Thursday, February 14, 2013

KAULI YA JAMAL MALINZI DHIDI YA KUENGULIWA KUGOMBEA URAIS WA TFF


Ndugu zangu,kupitia vyombo vyenu vya habari ninaomba niueleze umma wa watanzania,hususani wadau wa mpira wa miguu,yafuatayo kuhusu kuenguliwa kwangu.
Awali ya yote nieleze kusikitishwa kwangu na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya rufaa ya TFF ya kuniengua kugombea urais wa TFF.Sikubaliani na maamuzi haya .
Katika kuniengua kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF imetoa sababu mbili (nanukuu magazeti ya jana tarehe 12/02/2013 maana hadi leo sijakabidhiwa barua ya kuenguliwa).

1.  Kukosa uadilifu kwa kupinga waraka  uliotolewa na TFF wa kubadili Katiba ya TFF mwezi Desemba 2012.

2. Kukosa uzoefu wa miaka mitano ya uongozi.
Ndugu zangu,kiini cha maamuzi ya Kamati ya rufaa dhidi yangu ni pingamizi lililowekwa na mtu mmoja anayeitwa AGAPE FUE.Bwana Agape Fue aliniwekea pingamizi katika kamati ya uchaguzi  akidai mimi nilipinga waraka wa kubadili katiba ya TFF na pia sina uzoefu wa miaka mitano ya uongozi wa mpira.Kinyume na matakwa ya kamati ya uchaguzi kama yalivyotangazwa kuwa mtoa pingamizi aje mwenyewe kutetea pingamizi lake ,Bwana Agape Fue hakutokea mbele ya Kamati ya Bwana Lyatto.Matokeo yake tarehe  31/01/2012 kamati ya uchaguzi  ya TFF ilitoa maamuzi ya ya kutupilia mbali pingamizi hili.
Bwana  Agape Fue hakuishia hapo  kwa mara nyingine tarehe 06/02/2013 alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi akidai kamati ya uchaguzi haikumtendea haki. Rufaa hii haikuwa na anwani wala namba ya simu  ya Bw.Agape Fue.Rufaa ilisikilizwa tarehe 10/02/2013 na maamuzi ya kukata jina langu yakatangazwa jioni ya tarehe 11/02/2013.
Mpaka leo najiuliza hivi huyu Bw. Agape Fue ni mwanaume au  ni mwanamke?(hakueleza kama ni Bwana au Bibi Agape Fue). Agape Fue ni nani hasa? Anaishi wapi?Je ni Mtanzania au sio Mtanzania maana kikanuni  wasio watanzania hawaruhusiwi kujihusisha na uchaguzi wa TFF (rejea kifungu cha 9 cha kanuni za uchaguzi),pingamizi lake halikuambatana na udhibitisha wa uraia. Kwa nini alichukua maamuzi haya? Sipati jibu.  Iweje  mtu achukue maamuzi mazito ya kumkatia mtu rufaa kisha uishie kusaini karatasi na kuwaachia wengine wakusemee na usije hata kushuhudia kinachoendelea kama kweli una maslahi na madai yako? Waandishi wa habari mnisaidie kupata majibu.

Ndugu zangu ,mtoa pingamizi alidai haikuwa sahihi kupinga azimio la kubadili katiba ya TFF kwa njia ya waraka.Naomba nisistize mambo matatu:

Wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF wanawakilisha matakwa ya vyama vilivyowatuma kwenda  kwenye  mkutano  mkuu wa TFF,na ndio maana chama cha mpira cha mkoa wa Kagera (KRFA) kiliitisha kikao cha kamati ya utendaji  ili kamati iweze kutoa mwongozo  kwa wajumbe wake kuhusu nini kifanyike kuhusu waraka ulioletwa na TFF,hivyo maamuzi yaliyotolewa ya kuukataa waraka huu yalikuwa ni maamuzi ya chama cha mpira mkoa wa Kagera na wala hayakuwa ni maamuzi ya Jamal Malinzi,iweje malinzi niadhibiwe kwa maamuzi haya,kwa nini usiadhibiwe mkoa mzima na mikoa yote iliyopinga waraka?hii ni haki kweli? Siamini kama kuna mjumbe wa mkutano mkuu aliyekiuka maamuzi ya kamati yake ya utendaji.

2.  Katika mchakato wa kubadili katiba kwa njia ya waraka kilichokuwa kinagomba sio maudhui (content) ya mabadiliko ya Katiba bali utaratibu uliotumika kubadili Katiba. Swali la msingi tulilojiuliza wajumbe wa kamati ya utendaji KRFA  ni kwamba je kwa mujibu wa Katiba ya TFF kifungu 22 na kifungu 30 wapi katiba inatamka kuwa inaweza kubadilishwa kwa njia ya waraka? Mpaka leo hilo jibu hakuna,labda aliyeniwekea pingamizi atusaidie kupata jibu la swali hili. Katiba ya TFF iko wazi kabisa inatamka  kuwa Katiba itabadilishwa kwa njia ya Mkutano Mkuu tu (General Assembly).

3. Ni kweli FIFA iliagiza yafanyike mabadiliko ya Katiba ya kuingiza kipendele cha ‘club licencing’ katika Katiba ,lakini je FIFA katika agizo hilo ilisema Katiba ya TFF ivunjwe ili kutimiza azma hiyo? Ikumbukwe kuwa mwaka 2004 FIFA iliagiza TFF iingize kwenye Katiba kipengele cha Katibu Mkuu awe wa kuajiriwa badala ya kuchaguliwa,agizo hili lilitekelezwa kwa kupitishwa na Mktano Mkuu wa TFF,iweje leo utaratibu huu ukiukwe? Hata majuzi CAF walipotaka kubadili katiba ili Rais wa CAF atokane na wajumbe wa Kamati ya Utendaji jambo hili lilitekelezwa kwa kuitisha mkutano mkuu wa dharura  uliofanyika Seychelles majuzi. Katiba ndio msingi mkuu wa uendeshajiwa TFF,nitaipigania siku zote.Huo ndio utaratibu,si CAF si FIFA si Vyama vya mpira vya nchi,hakuna anayebadili  Katiba kwa njia ya waraka,kama kuna mwenye ushahidi aulete.

Kuengua jina langu eti kwa kuwa nilipinga waraka wa kubadili Katiba sio uamuzi sahihi.

Kuhusu uzoefu wa miaka mitano katika Uongozi:
Ikumbukwe kuwa katika uchaguzi mkuu wa TFF mwaka 2008 niligombea na jina langu lilikatwa na kamati  ya uchaguzi ya TFF.Nilikata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya TFF na kushinda . Hukumu hii ni halali hadi leo.Iweje leo hii miaka minne baadae Kamati hiyo hiyo ya rufaa (kubadili majina ya wajumbe sio kubadili taasisi) inione sina uzoefu?.Si hilo tu ,hata katika kujaza fomu namba moja ya kugombea niliambatanisha vielelezo vyote vya uzoefu wangu ikiwa ni pamoja na kudhibitisha kuwa katika kipindi cha miaka mine iliyopita  nimekuwa:
-Mjumbe wa Baraza la michezo mkoa wa Dar es salaam.
-Mwenyekiti wa kamati ya mashindano chama cha mpira mkoa wa Pwani COREFA.
-Mjumbe wa mkutano mkuu wa mkoa wa Kagera
-Mwenyekiti wa chama cha mpira mkoa wa Kagera
Hii ni pamoja na kuongoza Yanga 2002-2005.
Hivi katika nafasi hizi za uongozi ipi ni ya kuongoza ‘bonanza’? Nimedhalilishwa sana.


HITIMISHO
Vyombo vya habari kupitia makala,tahariri na maoni ya wasikilizaji/wasomaji/watazamaji vimesifia sana awamu mbili za uongozi wa Bwana Leodeger Tenga.Bwana Tenga amesifiwa kwa umahiri wake wa kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu Tanzania.Amesifiwa kwa kujenga taasisi imara ambayo mhimili wake mkuu ni sekretarieti makini na kamati mbali mbali zilizo imara .Let him rise to the occasion,muda wa kuonyesha uongozi imara ni huu,historia itamhukumu kwa jinsi gani atasimamia suala hili,haki sio lazima itendeke lakini pia inatakiwa ionekane inatendeka.
Kamati ya utendaji ya TFF inayo mamlaka ya kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa Tanzania.Ninamshauri Rais wa TFF aitishe kikao cha dharura cha kamati ya utendaji ili kijadili hali hii na kunirudishia haki yangu ya kugombea urais wa TFF.
Nihitimishe kwa kuwaomba wadau wa mpira wa miguu Tanzania  wawe watulivu wakati tukisubiri kupata ufumbuzi wa suala hili.

Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania.
Ahsanteni sana,

Jamal Emil Malinzi
Dar es salaam
13/02/2013

No comments: