asilia za uchambuzi zaidi ya 4,200 . Tofauti ya mtu kama Ndesanjo na baadhi ya blogaz ni kwamba yeye kiasilia ni mwanahabari hivyo anachanganya ujuzi na mitindo hii miwili ya kusanifu matukio. Si ajabu mwaka jana Ndesanjo alishinda tuzo la Mwanablog bora wa Afrika.
Lugha ya blogaz na vyombo asilia vya habari zi tofauti. Wanahabari lakini ni watu waliosemea sawasawa kazi zao na kufuata utaratibu wa lugha, kusahihisha na kuhariri kazi. Bloga ni mtu yeyote tu mitaani au kijijini anayetaka kuelezea jambo. Kuhe -samaki- by Revo Meza Samaki aitwaye Kuhe katika Ziwa Tanganyika. Picha nimeletewa na mwandishi Revocatus Meza. Mvua ya blogaz Tanzania imejaza bahari safi tena ya faraja. Blogaz ni wengi tena wa kila rangi na jinsia; wanatupasha matukio kila sekunde! Wakati tukianza, wanawake hawakua wengi. Mwaka jana mshindi wa Blogaz bora Bongo alikuwa Mwanamke na Nyumba. Nyingine zimekuwa makutano au baraza la maoni na malumbano muhimu- mfano Jamii Forums, iliyoundwa 2006. Zipo zenye mafunzo mazito- angalia Al Hidaaya inayofunza masuala ya Kiislamu na Korani tutaelewana n’na maana gani. Zile zenye kurasa moja (kama zangu) zimegeuzwa viwanda vidogo; mathalan ya Maggid Mjengwa ambayo ni kijigazeti cha ajira. Ajira zinazowahudumia na kuwafariji wanahabari wake. Mara nyingine zina maudhi maana hata kuzifungua zinakua shida maana matangazo yamejazana pale juu kiasi ambacho si tena habari bali duka. Ama kweli mtandao umekuwa biashara. Uzuri upo ndiyo; ubaya tuuseme pia! Msukuma Mkokoteni-Magomeni 2009-pic by F Macha Msukuma mikokoteni akitotwa jasho saa za alasiri, mitaa ya Magomeni Mapipa. Niliipiga picha hii mwaka 2009, Dar es Salaam. Watanzania tunakwenda na wakati si uongo. Maana ukitazama wenzetu nchi zilizoendelea wanaelekeza kila jicho katika mtandao na inteneti. Maduka makubwa makubwa asilia nchi magharibi yanapata hasara na kufunga virago vyake. Mwishoni mwa mwaka jana asilimia 25 ya biashara zote nchi zilizoendelea zilitokana na makampuni yenye mauzo ya mitandaoni – yakaingiza dola bilioni 1.7! Linaloongoza sasa hivi ni Amazon inayouza kila kitu bei rahisi na kwa ufanisi zaidi kuliko maduka asilia. Makisio ya faida ya Amazon mwaka jana yalikuwa dola bilioni 63. Uingereza duka maarufu la muziki, sinema na vitabu- HMV- lilipunguza wafanyakazi mwezi jana na tetesi ni kuwa wameshafifia kibiashara. Ama kweli mtandao ndiyo soko mzazi wa biashara leo na kesho (kama alivyosema Ndesanjo) na wanabloga wetu wanakwenda na wakati. Mwandishi gwiji wa Kiswahili Ebrahim Hussen aliwahi kuandika “wakati ukuta ukipigana nao utaumia.” Ndiyo maana wafanya biashara wanatangaza bidhaa kupitia blogu. Ndiyo hali halisi ilivyo. [caption id="attachment_1655" align="aligncenter" width="500"]Kitabu kipya cha Prof Said Ahmed 
Kitabu kipya cha Prof Said Ahmed[/caption] Kitabu kipya cha Mwandishi nguli, Profesa Said Ahmed- Mhanga Nafsi Yangu- ambacho kinamwangalia mwanamke wa Kibongo anayekwenda kusoma ughaibuni. Kimetolewa na Sasa Sema (Longhorn) wa Kenya,2012. Ila tutathmini zaidi hilo... Blogu zilibuniwa kutangaza mambo na kadhia ambazo hazipo ndani ya vyombo habari mama na runinga. Zilibuniwa kumfaidisha mwananchi yeyote wa kawaida akibeba kamera na simu yake mkononi akaeleza habari za pale anapoishi. Hicho ndicho chanzo... Kama hukua na nafasi kuna Twitter ambayo ni fupi zaidi (maneno 30 tu!). Zana hizi ni muhimu sana kwa jamii ya leo. Hizi ni “habari za raia wa kawaida” . Umuhimu wa Blog, Twitter na You Tube umeonekana pale yalipotokea machafuko na harakati mbalimbali duniani kama Tunisia, Misri, Libya na Mashariki ya Kati nzima miaka miwili iliyopita. Dhoruba za mauaji ya mwanahabari Daudi Mwangosi zilisambaa dunia nzima haraka kutokana na uwezo huu muadhama. Nguzo zake ndizo hizo. Google ambaye hulipa matangazo ya biashara kutokana na “maudhui ya habari” husisitiza wanablogu na waandishi kuwa wa kweli na kutochezea kazi za wenzao. Kwetu Bongo hapana. Miaka ya karibuni makampuni makubwa makubwa na mabenki kama National Microfinance (NMB) yanasaidia kuwekezea wajisiria mali wadogo wadogo (yaani Blogaz). Mara nyingi makampuni haya hayaangalii kama wanablog hawa wananukuu kazi za wenzao, wanaandika mambo yao wenyewe au wanakopi tu na kubandika. Logo- Sema Ndiyo-2 
Nembo ya kutetea haki za wanyama pori wanaouliwa ovyo. Kampeni hii inaongozwa na Kidon Mkuu Ngoille Mkuu, wa Arusha. Dili zinapatikana kwa kujuana juana, mathalan. Bahati mbaya kumezuka mtindo wa wanablogu wengi kutwaa kazi na picha za wenzao bila kuandika zimetoka wapi. Ukilinganisha sasa hivi Blogu zetu Tanzania ni tofauti sana na za nchi nyingine maana wengi hatuandiki vitu tulivyovibuni au tunavyoviona. Mmoja akishaandika tu basi wengine wote tunakopi na kubandika tu bila kuangalia sana kazi ikoje. Siku Google na mashirika miliki ya hizi blogu wakifahamu yatakua mengine. Kwa sasa tunajificha ficha tu. Saria akikochi vijana Dodoma 
Mwanamichezo na mwanahabari Israel Saria akiwa kazini na vijana Dodoma miaka ile ya Themanini. Niliongea na Israel Saria, anayeendesha blogu-tovuti la Michezo Tanzania (Tanzania Sports) tokea London karibuni. Saria ameendesha shughuli hii toka 2005 na anafadhiliwa na NMB. Mbali ya kuwa mtangazaji wa michezo BBC, Saria ni mwalimu rasmi wa mchezo wa mpira wa nyavu aliyekuwa kocha miaka mingi Tanzania. Alipendekeza wawekezaji kuangalia thamani ya blog mbalimbali kabla ya kuzipachikia matangazo: “Hebu linganisha blogu zetu na za majirani wa Kenya. Wakenya wengi huandika mambo wanayobuni. Sisi tunakosa ubunifu na uhalisia. Mwenzetu akiandika habari- baada ya dakika tano –mabloga wengine wote tunainukuu na kuitangaza ikiwa imejazana makosa. Tunalipua tu. Hatuna hata muda wa kuichunguza au kuihariri. Tunadhani kublogu ni suala la umaarufu na kuonekana kwamba na mimi nipo; eti sitaki nionekane kwamba nimekosa ile habari iliyotangazwa na mwenzangu!” Saria anaongeza kusema kwamba wengi wetu tunashindwa kutambua kwamba Google huwa wanajua na kuangalia kazi asilia. “Ukishatundika tu kazi yako, baada ya dakika chache tayari inasajiliwa kama ni mali yako. Yeyote anayeinukuu au kuitumia hatambuliwi kama mwenye hiyo kazi.” Mabloga wengi Bongo basi wanarudia rudia tu kazi za wenzao kwa kuzitapika na kuzitafuna kama ambavyo ng’ombe wanavyofanya baada ya kula majani. Matokeo baadhi ya blogu leo zimegeuka mabango ya matangazo badala ya kazi muhimu za kifasihi. Zipo blogu nyingi zinazobuni mambo- lakini pia zipo ambazo zinacheza tu. Maandazi 
Picha ya Maandazi toka tovuti la Taste of Tanzania. Picha ya Miriam Rose Kinunda... Miriam Rose Kinunda anayeendesha tovuti-blogu ya mapishi (Taste of Tanzania) amekuwa akisanifu blogu na kusaidia wenzake kuzijenga toka 2004. Anasema ni mara nyingi sana ambapo kazi na picha zake zimetumiwa bila idhini. “Awali nilikua nikiblogu Kiswahili na Kiingereza, lakini kutokana na huu wizi wa kazi, nimeondoa kabisa kitengo cha Kiswahili nikabakisha Kiingereza kwa wasomaji wa kimataifa.” Miriam ambaye karibuni atatoka na kitabu chake cha mapishi anataja mfano ambapo tovuti moja maarufu ya Kenya iliiba kazi na picha zake. Akaamua kuwapigia simu. “Baada tu ya dakika tano, jamaa walinitumia barua pepe kunitaka radhi. Walionyesha namna walivyo waungwana.” Miriam Rose Kitunda Miriam Rose Kinunda Je nini kifanyike? Saria na Bi Kinunda wanashauri wawekezaji (mathalan benki inayowafariji wanablogu kama NMB) kufadhili na kusaidia tu wale wanaokua wabunifu na wanaofuata kanuni za fani hii muhimu katika jamii. Kigoda 
Kigoda nyumbani kwa mpigania utamaduni wetu na mfanyabiashara mashuhuri wa Dar es Salaam, Mwafrika Merinyo anayeendesha shughuli za Afrika Sana. Nilipiga picha Novemba 2011. Makala hii iliandikwa pia kwa Kiingereza katika safu ya Mwandishi gazeti la Citizen mwezi jana "We don't need leaders; everyone should be a leader..." -Manu Chao, French-Spanish musician, speaking to Jungle Drums, Brazilian Mag, London Oct, 2007.

No comments: