HOTUBA YA WAZIRI WA FEDHA
MHE. DKT. WILLIAM AUGUSTAO MGIMWA (MB)
AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA KWA MWAKA 2012/13
Dodoma
15 Agosti, 2012
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea, kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato, Matumizi ya Kawaida na ya Maendeleo ya Wizara ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2012/13.
2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwako pamoja na Naibu Spika Mheshimiwa Job Yustino Ndugai, Mbunge wa Kongwa, Waheshimiwa Wenyeviti Jenista Joakim Mhagama (Mbunge wa Peramiho), Sylivester Massele Mabumba (Mbunge wa Dole) na Mussa Azzan Zungu (Mbunge wa Ilala), kwa kuongoza vema majadiliano ya Bunge la Bajeti.
3. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuishukuru kwa namna ya pekee Kamati ya Fedha na Uchumi chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Mtemi Andrew John Chenge, Mbunge wa Jimbo la Bariadi Mashariki kwa maoni, ushauri na mapendekezo waliyoyatoa kwa Wizara wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara ya Fedha. Wizara imezingatia ushauri na mapendekezo ya Kamati katika kukamilisha uandaaji wa hotuba hii.
4. Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Janet Z. Mbene (Mb), na Mheshimiwa Saada M. Salum (Mb) pamoja na Katibu Mkuu Ndugu Ramadhan M. Khijjah na Manaibu wake Ndugu Laston T. Msongole, Dkt. Servacius B. Likwelile na Ndugu Elizabeth J. Nyambibo kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Wizara. Aidha, nawashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo, Wakuu wa Taasisi na Wakala wa Serikali, chini ya Wizara na wafanyakazi wote wa Wizara ya Fedha kwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi .
5. Mheshimiwa Spika, naomba sasa, uniruhusu nisome maelezo haya kwa muhtasari na hotuba nzima iingie kwenye Hansard.
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2011/12
6. Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza majukumu yake kupitia mafungu manne ya kibajeti. Mafungu hayo ni Fungu 50 - Wizara ya Fedha; Fungu 21 – HAZINA; Fungu 22 - Deni la Taifa; Fungu 23 - Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na - Fungu 45 Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.
7. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/12, Wizara kwa kuzingatia jukumu lake la msingi la kukusanya mapato na kusimamia matumizi ya fedha za umma, ilijikita katika kutekeleza yafuatayo:
i. Kubuni na kusimamia utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla;
ii. Kusimamia na kuratibu shughuli za Taasisi na mashirika ya umma;
iii. Kukusanya mapato ya ndani yasiyopungua shilingi bilioni 6,435.28. Kati ya hizo shilingi bilioni 6,228.80 ni mapato ya kodi na shilingi bilioni 206.48 ni mapato yasiyo ya kodi;
iv. Kujenga uwezo wa uandaaji na usimamizi wa Bajeti ya Muda wa Kati pamoja na utoaji wa taarifa za utekelezaji kwa wakati;
v. Kuendelea na ukaguzi wa ndani na kuimarisha Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali;
vi. Kusimamia utekelezaji wa bajeti ya serikali na uratibu wa utekelezaji wa MKUKUTA;
vii. Kusimamia deni la taifa;
viii. Kusimamia na kuhakiki malipo ya mishahara ya watumishi wa Serikali na Taasisi zake;
ix. Kuendeleza kada za Uhasibu, Ukaguzi wa Ndani, Ununuzi na Ugavi, Uchumi, Uhakiki Mali, Mipango, Usimamizi wa Fedha, Watakwimu na Wataalamu wa Kompyuta;
x. Kuendelea kuhuisha Daftari la Mali ya Serikali;
xi. Kuendelea na ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kusimamia utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Millennium Challenge Corporation (MCC);
xii. Kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za mafao ya wastaafu na mirathi;
xiii. Kuimarisha Mtandao wa Malipo - IFMS katika ngazi zote za Serikali, na kusambaza matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia ya elektroniki katika HAZINA ndogo na Sekretarieti za Mikoa;
xiv. Kutoa mafunzo ya kuandaa hesabu za serikali katika viwango vya kimataifa;
xv. Kuhamasisha ushiriki wa Sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya ubia; na
xvi. Kutoa mikopo kwa asasi ndogo za fedha kupitia Mradi wa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (Small Enterprise Loans Facility Project - SELF) na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa madeni ya mikopo hiyo.
UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU KWA MWAKA 2011/12 NA MALENGO YA MWAKA 2012/13