Wednesday, October 17, 2012

WALIOACHIWA NA ICTR BADO HAWANA PA KWENDA

Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji wa Kimbari ya Rwanda (ICTR) Vagn Joensen akiwasilisha taarifa yake ya mwaka mbele ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa mwanzoni mwa wiki, katika taarifa yake hiyo ambayo alisema ni ya mwisho kwake kama Rais wa ICTR ambayo iko ukingoni mwa kukamilisha majukumu yake pamoja na ile ya iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani (ICTY) iliyowasilishwa na Rais wake Theodor Meron. Alieleza bayana kwamba baadhi ya changamoto zilizo mbele ya Mahakama hiyo ni Nchi za kuwahamishia watu ambao ama wameachiwa huru na Mahakama hiyo na au wamemaliza vifungo vyao. Watu hao ambao wanakadiriwa kuwa nane wanaendelea kuhifadhiwa katika nyumba salama ( Sefu House) Jijini Arusha Nchi Tanzania.
Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi akizungumza wakati wa upokeaji wa taarifa za mwaka za mahakama za kimataifa za ICTR na ICTY. Pamoja na Mambo mengine, Balozi Manongi alisizihisi nchi wanachama wanachama wa Umoja wa Mataifa kulipokea ombi la Mahakama ya ICTR kwa mtizamo chanya hususani kwa kutoa ushirikiano wa kuwapokea watu hao ambao wanahitaji nchi za kwenda. Akasema suala hilo ni nyeti na ni la haraka hasa kwa kuzingatia kuwa mahakama hiyo inamaliza muda wake. Kama watu hao watakosa mahali pakwenda kuna hatari ya kuendelea kuhifadhiwa nchini Tanzania. 

Na Mwandishi Maalum 

Tanzania inaweza ikajikuta ikiendelea kuwahifadhi watu walioachiwa huru na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda,( ICTR) kutokana na kile kilichoelezwa kukosekana nchi ya kuwahamishia. Rais wa ICTR , Vagn Joensen amesema anaunga na wale wote ambao wameelezea wasiwasio wao juu ya hatima ya watu hao ambao wamekuwa wakihifadhiwa katika nyumba salama ( Safe House) jijini Arusha kwa zaidi ya Miaka sita sasa tangu kuachiwa huru. 

Hakuna nchi ambayo imejitokeza kuwapokea watu hao wanaokadiriwa kuwa wanane , na inasemekana wao wenyewe hataki kurejea nchi kwao . Watano kati yao waliachiwa huru Mahakama hiyo na wengine watatu wamemaliza vifungo vyao. 

Taarifa zinaonyesha kwamba wakati Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipokubali kuwa mwenyeji wa makahama hiyo ilieleza bayana kwamba isingekuwa tayari kuwahifadhi watu watakaoachiwa huru au watakaokuwa wamemaliza vifungo vyako. 

Akiwasilisha mbele ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa, taarifa ya mwaka ya utendaji kazi wa mahakama hiyo, Rais huyu amesema wakati Mahakama hiyo ikielekea ukingoni mwa ukamilishaji wa majukumu yake, bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo hiyo ya wapi pa kuwapeleka watu hao walioachiwa huru.

 “Ninaungana wa wale wote walioonyesha wasiwasi wao juu ya hatima ya watu hawa. Watu ambao bado wako Arusha ,nchini Tanzania. Hawana hati za kusafiria, wametenganishwa na familia zao, hawana uhuru wa kutembea wala kujipatia ajira na hakuna nchi ambazo zimejitolewa kuwachukua” akasema Vagn Joensen. 

Na kuongeza kwamba sheria za kimataifa zinabainisha wazi kwamba wale wote ambao wameachiwa huru wanatakiwa kuruhusiwa kuendelea na maisha yao na kufurahia uhuru wao na haki zao. Lakini hali si hivyo kwa watu hao nane. 

Rais wa ICTR alitumia mkutano huo kuwasihi nchi wanachama kuwakubali watu hao. Katika taarifa yake aliyoitoa mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na ambayo alisema ni ya mwisho kwake, kama Rais wa ICTR pamoja na mambo mengine, ameabinisha kuwa jumla ya watuhumiwa tisa ambao walitakiwa kufikishwa mahakamani hapo kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mwaka 1994 bado hawajulikani walipo hadi sasa. 

 Aidha akaeleza kuwa kesi sita za watuhumiwa hao zimehamishiwa nchini Rwanda na tatu zitaendelea kushughulikiwa katika Tawi la Arusha ambalo limepewa jukumu la kuendesha Kesi Masalia za Mahakama hiyo na pia uhifadhi wa nyaraka na kumbukumbu zote muhimu zinazohusiana na mahakama hiyo.

 Akizungumza wakati wa kupokea taarifa ya Mahakama hiyo pamoja na Mahakama ya iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani ( ICTY), Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Tuvako Manongi yeye amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na mahakama hiyo hasa katika kipindi hiki inapoelekea kukamilisha majukumu yake. 

Akizungumzia kuhusu suala la watu walioachiwa huru au kumaliza vifungo vyao kukosa nchi za kwenda, Balozi Manongi alikuwa na haya ya kusema. “ Rais wa ICTR amekuwa akifanya jitihada kubwa za kuwatafutia mahali pa uhamisho watu hawa. Na kwa kweli jambo hili ni nyeti na lina uharaka wake na hasa ikizingatiwa kwamba mahakama hii inamaliza muda wake. 

Tunawaomba wenzetu mlichukulie ombi la mahakama hii kwa mtizamo chanya” akasihi Balozi Manongi Na kuongeza kwamba ushirikiano wa nchi wanachama wa UM ni muhimu sana katika kuhakikisha watu hao ambao ama wameachiwa huru, au wamemaliza vifungo vyao, na ama wanatakiwa kwenda kufungwa mahali pengine wakapata fursa hiyo. 

Akizungumzia uondokoaji wa wafanyakazi ambao wengine wao wamekuwa na historia na kumbukumbu na mahakama hiyo, Mwakilishi huyo wa Tanzania anasema kama ilivyokuwa huko nyuma. Tanzania inasikitishwa na ukweli kwamba wafanyakazi ambao ndio wamekuwa muhimili na historia ya mahakama hiyo wanalazimika kuondoka kwa sababu tu ya kutohakikishwa hatima yao. Akizungumza kuhusu jukumu la kuhifadhi ya nyaraka na kumbukumbu za mahakama hiyo. 

Balozi Manongi anasema Tanzania inalichukulia kwa uzito jukumu hilo na kwamba inalishukuru Baraza Kuu la Usalama wa Umoja wa Mataifa kwa uamuzi wake kwamba Tanzania ndiyo nchi inayostahili kuhifadhi na kutunza kumbukumbu na nyaraka zote zinazohusiana na mahakama ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda. 

Mahakama hizo mbili yaani ICTR na ICTY ambazo zitazimiza miaka 20 tangu kuanzishwa kwake hapo mwezi Mei mwaka 2013 ziko mbioni kumalizia majukumu yake kama yalivyoainishwa na mamlaka mbalimbali za Umoja wa Mataifa zikiwamo Baraza kuu la Usalama baada ya kufanya kazi iliyotukuka ya kuwaleta mbele ya haki wale wote waliotuhumiwa kuhusika na matukio ya kutisha na ambayo yalipoteza maisha ya wananchi wasiokuwa na hatia katika ile iliyokuwa Yugoslavia ya Zamani na Nchini Rwanda.

No comments: