Safari ya kukwea Mlima Everest ikipamba moto
Wilfred Moshi akifanya mahojiano na Urban Pulse katika kilele cha milima ya Volcano Holyrood Park Edinburgh
Wilfred Moshi akipeperusha bendera ya Tanzania kileleni Mlima Everest |
Frank Eyembe wa Urban Pulse na Wilfred Moshi baada ya kupanda moja ya milima mirefu Uingereza iliyopo Holyrood Park Edinburgh
Wilfred Moshi safarini kuelekea kileleni |
Mike Knox mwanzilishi wa Twende Pamoja
akifanya mazungumzo na Urban Pulse
Imeandikwa na Freddy Macha kwa ushirikiano na Urban Pulse
Picha zote Ihsani ya Wilfred Moshi na Urban Pulse
Kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya nchi yetu kijana Wilfred Moshi, Mbongo wa kawaida tu (anayefanya kazi ya upagazi kuwahudumia watalii wanaopanda mlima Kilimanjaro), ameweka rekodi mpya ya kuwa Mtanzania wa kwanza kupanda Everest - mlima mrefu kushinda yote duniani.
Hivi karibuni, Moshi, alialikwa majuma matano nchini Uingereza kutembelea shule mbalimbali za Scotland akakutana na takribani wanafunzi 5,000 .
Wanafunzi walitaka kufahamu namna alivyopanda mlima Everest wenye mita 8,848 (futi 29, 029). Mlima huu mgumu kuukwea kuliko yote ulimwenguni umewahi kupandwa na na watu 4,000 toka ulipoanza kufikiwa kileleni na Edmund Hillary na Sherpa Tenzig Norgay mwaka 1953. Kati ya hao 200 walifariki. Mwaka huu wanne wameshafariki wakiijaribu shughuli hii inayochukua miezi miwili na kugharimu Dola 100,000 (Shilingi milion 157,500,000) Linganisha na mlima Kilimanjaro unaodai siku tano na gharama (ikiwepo vifaa husika) Dola 2,000 (Shilingi milioni 3, 161).
Wilfred Moshi ni Mtanzania wa kwanza na Mwafrika wa tatu kufikia kilele cha kitendawili hiki (kilichoitwa “Chomolungma” na wenyeji kabla ya kubatizwa jina la Everest na Waingereza enzi za ukoloni) Mei 19, mwaka huu.
Wilfred aliyezaliwa mwaka 1979 na kumaliza kidato cha sita shule ya Kilimanjaro Boys, amekuwa akipanda mlima Kilimanjaro tangu angali bado shuleni na miaka 19.
Mara baada ya kuwasili Edinburgh, Scotland alikaribishwa bungeni akakutana na Waziri wa Sheria mheshimiwa Kenneth MacAskill na viongozi wengine. Safari ilikirimiwa na shirika la “Twende Pamoja” lililoanzishwa na Mike Knox miaka 30 iliyopita. “Twende Pamoja” imejenga ushirikiano kati ya wanafunzi wa Scotland na shule 34 za Kitanzania. Ni moja ya mashirika, watu binafsi na wafadhili mbalimbali ulimwenguni waliochangia fedha za kumwezesha Moshi kupanda mlima Everest.
Balozi wetu Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe vile vile alisafiri toka London kumtembelea Wilfred Moshi na kumpa heko. Umbali wa London had Scotland ni kama Dar es Salaam hadi Kigoma!
Kwanini Moshi anahusudu kupanda milima?
Ukweli sisi bado hatuoni umaana (au umuhimu) wa kupanda milima. Anasema lengo lake lilikuwa kutimiza ndoto ya Mtanzania wa kwanza kupanda Everest. Pili, upandaji milima ni moja ya njia zinazoweza kusaidia kujenga jamii kwa misaada na fadhila za mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO). Tujiulize vipi alisaidiwa na watu wengi namna hiyo kuchangia fedha takikana? Tatu, Moshi amethibitisha ukiwa na moyo na jitihada unaweza kufanya lolote. Ushujaa na ushupavu wake utasaidia kuwahamasisha Watanzania kuwa ukitaka kufanya jambo lolote lile unaweza ili mradi uwe na moyo na nidhamu.
Mpanda milima mashuhuri, Mike Hamill, aliyeshakwea milima yote mikubwa saba duniani anasema katika kitabu chake kipya (“Climbing Seven Summits”) wapanda milima ni watu wenye moyo wa kufikia malengo na kufanikiwa katika maisha yao.
Akiwa Uingereza Moshi alipanda mlima wa Ben Nevis mrefu kuzidi nchi hii- wenye mita 1,344 (futi 4, 409). Baada ya kuimudu milima mitatu sasa , Wilfred Moshi ameazimia kupanda milima katika mabara yote 7 duniani. Anasema amebakisha milima mitano: Aconcagua ( Marekani ya Kusini ), Kosciuszko (Australia), Vinson Massif ( Antarctica) McKinley(Alaska) na Elbrus(Urusi).
Mungu ambariki Mtanzania huyu mwenye
jazba na hamasa anayetuletea sifa.
Soma habari zaidi:
No comments:
Post a Comment