Friday, February 8, 2013

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO WA KUMI WA BUNGE LA MUUNGANO, DODOMA TAREHE 08 FEBRUARI, 2013

MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA 


UTANGULIZI

1.            Mheshimiwa Spika, tumekuwepo hapa Bungeni, Dodoma kwa takriban siku 11 ambapo leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano wa Kumi wa Bunge lako Tukufu. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.

2.            Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki waliopoteza Wapendwa wao katika ajali mbalimbali zilizotokea hapa Nchini, ikiwemo ajali ya Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika Bahari ya Hindi na Ajali ya Lori kule Mbarali ambapo Watu wamepoteza maisha na kupata majeraha. Aidha, tunawapa pole Majeruhi wote na Abiria waliopoteza mali katika ajali hizo. Kwa kipekee kabisa napenda kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Askofu Thomas Laiser wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati - Arusha ambaye amefariki jana Mchana na Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi ambaye  amefariki Usiku wa kuamkia leo huko Nairobi alikokuwa anapata matibabu. Wote tunawapa pole sana!

SHUGHULI ZA BUNGE

a)            Maswali
3.            Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya Maswali 116 ya Msingi na 286 ya nyongeza yalipatiwa majibu. Vilevile, Maswali 6 yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.

b)        Miswada
4.            Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara ya Kwanza:
i)             Muswada wa Sheria ya Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 [The Cooperative Societies Bill, 2013]; na

ii)            Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013 [The Written Laws Miscellaneous Amendments, Bill 2013].

5.            Mheshimiwa Spika, Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2012 [The Written Laws Miscellaneous Ammendments (No. 3) Act, 2012] ulisomwa kwa mara ya Pili na kupitia ngazi zake zote;

c)         Hoja Binafsi za Wabunge
6.            Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, pia  Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuwasilisha Hoja Binafsi kama ifuatavyo:
i)             Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi ya kuitaka Serikali iwasilishe Bungeni Muswada wa Sheria ya Uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu ya Juu (The Higher Education Fund Act);

ii)            Hoja Binafsi ya Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa kuhusu udhaifu ulioko katika Sekta ya Elimu Nchini;

iii)           Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa Nzega ya kuitaka Serikali ianzishe Mpango Maalum wa Kukuza Ajira kwa Vijana na kuanzisha Mfuko wa Mikopo ya Vyama Wanaowekeza kwenye Kilimo na Viwanda vyenye uhusiano wa moja kwa moja na Kilimo; na

iv)           Hoja Binafsi ya Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Ubungo juu ya Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiaji wa Maji Taka katika Jiji la Dar es Salaam.

d)        Maazimio
7.            Mheshimiwa Spika, vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza kujadili na kupitisha Maazimio Mawili yafuatayo:
i)             Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Watu wenye Kinga ya Kimataifa pamoja na Wakala wa Ki-Diplomasia (Convention on The Prevention and Punishment of Crimes Against Internationally Protected Persons Including Diplomatic Agents 1973); na

ii)            Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Vitendo vya Ugaidi wa Kutumia Nyuklia (International Convention for Suppression  of  Act  of  Neuclear Terrorism, 2009).

Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kukamilisha Mijadala hiyo.

UJENZI WA UMOJA WA KITAIFA

8.            Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee Taifa letu limejaliwa na Mwenyezi Mungu kutimiza miaka zaidi ya 51 sasa  ya Uhuru likiwa bado linaendelea kudumisha Umoja wa  Kitaifa.  Umoja  huu wa Kitaifa umejengwa kwenye nguzo na misingi imara ya Amani, Utulivu na Mshikamano. Mimi naamini sote tunapaswa kujivunia Umoja huu wa Kitaifa ambao ni Tunu kubwa na nguzo muhimu ya maendeleo yetu. Msingi mkubwa wa Umoja wa Kitaifa tunaoshuhudia leo uliwekwa na malezi mazuri ya Waasisi wa Taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza, pamoja na mambo mengine, kujenga Jamii inayozingatia misingi ya Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Ni jukumu la kila Mwananchi kulinda Umoja huu ambao hauna mbadala.

9.            Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ina Makabila zaidi ya 120 ambayo kwa Mujibu wa Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 yamefikisha Idadi ya Watu Milioni 44.929. Aidha, hivi sasa tuna Madhehebu ya Dini yaliyoandikishwa takriban 885 na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali zaidi ya 6,675 na tumejenga Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ambapo hadi sasa tuna Vyama vya Siasa 19 ambavyo vimepata Usajili wa Kudumu. Licha ya kuwepo kwa Idadi kubwa ya Watu wa Makabila tofauti yenye desturi mbalimbali na makundi mbalimbali ya Madhehebu ya Dini, Itikadi za Kisiasa na Watu wenye Rangi mbalimbali, bado tunajivunia kwamba tunaheshimiana na hatubaguani kwa namna yoyote ile. Hali hii ya amani imeipatia Nchi yetu sifa Kitaifa na Kimataifa na mfano wa kuigwa.

10.         Kutokana na Demokrasi pana iliyopo, Wananchi wetu wana Uhuru mkubwa wa kutoa maoni, kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Siasa pamoja na kushiriki katika kuchagua Viongozi wa Chama chochote wanachokipenda kwa kuzingatia Misingi ya Katiba na Sheria za Nchi. Vilevile, Serikali imetoa uhuru mkubwa wa kupata na kutoa habari kwa uwazi bila vikwazo vyovyote kwa kuzingatia Katiba, Sheria na Kanuni mbalimbali na Maadili ya Vyombo vya Habari. Kutokana na Uhuru huo, Idadi ya Vyombo vya Habari imeongezeka sana ambapo hadi sasa Idadi ya Vituo 86 vya Redio vilivyopewa Leseni na vinafanyakazi, Vituo vya Televisheni 26 na Magazeti 768 yaliyoandikishwa na yanayotolewa na Taasisi mbalimbali.

11.         Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo yanayodhihirika wazi, hivi karibuni kumekuwepo na dalili za kupoteza sifa yetu nzuri ya Umoja wa Kitaifa na Amani ambayo imedumu kwa miaka mingi. Tumeshuhudia Wananchi mmoja mmoja wakishindwa kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo tu miongoni mwao. Aidha, tumeshuhudia Vyama vya Siasa vikionesha dalili ya kuhamasisha Wanachama wao kuingia kwenye  malumbano  ya  Siasa  baina  yao  wenyewe  kwa  wenyewe au baina ya Chama kimoja cha Siasa na Chama kingine. Baadhi ya Wanachama wameshikana mashati na kujeruhiana.

12.         Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaasa Viongozi wa Vyama vya Siasa kuepuka kutumia majukwaa ya Siasa kuvuruga Amani yetu na Utulivu uliopo. Waepuke matamko ya vitisho na kuhamasisha Wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani na kujenga chuki na uhasama miongoni mwa Jamii na kwa Serikali halali iliyopo madarakani.  Pamoja na kutofautiana kwa mawazo na Sera za Vyama vya Siasa, ni muhimu tujenge mazingira ya kuvumiliana kwa hali ya juu katika kujenga Demokrasia ya kweli hapa Nchini. Viongozi wa Vyama wanatakiwa kueleza Sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana. Tujenge Nchi yetu kwa Amani na Utulivu ndipo tutapata maendeleo endelevu.

13.         Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia pia kuibuka kwa choko choko za Kidini. Baadhi ya Waumini wa Dini wamekuwa wakikashifu Dini nyingine kwa kejeli na vitendo vingine visivyostahili. Aidha, baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wamekuwa wakiwaingiza Waumini wao katika Migogoro isiyoisha, ikiwa ni pamoja na kufungiana milango na kuzuia Waumini Wasiabudu siku za Ibada. Napenda kusisitiza kuwa Madhehebu ya Dini yana nafasi kubwa ya kujenga Umoja wa Kitaifa, Amani na mshikamano. Nawaomba Viongozi wa Madhehebu ya Dini kutatua kwa amani migogoro iliyopo na kuelimisha Waumini wao kuthamini, kujenga na kuenzi Amani na Utulivu uliopo Nchini. Serikali imetoa uhuru wa Wananchi wake Kuabudu, kila mtu kwa Dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya Dini moja kukashifu Dini nyingine. Aidha, tupinge kwa nguvu zetu zote choko choko za Kidini ambazo zimeanza kujitokeza katika sehemu mbalimbali Nchini.

14.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baadhi yao yamekuwa yakihusishwa kuwa mstari wa mbele katika kuwarubuni Wananchi kufanya vurugu zinazolenga kuleta uvunjifu wa Amani. Napenda kusisitiza kuwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yana jukumu kubwa la kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kujenga Umoja wa Kitaifa. Viongozi wa Mashirika haya waepuke kutumiwa na baadhi ya Viongozi kujenga mbegu mbaya kwa Wananchi kuvuruga Amani.

15.         Mheshimiwa Spika, nigusie pia Vyombo vya Habari, ambapo kumekuwa na kutiliana mashaka kwa baadhi ya Vyombo hivyo kuandika habari za Uchochezi, hivyo kuashiria Uvunjifu wa Amani na Mshikamano wa Kitaifa tuliojijengea. Vyombo vya Habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha Umma na kuhabarisha kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo, kama wafanyavyo wenzetu jirani, husan Vyombo vya Habari vya Nchi ya Rwanda. Aidha, Vyombo hivi vina fursa nzuri ya kutumia uhuru uliopo kudumisha Amani na Utulivu Nchini.

Tufanye Nini

16.         Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto zilizopo za baadhi ya Watu waotaka kubomoa Umoja wa Taifa letu na kuhatarisha Amani na Utulivu Nchini, sisi kama Taifa hatuna budi kufanya yafuatayo:
i)             Serikali, Wananchi na Wadau wote ikiwemo Vyama vya Siasa, Madhehebu ya Dini, Vyombo vya Habari, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, n.k. tunapaswa tukae chini tuzungumze na kutafakari kuhusu hali hii;

ii)            Tunapaswa kwa namna zote tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia Utamaduni wa Kitanzania na Misingi ya Amani na Utulivu tuliojijengea kwa muda mrefu; na

iii)           Wananchi wote tuzingatie na kuheshimu Utawala Bora wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo.

17.         Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Wananchi na Watanzania wenzangu kuendeleza  umoja  na  mshikamano  wa Kitaifa ili kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini.  Ni vyema kutambua  kuwa  Amani  na Utulivu uliopo Nchini ni mazingira wezeshi ya kusaidia  kila mmoja wetu kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo.  Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo ya Watu. Kwa upande wa Serikali itahakikisha kwamba, Umoja tuliojijengea unadumishwa. Taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Vyombo vya Dola ni lazima zihakikishe kwamba, Wananchi wanaishi kwa Amani na Utulivu. Vilevile, kuhakikisha kuwa, Umoja wa Kitaifa tulioujenga kwa miaka mingi haupotei. Naziomba Taasisi zote zinazohusika na kusimamia Amani na Usalama kuhakikisha kuwa, pamoja na Changamoto zilizopo, Umoja wa Kitaifa unadumishwa.

HALI YA CHAKULA NCHINI

i)             Hali ya Mazao na Mvua
18.           Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika hivi karibuni juu ya upatikanaji wa chakula Nchini na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa, yale yanayopata mvua za msimu kama vile Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora, na Mtwara mazao mengi yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji. Inatarajiwa kwamba, endapo mvua hizi zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo utakuwa mzuri.

19.         Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ya hewa, tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe iliyofanyika mwezi Januari 2013 inaonesha upungufu wa chakula katika Wilaya 47 zilizoko katika Mikoa 15 ambazo zitahitaji msaada wa chakula katika vipindi tofauti. Inakadiriwa kuwa jumla ya Watu 1,615,445 watahitaji jumla ya Tani 32,870 za chakula.

ii)         Hatua Zinazochukuliwa na Serikali
20.         Mheshimiwa Spika, kutokana na matarajio hayo ya uhaba wa Chakula, Serikali itahakikisha kuwa Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea kusambaza mahindi katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Hadi sasa jumla ya Tani 20,000 zilishatolewa kwa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora. Aidha, Kitengo hicho (NFRA) kitaendelea kununua nafaka mapema baada ya mavuno ili kuhakikisha kuwa Serikali ina hifadhi ya kutosha ya chakula kwa ajili ya kusambaza katika maeneo yatakayokuwa na uhaba wa chakula. Hadi tarehe 6 Februari 2013 Ghala la Taifa la Chakula lilikuwa na jumla ya Tani 68,712.9 za mahindi pamoja na Tani 3,335.989 za Mtama.

21.         Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji  wa chakula  Nchini  na kuhakikisha kuwa hakuna Mwananchi atakayepoteza maisha kutokana na njaa. Nitoe wito kwa Wananchi kuendelea kuweka utaratibu wa kuhifadhi sehemu ya mavuno yao baada ya kuvuna kwa ajili ya akiba ya baadaye badala ya kuuza mavuno yao yote.

MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA MALARIA NCHINI

i)               Hali Halisi ya Ugonjwa wa Malaria Nchini
22.         Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inayo changamoto kubwa ya kukabiliana na Magonjwa makubwa Duniani, yakiwemo Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI, Saratani, n.k. Niruhusu leo katika Hotuba yangu nizungumzie kidogo kuhusu Ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa wa Malaria bado unaongoza kuwa sababu kubwa za Wagonjwa wengi wanaohudhuria katika Vituo vya huduma za Afya Nchini. Aidha, ugonjwa huu unaongoza kwa kusababisha vifo, hasa kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka Mitano. Takwimu kutoka Vituo vya kutolea huduma ya Afya Nchini zinaonesha kuwa, takriban Wagonjwa Milioni 11 hadi 12 huhudhuria katika Vituo vya huduma za Afya kwa sababu ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile, tafiti zilizofanyika katika Jamii [Tanzania HIV/Malaria Indicator Survey (THMIS) 2011/2012] zinaonesha kuwa Asilimia 10 ya Watoto katika Kaya wana maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria.

ii)         Jitihada za Serikali katika kumaliza tatizo la Malaria Nchini
23.          Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo hili katika kuhakikisha Wananchi wanaendelea kujikinga na maambukizi dhidi ya ugonjwa wa Malaria, Serikali imefanya mambo muhimu yafuatayo:
Moja:        Kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Malaria wa Miaka Mitano (2008-2013) ambao una lengo la kupunguza vifo kwa Asilimia 80 ifikapo mwaka 2013 mwishoni. Utekelezaji wa Mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na Wadau mbalimbali hadi katika ngazi ya Jamii;

Pili:           Kusambaza na kuongeza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu katika Kaya. Hadi sasa zaidi ya vyandarua Milioni 26 vimesambazwa kupitia Kampeni iliyolenga Watoto wenye umri chini ya miaka Mitano;

Tatu:        Kutekeleza Mpango wa Hati Punguzo unaolenga kuhakikisha Akina Mama Wajawazito na Watoto wanaozaliwa wanaendelea kupata vyandarua hivyo na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Malaria;

Nne:         Kuendeleza Mpango wa kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili kutokomeza mazalia ya Mbu. Mpango huo unaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ambapo zaidi ya Kaya 1,440,000 sawa na Asilimia 90 katika Wilaya za Mikoa hiyo zitanyunyiziwa viuatilifu. Kutokana na Mpango huo, zaidi ya Watu 6,500,000 wameendelea kukingwa dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Malaria;

Tano:       Kuendeleza Mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia. Mpango huu ambao unafanywa na Serikali kwa ushirikiano na Serikali ya Nchi ya Cuba unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwaka 2011;

Sita:          Kutumia Mwongozo wa kutibu ugonjwa wa Malaria isiyo kali kwa kutumia Dawa ya Mseto ya Artemether/Lumefantrine (ALu). Mwongozo huu unaendelea kutumika katika Vituo vyote vya Umma vya kutolea huduma za Afya; na

Saba:       Kusambaza kipimo cha haraka cha kutambua na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya Malaria kwenye damu katika Vituo vyote vya Umma vya kutoa huduma za afya Nchini.

iii)        Changamoto
24.         Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana, bado kuna changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi. Changamoto hizo ni pamoja na:

Moja:        Kujitokeza kwa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vya aina ya “pyrethroids” vinavyotumika katika vyandarua na unyuziaji dawa ya ukoko majumbani;

Pili:           Kupata vyanzo zaidi vya fedha za ndani za kuendeleza mkakati wa unyunyiziaji dawa ya ukoko majumbani;

Tatu:        Uwezo mdogo wa uzalishaji wa dawa za kuangamiza viluwiluwi vya Mbu na kuanza kuangamiza Viluwiluwi hivyo katika Jiji la Dar es Salaam; na

Nne:         Kuendeleza uhamasishaji Wananchi kutumia nyenzo na kushiriki katika mikakati iliyopo, hasa inayohitaji ushiriki wao wa moja kwa moja, kama kuharibu mazalia ya Mbu.

iv)        Matarajio ya Mkutano wa United Against Malaria – Afrika Kusini
25.         Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kupambana na Malaria Duniani, Shirika la Roll Back Malaria Partnership wakishirikiana na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini wanatarajia kufanya Mkutano mkubwa unaohusu mapambano dhidi ya Malaria kwa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia tarehe 9 - 11 Februari, 2013. Mkutano huo unatarajia kukutanisha Viongozi wa ngazi ya juu kutoka Nchi za SADC ikiwa ni pamoja  na  baadhi  ya Marais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa  Afya  na  Mawaziri wa Michezo katika Nchi hizo. Mkutano huo pia utajumuisha Viongozi wa juu wa Makampuni mbalimbali ya Sekta Binafsi.

26.         Mheshimiwa Spika, lengo la Mkutano huo ni kukutanisha Viongozi mbalimbali kwa lengo la kuendesha mjadala kuhusu janga la Malaria katika Nchi za Afrika; ikizingatiwa kuwa ufadhili wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali unazidi kupungua. Mkutano huo unategemewa kuwa chachu kwa Viongozi kuongeza Bajeti za udhibiti wa Malaria Nchini mwao na kuongeza ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja na Sekta ya Michezo, hususan katika Mpira wa Miguu katika dhana nzima ya Mpango wa “Safe Companies”. Aidha, Mkutano huo unatarajiwa kuongeza kasi ya Kupambana dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika Nchi hizo.

27.         Ni matumaini yangu kuwa, Mkutano huo utakuwa wa mafanikio makubwa kwa Nchi za Kusini mwa Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile, utatupatia uzoefu kwa Nchi yetu katika kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria.

v)         Jitihada za Chama cha Wabunge cha Kupambana na Malaria
28.         Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kupambana na Malaria Nchini, Muungano wa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Tanzania walianzisha Asasi inayojulikana kama Tanzania Parliamentary Against Malaria (TAPAMA). Lengo la kuanzishwa kwa Asasi hii ni kuongeza utashi wa Kisiasa katika kushiriki na kutekeleza  Mpango na Sera ya Taifa ya kutokomeza Ugonjwa wa Malaria Nchini. Asasi hii ilisajiliwa mwaka 2008 na hadi sasa imetekeleza masuala mbalimbali katika jitihada zake za kupambana na Malaria Nchini kama ifuatavyo:
Moja:        Ugawaji wa Vyandarua kwa Watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa Mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro na Mwanza ambapo zaidi ya Watoto 2,500 walifaidika na huduma hii;

Pili:           Kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa Bunge la Jumuiya ya Ulaya mwaka 2009 waliotembelea Tanzania na kuona uwezekano wa Jumuiya ya Ulaya kusaidia zaidi Mapambano dhidi ya Malaria Tanzania. Aidha, walifanya mazungumzo na Viongozi na Wawakilishi wa Asasi ya Malaria No More ya Marekani, ambao waliongozwa na Balozi Mark Green na kuwezesha kuanza kwa Mradi wa Zinduka, Malaria Haikubaliki;

Tatu:        Kushiriki  Kikao cha Nchi za Jumuiya ya Ulaya Nchini Ufaransa mwaka 2009 ili kujadili juhudi za Viongozi wa Kisiasa katika Kupamabana na Malaria Nchini;

Nne:         Kushiriki kutayarisha Mwongozo (Advocacy Guideline) utakaotumiwa na Wabunge, Madiwani na Viongozi wengine wa Kisiasa na Kijamii katika Utekelezaji na ushawishi wao katika kutokomeza Malaria Tanzania.

29.         Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa TAPAMA chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Riziki Said Lulida, Mbunge wa Viti Maalum kwa juhudi zao za kuhakikisha kuwa wanaungana na Wadau wengine Nchini na Duniani katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Nazipongeza pia Taasisi Zisizo za Kiserikali kwa ujumla wao ambazo zimejitokeza katika Mapambano dhidi ya Magonjwa mbalimbali, yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Saratani, n.k. Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge zaidi wazidi kujiunga na Asasi hizi na hasa za Magonwa ili kuweka hamasa kwa Wananchi katika Kupambana na Maradhi hayo. Aidha, natoa wito kwa Wananchi wote kwa ujumla kuunganisha nguvu za Kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria ili kunusuru nguvukazi ya Watanzania. Suala kubwa ni kuzingatia masharti ya Wataalam kuanzia katika kutunza mazingira yetu na kutumia Vyandarua kama kinga iliyo ya uhakika.




LISHE

30.         Mheshimiwa Spika, wakati nikitoa hoja ya kuahirisha Mkutano  wa Tisa wa Bunge, mwezi Novemba, 2012 nilieleza  kwa  kifupi utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa Mwaka 2011/2012 – 2015/2016. Pamoja na mambo mengine nilionesha hatua ambazo Serikali inachukua  kuondokana  na  tatizo  la  Lishe  Nchini.  Jambo kubwa na la msingi katika kupambana na tatizo la Lishe ni kutoa elimu kwa Jamii ili kula vyakula vyenye Virutubisho muhimu hasa kwa Mama Wajawazito na Watoto Wachanga. Jitihada za Serikali za kuwashirikisha Wadau mbalimbali katika kutoa Elimu ya Lishe Nchini zimeleta mwamko mzuri ambapo Wadau mbalimbali wakiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wa Maendeleo sasa wanashiriki kikamilifu katika utoaji elimu na kukuza kilimo cha mazao yenye virutubisho muhimu ili kuongeza vyakula vyenye virutubisho.

31.           Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe Nchini, hivi karibuni Waheshimiwa Wabunge chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o Mbunge wa Viti Maalum wameunda Kikundi cha kuongeza hamasa na kuzidisha chachu ya kutoa elimu kuhusu Lishe Bora hapa Nchini. Nimearifiwa kwamba, Kikundi hicho cha Wabunge kimekutana tarehe 10 hadi 12 Januari, 2013 na kukubaliana kuhusu kazi ambazo watafanya ili kuongeza sauti yao kwenye jamii juu ya umuhimu wa Lishe Bora.  Kikundi pia kimeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu (2013-2015) wenye malengo ya kukuza uelewa wa Umma juu ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto. Aidha, kikundi hicho kiliazimia kushawishi uwekaji wa vipaumbele vya Lishe katika Mipango ya Maendeleo na Bajeti za Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuingiza masuala ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto katika Sera na Mikakati mbalimbali ya Serikali. Azimio lingine ni kuimarisha usimamizi wa kazi za Bunge kuhusu Lishe, Chakula na Haki za Watoto.

32.           Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kukishukuru kwa dhati kikundi hiki ambacho kimeona umuhimu wa kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe, ikiwemo Utapiamlo. Nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuanzisha kikundi hiki. Niwashukuru kwa kuona umuhimu wa kusimamia tatizo hilo ili kupata suluhu ya kudumu. Ninatambua pia umuhimu wa Waheshimiwa Wabunge kuhamasisha masuala ya Lishe kwa Wananchi wa Majimbo yao. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wengine wote kushiriki kutoa msukumo wa pekee kwa Wananchi wa Majimbo yenu katika Mapambano dhidi ya Utapiamlo ili kwa pamoja tujenge Taifa lenye Watu walio na Lishe Bora. Lengo ni kuwawezesha kuchangia zaidi katika uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi wa Nchi kwa ujumla.

MCHAKATO KUELEKEA KATIBA MPYA

33.         Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetangaza kumaliza kazi ya kukusanya maoni binafsi ya Wananchi mmoja mmoja kama mchango wao kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya. Aidha, imekamilisha kazi ya kukutana na Makundi Maalum, Viongozi wa Kitaifa Wastaafu na Viongozi wa Kitaifa waliopo Madarakani. Kwa maana hiyo, Tume sasa imekamilisha kazi ya ukusanyaji maoni kama ilivyopangwa. Hivi sasa Tume inaendelea na kazi za uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na Wananchi na yale yaliyotolewa na Makundi Maalum ili baadaye kutayarisha Rasimu  ya Katiba ambayo itawasilishwa katika Mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na Tume Nchini kote.

34.         Kulingana na Ratiba, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba itafanyika kuanzia mwezi Juni, 2013 na itajumuisha Wajumbe watakaochaguliwa na Wananchi wenyewe kuanzia ngazi ya Kijiji. Wajumbe hao ndio watapaswa kuwasilisha maoni ya Wananchi katika Mikutano ya Mabaraza.

35.         Mheshimiwa Spika, nimearifiwa kuwa Tume imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa namna bora na ya Kidemokrasia ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambao unaendelea kusambazwa Nchi nzima. Mwogozo huo tayari umetangazwa katika Vyombo vya Habari ili Wananchi waufahamu na kutoa maoni kuhusu namna ya kuuboresha.

36.         Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Rasimu hiyo ya Mwongozo, katika Mikoa ya Tanzania Bara ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam, kila Kata itawakilishwa na Wajumbe wanne (4) watakaochaguliwa kutoka miongoni mwa Wakazi wa Vijiji vilivyopo kwenye Kata ambao wataungana na Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti Maalum kuunda Baraza la Katiba la Wilaya. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Tume imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambapo kila Kata watatoka Wajumbe wanane (8) ambao wataungana na Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti Maalum.  Kwa msingi huo, kutakuwa na jumla ya Wajumbe 18,169 watakaohudhuria Mabaraza ya Katiba ya Wilaya Kwa Tanzania Bara.

37.         Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, kutakuwa na Mabaraza ya Katiba ya Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 13.  Kila Shehia itawakilishwa na Wajumbe watatu (3), ambao wataungana na Madiwani wa Wadi, Madiwani wa Viti Maalum na Madiwani wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Kwa msingi huo, Wajumbe wote wa Mabaraza ya Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198.

38.         Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya watatakiwa kuwasilisha majina  yao kwa Maafisa Watendaji  wa Vijiji na Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Tanzania Zanzibar watawasilisha kwa Sheha kwa tarehe itakayoelekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapo baadaye.

39.         Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa Viongozi wote katika ngazi za Wilaya na Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu utaratibu ambao umewekwa na Tume. Kwa kufanya hivyo, Wajumbe ambao watashiriki katika Mabaraza ya Katiba  watapatikana  kwa  njia za Kidemokrasia na hivyo,  kufanikisha Vikao vya Mabaraza ya Katiba. Ni matumaini yangu kuwa Wananchi watausoma Mwongozo huo, na baadaye kuwasilisha mapendekezo na maoni yao kwa Tume kabla ya kazi ya uchaguzi wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanza rasmi.

40.         Nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi wote kushiriki kikamilifu kutoa maoni kuhusu Mwongozo huo na pia katika kuwapata Wajumbe watakaoshiriki katika Mabaraza ya Katiba kwa mujibu wa Sheria, na vilevile Wajumbe hao washiriki kikamilifu katika Vikao vya Mabaraza ya Katiba na kutoa maoni kwenye Rasimu ya Katiba.

RIPOTI YA TATHMINI YA UTAWALA BORA AFRIKA (APRM)

41.          Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza dhamira ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala bora nchini kwa kuwashirikisha Wananchi, Nchi yetu imekuwa miongoni mwa Nchi 33 za Umoja wa Afrika zilizoamua kwa hiari yake kujiunga na Mpango wa Bara la Afrika wa Kujitathmini Kiutawala Bora (The African Peer Review Mechanism - APRM). Tanzania ilijiunga na mchakato huo mwaka 2004, na Bunge liliuridhia  mwaka 2005.

42.          Mheshimiwa Spika, Mpango huu wa kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa Afrika na unatoa fursa kwa Wananchi kutathmini hali ya Utawala Bora katika Nchi zao na kuainisha kwa pamoja mambo mazuri yanayopaswa kuendelezwa na yale yenye changamoto za kufanyiwa kazi. Miongoni mwa sababu za Nchi yetu kujiunga na Mpango huu ni kutokana na ukweli kwamba Watanzania tuna mengi ya kuifundisha Afrika na Watu wake kuhusu Utawala Bora na sisi pia kujifunza kutoka kwa wenzetu.

43.         Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa baada ya zoezi la muda mrefu la kukusanya maoni Nchi nzima kuhusu Mpango huu ambapo Waheshimiwa Wabunge nao walishiriki kutoa maoni yao kuhusu Utawala Bora, sasa hivi Nchi yetu, imefikia hatua muhimu katika Mchakato huo wa kujitathmini kiutawala bora.

44.         Tarehe 26 Januari 2013, Ripoti ya Hali ya Utawala Bora hapa nchini iliwasilishwa mbele ya Wakuu wa Nchi za APRM Addis Ababa, Ethiopia ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu alipata fursa ya kuzungumzia mwelekeo wa Nchi yetu katika kujenga Taifa imara zaidi katika kipindi cha miaka 50 ijayo.

45.         Mheshimiwa Spika, katika Ripoti hiyo ambayo itatumika kama rejea, zimeainishwa juhudi zetu kubwa za kulinda amani Nchini. Pamoja na kuimarisha Utawala Bora wa Sheria na Haki za Binadamu. Aidha, kupitia Ripoti hiyo, wenzetu katika masuala ya kuendesha Utawala Bora, Barani Afrika na Duniani kwa ujumla wametambua jitihada zetu pamoja na mambo mengine katika kuulinda Muungano, kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Rushwa na zaidi ya yote wamejua sura ya Tanzania katika ukombozi na utetezi wa amani Afrika ambao Nchi yetu imepongezwa sana kwa juhudi zake.

