Thursday, November 15, 2012

UMOJA WA MATAIFA WAWAKUMBUKA WALIOPOTEZA MAISHA KATIKA OPERESHENI ZA KULINDA AMANI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon kwa pamoja na Rais wa Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa, Bw. Vuk Jeremic, na Rais wa Baraza Kuu la Usalama kwa mwezi wa Novemba, Balozi wa India, Hardeep Singh Puri wakiwasha mishumaa, ikiwa ni ishara ya kuwaenzi na kuwakumbuka raia, wanajeshi na polisi 29 ambao wamepoteza maisha katika kipindi cha kuanzia Novemba 2011 hadi Agosti 2012 wakati wakitekeleza majukumu ya ulinzi wa Amani katika Misheni 11 za Kulinda Amani za Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa marehemu hao waliokumbukwa katika hafla hiyo wapo wanajeshi watatu kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ( JWTZ) ambao ni Koplo Yusuf Said Chinguile, Staff Sajenti, Julius Chacha Marasi na Private Anthony Daniel Paul waliokuwa wakihudumu katika Jimbo la Darfur.
Baadhi ya wageni wakiwamo mabalozi na Waambata jeshi wakifuatilia hafla maalum ya kuwaenzi na kuwakumbuka raia, wanajeshi na polisi 29 waliopoteza maisha katika kipindi cha kuanzia Novemba 2011 hadi Agosti 2012. Hafla hiyo imefanyika siku ya Jumatano hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, wengine waliopoteza maisha katika kipindi hicho wanatoka, Nigeria, Kenya, Rwanda, India, Ethiopia, Niger, Jordan, Syria, Bangladesh, Sierra leone, Senegal, Brazil, Afghanistan, Togo, Egypt.

Na Mwandishi Maalum

Umoja wa Mataifa jana jumatano umefanya hafla maalum ya kuwaenzi na kuwakumbuka wanajeshi, polisi na raia ambao wamepoteza maisha wakati wakitekeleza jukumu la kulinda Amani chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Mataifa.

Hafla hiyo iliyojaa simanzi ya aina yake huku ikisindikizwa na nyimbo za maombelezo kutoka kwaya maalum, iliwahusu jumla ya wahanga 29 kati yao wakiwamo watanzania watatu ambao walikuwa Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi la Tanzania ( JWTZ).

Wanajeshi hao walikuwa wakihudumu katika kikosi cha Tanzania kilichoko katika jimbo la Darfur nchini Sudan, chini ya Jeshi la Pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika maarufu kama UNAMID.

Marehemu Koplo Yusuf Said Chinguile, Staff Sajent Julius Chacha Marasi na Private Anthony Daniel Paul walipoteza maisha kati kati ya mwaka huu.

Mbali ya Wanajeshi hao kutoka Tanzania, nchi nyingine ambazo zimepoteza wapiganaji wao katika kipindi cha kuanzia Novemba 2011 hadi Agosti 2012, na idadi ya marehemu kwenye mabano ni Nigeria (5), Togo(1), Sierra Leone(1), Rwanda(1),Kenya(1),India(2),Jordan(1),Egypty(1),Ethiopia(1),Niger(7),Afghanistan(1), Senegal(1) , Syria(1), Brazil(1) na Bangladesh(1).

Katika salamu zake mara baada ya tukio la kuwasha mishuma ikiwa ni ishara ya kuwakumbuka na kuwaombea pumziko la milele marehemu hao, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikuwa na haya ya kusema.

“ Leo hii tunawakumbuka wenzetu 29, raia, wanajeshi na polisi ambao wamepoteza maisha katika misheni 11 walikokuwa wakihudumu. Wenzetu hawa wanawakilishi mataifa 16. Kwa kupitia majina yao na historia yao, tunauona Umoja wa Mataifa, hawa wametoka kila pembe ya dunia, hawa kuwa na makuu, walijitolea kwa moyo wote kutekeleza jukumu hili mbali na nchi zao. Baadhi yao wanatoka katika maeneo ambayo yamegubikiwa na machafuko. Na walikuwa wamedhamiria kuleta amani kwa watu wengine”.

“ Tunakumbuka heshima ya kufanya kazi na wenzetu hawa, tunajivunia uamuzi na dhamana waliyoichukua kufanya kazi katika Umoja wa Mataifa. Tunaombeleza pamoja na familia zao na rafiki zao huku tukienzi uwezo wa kila mmoja wao na mchango walioutoa kwenye kazi zetu na kwa dunia yetu. Tafadhli ninawaomba muungane nami kwa dakika mmoja kuwakumbuka ndugu zetu na rafiki zetu”. Akasema Ban Ki Moon, Katibu Mkuu wa Umoja huo.

Akabainisha kwamba, vifo hivyo havikupashwa kutokea, lakini ni kielelezo dhahiri cha mazingira magumu na ya hatari wanayokabiliana nayo wale wote wanaojitolea kuhudumu katika Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa.

“Matumaini yangu ni kutokokea kwa matukio kama haya ambayo si ya lazima, kwamba watu wetu wote waweza kutekeleza majukumu yao bila ya kuhatarisha maisha yao. Lakini, tunatambua wazi kwamba Operesheni za kulinda Amani za Umoja wa Mataifga na watu wote wanaohudumu katika operesheni hizo, wamekuwa wakikabiriwa na mazingira hatarishi kwa usalama wao” akasema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Na Kuongeza “ Na wapumzike kwa amani, wakati tukiendeleza yale waliyokuwa wakiyafanya”.

Baada ya salamu za Katibu Mkuu pamoja na zile ziliyotolewa na Rais wa Baraza la 67 la Umoja wa Mataifa Bw, Vuk Jeremic , Rais wa Baraza Kuu la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba, Balozi wa India, Hardeep Sing Puri ns Bi Paulina Analea Mwakilishi wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa, kulifuatia tukio la kusomwa kwa jina moja baada ya jingine la marehemu hao 29.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa wimbo mwingine wa maombolezo “ The Lord Bless You and Keep You”.

No comments: