Tuesday, August 21, 2012

RIPOTI MAALUMU YA TUNDU LISU: MATUMIZI YA BUNGE KUDHALILISHA MAHAKAMA NA MAJAJI WAKE?


Na George Jinasa

Kwa mujibu wa ibara ya 63  ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977 (“Katiba”) Bunge linayo mamlaka ya kuisimamia na kuishauri Serikali. Mamlaka haya hutumiwa na Bunge katika vikao vyake mbalimbali kwa kujadili bajeti na taarifa mbalimbali za Wizara na inapobidi kutunga sheria zinazolenga katika kurekebisha kasoro katika mwenendo wa Serikali.
Kwa mujibu wa ibara ya 107 A, mamlaka ya kufasiri sheria na kutoa haki yako mikononi mwa Mahakama.  Hakuna hata sehemu moja katika Katiba ambapo Bunge limepewa mamlaka yoyote ya kuisimamia na kuishauri Mahakama. Nafasi ya Bunge kuirekebisha Mahakama katika mfumo wa “checks and balance”, ni kwa njia ya kutunga sheria.
 Na hilo limefanyika mara nyingi japo mara nyingine limetumika vibaya kama pale Mahakama Kuu ilivyobatilisha kifungu katika Sheria ya Uchaguzi kilichokuwa kinazuia mgombea binafsi na Bunge likajibu kwa kurekebisha Katiba na kuliingiza sharti hilo katika Katiba. Kwa kufanya hivyo, suala la mgombea binafsi lilifanywa kuwa la kikatiba badala ya sheria ya Bunge kama ilivyokuwa mwanzo.
Madhara ya uamuzi huo wa Bunge yalionekana katika rangi yake sawia katika kesi maarufu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mtikila ambapo Mahakama ya Rufaa ilijiona haina mamlaka ya kubatilisha kifungu cha mgombea binafsi katika Katiba kwa misingi kwamba Katiba ipo juu ya Mahakama. Kuna maswali mengi ya kifalsafa yanayozuka kutokana na kesi hiyo bali kwa minajili ya makala yangu hii nisingependa kujielekeza kwayo.
Katika nchi zinazooongozwa na utawala wa sheria kama Tanzania, mamlaka ya kusikiliza tuhuma dhidi ya watu na kutolea maamuzi ni ya Mahakama. Bunge halina mamlaka hayo isipokuwa tu katika maeneo machache ya kiutawala ambapo mamlaka ya Mahakama yamekasimiwa kwa njia ya Sheria.
Ni mhimu pia kugusia kwamba kwa mujibu wa ibara ya 13 (6) (a) ya Katiba, maamuzi yoyote yanayoathiri haki au wajibu wa  mtu hayawezi kufanyika bila ya yeye kusikilizwa.
Hvi karibuni imekuwa kawaida kusikia masuala mbalimbali yanayowahusu watu binafsi yakijadiliwa Bungeni na hatimaye wahusika kudhalilika na kuhukumika na ile hali hamna utaratibu wowowte wa kisheria unaowaruhusu wao kwenda Bungeni na kukanusha tuhuma dhidi yao kwa ushahidi. Ipo mifano mingi ya kuthibitisha kauli yangu lakini kwa minajili ya andiko hili ninapenda kujikita kwenye taarifa iliyoripotiwa na gazeti la Jamhuri la toleo ya August 14-20 yenye kichwa cha nabari “Majaji ‘vihiyo’ watajwa”.
 Ndani ya taarifa hiyo iliyorejewa kama “Ripoti Maalumu” pamoja na mambo mengine, majina ya baadhi ya majaji yalitajwa na kuhusishwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za rushwa, upendeleo, kutokuwa na sifa ya ujaji na ukiukwaji wa sheria. Taarifa hizo, mwandishi anasema, amezinukuu neno kwa neno  kutoka katika utetezi wa mheshimiwa Tundu Lisu (Mbunge) aliouwasilisha katika Tume ya Maadili ya Bunge.
Suala la kujiuliza kwanza ni kama Kamati ya Maadili ya Bunge inauwezo wa kuamua kama tuhuma hizo zimethibitika au la?  Kama nilivyoeleza hapo mwanzo jibu ni hapana. Bunge, achilia mbali kamati zake, halina mamlaka yoyote ya kikatiba ya kuichunguza Mahakama wala majaji wa Mahakama Kuu.  Tume ya Maadili ya Bunge ni chombo nusu mahakama (Quasi-Judicial Board) kilichokasimiwa mamlaka ya kimahakama ya kusikiliza mashauri ya kinidhamu yanayowahusu wabunge. Hakina mamlaka yoyote ya kuthibitisha tuhuma dhidi ya majai wa mahakama kuu au maofisa wowowte wa mahakama.
Tuhuma hizo nzito dhidi ya majaji wa Mahakama Kuu japo inadaiwa kwamba zimepelekwa katika Kamati ya Madili ya Bunge kama utetezi wa Mbunge, zimeshasambazwa kwa umma hata kabla hazijajadiliwa na Kamati hiyo. Kwa kufanya hivyo ni wazi kwamba majaji waliotajwa pamoja na idara nzima ya Mahakama wamehukumiwa hata kabla tuhuma hizo hazijathibitika. Ni wazi kabisa kwamba imani ya watu katika chombo hiki mhimu cha kutoa haki itashuka.
 Ni mhimu kusema hapa kwamba tuhuma alizotakiwa kuthibitisha katika Kamati ya Maadili ya Bunge ni juu ya uwepo wa majaji wanaoteuliwa na Raisi bila kupitia  Tume ya Utumishi wa Mahakama. Badala ya kujikita katika kuthibitisha madai hayo mheshimiwa Tundu Lisu aliamua kutoa tuhuma nzito mpya dhidi ya baadhi ya majaji wa Mahakama Kuu.
TUHUMA ZENYEWE
1.  MAJAJI KUONGEZEWA MKATABA WA AJIRA KINYUME CHA KATIBA
Madai ya mheshimiwa Tundu Lisu katika nukta tajwa hapo juu ni kwamba majaji wanaoongezewa muda wao baada ya kufikia muda wa kustaafu kwa lazima (yaani miaka 60 kwa Mahakama Kuu na 65 kwa Mahakama ya Rufaa) si majaji kwa mujibu wa ibara 110 na 120 ya Katiba maana jaji anapostaafu kiapo cha ujaji kinaisha na kuufanya ujaji wa mkataba kuwa nje ya kiapo. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hoja ya mh. Tundu Lisu katika nukata hii pia inaungwa mkono na tamko lililowahi kutolewa na mh. Jaji Luanda (kabla hawaja Jaji wa Mahakama ya Rufaa) na mheshimiwa Jaji Mkuu Staafu Ramadhani (kabla hajawa Jaji Mkuu).
Ibara ya 110 (3) ya Katiba inasema kwamba “Iwapo Raisi ataona kuwa kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji alietimiza umri wa miaka sitini aendelee kufanya kazi, na huyo Jaji mwenyewe anakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi, basi Raisi aweza kuagiza kuwa Jaji huyo aendelee kufanya kazi kwa muda wowowte atakaotaja Raisi”. Kifungu cha 120 (3) kina maneno kama hayo kuhusiana na Majaji wa Mahakama ya Rufaa ila tu muda wao wa kustaafu kwa lazima ni miaka sitini na tano.
Maneno yaliyomo katika ibara hizo mbili kama yalivyo, yanaruhusu Jaji aliyefikia miaka 60 kuendelea kuwa jaji kwa kipindi Raisi atakachoongeza ili mradi tu iwe ni kwa maslahi ya umma na jaji mhusika aridhie. Kwa maoni yangu, sioni tatizo lolote kwa jaji kuongezewa muda wa ujaji baada ya kufikia muda wa kustaafu ili mradi masharti ya ibara ya 110 (3) na 120 (3) ya Katiba yanazingatiwa. Ibara za 110 (3) na 120 (3) hakijaweka ukomo wa muda ambao Raisi anaweza kumuongezea Jaji aliyestaafu na wala havijaweka tafsiri ya neno “ maslahi ya umma”. Hiyo inamaana kwamba suala la kuamua kama kuna maslahi ya umma au la katika kuongeza muda lipo katika “discretion) ya Raisi.
Maoni ya mh Tundu Lisu na watu wengine wanayomuunga mkono katika suala hili ni maoni ya kifalsafa zaidi ambapo wasomi wa fani ya sheria wanaweza kuwa na maono tofauti. Na wala maoni ya jaji mkuu mstaafu na jaji wa mahakama ya Rufaa hayakutolewa kama sehemu ya uamuzi, bali ni maoni kama maoni ya raia yeyote. Ndio maana mheshimiwa Ramadhani anakiri uwezekano wa hoja zake kuathiriwa na chimbuko lake la kijeshi. Lakini Katiba kama ilivyo inahalalisha nyongeza ya muda wa ujaji kwa maslahi ya umma kwa kadili Raisi anavyoona inafaa. Maamuzi ya kuongeza muda, kwa kadili nijuavyo, hufanywa kabla muda wa kustaafu haujafika. Na hivyo Jaji anapoongezewa muda wa ujaji anakuwa bado ndani ya kiapo kile kile. 
Isitoshe, ya Jaji Ramadhani na wenzake, kama yalivyonukuliwa katika gazei la Jamhuri  la tarehe la Augus 21-27/2012, kwenye makala yenye kichwa cha habari “RIPOTI MAALUMU MAJAJI MAJI SHINGONI”, hayapingi jaji kuongezewa muda baada ya kufikia umri wa kustaafu, bali yanapinga kuwepo ajira ya mkataba baada ya jaji kustaafu kwa misingi kwamba ajira ya Mkataba inamuondolea jaji kinga ya ajira “security of tenure” na kuiweka ajira yake chini ya sheria za kawaida za Mkataba. Ni hoja yao pia kwamba  ajira hiyo inahesabika kama ajira mpya maana jaji anakuwa ameshapewa marupurupu yake baada ya kustaafu. Kwa maneno yake mwenyewe, mheshimiwa Jaji Mstaafu Ramadhani amenukuliwa na aliejiita  “mwandishi wetu”  katika ukulasa wa 3 wa gazei la Jamhuri akisema kama ifuatavyo:-
‘ Tafsiri yangu hapa ni kuwa, Raisi anasema Jaji “XYZ” badala ya kustaafu akitimiza umri wa miaka 65 na kuongezea miaka ABC uendelee kufanya kazi na utastaafu umri wa miaka OPQ. Hii haina maana kuwa jaji wa Rufaa anaehusika atastafu baada ya kutimiza miaka 65 na kupata marupurupu yake halafu aajiriwe kwa Mkataba. Tafsiri yangu kuwa aendelee na kazi mfululizo na aje kustaafu baada ya kicho kipindi cha ziada alichopewa. Akistaafu na kupata haki yake haendelei na kazi bali anaanza ajira mpya ya mkataba.”
Kutokana na taarifa kutoka katika vyanzo vya kuamika, majaji wanaoendelea kufanya kazi baada ya muda wa kustaafu, huongezewa muda na Raisi kabla ya muda wa kustaafu na sio kusaini Mkataba baada ya kustaafu. Kwa mfano, muda wa nyongeza wa mheshimiwa Jaji Kiongozi unaolalamikiwa, ulitolewa kwa barua ya tarehe 13.06.2012 yenye kumbu kumbu namba SAB289/482/01/120 wakati muda wake wa kustaafu ulikuwa uwe tarehe 20/07/2012, takribani mwezi mmoja kabla hajapewa barua ya kuongezewa muda. Hamna Mkataba wowote aliousaaini wala Ripoti ya mheshimiwa Tundu Lisu haijaonyesha mkatba huo.
Ni mhimu pia kusisitiza kwamba hata Ripoti ya “Kikundi Kazi” kama ilivyonukuliwa na gazeti tajwa hapo juu, hamna sehemu yoyote ambapo nyongeza ya muda wa ujaji imepingwa. Kinachopingwa katika Ripoti hiyo ni uwepo wa ajira ya mkataba kwa jaji baada ya kustaafu. Inashangaza hata hivyo kuona kuwa japo katika Ripoti hiyo inadaiwa kwamba mheshimiwa Jaji Lyimo baada ya kustaafu aliingia ajira ya Mkataba, kielelezo kilichoambatanishwa sio Mkataba bali ni barua ya nyongeza ya muda wa ajira kitu ambacho kwa mujibu wa Jaji Ramadhani na Ripoti ya Kikundi Kazi, hakina matatizo ya kisheria.
Katika hali ya kushangaza kidogo, suala la kuongezewa muda wa ujaji linahusishwa na malalamiko ya wale wanaojiita “wanamhimili wa Mahakama” kwamba Jaji Kiongozi ameshindwa kumudu mamlaka yake kwa kutishia kumhamisha hakimu mmoja alietoa maamuzi ambayo hakuridhika nayo. Katika Ripoti hiyo hiyo, uamuzi wa Jaji Kiongozi kumhamisha hakimu kwa maamuzi asiokubaliana nayo unakubaliwa na kutumika kumhukumu wakili aliehusika katika kesi hiyo kuwa amekiuka maadili na hakustahili kuwa Jaji.
 Katika Ripoti yake mheshimiwa Tundu Lisu hakutoa uthibitisho wowote kwamba kuhamishwa kwa hakimu huyo ilikuwa ni adhabu. Nijuavyo mimi, uhamisho kwa mahakimu na majaji ni utaratibu wa kawaida wa kazi na wala hamna hakimu yoyote mwenye hati miliki ya kuwa Dar es Salaam. Wala mahakimu walioko mikoani hawako huko kwa sababu ya adhabu na walipo Dar es Salaam hawako Dar es Salaam kwa sababu ni weledi zaidi ya walio mikoani.
Ripoti yake inaonesha kwamba maamuzi ambayo Jaji kiongozi hakukubaliana nayo, yanahusu kesi aliyoiita maarufu ya “kibaghalashia”. Kumbukumbu zangu zinaonesha kwamba kesi hiyo iliwahi kuripotiwa kwa mshangao katika magazei kadhaa. Kwamba hakimu mmoja amemhukumu mtu kwenda jela kwa kuvaa kibaghalashia Mahakamani.
Kwa nchi kama Tanzania ambako vazi la kibaghalashia ni vazi rasmi katika baadhi ya dini,  haikutegemewa kwa hakimu huru na mwenye busara kumfunga mtu kwa kuvaa kibaghalashia Mahakamani. Kwa namna suala hilo lilivyovuta hisia za watu wengi hapa nchini na mbaya zaidi hisia za kidini, nisingeshangaa hata kidogo kama hakimu huyo angechukuliwa hatua yoyote ya kinidhamu achilia mbali kuhamishwa. Mahaka kama chombo cha kutoa haki kinapaswa kujiweka katika hali ambayo kila mtu atakiona kama chombo huru kisichokuwa na muegemeo wowowote wa kisiasa, kidini au kikabila. Maamuzi mabovu kama hayo hayakupaswa kutolewa na chombo cha Mahakama.
2.   MAJAJI KUTOKUWA NA MAADILI
Katika nukta tajwa hapa juu, Tundu Lisu ametoa mfano wa majaji wanne ambao nitawazungumzia bila kutaja majina yao.
Jaji mmoja analaumiwa kwa sababu kampuni ya uwakili aliokuwa akifanyia kazi kabla hajakuwa Jaji ilikuwa ni mawakili wa kampuni inayotuhumiwa kujihusisha na ufisadi. Tuhuma hizi zinashangaza sana maana katika maadili ya kazi za uwakili wakili hazuiwi kumtetea mtu anaetuhumiwa kuwa mhalifu.
Na kwa mujibu wa sheria za nchi, mtuhumiwa yoyote wa makosa makubwa kama mauaji na uhaini hata kama hana uwezo, ana haki ya kutetewa. Kwa hilo serikali hutenga mamilioni ya pesa kuwalipa mawakili kwaajili ya kutetea watuhumiwa wa mauwaji. Kama hoja za mh. Tundu Lisu itakuwa sawa, ina maana kwamba mawakili wote waliowahi kuwatetea wauwaji na mwishowe wakaonekana na hatia, hawatakuwa na sifa ya kuwa majaji. Haki ya kupata uwakilishi wa kisheria anaizungumziaje mheshimiwa Tundu Lisu? Ina maana watu wenye hatia hawana haki ya kutetewa na kupata huduma za kisheria? Nijuavyo mimi hata mhalifu anahaki ya kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria na kazi ya wakili inaweza kuwa kuhakikisha mhalifu haonewi kwa kupewa adhabu kubwa zaidi ya anayostahili kwa mujibu wa sheria. 
Nilitegemea kuona katika Ripiti ya mh. Tundu Lisu sehemu yoyote inayoonesha namna mheshimiwa huyo alivyohusika yeye mwenyewe binafsi na tuhuma hizo wakati bado anafanya kazi ya uwakili katika kampuni husika. Au japokuwa angeonyesha namna kampuni yake ya zamani ya uwakili ilivyohusika na uhalifu na kama mheshimiwa pia alikuwa na habari kuhusiana na uhalifu huo. Vinginenvyo sioni kama mheshimiwa Tundu Lisu alikuwa na uhalali wowote wa kuliingiza jina la wakili huyo katika utetezi wake.
Jaji mwingine ametuhumiwa kwa kupinga amri ya mahakama kwa njia ya mapitio (Review). Kama anavyoeleza kwenye Ripoti yake, Jaji husika enzi zile alipokuwa bado wakili aliwahi kutoridhishwa na uamuzi wa mahakama na kuupinga kwa njia ya mapitio na hatimaye mahakama ikabatilisha uamuzi wake wa kumfunga mshitakiwa bila faini na badala yake kuamua kwamba atumikie kifungo au atoe faini. Mh. Tundu Lisu hasemi kama kifungu cha sheria kilichotumika kumhuku mshitakiwa hakikuwa na “options” hizo.
Sasa sioni kwa nini suala hili limechukuwa sura ya kimaadili badala ya taratibu za kawaida za kutetea wateja. Kama suala ni kukosea kiutaratibu katika kupinga uamuzi huo, hayo ni masuala ya kawaida maana jaji au wakili si Mungu ajue kila kitu. Ndio maana mara nyingi hukumu za majaji wa Mahakama Kuu huwa zinapingwa Mahakama ya Rufaa kwa kujenga hoja kwamba Jaji mhusika alikosea ima kisheria au kimantiki. Hujawahi kusikia jaji yoyote anahukumiwa kutokuwa na maadili au kutokuwa na uwezo  kwa sababu maamuzi yake yalitenguliwa na mahakama ya juu kwa sababu ya kuwa na makosa. Maamuzi ya Mahakama Kuu baada ya kulifanyia marejeo jalada hilo hayaoneshi hata kidogo kama jaji anaetuhumiwa alifanya jambo lolote la kukiuka maadili ya uwakili. Zaidi ya hapo, kumbukumbu katika jalada zinaonesha kwamba hata mtu aliewasilisha hoja za mapititio mbele ya mheshimiwa hakimu wa wilaya alikuwa ni wakili mwingine aliebeba mikoba ya jaji anaetuhumiwa.
Jaji mwingine ametuhumiwa kuwahi kuhusika katika kumwandikia hakimu hukumu enzi za uwakili wake. Hamna ushahidi wowote uliotolewa kuthibitisha tuhuma hizo na wala Jaji katika hukumu husika hakumuona Jaji huyo kuwa na hatia yoyote. Ni vizuri pia kuzingatia hapa kwamba sifa maalumu za jaji kwa mujibu wa ibara ya 109 (8) ya Katiba ni sifa zilizotajwa katika Sheria ya Mawakili. Kwa mana hiyo kama tuhuma dhidi ya Jaji huyo zingesimama, angeondolewa uwakili kabla hajawa Jaji. Ni jambo la mhimu kuzingatia hapa kwamba kutuhumiwa kosa sio kutenda kosa.
 Kwa kulilinda hilo, Katiba katika ibara ya 13 inaweka dhana ya mtu kutokuwa na hatia hadi Mahakama imithibitishe kuwa hivyo. Ndio maana hamna mtu anaeweza kusema kwa sasa kwamba Tundu Lisu ni mtovu wa nidhamu ya ubunge mpaka Kamati ya Maadili ya Bunge itakapomuona ana hatia. Ni maneno hayo hayo naweza kusema kuhusiana na Majaji waliotuhumiwa kutokuwa na sifa kwa sababu waliwahi kuundiwa tume ya kuchunguza ukiukwaji wa maadili. Utetezi wa Tundu Lisu unaonesha kwamba walishinda katika tuhuma zao na kuonekana hawana hatia. Katika kazi ya ujaji na uhakimu ni mara ngapi watu wanaopoteza kesi kuwazushia majaji tuhuma ili mradi wafanikiwe katika kesi zao? Mara ngapi majaji wanaombwa kujitoa katika kesi kwa sababu ya migogoro ya kimaslahi na wkati tuhuma hizo ni za kisanii tu.
3.  JAJI  KUAJIRIWA BILA KUWA NA SIFA KITAALUMA
Jaji anaelalamikiwa kuhusina na tuhuma tajwa hapo juu inadaiwa kwamba kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Mh Tundu Lisu anakiri kwamba sifa za kitaaluma za mtu kuwa Jaji Tanzania Zanzibar ni sawa na za Tanzania bara. Ibara ya 118 (3) ya Katiba inabainisha wazi kwamba Raisi kwa kushirikiana na Jaji Mkuu anaweza kumteuwa mtu kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa yule ambaye anasifa ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania au Mahakama Kuu ya Zanzibar. Jaji mhusika wakati anateuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa alishakuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar. Mh. Raisi na Jaji Mkuu hawakuwa na sababu yoyote ya maana kutilia shaka uteuzi wake kuwa  Jaji wa Mahakama Kuu ya Zanzibar.
4.  MAJAJI WA MITAANI
Katika utetezi wake mheshimiwa Tundu Lisu ametaja baadi ya majaji kuwa waliajiriwa bila majina yao kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama kwaajili ya uchunguzi. Bahati mbaya chanzo cha taarifa hiyo hakijaonyeshwa. Uchunguzi wangu nilioufanya unaonyesha kwamba majaji wote wane wanaotuhumiwa sio majaji wa mitaani na uteuzi wao ulipata Baraka za Tume ya Utumishi wa Mahakama. Wakati kwa mara ya kwanza tuhuma hiyo inatolewa, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Tume hiyo alikanusha.  Wajumbe wengine katika Tume hiyo ni pamoja na Jaji Mkuu na Jaji Kiongozi ambao kwa namna yoyote wasingekubali mtu ateuliwe Jaji bila kupitia katika Tume yao. Hatuoni ni kwanini mhesimiwa Tundu Lisu kabla hajatoa tuhuma nzito kama hizo hakuona umhimu wa kuonana na makamishina wa Tume hiyo na kupata taarifa sahihi.
Kumbu kumbu zinaonesha kwamba mmoja kati ya majaji wanaotuhimiwa kuwa wa mitaani, kabla ya kuteuliwa kuwa jaji alikuwa ni Mkurugenzi Msaadizi katika ofisi za Mkurugenzi wa Mashitaka Tanzania. Alipohitimi shahada ya sheria ajira yake ya kwanza ilikuwa ni mwanasheria wa serikali na alipanda kidogo kidogo hadi akafikia cheo cha mkurugenzi msaidizi katika ofisi nyeti katika masuala ya sheria ya DPP. Ni jambo la mzaha mtu kama huyo kuitwa “jaji wa mitaani”
Jaji wa pili anaetuhumiwa alianza kazi kama mwanasheria wa serikali mwaka 1993 baada ya kuhitimu shahada ya sheria. Mpaka anateuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu alikuwa ni Mkurugenzi wa Utekelezaji wa Sera wa Utumishi. Pamoja na kazi kubwa alizozifanya kulitumikia taifa katika nafasi mbalimbali anaishia kuitwa jaji wa mitaani.
Jaji wa tatu anaetuhuumiwa kwa hili alianza kazi katika Idara ya Mahakama mwaka 1974 kama Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo. Mda mchache kabla hajateuliwa kuwa Jaji alishapanda hadi kufikia ngazi ya Ukurugenzi wa Mahakama za Mwanzo Tanzania, nafasi  aliteuliwa na mheshimiwa Jaji Mkuu wa wakati huo Samata baada ya kuridhika na uadilifu wake na uwezo wake wa kazi. Mtu kama huyu kuna uhalali gani wa kumwita jaji wa mitaani
Wa mwisho katika tuhuma hii mpaka anateuliwa kuwa jaji wa Mahakama Kuu mwaka 2009 alikuwa Mkurugenzi wa Mahakama za Wilaya mpaka Mahakama ya Rufaa Tanzania. Na katika maisha yake yote ya ajira za umma amekuwa akifanya kazi kwa uaminifu mkubwa katika Idara ya Mahakama. Ni bahati mbaya sana wanasiasa wameamua kumpa jina la jaji wa mitaani.

5.  TUEPUKE  KUELEKEZA SIASA KATIKA IDARA YA MAHAKAMA
Moyo wa nchi yoyote inayotawaliwa na utawala wa sheria ni mahakama. Mahakama ni kimbilio la wote na ni mlinzi na mtoaji mkuu wa haki. Hili linafanikiwa pale mahakama inapoheshimiwa na kuaminiwa kama  chombo huru kisichofungamana na makundi yoyote ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni.
Kwa kuzingatia umhimu wa hilo, Katiba imekataza bayana kwa maofisa wa mahakama kuwa na uhusiano na vyama vya kisiasa. Kiapo cha ujaji na uhakimu kinawataka majaji katika kufamya kazi zao kuwa huru na kutoa maamuzi bila kuathiriwa na upendeleo wa aina yoyote. Zaidi ya hilo, Katiba imeweka ibara zinazolinda uhuru wa Mahakama na kuondoa uwezekano wowote wa kuingiliwa na vyombo vyenye nguvu sana kama serikali na Bunge. Hata pesa zinazotumika kulipa mishahara ya majaji na mahakimu hazipaswi kuwa pesa za bajeti ya kawaida zinazojadiliwa na kupitishwa na Bunge. Dhamira ya sheria hapa ni kuzuia uwezekano wa Bunge kuingilia uhuru wa Mahakama kwa sababu wana uwezo wa kuamua juu ya mishahara na marupurupu ya majaji.
Pamoja na uhuru mkubwa mahakama iliyopewa kwaajili ya kufanya maamuzi yake yawe ya haki, Mahakama haijawekwa kuwa juu ya sheria. Maamuzi yao yanapaswa kuwa kwa mujibu wa sheria na pale jaji anapokosea kuna utaratibu maalumu wa kumrekebisha na hata kumvua kofia ya ujaji. Kama jaji anaonekana kuteuliwa kinyume cha sheria, Katiba na sheria mbalimbali za nchi zimeweka utaratibu ambao kwao maamuzi ya uteuzi wa jaji yanaweza kubatilishwa. Hamna uhalali wowote kwa wanasiasa kutumia Bunge na vyombo vya habari kuichafua Mahakama na maofisa wa Mahakama. 
Ni vizuri watanzania tukajihadhari na kuiingiza siasa katika Mahakama. Tuache mahakama ziendelee kuwa huru maana ni kimbilio letu sote. Kama kuna mapungufu katika Idara ya Mahakama (na of course hayawezi kukosekana) tutumie taratibu zinazokubalika kisheria kuyarekebisha.

1 comment:

Anonymous said...

Utetezi huu ni dhaifu na hauna mashiko. Kwanini mleta mada asiache majaji wenyewe wakasimama na kujitetea badala ya kutumika kama a gun for hire kwa ajili yao. Jinasa ni nani hadi atupe tumbo moto wakati anatetea kitumbua cha mabwana zake? Kitu au ushauri wa maana kwa Jinasa kabla hajanasa kisheria ni kuwashauri watu wake waende mahakamani kama wameona wamehujumiwa. Waje na ushahidi wa kupinga tuhuma zilizotolewa na mheshimiwa Lissu.