Na Mwandishi Maalum
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim (Mb)pichani juu, ameliambia Baraza
Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa, kwamba Tanzania na Afrika kwa ujumla iko katika
mwelekeo mzuri wa kuutokomeza ugonjwa wa malaria licha ya changamoto
mbalimbali.
Ameyasema hayo siku
ya jumatano wakati Baraza Kuu lilipokuwa
likijadili ajenda tatu ambazo zilihusu
ni Muongo wa kutokomeza Malaria katika
nchi za Afrika, taarifa ya Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ushirikiano
Mpya wa Maendeleo ya Kiuchumi (
NEPAD) kati ya Umoja wa Mataifa na Afrika na chanzo za migogoro Barani Afrika
na uimarishaji wa amani ya kudumu.
Katika majadiliano
hayo ambayo yalifunguliwa na Rais wa Baraza hilo, Bw. Vuk Jermic, Naibu Waziri anasema katika kuukabili ugonjwa wa malaria, serikali nyingi za Afrika
ikiwamo ya Tanzania zinatambua njia zipi zinafanya kazi katika kuukabili
ugonjwa huo na ni njia zipi
hazifanyi kazini.
Kwa mfano anasema,
Tanzania bara na visiwani imefanikiwa katika kuhakikisha pamoja na mambo
mengine kwamba, vyandarua vyenye
viatilifu siyo tu vinapatikana lakini pia vinapatikana kwa bei nafuu kwa
kuondoa kodi mbalimbali.
“ Serikali yangu
ilifanya maamuzi ya makusudi kabisa ya
kuhakikisha kwamba inagawa bure
vyandarua vyenye viatilifu, mpango huu ambao unakwenda sambamba na
uangamizaji wa mazalia ya mbu,
upatikanaji wa kinga na huduma za upimaji na matumizi ya dawa mseto
za malaria, mbinu hizi zote zimesaidia sana katika kupunguza idadi ya kesi
za malaria na hata vifo vitokanavyo na
ugonjwa huo.” Akaeleza.
Akatumia fursa hiyo
kuzihimiza serikali za nchi nyingine kuiga mfano wa Tanzania hasa katika
kupunguza au kuondoa kodi na ushuru
kwenye vyandaru na bidhaa nyingine zinazohitajika katika kuudhiti ugonjwa,
kupunguza bei ya bidhaa hizo kwa
watumiaji na kuboresha biashara huru.
“Tanzania ilikuwa
nchi ya kwanza katika Afrika kufanya hivyo, kwa kuondoa kodi
na ushuru imesaidia kupunguza muda wa uagizaji wa bidhaa hizo na kuwapo
kwa unafuu kwa sekta za umma na binafsi. Faida ya
kiafya iliyopatika kwa kutumia utaratibu huu ni kubwa mno ikilinganishwa
na mapato tuliyopoteza” akasisitiza Naibu
Waziri.
Hata hivyo akasema, licha ya mafanikio chanya
ambayo yamekwisha kupatikana kupitia mbinu hizo na nyingine, bado
kunachangamoto kadhaa.
“ Hapana shaka kwamba
vita dhidi ya malaria inahitaji mambo mawili, uongozi na raslimali. Viongozi wa Afrika kupitia Muungano wao dhidi ya Malaria ( ALMA) wameonyesha uongozi wa pamoja
wa kuukabili ugonjwa huu. Hata hivho wanakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa
raslimali. Sote tunafahamu kuwa ugonjwa
wa malaria unatibika lakini mkazo wetu umekuwa katika kuudhibiti kwa
sababu ndiyo njia nafuu na rahisi” akaeleza Naibu Waziri
Na kuongoza kwamba
matibabu sahihi na kamili ya ugonjwa huo
na kuwepo wa miundombinu ya kuutibu
ikiwa ni pamoja na uwepo wa vituo vya afya kwa umbali mfupi
vikiwa na wataalamu wakutosha wa afya ni
njia sahihi zaidi.
Lakini anasema Naibu
Waziri “ Hapa ndipo hasa penye
tatizo, karibu serikali zetu nyingi
hususani katika nchi zinazoendelea hazina uwezo wa kuwakikishia wananchi
wao upatikanaji wa huduma hizo na hasa
katika maeneo ya vijijini ambako wananchi wengi wanaugua malaria bila wao
wenyewe kutambua kwamba wanaugua ugonjwa huo”.
Na kwa sababu hiyo,
Naibu Waziri Mahadhi amezitaka nchi
zilizoendelea ikiwa ni pamoja na Umoja wa Mataifa kuendelea kushirikiana kwa
karibu na Viongozi wa Afrika ili
hatimaye ugonjwa huu uweze kutokomezwa au kupunguzwa kabisa Barani Afrika
ifikapo 2015.
Baadhi ya wachangiaji
wa ajenda hiyo ya Malaria, akiwamo Naibu Waziri Mkuu
na Waziri wa Mambo ya Nje wa
Luxembourg, Bw. Jean Asselborn
yeye ameeleza kwamba nchi yake
imekuwa ikishirikiana na Shirika la Afya
Duniani (WHO) ambapo nchi hiyo inafadhili
shughuli mbalimbali za kupambana na Malaria, na utafiti wa magonjwa mengine ya kitropikali maeneo ambayo kila mwaka imekuwa ikichangia
euro milioni tatu.
Aidha akasema mchango
wao wa hiari katika Mfuko wa Kupambana na
Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria bajeti yake inafikia euro milioni
2.5
“ Tunahitaji kuwa
wabunifu zaidi na siyo tu pale inapokuja katika kufadhili upatikanaji wa huduma
za kuudhibiti na kuutibu ugonjwa wa malaria, lakini pia katika kutopoteza mwelekeo na kuwa na mtazamo mpana zaidi wa kuimarisha mifumo wa kitaifa
wa huduma za afya ili iwe endelevu”
akasisitiza Naibu Waziri Mkuu na
Waziri wa Mambo ya Nje, Jean Asselborn..
No comments:
Post a Comment