Na Mwandishi Maalum
Palestina jana ( alhamisi) imeibuka kidedea baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kuweka
historia kwa
kupiga kura Azimio
lililoipandisha hadhi ya kutambuliwa kama Nchi Muangalizi asiye Mwanachama wa Umoja wa Mataifa.
Azimio hilo lilipitishwa kwa kura 138 za ndiyo , kura tisa za hapana na 41
za kutofungamana na upande wowote. Kati
ya nchi zilizopiga kura ya hapana na ambazo zilitegemewa ni Marekani,
Israel na Canada huku Ujerumani na
Uingereza zikipiga kura ya kutofungamana na
upande wowote
Ukumbi Mkuu wa
Mikutano wa Baraza hilo ulifurika wajumbe wa katika tukio hilo la kihistoria lililokuwa na sura ya mchuano mkali wa mpira
wa miguu ambapo kila upande ulikuwa ukijitahidi
kushangilia kwa nguvu kila msemaji wa upade fulani aliposimama kujenga
hoja ya kutaka Azimio liungwe mkono au akijenga hoja ya kupinga Azimio
hilo.
Azimio hilo limeungwa mkono na mataifa mengi kutoka pande
zote yaani mataifa yale makubwa kama
vile Ufaransa, China, na Urusi nchi ambazo ni wajumbe wa kudumu wa Baraza
Kuu la Usalama. Zikiwamo pia nchi
nyingi za Jumuiya ya Ulaya, Afrika,Asia na Visiwa vya Karibian
Tukio hilo pia
lilishuhudiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, ambaye alisema,
kura ya kupitisha azimio hilo ilikuwa ikisisitiza umuhimu wa kutoa msukumo mpya
wa kuanza mazungumzo na akazisihi pande
hizo mbili kuonyesha dhamira ya kurejea kwenye meza ya mazungumzo.
Licha ya ukweli kwamba bado Palestina ina safari ndefu ya
kuweza kukubaliwa kuwa mwanachama kamili
wa Umoja wa Mataifa, lakini kwa
kukubaliwa kwake kuwa na hadhi ya kuwa
nchi muangalizi asiye mwanachama, kunaifungulia milango ya kujiunga na taasisi
nyingine za kimataifa, ikiwamo Mahakama
ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai(
ICC) kama ikitaka kufanya hivyo.
Akizungumza kabla
ya kupiga kura, Rais wa Mamlaka ya
Palestina, Mahmoud Abbas, aliwataka
wajumbe wa Baraza hilo kuchukua hatua
muhimu ya kurekebisha dhuluma ambayo wametendewa wananchi wa palestina
kwa muda mrefu.
Kwamba alikuwa anaitaka jumuiya ya kimataifa kuliunga
mkono azimio hilo na hivyo kupeleka ujumbe wa matumaini kwa wananchi wa
Palestina ambao amewaelezea kama walioteseka kwa muda mrefu na waliokuwa
wakielekea kukata tamaa.
Katika hotuba yake
iliyokuwa ikikatishwa mara kwa mara kwa
makofi na miluzi kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo. Kiongozi huyo wa Palestina,
akabainisha kwamba walikuwa wameamua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona
mazungumzo ya kutafuta amani kati yake na
Israeli ni kama vile yalikuwa yamekufa.
Hata hivyo
akasisitiza kwamba wamefikia hatua hiyo ya kupita Baraza Kuu kuomba kupandishwa hadhi na kutambuliwa kuwa nchi muangalizi asiye mwanachama hasa baada ya ombi lao kupitia Baraza
Kuu la Usalama kutofanyiwa kazi.
Lakini pia
wamechukua hatua hiyo kama kielelezo cha kuthamini amani na haki yao ya msingi
kama raia wengine ya kuwa na uhuru wa si tu kuwa na taifa lao linalotambuliwa bali pia haki na fursa ya kujiamulia mambo
yao wenyewe.
“ Hatukuja hapa
kutaka kufuta uhalali wa taifa fulani
yaani Israeli, lakini tuko hapa kutafuta uhalali wa taifa jingine yaani
Palestina,kwamba lazima sasa iijipatie uhuru wake” akasema Mahmoud Abbas
Na kuongeza “ Tunawaomba
leo hii mtupatie cheti chetu cha kuzaliwa”. Akasama Abbas na kuongeza
kwamba uamuzi huo hauna maana kwamba
wanaachana na mchakato wa kurejea kwenye meza ya mazugumzo. Wala haukuwa na nia
ya kutaka
Azimio la kuipandisha hadhi Palestina limepigiwa kura katika tarehe ( Novemba 29) ambayo Baraza hilo lilikuwa likiadhimisha miaka 65
tangu lililopitisha azimio namba 181
lililoigawa Palestina kuwa
mataifa mawili lile la Kiyahudi na la Kiarabu.
Aidha Tarehe hiyo pia huadhimishwa siku ya kimataifa ya
mshikamano na wananchi wa Palestina. Siku ambayo ilipitishwa mwaka 1977
Kwa upande wake Balozi wa
Israeli katika Umoja wa Mataifa,
Ron Prosor yenyewe imesema nchi
yake haikubaliani na azimio hilo na kwamba Palestine ilikuwa inafanya kosa
kubwa na itakuja kujuta hapo baaaye.
Aidha Israel inasema haliitambui Azimio hilo kwa sababu lilikuwa limeegemea
upande mmoja na lilikuwa haliitambua taifa la
Kiyahudi.
Mjumbe huyo wa
Israeli akiongea kwa kejeli alieleza
baya kwamba, azimio hilo haliwezi kwa
namna yoyote ile kuleta amani bali lilikuwa
linarejesha nyuma mchakato wote wa kuleta amani, na kwamba yenyewe ilikuwa inamini katika majadiliano badala ya
njia za mkato mkato kama iliyofanya Palestina hiyo jana.
Nayo Marekani
kupitia Balozi wake Susan Rice imeeleza bayana kwamba haikubaliani na azimio
hilo ambalo kwao ilikuwa ni kama
kupoteza muda.
Hata pamoja na
kukandia na kuzikejeli nchi zilizopiga
kura ya kuunga mkono azimio hiyo, Marekani inasema itaendelea na juhudi zake
za kuhakikisha kwamba mazungumzo ya kutafuta suluhu ya kudumu kati ya pande hizo mbili
yanaendelea.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikuwa ni kati ya nchi zilizopiga kura ya
kuunga mkono azimio hilo, na Balozi
Tuvako Manongi alielezea ni kwa nini Tanzania iliamua kupiga kura ya
ndiyo.
Baadhi ya sababu alizotoa ni kwamba Tanzania ilishaitambua Palestina kama nchi huru tangu
mwaka 1961 na imekuwa na uhusiano wa kidiplomasia na nchi hiyo kwa miaka mingi.
Aidha akasema kwa
kupishwa kwa azimio hilo jumuia ya kimataifa ilikuwa inalitambua taifa huru la wapalestina kama vile ilivyoitambua
Israel na kwa Tanzania mataifa yote mawili yana uhalali wake.
Akaongeza pia kwamba Tanzania inaamini Palestina ilikuwa na kila sababu ya siyo tu kutambuliwa lakini pia kuwa na uhuru wa kujiamulia mambo yake.
Akasisitiza kuwa Tanzania inaamini katika makubaliano na
majadiliano yanayolenga kufika suluhu
ya kuwa na mataifa mawili yakiishi sambamba na
kwa amani kulingana na makubaliano ya mwaka 1947.
No comments:
Post a Comment