Wednesday, October 10, 2012

ATCL yatangaza kuanzisha safari za ndani nyingine baada ya kurejesha huduma zake Ijumaa hii

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Kapteni Milton Lusajo Lazaro akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini D ar es Salaam jana juu ya mpango wa shirika hilo kurejesha safari zake kuanzia Ijumaa hii
 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Kapteni Milton Lusajo Lazaro (kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini D ar es Salaam jana juu ya mpango wa shirika hilo kurejesha safari zake kuanzia Ijumaa hii. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Biashara wa Shirika hilo Mwanamvua Ngocho 
Baadhi ya waandishi wa habari wakisikiliza malezo ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Kapteni Milton Lusajo Lazaro. Picha na mpiga picha wetu.

======  ========  ======


ATCL yatangaza kuanzisha safari za ndani nyingine baada ya kurejesha huduma zake Ijumaa hii.

Na Mwandishi Wetu.

SHRIKA la Ndege la Air Tanzania (ATCL) limejipanga kurudisha safari zake Ijumaa hii na kuahidi kuongeza safari nyingine za ndani na za kimataifa kupitia mpango wa Shirika hilo madhubuti unaolenga kurudisha heshima ya shirika hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za makao makuu yashirika hilo jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa ATCL, Kapteni Milton Lusajo Lazaro alisema kuwa shirika lake limeanza kutekeleza mpango wa maendeleo utakaosaidia kuboresha utoaji huduma pamoja na upanuzi wa safari zake.

 “Tumejipanga kurejesha huduma zetu Ijumaa huku tukiwa tumepanga kuongeza safari nyingine katika mkakati wetu wa kuhakikisha kuwa tunafika maeneo mengi nchini.  Tutaanza na safari ya Dar es Salaam-Mwanza-Kilimanjaro kabla ya kuanzisha safari ya Dar es Salaam-Arusha-Zanzibar itakayozinduliwa mwezi Novemba tarehe 2, 2012.

 “Tunawashukuru wateja wetu kwa kuwa nasi katika kipindi hichi kigumu tulipo simamisha huduma zetu na tunaahidi kuwapatia huduma bora na za kipekee kipindi tutakapoanza safari,” alisema Lazaro.

Lazaro alisema kuwa shirika hilo la kitaifa pia lina mpango wa kuzindua safari ya Dar es Salaam-Mtwara itakayoanza mwezi Novemba tarehe 16, 2012 kwa kutumia ndege ya Dash 8-300 iliyokuwa katika matengenezo baada ya kuhusika kwenye ajali kipindi kifupi kilichopita na badae kurejesha safari zake za Dar-es Salaam- Hahaya(Moroni).

Hata hivyo alisema kuwa shirika lina mpango wa kununua ndege mbili kubwa zitakazotumika katika safari zake za kimataifa zinazotarajiwa kuanza mnamo mwezi Desemba au mapema mwakani na kuzitaja safari za Dubai, China na Ulaya kuwa miongoni mwa safari hizo.

 “Sisi ni shirika la ndege la taifa, tunahitaji kutunza heshima hii kwa kutoa huduma zinazokidhi matakwa ya wateja wetu. Tumeweza kukabiliana na changamoto mbalimbali na kupata suluhisho madhubuti. Kiukweli mara hii, huduma zetu ni za kudumu.

 “Changamoto kubwa sasa ni kujikita katika urejeshaji wa heshima ya shirika. Tumejipanga kununua ndege mbili mpya ili kupanua huduma zetu na wakati mwingine tutaingia ubia na mashirika makubwa ya ndege ili kuongeza safari zetu,” aliongeza.

Aidha, akizungumzia kuhusu usitishwaji wa mkataba baina ya Kampuni ya ATCL na kampuni ya Aero Vista mwezi Agosti ambayo iliwakodisha ndege aina ya Boeing 737-500, Lusajo alisema kuwa mazungumzo baina ya kampuni hizo mbili yanaendelea na kusema wanategemea kufikia makubaliano muda si mrefu.

 “Mazungumzo yanaendelea. Sitegemei kuwa tutafika pabaya. Najua tuu tufafika muaafaka,” alisema.

No comments: