Friday, October 12, 2012

TANZANIA YAUNGA MKONO MAKOLONI KUJIAMLIA MAMBO YAKE YENYEWE

Naibu Balozi wa Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Ramadhan M. Mwinyi, akizungumza wakati wa majadiliano kuhusu ajenda ya Umalizaji Ukoloni, katika Mkutano wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa, Kamati hiyo ambayo ni maalum inajihusika na Masuala ya Siasa na Umalizaji wa Ukoloni.

Na Mwandishi Maalum 

Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Balozi katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akizungumza wakati wa mkutano wa Kamati ya Nne ya Baraza Kuu la 67 la Umoja wa Mataifa. 

Kamati hiyo ni Kamati Maalum inayohusika na masuala ya Siasa na umalizaji wa Ukoloni na kwa wiki nzima imekuwa ikijadili ajenda zinazohusiana na suala zima la umalizaji wa Ukoloni kama inavyoelekezwa katika Katiba ya Umoja wa Mataifa na Maazimio mengine mbalimbali. Hadi sasa kuna makoloni 16 ambayo bado yapo chini ya Ukoloni na hayajawa huru kujiamulia mambo yake yenyewe. 

Baadhi ya Makoloni hayo ni Sahara ya Magharibi ambayo ni koloni pekee lililobaki Barani Afrika. Kwa zaidi ya miaka 57 Sahara ya Magharibi ambayo imejitangaza kujitenga kutoka Morocco imekuwa katika mgogoro mkubwa na serikali ya Morocco. 

Mgogoro ambao umesababisha wananchi wengi kupoteza maisha, wengine kuishia kuwa wakimbizi huku zikiwamo shutuma za ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Aidha Kamati hiyo ilipata fursa ya kuwasilikiliza Wadai (Petitioners) 68 ambao ama walikuwa wakitetea haki ya Sahara Magharibi kujipatia uhuru wake na fursa ya kujiamulia mambo yao au walikuwa wakiitetea Morocco dhidi ya Sahara Magharibi. 

Akichangia maoni ya Tanzania katika mkutano huo, Naibu Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu wa Serikali ya Morocco na POLISALIO kuendelea na mazungumuzo ya kutafuta suluhu ya kudumu na kubwa zaidi ni kwa Morocco kuiachia Sahara Magharibi ijitawale na kujiamulia mambo yake yenyewe. 

Aidha Tanzania kupitia msemaji wake huyo imeungana na mataifa mengine ambayo yalizungumzia kwa kina haki na uhuru wa Sahara ya Magharibi huku ikitoa wito kwa Morocco kujiunga tena na Umoja wa Afrika (AU) kama njia moja wapo itakayosaidia kuutafutia ufumbuzi mgogoro huo.

 Aidha Tanzania kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine imempongeza na kumtia shime Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na mshauri wake katika suala la Sahara ya Magharibi Balozi Christopher Ross, kuendelea na juhudi zao za kuhakikisha kwamba mazungumao kati ya pande hizo mbili yanaendelea kufanyika kwa njia ya uwazi, kuaminiana na kwa kuzingatia Katiba ya Umoja wa Mataifa na maazimio mengine yahusuyo suala la Sahara ya Magharibi.

 Tanzania pia imezitaka nchi zile ambazo zinaendelea kuyashikilia makoloni kuonyesha utashi wa kisiasa na kushirikiana na Kamati hiyo maalum ili kufikia muafaka kuhusu makoloni hayo 16 ambayo bado yanaendelea kutawaliwa. 

Mbali ya Sahara Magharibi, makoloni mengine ni Falkland Islands/Malvinas koloni linalogombewa kati ya Uingereza na Argentina, Gibraltar ambalo pia linagombewa kati ya Uingereza na Spain, New Caledonia, America Samoa, Anguilla, Bermuda, British Virgin Islands, Cayman Islands, Guam, Montserrat, Pitcairn, Saint Helena, Turks and Caicos Islands, United States Virgin Islands, na Tokelau. Baadhi ya makoloni hayo yanashikiliwa na Marekani.

No comments: