Katibu
wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na waandishi wa
habari leo, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es
Salaam. Amezungumzia mambo kadhaa ikiwemo maandalizi ya uchaguzi mkuu wa
CCM na kulaani matukio ya vurugu yaliyotokea Mbagala, Dar es Salaam.
Kikao cha
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa kilichofanyika tarehe 13/10/2012
pamoja na mambo mengine kilipanga ratiba ya Mkutano Mkuu wa Taifa iwe
kama ifuatavyo:-
Mkutano
Mkuu wa Nane wa Kawaida wa CCM utafanyika tarehe 10 - 12 Novemba, 2012
. Kwa kawaida Mikutano Mikuu ya CCM imekuwa ikifanyika kwa siku
mbili. Lakini safari hii CCM imeamua mkutano huo uwe wa siku tatu
ili kutoa fursa kwa Wajumbe kujadili kwa kina taarifa muhimu zitakazowasilishwa.
Mkutano
huo utafanyikia KIZOTA - Dodoma mahali ulipofanyika Mkutano Mkuu uliopita
mwaka 2010.
Shughuli muhimu
zitakazofanywa wakati wa Mkutano huo zitakuwa:-
Kufanya
marekebisho ya Katiba ya CCM ya 1977 toleo la 2010 kwa kuzingatia mapendekezo
ya Halmashauri Kuu ya Taifa yatakayowasilishwa kwenye Mkutano huo.
Kupokea na
kujadili taarifa mbalimbali zikihusu:-
Taarifa
ya Kazi za Chama kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2007-2012
itakayowasilishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa.
Taarifa
ya Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ya Serikali
ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Shughuli za
Uchaguzi ambazo zitahusu Uchaguzi wa:-
Wajumbe
wa Halmashauri Kuu ya Taifa Viti Kumi vya Bara na kumi vya Zanzibar.
Mwenyekiti
wa CCM.
Makamu wawili
wa Mwenyekiti mmoja kutoka Bara na mwingine kutoka Zanzibar.
Shughuli
za Mkutano Mkuu zitatanguliwa na kuweka Jiwe la Msingi la Majengo ya
Ukumbi wa Mikutano na Makao Makuu ya CCM eneo la Medelii katika Manispaa
ya Dodoma. Shughuli hii itafanywa na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete.
MAANDALIZI
YA MKUTANO
Shughuli
za Maandalizi ya Mkutano zinaendelea vizuri. Shughuli hizi ni
pamoja na uchapaji wa Nyaraka mbalimbali; usafiri wa Wajumbe, Maandalizi
ya Ukumbi na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya kufanikisha Mkutano
huo.
VURUGU ZILIZOTOKEA
MBAGALA
Chama cha
Mapinduzi kimesikitishwa na matukio yaliyotokea Mbagala, jijini Dar
es Salaam, tarehe 11 Oktoba 2012. Chama cha Mapinduzi kinalaani kitendo
cha kukojolewa kwa kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislam, yaani Kuran.
Vilevile, Chama cha Mapinduzi kinalaani vitendo vya vurugu na kuvamiwa
na kuchomwa moto makanisa.
Vitendo
vyote hivi havifanani na mila na desturi za Watanzania. Kitendo cha
kukojolea kitabu kitakatifu cha Waislamu hakikubaliki. Na kitendo cha
kuvamia na kuchoma moto nyumba za ibada za Wakristo na kufanya vurugu
pia hakikubaliki. Tanzania ni nchi inayofahamika na kusifika kwa amani
na utulivu na kwa umoja na mshikamano wa watu wake wa kabila, rangi
na dini zote. Chama cha Mapinduzi kinawasihi wananchi wawe na subira
na uvumilivu yanapotokea matukio kama haya na waviachie vyombo vya dola
vifanye kazi yake.
Ni imani
ya CCM kwamba vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki kwa wote waliohusika
na matukio haya. Pia, tunatumaini kwamba hali ya amani na utulivu itarejea
Mbagala kama kawaida.
UTEUZI WA
MAJINA YA WAGOMBEA NAFASI MBALIMBALI
MKOANI KILIMANJARO
Kamati Kuu
pia imefanya uteuzi wa mwisho wa majina ya Wanachama wa CCM walioomba
nafasi za Uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi katika nafasi za Uenyekiti
wa CCM Wilaya na Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nafasi ya Wilaya
za Siha na Moshi Vijijini.
Kwa mujibu
wa Katiba ya CCM; uteuzi wa mwisho wa nafasi hizi hufanywa na Halmashauri
Kuu ya Taifa, lakini Kikao cha tarehe 25/9/2012 kilichofanyika Mjini
Dodoma hakikufanya uteuzi wa wagombea wa nafasi hizi katika Wilaya za
Siha na Moshi Vijijini. Hivyo, Kikao hicho kilikasimu madaraka yake
ya uteuzi kwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa.
Nafasi za
Uongozi zinazogombewa na majina ya walioteuliwa ni kama ifuatavyo:-
(1) Nafasi
ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini
Waliojitokeza
kugombea nafasi hii ni 13. Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-
(a) Ndugu
Shayo Isack EDWARD
(b) Ndugu
Masenga John GABRIEL
(c) Ndugu
Shao C. GEOFREY
(d) Ndugu
Mallya Mathew MARTIN
(2) Nafasi
ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha
Waliojitokeza
kugombea nafasi hii ni wanne (4). Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-
(a) Ndugu
Tawida Nahato BASSO
(b) Ndugu
Simon Lekshon MOLLEL
(c) Ndugu
Happiness Mathias MUNUO
(d) Ndugu
Oscar Jeremiah TEMI
(3) Nafasi
ya Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa Wilaya ya Siha
Waliojitokeza
kugombea nafasi hii ni saba (7). Walioteuliwa ni wanne (4) wafuatao:-
(a) Ndugu
Meijo Loloinyo LAIZER
(b) Ndugu
Joha Shabani MTAWAZO
(c) Ndugu
Happiness Mathias MUNUO
(d) Ndugu
Cosmas Sebastian MUSHI
Imetolewa
na:
*
Nape Moses
Nnauye,
KATIBU WA
HALMASHAURI KUU YA TAIFA
IDARA YA
ITIKADI NA UENEZI
14/10/2012
No comments:
Post a Comment