46.          Ripoti hiyo pia imeainisha changamoto ambazo wenzetu wa Afrika wanadhani tunapaswa kuzifanyia kazi zaidi. Changamoto hizo ni pamoja na suala la kushughulikia Kero za Muungano, kuimarisha zaidi juhudi za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya Nchi yetu hasa kutokana na chokochoko za Kidini zilizoanza kujitokeza. Tumeaswa kuutumia vyema mchakato wa sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika miaka 50 ijayo.

47.         Mheshimiwa Spika, kuwasilishwa kwa Ripoti hiyo ya APRM kwa Wakuu wa Nchi wa Mpango huu ndio mwanzo sasa wa Serikali yetu ya kuimarisha maeneo yaliyoonekana kuwa tunafanya vyema. Pia hatua hiyo inatoa fursa ya kuanza kutekeleza Mpangokazi wa Miaka Mitano ambao umeainisha namna gani ya kuyafanyia kazi maeneo ambayo wananchi waliyaona kuwa yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Suala hili liliwekewa msisitizo na Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ya Mwisho wa Mwezi Januari 2013 aliyoitoa kwa Taifa.

48.         Mheshimiwa Spika, kutokana na manufaa ya APRM kama daraja kati ya Serikali na Wananchi wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja, Serikali itaendelea kuiimarisha Taasisi ya APRM hapa Nchini ili iweze kuwa kitovu chetu cha fikra (think tank) katika kushauri kuhusu masuala ya Utawala Bora Nchini. Vilevile, kuiwezesha Taasisi hii kuendelea kuwa kiungo kati ya Serikali yetu na Wananchi wake katika kutathmini na kutupatia mrejesho juu ya mipango na Sera zetu za maendeleo.

49.         Aidha, Serikali itaendelea kufadhili shughuli za APRM, kuiimarisha Taasisi kwa raslimali watu na fedha kwa ajili ya kazi pana zaidi za kutoa ushauri, kuunganisha Wadau mbalimbali na kuendelea kuratibu tathmini nyingine katika siku zijazo kwa lengo la kujipa nafasi ya kujikosoa ili kujisahihisha. Napenda kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama wakishirikiana na Sekretariati ya APRM Tanzania kwa kazi nzuri waliyoifanya ambayo imetuwezesha kufikia mafanikio hayo.

UANZISHAJI WA MAENEO MAPYA YA UTAWALA

i)           Uanzishaji wa Mikoa na Wilaya
50.         Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, mwezi Machi 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuanzisha Mikoa Mipya Minne (4) na Wilaya 19. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali sasa imekamilisha mchakato wa kuanzisha maeneo hayo Mapya ya Utawala, kwa kuanzisha Mikoa Minne ya Geita, Simiyu, Njombe na Katavi. Aidha, imekamilisha uanzishwaji wa Wilaya 19 za Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi, Itilima, Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama, Mlele, Momba, Nyang’wale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe. Mikoa na Wilaya hizo tayari zimeshaanza kufanya kazi na kutoa huduma mbalimbali kwa Wananchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais alishafanya Uteuzi wa Viongozi Wakuu wa Mikoa na Wilaya Mpya. Serikali imeendelea kupeleka Watumishi na kuanza kujenga miundombinu muhimu katika maeneo husika. Hata hivyo, pamoja na dhamira njema ya Serikali ya kuanzisha maeneo hayo, bado zipo changamoto nyingi, ikiwemo kupata Watumishi wa kutosha ambazo Serikali inaendelea kuzitatua.

ii)            Uanzishaji wa Halmashauri
51.         Mheshimiwa Spika, ili kupeleka huduma karibu zaidi kwa Wananchi, Serikali pia iliazimia kuanzisha Halmashauri Mpya 37. Uanzishaji wa Halmashauri hizo unaendelea na upo katika hatua mbalimbali kwa kuzingatia makundi yafuatayo:

Kundi la Kwanza, linahusu Halmashauri Mpya 8 za Manispaa, Miji na Jiji pamoja na Halmashauri Moja (1) ya Wilaya ambazo mchakato wa uanzishaji wake tayari umekamilika Kisheria na zimeanza kufanya kazi. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Jiji la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Mji wa Kahama, Halmashauri ya Mji wa Masasi, Halmashauri ya Mji wa Makambako, Halmashauri ya Mji wa Geita, Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya Busokelo. Halmashauri hizo tayari zimepata Hati na kupangiwa Wakurugenzi.

Kundi la Pili, linajumuisha Halmashauri Kumi (10) ambazo mchakato wa kuzianzisha umekamilika na tayari zimetangazwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 23 Novemba 2012. Halmashauri hizo ni Kalambo, Nsimbo, Mlele, Bumbuli, Ushetu, Msalala, Mbogwe, Busega, Momba na Kyerwa. Halmashauri hizo kwa sasa zinaandaliwa Hati ili zianze.

Kundi la Tatu, ni Halmashauri za Wilaya Kumi (10) ambazo mchakato wa uhakiki wake umekamilika na Amri za Uanzishaji zimeshasainiwa na wakati wowote zitatangazwa katika Gazeti la Serikali. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Wilaya za Buhigwe, Kaliua, Nyang’hwale, Wanging’ombe, Chemba,  Mkalama, Gairo, Nyasa, Itilima na Kakonko. Aidha, zipo Halmashauri nyingine Nne (4) katika kundi hili ambazo Amri zake zinakamilishwa na hatimaye zitasainiwa hivi karibuni. Halmashauri hizo ni Butiama, Tarime, Uvinza na Ikungi.

Kundi la Nne, linajumuisha Halmashauri Nne ambazo Mchakato wa uanzishaji wake umekamilika isipokuwa taratibu za Kisheria haziwezi kuanza kwa sababu baadhi ya Kata katika Halmashauri hizo ni mpya, hivyo hakuna Madiwani. Halmashauri hizo Nne (4) ni za Miji ya Kasulu, Handeni, Tunduma na Nzega. Mathalani, katika Halmashauri ya Mji wa Kasulu kuna Kata 14, na kati ya hizo, Kata 6 ni mpya na hazina Madiwani. Kwa upande wa Halmashauri  ya  Mji  wa  Handeni  ina  jumla ya Kata 12, kati ya hizo 9 ni mpya na hazina Madiwani. Aidha, Halmashauri ya Mji wa Tunduma ina Kata 5 mpya na zote hazina Madiwani na Halmashauri ya Mji wa Nzega ina Kata 10, na kati ya hizo Kata 3 ni mpya na hazina Madiwani.

52.         Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha maeneo hayo mapya ni kuwawezesha Wananchi kupata huduma karibu zaidi kwa Wananchi. Nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Watendaji wote kuwaongoza Wananchi kutumia fursa hiyo ya kuanzishwa kwa maeneo hayo katika kujiletea maendeleo. Serikali itaendelea kupeleka huduma zaidi karibu na Wananchi ili kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo hayo. Aidha, Serikali itaweka utaratibu wa kuzipatia Halmashauri zinazoanzishwa Watumishi hatua kwa hatua.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA NA SERIKALI DHIDI YA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA HARAMU NJE YA NCHI

53.         Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba, 2012, Bunge lilipitisha Azimio Na. 9/2012 kuhusu kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Nchi kufuatia Hoja Binafsi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Zitto Kabwe (Mb). Azimio hilo linahitaji, pamoja na mambo mengine, Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia Kitengo cha Asset Recovery Unit ili mabilioni yanayomilikiwa na Watanzania katika Mabenki nje ya Nchi ambapo hufichwa kwa kukwepa kulipa kodi yarudishwe na kwamba Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya Nchi waeleze wamezipataje ili TAKUKURU wachukue hatua za Kisheria dhidi ya watu wote wenye kumiliki fedha na mali kinyume na mapato yao halali. Aidha, iliazimiwa na Bunge na Serikali ikakubali kwamba, katika Mkutano wa Bunge wa 11 italeta Taarifa ya hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya Nchi.

54.         Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Desemba, 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuundwa kwa Kamati Maalum ya Kitaifa kushughulia hoja hiyo ya kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaundwa na Wajumbe wanane wanaotoka katika Taasisi za Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Jeshi la Polisi; Benki Kuu ya Tanzania; Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kazi za Kamati hiyo ni:
(i)            Kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya Nchi kinyume na Sheria na Kanuni za Nchi;

(ii)                  Kuchunguza iwapo fedha hizo ni haramu au la;

(iii)                 Kutambua Mabenki na Nchi zilizofichwa fedha hizo;

(iv)         Kuandaa mashtaka dhidi ya Watanzania watakaobainika kuficha fedha haramu nje ya Nchi; na

(v)          Kuishauri Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha.

55.         Mheshimiwa Spika, Kamati hii imeanza kazi zake rasmi tarehe 9 Januari 2013 kwa kupanga namna ya kutekeleza kazi zake ikiwemo kukusanya taarifa kuhusu Watanzania wanaodaiwa kutorosha fedha haramu nje ya Nchi na kuangalia namna ya kupata taarifa muhimu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

56.         Ili kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa ufanisi ni wazi kwamba itahitaji kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wananchi kwa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu suala hili. Hivyo, natoa wito kwa Wananchi wote wenye taarifa sahihi na za ukweli zinazoweza kuisadia Kamati kutekeleza kazi hii wanahimizwa wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kushirikiana kwa karibu na Kamati iliyoundwa na Serikali. Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge nao kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi za Kamati hii.

HITIMISHO

57.         Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda niwashukuru wote waliofanikisha Mkutano huu wa Kumi wa Bunge. Kipekee nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge lako Tukufu. Nimshukuru vilevile, Naibu Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Vikao vya Bunge kwa ufanisi. Aidha, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake kwa huduma nzuri walizozitoa wakati wote tukiwa hapa. Niwashukuru Watendaji  wa Serikali na Taasisi mbalimbali kwa kutekeleza majukumu yao vizuri ili kufanikisha shughuli za Bunge zilizopangwa. Niwashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kutufikishia habari kwa Wananchi yale yaliyojiri hapa Bungeni na kwa wakati. Vilevile, navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kazi yao nzuri na Madereva wote kwa huduma zao kwa Washiriki wa Bunge hili.

58.         Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niwatakie Safari Njema na sasa natoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi Siku ya Jumanne tarehe 9 Aprili, 2013 Saa 3:00 Asubuhi kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

59.         Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: