Wednesday, September 5, 2012

taarifa ya mamlaka ya hali ya hewa kuhusiana na mwelekeo wa mvua za vuli



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt Agnes Kijazi (kulia) akizungumza na vyombo vya habari na wadau mbalimbali kuhusiana na utabiri wa mvua za vuli 2012,huku ikielezwa uwezekano wa kuwepo  kwa ongezeko la mvua kwa msimu huu na kutoa athari na ushauri wa matokeo ya mvua hizo zinazotarajiwa kuanza mwezi oktoba - Desemba 2012


ATHARI NA USHAURI
Maeneo mengi ya nchi yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani. Athari zitokanazo na mvua hizo katika shughuli za kijamii na kiuchumi na ushauri husika zimeainishwa kama ifuatavyo.

Kilimo na Usalama wa Chakula

Unyevunyevu wa udongo unatarajiwa kutosheleza shughuli za kilimo. Hata hivyo unyevunyevu wa udongo kupita kiasi na mafuriko hususani kwenye maeneo ya mabondeni na magonjwa ya mimea kama vile ukungu vinaweza kuathiri hali ya mazao. Aidha, mvua za juu ya wastani zinaweza kusababisha matumizi makubwa ya pembejeo na hivyo kuongeza gharama za uzalishaji. Wakulima wanashauriwa kuandaa mashamba na pembejeo mapema pamoja na matumizi sahihi ya ardhi na mbegu.

Malisho na maji kwa ajili ya mifugo na wanyama pori

Hali ya malisho na maji inatarajiwa kuwa nzuri katika maeneo mengi nchini. Hata hivyo milipuko ya magonjwa kama vile miguu na midomo (FMD) na homa ya bonde la ufa (RVF) inaweza kutokea. Wafugaji wanashauriwa kuvuna na kuhifadhi malisho kwa matumizi wakati wa kiangazi. Aidha, chanjo na uogeshaji wa mifugo wa mara kwa mara dhidi ya magonjwa na wadudu waharibifu unapaswa kuzingatiwa. 

Kuhama kwa wanyama pori na uharibifu wa miundo mbinu ndani ya hifadhi inaweza kusababisha migogoro kati ya wanyama pori na wakulima. Aidha, mvua za juu ya wastani zinaweza kuharibu miundombinu ndani ya hifadhi na mbuga za wanyama. Inashauriwa kuepuka kufanya shughuli za kilimo kwenye mapito ya wanyama pori.

Maji na Nishati

Vina vya maji katika mabwawa na mito vinatarajiwa kuongezeka kutoka kwenye viwango vilivyopo. Pamoja na matarajio ya kuwepo kwa mvua za juu ya wastani maji kwa ajili ya uzalishaji wa umeme yatumike kwa uangalifu na pia inashauriwa kuzingatia uvunaji, uhifadhi na matumizi endelevu ya maji.

Mamlaka za Miji

Mamlaka za miji zinashauriwa kusafisha mifumo ya maji taka ili kuepusha maji kutuama na kupunguza madhara yanayoweza kutokea kutokana na mvua zinazotarajiwa.

Sekta ya Afya

Kuna uwezekano wa kutokea milipuko ya magonjwa kama vile Malaria na Kipindupindu kutokana na kutuama kwa maji na kufurika kwa mifumo ya maji taka. Mamlaka husika zinashauriwa kuchukuwa hatua stahiki.

Menejimenti ya Maafa

Taasisi za maafa na wadau husika, wanashauriwa kuchukua hatua muafaka zinazojumuisha utunzaji wa mazingira na usambazaji wa madawa na maji safi na salama ikiwa ni hatua za kujiandaa na kukabiliana na majanga yanayoweza kutokea kutokana na mvua zinazotarajiwa.

Vyombo vya habari

Vyombo vya habari vinashauriwa kufuatilia, kupata na kusambaza taarifa sahihi za mienendo ya hali ya hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Aidha, jamii inashauriwa kufuatilia taarifa sahihi za utabiri wa misimu na mirejeo kama zitolewavyo na vyombo vya habari na kuzingatia ushauri unaotolewa.

Mamlaka inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.

No comments: