Wednesday, August 15, 2012

HOTUBA YA WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI

HOTUBA YA WAZIRI KIVULI NA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA
UPINZANI WIZARA YA FEDHA NA UCHUMI NDUGU KABWE ZUBERI ZITTO
KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA
MWAKA WA FEDHA 2012/2013
1.0 UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kanuni ya 99(7),toleo la mwaka 2007 na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,napenda kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani
kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mafungu ya Wizara ya fedha – Fungu 50 Wizara ya Fedha, Fungu 21 Hazina, Fungu 22 Deni la Taifa na Fungu 23 Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali. Vile vile Fungu 10 Tume ya Pamoja ya Fedha na Fungu 13 Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu na Ufadhili wa Ugaidi.

Mheshimiwa Spika, mafungu yote yaliyo chini ya Wizara ya Fedha yanaomba kuidhinishiwa na Bunge lako tukufu jumla ya shilingi Bilioni 4,208 (trilioni 4.2) ili yaweze kutekeleza majukumu yake. Mafungu haya maombi yake ya Fedha ni sawa na asilimia 28 ya Bajeti nzima ya Serikali ya mwaka wa Fedha 2012/13.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ndiyo msimamizi mkuu wa Uchumi wa nchi ikitekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo,kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani na ya nje, kusimamia
matumizi ya Serikali, kusimamia utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia manunuzi ya Serikali na Taasisi na Mashirika ya Umma, kusimamia Deni la Taifa na dhamana za Serikali, kutafuta
suluhisho na kusimamia mfumo wa kodi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na kupambana na Fedha haramu. Sambamba na hayo ni kusimamia na kutekeleza mpango wa kupunguza umasikini nchini kupitia utekelezaji wa MKUKUTA II.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha na mafungu yote yaliyo chini yake ndio moyo wa Serikali na hivyo ni lazima kuitazama Wizara hii kwa jicho kali na kutilia mashaka kila jambo ambalo inalifanya ili kuhakikisha kuwa moyo huu hausimami maana madhara yake ni kwa taifa zima na watu wake. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kupitia Waziri Kivuli wa Fedha inatekeleza wajibu huu kwa Uzalendo,Uadilifu na kwa misingi ya Uwajibikaji. Tumetekeleza wajibu huu na tunaendelea kuutekeleza bila kujali maneno na kuweka maslahi ya Taifa letu mbele ya kila kitu kingine. Maslahi ya Taifa ni zaidi ya vyama vya siasa, mahala tunapotoka au dini tunazoamini. 

Maslahi ya Taifa ni kwa ajili ya Watazania na hasa Watanzania milioni 30 (The Bottom 30M) ambao bado wanaishi katika ufukara mkubwa sana wakikosa huduma muhimu za jamii na wanaoishi vijijini ambapo hakuna umeme, barabara hazipitiki na wanahangaika kutwa kutafuta maji safi na salama. Maslahi ya Taifa sio faida ya wachache wenye kuishi mijini au wanasiasa wanaotafuta ushawishi
kwa umma bila kujali matakwa ya Umma. Watanzania wanyonge wa vijijini wanajua maslahi yao ni nini. Wanajua kina nani wanapigania maslahi ya Wanyonge.

2.0 MAPATO YA SERIKALI
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa Uchumi ya mwezi Julai (Monthly Economic Review, July 2012) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania, katika kipindi cha mwezi Juni
Serikali iliweza kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 998.0. Hata hivyo matumizi halisi yalikuwa kiasi cha shilingi bilioni 1,911.8 hali iliyopelekea kuwepo kwa nakisi baada ya kuondoa msaada wa masharti wa masharti wa shilingi bilioni 400.2; nakisi hiyo ililipwa kwa vyanzo vya ndani na nje.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo ilionyesha kuwa mapato yote ukiondoa fedha zilizokusanywa na Serikali za mitaa kwa mwezi Juni,yalikuwa kiasi cha shilingi bilioni 887.5 ambacho ni zaidi ya asilimia 38.1 ya malengo yaliyokuwa yamewekwa kukusanywa mwezi huo.

Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 753.3, kiasi ambacho ni zaidi ya asilimia 22.3 ya malengo ya makusanyo kilichokuwa kimewekwa na mamlaka hiyo.

Makusanyo haya ni makubwa zaidi kukusanywa na TRA kwa mwezi mmoja tangu Mamlaka hiyo ianzishwe.

Mheshimiwa Spika, katika makusanyo hayo ya mwezi Juni Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikuwa imejiwekea lengo la kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 242.4 kama kodi ya Mapato, lakini ilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 366.0 kiasi ambacho ni zaidi kwa asilimia 60.8 ya malengo yaliyokuwa yamewekwa.

Kambi ya Upinzani inapenda kulikumbusha Bunge na Taifa kwamba katika Bajeti Mbadala iliyowasilishwa hapa Bungeni tulisema kwamba TRA wanao uwezo wa kukusanya mpaka shilingi trillion moja kwa Mwezi iwapo tutadhibiti misamaha ya kodi, tutakusanya kodi stahili katika Sekta ya Madini na tutasimama kidete kuzuia ukwepaji kodi wa Makampuni ya Kimataifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inaitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania kuimarisha zaidi marekebisho yanayofanyika katika mfumo wa kodi ili kufikia lengo tajwa la kufikia makusanyo ya zaidi ya asilimia 20 ya Pato la Taifa. Mabadiliko kadhaa tunayoyafanya kwenye Sheria ya Fedha itakayosomwa hapa Bungeni katika mkutano huu wa Bunge yana lengo hilo la kupanua wigo wa kodi
na hivyo kulifanya Taifa lijitegemee.

2.1 Mauzo ya Nje
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha kupitia Benki Kuu ya Tanzania inapaswa kuhakikisha kuwa Akiba ya Fedha za Kigeni nchini inakuwa imara muda wote. Biashara ya nje ndio inaingiza Fedha za
kigeni nchini kwa hiyo ni eneo la kutazama kwa makini na kuchukua hatua mwafaka. 

Taarifa ya mwenendo wa uchumi kwa mwezi Julai iliyotolewa na Benki kuu inaonyesha kuwa jumla ya mauzo ya Tanzania nje yalikuwa dola za kimarekani 7,990.0 milioni ukilinganisha na kiasi cha dola 7,050.7 milioni kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2011 na hali hii ilisababishwa kwa kiasi kikubwa

kutokana na kuongezeka kwa bei ya mauzo ya dhahabu. Hata hivyo Manunuzi yetu kutoka nje yamefikia dola za Kimarekani 12,959 milioni.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo inaonyesha kuwa mauzo ya dhahabu Nje kwa mwaka 2011 yalikuwa kiasi cha dola 2,330.7 milioni sawa na aslimia 56.7% ya mauzo yote nje, wakati mauzo ya nje kutokana na bidhaa zilizozalishwa viwandani yalikuwa na jumla ya dola 922.0 milioni sawa na asilimia 22.4% ya mauzo yote ya nje.

Aidha mauzo ya mazao mbalimbali kama Pamba, Katani, Korosho,Chai, Kahawa na mengineyo yalikuwa na thamani ya dola 761.1 milioni kwa kipindi hicho cha mwaka 2012.

Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo imeendelea kuonyesha kuwa tuliagiza bidhaa kutoka nje zenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 12,958.7. Katika manunuzi hayo tuliyofanya mafuta peke
yake yalikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 3,586.1 ambalo ni ongezeko la asilimia 60.08% ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2011.

Mheshimiwa Spika, takwimu hizi zinaonyesha kwamba fedha zote za kigeni zilizotokana na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani na Korosho zilitumika kuagiza mafuta pekee yake! Hali hii ni mbaya
sana kwa uchumi wa Taifa letu na juhudi zote za kuongeza mauzo nje zinaliwa na uagizaji wa Mafuta ambao umepanda sana katika siku za hivi karibuni.

Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kuwa kuanzia mwaka jana Serikali imekuwa ikitekeleza mpango wa Umeme wa dharura ambao umepelekea matumizi makubwa ya Mafuta. Hata hivyo ieleweke kuwa Mpango mzima wa Manunuzi ya Mafuta ya kuendesha mitambo ya Umeme inaligharimu Taifa Fedha nyingi sana. Takwimu zinaonyesha kuwa Serikali inapaswa kutumia zaidi ya shilingi 42 bilioni kila Mwezi kuendesha mitambo ya dharura ya Umeme. Manunuzi yenyewe ya Mafuta yamejaa mazonge ya ufisadi uliokithiri. 

Licha ya kutaka Spika aunde timu ya kuchunguza ufisadi katika manunuzi ya Mafuta na licha ya Kamati ya Bunge kutaka Uchunguzi wa kibunge kufanyika katika manunuzi haya
bado hakuna hatua inayochukuliwa. 

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Mamlaka ya Manunuzi ya Umma PPRA kufanya uchunguzi wa kina kuhusu manunuzi ya mafuta kuzalisha Umeme ambayo yanachoma bilioni 42 za Serikali kila Mwezi. PPRA hapaswi kufumbia macho manunuzi yanayotafuna shilingi 1.4 bilioni kila siku na yanayoongeza manunuzi ya nchi kutoka nje (imports) na hivyo kupoteza fedha za kigeni hovyo.

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha ambayo ndio wizara mama ya PPRA kupitia Fungu 50, na ndio Wizara yenye kusimamia uchumi wa nchi kwa ujumla ituletee Bungeni Taarifa ya Uchunguzi
utakaofanywa na PPRA kuhusu manunuzi shilingi 1.4 bilioni kila siku ya mafuta kuendesha mitambo ya kuzalisha Umeme.

2.3 Deni la Taifa.
Mheshimiwa Spika, Fungu 22 linaombewa jumla ya shilingi bilioni 2,735 ili kuweza kulipa madeni ikiwemo deni la nje la shilingi bilioni 373 na trilioni 1.5 kama deni la ndani. Kwa mujibu wa taarifa ya
mwenendo wa uchumi ya mwezi Julai 2012, deni la nje la Taifa (external debt) mpaka mwisho wa mwezi Juni 2012 lilikuwa limefikia kiasi cha dola za Kimarekani milioni 10,354.6 kiasi ambacho ni
ongezeko la zaidi ya dola milioni 385.9 kwa kipindi kama hicho mwaka 2011. Aidha katika kipindi hicho deni la ndani lilikuwa kiasi cha shilingi bilioni 4,174.2. 

Kambi ya Upinzani Bungeni ina taarifa kwamba takwimu hizi za Deni la Taifa hazihusishi dhamana ambazo Serikali imezitoa kwa Mashirika ya Umma na Kampuni binafsi.

Dhamana lazima katika siku za usoni ziwe ni sehemu ya deni la Taifa maana tumeshuhudia sasa ambapo Kampuni nyingi binafsi zimeshindwa kulipa mikopo iliyodhaminiwa na Serikali. Mfano ni
malipo ya deni lenye thamani ya shilingi bilioni 60 la kukodisha ndege ya Airbus kwa Shirika la ATCL kutoka kampuni ya Wallism Traders ya Lebanon na Deni lililochukuliwa na Kampuni ya Kiwira
Coal and Power limited ambayo mbia wake alishindwa kuendesha mradi wa Makaa ya Mawe Kiwira licha ya kudhaminiwa na Serikali Mkopo kutoka kwenye taasisi za Fedha hapa nchini ambapo sasa
Serikali imepanga kulipa shilingi bilioni 40 katika Bajeti ya mwaka huu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani haina tatizo na uhimilivu wa Deni la Taifa (Debt sustainability) kwani tunajua kuwa mataifa makubwa yanakopa sana na yana uwiano mkubwa wa
Deni kwa GDP kuliko sisi. Tatizo letu ni namna ambavyo fedha za mikopo zinatumika. Matumizi ya mikopo tunayochukua sio endelevu maana sehemu ya mikopo hiyo hutumika kwa matumizi ya kawaida badala ya matumizi ya uzalishaji au kuongeza uwezo wetu wa kuzalisha.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaendeleza wito wake wa kutaka Fungu 22 la deni la Taifa lifanyiwe ukaguzi maalum (Special Audit) ili tuweze kujua mikopo hii tunayochukua kila wakati inatumika kufanyia nini?

Miradi iliyotekelezwa kutokana na Madeni ambayo Waziri wa Fedha aliitangaza wakati wa kufunga mjadala wa Bajeti kuu ya Serikali ifanyiwe ukaguzi kutambua ukweli na kuona thamani ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaendelea kuhoji kama tulivyohoji mwaka 2011/2012 kuhusu matumizi mabaya ya fedha za umma. Katika fungu 21, kasma 229929, Serikali imetenga
Shilingi bilioni 26.4 kwa ajili ya kulipa fidia kwa mikataba mbalimbali ambayo Serikali imeingia. Hii inaonyesha kuwa Serikali inatumia fedha nyingi sana kwa ajili ya mikataba iliyoingiwa na Mashirika ya Umma na kuliletea hasara Taifa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kutaka majibu kutoka kwa serikali, bado tunataka kuwe na usimamizi thabiti

ili kulinda fedha za umma zinazotumika kwenye Mashirika ya Umma,ambapo kumekuwa na usimamizi mbovu sana na unaopelekea Taifa kupoteza fedha nyingi sana kutokana na ubadhirifu katika Mashirika ya Umma. Hii ni kweli kwa Mashirika ambayo Serikali inamiliki sehemu ya hisa.

2.5 MKOPO WA KUNUNUA RADA ILIYOGUBIKWA NA UFISADI
Mheshimiwa Spika, sehemu ya Malipo ya Deni la Taifa ni Mkopo ambao Serikali ilichukua ili kununua Rada kutoka kampuni ya BAE ya Uingereza. Suala hili la rada limejadiliwa sana nchini kwa upande mmoja tu wa ufisadi wa kupandisha bei ya Rada na hatimaye kurejeshwa kwa iliyoitwa chenji ya Rada. Hiyo ilikuwa ni nusu tu ya ukweli kuhusu suala la Rada kwani Serikali ilikopa kiasi cha dola za kimarekani 40 milioni kutoka Benki ya Barclays ya Uingereza kwa ajili ya kununulia Rada. Mkopo huo ulikuwa na Riba ya asilimia 4.9 juu ya kiwango cha riba zinazotolewa na Benki ya Dunia au IMF.
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama mkopo huu umeshalipwa wote na jumla tulilipa kiasi gani cha fedha.

Ukilinganisha fedha iliyorejeshwa kama chenji ya Rada na Fedha ambayo Tanzania iliilipa Benki ya Barclays (Principal amount na Interest), je chenji ya Rada ilikuwa na thamani yoyote kifedha?
Mjadala wa ununuzi wa Rada hauwezi kuisha kwa kufurahia kurejeshewa chenji tu. Mjadala huu bado mbichi kabisa kwani tunataka ukweli na ukweli mtupu uelezwe kwa umma na kuona

Taifa lilipata hasara kiasi gani kwa ufisadi huu wa kimataifa na hatua stahiki za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wote walioingiza hasara kwa Taifa letu.

2.4 Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu
Mheshimiwa Spika, taifa letu limekuwa na sheria nyingi ambazo ziliwahi kutungwa kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la fedha haramu,rushwa na uhalifu uliopangwa hapa nchini mwetu tangu tupate
uhuru na hii inathibitishwa na uwepo wa sheria zaidi ya 15 kuwahi kutungwa tangu uhuru (tazama kiambatanisho A). 

Vile vile Bunge liliimarisha Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu mwaka 2011. Hata hivyo bado nchi yetu imegubikwa na fedha chafu na hasa wizi katika Mabenki hapa nchini. Wakati sheria ya Fedha haramu inayataka Mabenki kutunza kumbukumbu sahihi za wateja,kumekuwa na matukio (yaliyoripotiwa na yasiyoripotiwa) ya Wafanyakazi wa mabenki hapa nchini kushirikiana na baadhi ya wananchi kuiba fedha za wateja na hasa wateja ambao wamefariki dunia na ndugu na jamaa zao kutojua taarifa za kibenki za marehemu hawa. Serikali inapaswa kufahamu kuwa wizi kwenye
mabenki ni moja ya sifa mbaya sana ya mfumo wetu wa fedha na hivyo kusababisha Benki kuweka riba kubwa sana ili kufidia ‘risk’ kama hizi za watu ‘kupiga’ amana za wateja kwenye mabenki.

Kambi Rasmi ya upinzani inaitaka Wizara ya Fedha kupitia Kitengo cha Udhibiti wa Fedha haramu kudhibiti wizi kwenye Benki za hapa nchini.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina juu ya matatizo ya mtaji “Capital under pressure” yanayoikabili benki ya NBC na hatua zilizochukuliwa na Serikali kama
mmoja wa wanahisa dhidi ya mwanahisa mwenye dhamana ya kuisimamia Benki hiyo (ABSA) kwa kushindwa kuisimamia kwa umakini na hivyo kuiingiza katika matatizo hayo ya mtaji.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa wanahisa (ambapo Serikali ni mmoja wao) wanapaswa kuongeza mtaji katika benki ya NBC ili kuinusuru,Benki ambayo ni moja ya Benki kubwa kabisa hapa nchini ambayo
kama ingekuwa na usimamizi mzuri ingepaswa kujiendesha yenyewe na kutoa gawio kwa wanahisa.

Mheshimiwa Spika, taarifa iliyotolewa na Benki Kuu ya Uswissi na kuchapishwa na magazeti mbalimbali ya hapa nchini mwezi June,2012 inanonyesha kuwa viongozi wa Serikali pamoja na
wafanyabiashara wakubwa wametorosha fedha zao katika mabenki ya Uswissi kiasi cha shilingi bilioni 315.5. 

Habari zaidi zinaeleza kwamba mabilioni haya yanatokana na ‘deals’ zilizofanywa na watendaji wa Serikali na wafanyabiashara kadhaa kwenye sekta za Nishati na Madini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepata taarifa kuwa mmoja wa Viongozi wa juu kabisa wa Tanzania na baadhi ya Mawaziri wa Serikali za awamu zilizopita ni miongoni mwa wamiliki wa Fedha hizi. Sehemu kubwa ya Fedha
zililipwa na Kampuni za utafutaji wa Mafuta na Gesi katika Pwani ya Mkoa wa Mtwara zilizopewa mikataba kati ya mwaka 2004 na 2006.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa rasmi ya hatua gani imechukua mara baada ya taarifa ile kutoka Benki ya Taifa ya Uswissi ilipotolewa. Tunaitaka Serikali kuliambia Taifa hatua
itakazochukua kurejesha fedha hizi na nyingine zozote ambazo zimefichwa ughaibuni. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni italazimika kuweka wazi taarifa na majina ya watu wenye umiliki wa fedha
katika Benki za nchini Uswissi iwapo Serikali haitatoa taarifa rasmi kuhusu suala hili.

Mheshimiwa Spika, Aidha, kuna taarifa nyingine zinaonyesha jinsi ambavyo taifa linaibiwa kupitia kesi mbalimbali ambazo Serikali imeshitaki au kushitakiwa kwenye Mahakama za Kimataifa. Mfano
mzuri ni Kesi ya IPTL na Standard Chartered Bank ya Hong Kong ambayo imechukua muda mrefu bila kuisha na kuliingizia taifa hasara kubwa sana. Tunapenda kufahamu ni kwa nini mpango wa
kumaliza kesi hii nje ya Mahakama hautekelezwi na vile vile mpango wa kugeuza Mtambo wa kufua umeme wa IPTL kuwa wa Gesi kwa nini hautekelezwi?

Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kupata majibu kuhusu mambo yafuatayo;

Kwanza, fedha zilizoko kwenye Escrow Akaunti Benki Kuu za IPTL (Tegeta escrow) zimefikia kiasi gani mpaka sasa, na usalama wa fedha hizo ukoje? Ikumbukwe kwamba kuna uamuzi wa Bunge
kwamba Fedha hizi zisitumike wala kutolewa mpaka maamuzi kuhusu mtambo wa IPTL kufikiwa na hasa uamuzi wa kugeuza mtambo huu kutumia Gesi Asilia.

Pili, Suala hili la kesi ya IPTL limechukua muda mrefu sana na sasa ni wakati muafaka likamalizwa nje ya mahakama kwa Waziri wa Fedha kukutana na pande zote za mgogoro huu ili liweze kufikia
mwisho.

2.6 Kampuni ya Oxford University Press Tanzania Kufungiwa
Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 03 Julai 2012 Benki ya Dunia ilitangaza kuifungia kampuni ya uchapishaji ya Oxford University Press Tanzania Ltd (OUPTL) kutokana na vitendo vya rushwa
ambavyo kampuni hiyo ilikiri kuhusika kwake kwenye miradi mbalimbali ya elimu iliyokuwa inafadhiliwa na Benki hiyo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, kampuni hiyo ilikiri kuhusika katika kuwahonga maafisa mbalimbali wa Serikali katika mkataba wake wa kusambaza vitabu na kampuni hiyo ilikubali kuilipa Benki ya Dunia
kiasi cha dola 500,000 kama sehemu ya makubaliano yake kutokana na kashfa hiyo.

Mheshimiwa Spika, mamlaka ya manunuzi ya umma ilitangaza kuifungia kampuni hiyo hapa nchini kwa kipindi cha miaka saba,wakati ambao tayari tulishawapa zabuni ya kusambaza vitabu vilivyotokana na chenji ya rushwa ya Rada ambazo ziliamuliwa kuwa zitaenda kununua vitabu.

Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuinyang’anya kampuni hii zabuni ya kuchapisha na kusambaza vitabu hivyo na badala yake kazi hiyo yapewe makampuni ya ndani ya nchi. Tabia ya Serikali kufanya kazi na Kampuni ambazo tayari zina dosari ama za kifisadi au kukiuka sheria na maagizo ya Serikali inatoa picha mbaya kwenye uchumi. Hali kadhalika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwachukulia hatua maafisa wote wa Wizara waliohusika katika “rushwa ya Oxford”.

3.0 Mishahara hewa nchini
Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka wa fedha 2012/2013, tulitaja kiasi cha shilingi bilioni 91 ambazo zililipwa kama mishahara kwa watumishi hewa kama ilivyoripotiwa na magazeti ya ‘The Daily News’ na ‘The Guardian’ ya Machi 23, 2011.

1

Mheshimiwa Spika, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya tarehe 31 Machi, 2012 inaonesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2010/2011 jumla ya shilingi 142,715,827.99
2
zililipwa kama mishahara kwa wastaafu, watumishi walioacha au kufukuzwa kazi na watumishi wengine ambao hawakustahili. Aidha, ripoti hiyo imeonesha kiasi cha shilingi 1,842,607,565.29 zilizolipwa kama mishahara hewa kwa mwaka wa fedha 2009/2010.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa taarifa ya Waziri wa Fedha kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya fedha na uchumi ya tarehe 7 Agosti, 2012 ni kwamba uhakiki wa watumishi uliofanyika mwezi
Januari, 2012 kwenye Halimashauri 133 na kwenye taasisi na wakala za Serikali 154 ulibaini majina 9,949 ya watumishi wasiostahili kuwemo kwenye orodha ya mishahara. Idadi hii ya watumishi hewa ni sawasawa na takribani idadi ya watumishi walioajiriwa katika sekta nzima ya madini kwenye migodi ya dhahabu hapa nchini.

Watumishi hewa wanaokaribia 10,000 ni wengi mno na inaonyesha dhahiri namna Serikali isivyo makini katika suala hili ambalo linasababisha upotevu mkubwa wa Fedha za Umma.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha alikiri mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi kwamba mwezi Februari Serikali ililipa shilingi bilioni 5.1 kama mishahara hewa. Hii maana yake ni kwamba Serikali
2 Tazama Ripoti ya CAG toleo la Kiingereza uk.37.

Huhutumia zaidi ya shilingi bilioni 70 kila mwaka kwa watumishi hewa wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, tunataka fedha hizi wanazolipwa watumishi hewa zitumike kuwalipa walimu na madaktari madai yao kwani ni nyingi na zinatosha sana. Siku zote sababu za Serikali kutotimiza
matakwa ya wafanyakazi kwenye sekta ya Afya na Elimu ni
kwamba Serikali haina Fedha. 

Lakini hapa tunashuhudia Shilingi
bilioni 70 kila mwaka zikiteketea kulipa watumishi hewa ambao
hawapo, hawafanyi kazi na hivyo kufaidisha mtandao wa kifisadi
ambao kwa vyovyote vile unaanzia Wizara ya Fedha na Wizara ya
Utumishi. Serikali inakosa vipi fedha za kulipa madai ya Walimu na
inapata za kulipa watumishi hewa? Serikali inakosa vipi fedha za
kulipa Madaktari na Manesi lakini inapata shilingi bilioni 70 kila
mwaka kulipa watumishi hewa?

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka mradi huu wa
watumishi hewa wenye mauzo (turnover) ya shilingi 70 bilioni kwa
mwaka uvunjwevunjwe ili kupata fedha za kulipa Walimu na
Madaktari. Waziri wa Fedha asambaratishe mtandao huu mwovu
ambao sasa umeota mizizi kwenye Taasisi za Serikali. Vile vile Waziri
agawe kwa Wabunge taarifa ya uhakiki wa wafanyakazi wa Serikali
na pia hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya vinara wa
mtandao wa watumishi hewa Serikalini.
4.0 Benki Kuu ya Tanzania-(BOT)
Page 17
17
Mheshimiwa Spika, taasisi hii ndiyo yenye dhamana ya kutayarisha
na kusimamia sera za fedha na utendaji mzima wa taasisi za fedha
kwa ujumla. Katika kutekeleza hilo Benki Kuu ndicho chombo
kinachoweka miongozo kwa taasisi za fedha, taasisi za bima na
taasisi za hifadhi za jamii ili kuhakikisha fedha za wanachama katika
taasisi hizo zinalindwa.
Mheshimiwa Spika, taasisi za fedha zimegawanyika katika sehemu
kuu mbili, ambazo ni tasnia ya benki (Banking industry) na tasnia
ndogo ya fedha (Microfinance industry). Tasnia zote hizi
zinahudumia wateja tofauti kwa kulingana na wanachojishughulisha
nacho katika kuinua kipato cha familia inayomtegemea, mteja yuko
kwenye sekta binafsi au sekta rasmi ya ajira.
Mheshimiwa Spika, Benki Kuu katika kutimiza wajibu wake inailazimu
kutoa vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji wa mikopo ili
kukabiliana na wakopaji ambao wanaweza kuwa na lengo la
kuchukua fedha wakati hawana nia ya dhati ya kurejesha mikopo
yao.
4.1 RIBA KATIKA TAASISI ZA FEDHA
Mheshimiwa Spika, tofauti kati ya viwango vya riba vinavyotozwa
kwenye mikopo na vile vinavyotolewa kwenye amana kama faida
vimeendelea kuwa juu, licha ya kuongezeka kwa ushindani katika
sekta ya kibenki. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana
kwa taarifa sahihi za wakopaji (credit reference data bank) na
Page 18
18
kutokuwepo kwa taasisi ya utoaji wa taarifa sahihi za waombaji
mikopo (Credit Rerefence Bureau) nchini. Aidha, gharama kubwa
za kufanya biashara kutokana na miundombinu hafifu, nazo
zimechangia kuongeza viwango vya riba vinavyotozwa kwenye
mikopo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaomba taarifa ya
kuanzishwa kwa Credit Reference Bureaux kwa mujibu wa Sheria ya
Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
4.2 Usimamizi Wa Tasnia Ndogo ya Fedha (Microfinance Industry-
MFI)
Mheshimiwa Spika, tasnia hii ndiyo inayoshughulika moja kwa moja
na kundi kubwa la Watanzania ambao hawako kwenye mfumo
rasmi wa ajira kwa kuwapa mikopo midogo midogo kwa shughuli
rasmi au zisizo rasmi, ili kuhakikisha kuwa kipato cha familia
kinapanda na hivyo uchumi wa mwananchi mmoja mmoja unakua.
Mheshimiwa Spika, tasnia hii inalenga kuboresha maisha ya
wananchi wa vijijini na maeneo mbalimbali ya mijini. Tasnia hii
inalenga kuboresha maisha kwa wananchi mmoja mmoja au
makundi (Saccoss) na benki jamii (vicoba) ambazo zimekuwa na
wanachama wengi wanaoendelea kujiunga ili kujikwamua
kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa mdhibiti anayeelewa jinsi tasnia
hii inavyofanya kazi zake na aina ya wateja inaowahudumia ni
Page 19
19
udhaifu mkubwa unaosababisha tasnia hii kushindwa kukua.
Kukosekana kwa udhibiti wa sekta ndogo ya Fedha kunasababisha
wananchi masikini kuumia sana. Mfano tumeshuhudia namna
Kampuni za kukopesha zinavyowafanya Walimu vijijini kuwa masikini
zaidi kwa kuweka riba kubwa sana. Hata hivyo Serikali imekaa kimya
bila kusaidia wanyonge hawa kwa kuchukua hatua madhubuti za
kudhibiti na kusimamia sekta hii. Mfano mzuri wa Serikali kushindwa
kusaidia wanyonge ni pale ambapo wannachi wengi sana kujikuta
wamepoteza fedha zao kupitia ‘schemes’ kama vile DECI ambapo
wananchi walikusanya zaidi ya shilingi bilioni 16 ambazo mpaka sasa
hata riba yake hatujui inakwenda wapi? Kungekuwa na Mamlaka
ya kusimamia sekta ya fedha kwa ajili ya wanyonge tusingeshuhudia
unyonyaji huu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuunda
Mamlaka ya Usimamizi wa sekta ndogo ya Fedha (Tanzania
Microfinace Regulatory Authority) hapa nchini badala ya Benki Kuu
ya Tanzania ambayo ndiyo msimamizi wa tasnia ya benki. Lengo ni
kuhakikisha kuwa wananchi wa vijijini wanaopata mikopo kutoka
kwenye taasisi za Benki wanalindwa na dola. Mamlaka italinda Haki
za wanyonge dhidi ya ‘loan sharks’ na Wajibu wa wanyonge wenye
kuchukua mikopo.
Mheshimiwa Spika, kuundwa kwa chombo chenye mamlaka ya
kusimamia taasisi ndogo ya fedha ni lazima kutokana na ukweli
Page 20
20
kwamba kuna utofauti wa muundo baina ya mabenki na taasisi
ndogondogo za fedha; inakuwa ni vigumu kudhibiti riba na utoaji
wa vigezo vya kifedha katika kuhudumia wananchi na kutoa
mikopo kwa wateja wa tasnia hizo mbili zilizo tofauti kimuundo.
Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa chombo chenye mamlaka pia
itasaidia kuwa na Credit Reference Bureau itakalokuwa na taarifa
za wakopaji kutoka taasisi ndogondogo za fedha tofauti na
itakayosimamia wadaiwa wa mabenki na taarifa hizi zitasaidia
udhibiti wa wateja wa taasisi hizi kuchukua zaidi ya mkopo mmoja
kwenye taasisi tofauti tofauti ambapo hali hii husababishwa na
ucheleweshaji wa mikopo inayotolewa na taasisi hizi pamoja na
uhafifu wa mikopo katika kumsaidia mlengwa.
4.3 Mifuko ya Hifadhi za Jamii
Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi za Jamii ni mojawapo ya sekta
ambayo ina uwezo mkubwa wa kupunguza ukosefu wa ajira kwa
vijana wetu, kama uwekezaji unaofanywa kwa kutumia mifuko hiyo
utasimamiwa vizuri.
Meshimiwa Spika, inaonesha kwamba mifuko hii imekuwa ikikusanya
michango ya wanachama na kulipa wastaafu wanachama wa
Mifuko hii vizuri. Kutokana na maelekezo ya sheria mpya iliyoleta
mjadala baina ya wafanyakazi na serikali juu ya mabadiliko ya
sheria na utoaji wa mafao kwa wafanyakazi, pamoja na Bunge
Page 21
21
kutaka mabadiliko ya sheria hiyo bado kuna haja ya kutazama
namna mifuko ifanyavyo kazi.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuweka wazi utendaji wa
Mifuko hii katika maeneo nyeti yafuatayo, kwanza Ukwasi wake
(Liquidity of the Social Security funds), pili Uwekezaji (Investments) pia
Risk Management reports. Taarifa katika maeneo haya hupelekwa
na mifuko kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma na kutokana na utaratibu wa Kazi wa Kamati hii ya POAC ni
vigumu wananchi wote kuona taarifa hizi ambazo ni muhimu kuwa
wazi kwa umma. Taarifa kama hizi zitaliwezesha Bunge kuelewa
kiwango cha usalama wa Mifuko hii na uwezo ziada (excess
financial capacity) kuendelea kutoa huduma zinazohitajika. Kama
ilivyo kwa Mabenki, tunashauri kuwa taarifa za robo mwaka za
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ziwe zinatangazwa kwenye magazeti
yanayosomwa zaidi nchini ili wananchi na hasa wanachama wa
mifuko waone namna mifuko yao inavyofanya kazi.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa
kipindi chote imekuwa ikitoa ushauri katika sekta hii, hatuna budi
kurudia ushauri tulioutoa mwaka jana kama ifuatavyo:
“Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapendekeza kwa Mifuko
ya PSPF na PPF kuangalia namna ya kuwekeza katika maeneo
yanayochochea ukuaji wa uchumi na hivyo kuzalisha ajira na
Page 22
22
kupata wanachama zaidi. Maeneo kama uwekezaji kwenye
Bandari na Reli yanapaswa kuangaliwa kwani kutokana na Jiografia
ya nchi yetu ni maeneo yanayoweza kuzalisha faida kubwa sana.
Tunaitaka Serikali ilieleze Bunge kuna mipango gani katika Mashirika
haya (PSPF na PPF) kuangalia maeneo mapya ya uwekezaji katika
miundombinu na hasa Bandari.
Mheshimiwa Spika, Mifuko ya hifadhi ya jamii imewekeza katika
miradi ya ujenzi wa nyumba nafuu kwa ajili ya wanachama wao na
pia wanachi kwa ujumla. Tunasisitiza Miradi hii isiwe Dar es salaam
na Mwanza tu bali ienee nchi nzima kama ambavyo mfuko wa PSPF
umeanza.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani pia inashauri kwamba fao la
Elimu ambalo Mfuko wa PPF unatoa kwanza litolewe na Mifuko
mingine pia lakini pia lipanuliwe hadi kufikia elimu ya Chuo Kikuu.
Fao hili la Elimu ambalo ni muhimu sana na twapongeza mfuko wa
PPF kwa kulianzisha ni fao ambalo litasaidia sana kuhakikisha kuwa
yatima ambao wazazi wao wanakuwa wamefariki wanapata
uhakika wa kuendelea na masomo. Fao hili liwe fao la lazima kwa
mifuko yote nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni bado inasisitiza
ushauri wake kuwa Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ihamishiwe
Wizara ya Kazi na Ajira kama Wizara inayohusika na ‘social security’.
Hoja hii inatiliwa nguvu na uhalisia kwamba Mdhibiti wa Mifuko
Page 23
23
(SSRA) yupo chini ya Wizara ya Kazi. Vile vile Wizara ya Fedha kama
mlipaji mkuu wa Pensheni asiwe na Taasisi hata moja ya Pensheni
chini yake ili kuweka ‘checks’.
Mheshimiwa Spika, Hali kadhalika hakuna sababu ya kuwa na utitiri
wa mifuko mingi kama ilivyo sasa. Ipunguzwe na kubakia na mifuko
miwili tu, mmoja wa wafanyakazi walio katika sekta binafsi na sekta
isiyo rasmi na mwingine kwa wafanyakazi wa sekta ya umma.
Tunarejea pendekezo letu kwamba mifuko ya NSSF na PPF
iunganishwe kuwa mfuko mmoja kwa ajili ya sekta binafsi na sekta
isiyo rasmi na mifuko ya PSPF, LAPF na GEPF iunganishwe kuwa
mfuko mmoja kwa ajili ya kushughulika na wafanyakazi wa Sekta ya
Umma”.
Mheshimiwa Spika, mojawapo ya vipaumbele vya Kambi Rasmi ya
Upinzani kwa mwaka 2012/2013 ni kupunguza misamaha ya kodi ya
kutozidi asilimia moja ya GDP, kutokana na Mapato mengi ya Serikali
kupotea kwa sababu ya kutoa misamaha ya kodi kwa wadau
mbalimbali wanaotakiwa kulipa kodi, na ikizingatiwa moja ya
michango ya waziri akiwa mbunge tarehe 25/8/2011 alisema
“kupunguza misamaha ya kodi ya kutozidi asilimia moja ya GDP”.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini waziri alikuwa na nia ya dhati na
kukubaliana na Kambi Rasmi ya Upinzani uwezekano wa jambo hili.
Hivyo basi, ili kuonesha kuwepo kwa dhamira ya kweli Kambi Rasmi
Page 24
24
ya Upinzani inataka waziri alijulishe bunge juu ya utekelezaji wa
azimio hili.
6.0 MSAJILI WA HAZINA NA BODI ZA MASHIRIKA YA UMMA
Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa mnamo mwaka 2010 Sheria
namba 2 (the written laws (miscellaneous amendments) No 2. ACT
2010 ilipitishwa na katika eneo la kumi (part X) ilifanyia marekebisho
sheria ya mashirika ya umma (the public Corporations Act, CAP
257). Sheria hii ilisainiwa na Rais mnamo tarehe 20 Mei 2010.
Mheshimiwa Spika, katika mabadiliko hayo ya sheria ibara ya 20 na
21 ilibainisha bayana majukumu ya msajili wa hazina na ndipo
iliweka majukumu yake ya kazi kuwa ni kusimamia mashirika yote ya
umma. Aidha, mabadiliko hayo yalibainisha wazi kuwa msajili wa
hazina hatakuwa mjumbe wa Bodi za mashirika haya na wala
hapaswi kushiriki kwenye vikao vya bodi vya mashirika haya kwani
yeye ni msimamizi mkuu wa mashirika hayo na anapaswa kusimamia
utendaji kazi wake.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mabadiliko hayo ya sheria bado
msajili wa hazina amekuwa akihudhuria vikao mbalimbali vya bodi
za Mashirika ya Umma kama mjumbe jambo ambalo ni kinyume na
sheria, na amekuwa akishiriki moja kwa moja kwenye maamuzi ya
bodi hizo jambo ambalo linamfanya kushindwa kutimiza wajibu
wake wa kuwa msimamizi kama ambavyo sheria inaelekeza
Page 25
25
Kambi ya Upinzani inataka kupata maelezo ya kina ni kwa nini hali
hii imeendelea kuachwa iwe ilivyo kwa msajili wa hazina kuendelea
kuwa mjumbe wa vikao vya Bodi za mashirika ya umma kinyume na
sheria. Aidha tunataka kauli ya serikali kuhusiana na suala hili.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inapenda kupata maelezo ya
Serikali kuhusu masuala yafuatayo.
Moja, Sakata la uuzwaji wa hisa za Shirika la UDA umefikia wapi?
Pili, Serikali imefikia wapi katika utungaji wa Sheria mpya ya Ofisi ya
Msajili wa Hazina ili kuimarisha usimamizi wa Mashirika ya Umma.
Tatu, Serikali imefikia wapi katika pendekezo la kuifanyia
marekebisho Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) ili liweze
kumiliki, kusimamia na kuziendesha hisa za serikali katika Kampuni
binafsi ambapo umiliki wa Serikali ni chini ya asilimia 50. Pendekezo
hili lilikuwa ni uamuzi wa Bunge na hivi sasa mwaka mzima umepita
bila Bunge kupatiwa taarifa yeyote kinyume na maelekezo yake.
Nne, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa Waraka namba
moja wa mwaka 2012 kuhusu usimamizi na uendeshaji wa Mashirika
ya Umma na hasa mahusiano kati ya Mashirika ya Umma na Wizara
mama. Waziri wa Fedha kama msimamizi mkuu wa Mashirika ya
Umma amechukua hatua gani kuhakikisha falsafa ya ‘eyes on,
hands off’ katika kusimamia Mashirika ya Umma inatekelezwa
Page 26
26
kikamilifu na kuhakikisha Mashirika ya Umma yanaendeshwa kwa
faida na bila kuingiliwa ingiliwa na Wanasiasa?
7.0 Ofisi ya Takwimu ya Taifa
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of
Statistics – NBS) ilizinduliwa rasmi tarehe 26 Machi, 1999 kama
Wakala wa Serikali (Executive Agency) kwa mujibu wa Sheria ya
Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997, (The Executive Agencies
Act 1997) (Act No. 30 of 1997), na ndio chombo rasmi
kinachojihusisha na kutafuta, kuandaa na kusambaza takwimu
hapa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, katika kupanga mipango ya maendeleo na
kuandaa sera mbalimbali za nchi husika, upatikanaji wa takwimu
rasmi zinazotokana na Kanuni na Mbinu za Kitaalamu iliyowekwa na
Ofisi ya Takwimu ya Umoja wa Mataifa (United Nations Statistical
Division) ni muhimu. Takwimu zote zilizo rasmi duniani hutolewa na
Ofisi za Takwimu za nchi husika kupitia Sheria za Takwimu za nchi
mbali mbali.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imekua ikitoa
Mapendekezo ya kuboresha utendaji wa Ofisi ya Takwimu katika
Nyanja mbalimbali na serikali kutothubutu kuchukua mapendekezo
hayo na kuyafanyia kazi.
Page 27
27
Mheshimiwa Spika, katika taarifa ya miaka hamsini ya wizara,taarifa
inaonesha wizara kuwa na nia ya kuboresha ofisi ya takwimu ya
taifa kwa kuboresha miundombinu ya utoaji takwimu nchini
,kuimarisha mfumo wa takwimu nchini (NBS), kutoa takwimu sahihi
na kwa wakati, kutokana na nia hii ya serikali Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka serikali kuzingatia Ofisi ya Takwimu Kuwa na
uhisiano wa moja kwa moja wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa na ngazi
za Mikoa, Halmashauri za Wilaya, Kata na Vijiji kurahisisha upatikanaji
wa takwimu ili zisaidie katika kupanga mipango ya maendeleo.
8.0 Mamlaka Ya Mapato-TRA
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza
kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania ijenge uwezo wa kukagua
mahesabu ya kikodi kwenye Kampuni za Utafutaji wa Mafuta na
Gesi, Kampuni za Madini na Kampuni za Simu ambazo uzoefu
unaonyesha kuwa katika maeneo haya kuna mbinu nyingi sana za
kukwepa kodi.
Mheshimiwa Spika, kwa msisitizo mkubwa sana Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka mamlaka ya Mapato Tanzania
kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano nchini kukagua
mapato ya Kampuni za simu na hasa kampuni ambazo zinatoa
huduma kwenye kampuni za Simu.
Page 28
28
Mheshimiwa Spika, Katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya
Mawasiliano kulikuwa na mjadala kuhusu namna ambavyo wasanii
wa Tanzania wanavyonyonywa mapato na Kampuni zinazotoa
huduma ya miito kwenye kampuni za simu. Bunge lako lilielezwa
kwamba Biashara ya miito kwenye simu ina thamani ya shilingi bilioni
43 kwa mwaka lakini msanii anayetengeneza kazi zinazouzwa
anapata asilimia 7 tu ya mapato hayo.
Mheshimiwa Spika, taarifa zaidi za ziada zinaonyesha kuwa kampuni
ya On Mobile yenye mkataba na Kampuni za Simu za Vodacom na
Airtel kama ‘aggrigator’ wa miito ya simu yenye miziki ya wasanii
hapa nchini hailipi kodi kutokana na mapato yake. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa za kikodi za kampuni hii na
washirika wake na hatua ambazo Serikali imechukua dhidi yao.
Kambi ya upinzani inashauri pia kwamba Mapato yanayotokana na
miradi kama hii kwenye Kampuni za simu yawe ‘ring fenced’ na
kutozwa kodi stahiki au kodi maalumu.
9.0 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani-Internal Auditor General
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Mkuguzi Mkuu wa Ndani (Internal Auditor
General) iliyoanzishwa na mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya mwaka
2010 inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa
zikileta migongano katika maeneo ya kiutendaji na uwajibikaji,
sheria haipo wazi juu ya upatikanaji wa mtaalam huyo kama
Page 29
29
inavyotakiwa na sheria na 8 ya utumishi wa umma, kwa mfano
kutangazwa kwa nafasi hizo na waombaji kufanyiwa usaili.
Mheshimiwa Spika, pamoja na utata wa uteuzi wa mkaguzi wa
ndani kama sheria ya utumishi wa umma inavyoelekeza mkaguzi wa
ndani anasimamiwa na Katibu Mkuu Hazina (Paymaster General)
ambaye naye ni mkaguliwa- kwa hiyo kunakuwa na mgongano wa
kimaslahi uhuru wa ofisi ya mkaguzi wa ndani inaweza kukosa uhuru
Kambi Rasmi ya Upinzani inaishauri serikali katika ofisi ya Mkaguzi wa
Ndani (Internal Auditor General office) ingepaswa iwe na bodi
ambako maalumu wangekuwa wanaripoti ili kuweka uhuru
unaofaa.
Mheshimiwa Spika, wakaguzi wa ndani ni waajiriwa wa serikali na
hufanya kazi zao za ukaguzi kwa kipindi chote ambacho shughuli za
serikali zikifanyika, mfano; katika halmashauri wakaguzi hutakiwa
kuwajibika kuanzia upokeaji wa fedha kutoka hazina, hadi kutumika
kwake, Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji serikali nini nafasi ya
wakaguzi wa ndani kama ubadhirifu wa fedha za umma
umeendelea kuwepo kama ripoti za mkaguzi mkuu wa hesabu za
serikali zinavyothibisha?
Mheshimiwa Spika, katika ushughulikiaji wa matumizi mabovu ya
rasilimali za umma serikali imekuwa legelege hasa pale taarifa
Page 30
30
zinapotolewa na wakaguzi wa ndani ambao hutoa taarifa mara
kwa mara na seriakali kukaa kimya, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka serikali kutambua umuhimu wa taarifa hizi za wakaguzi wa
ndani na kuhakiki inachukua hatua stahiki pasipo kusubiri taarifa za
mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambazo ukaguzi wake
hufanyika kwa kuchelewa zaidi.
10.0 Utekelezaji wa Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012 Pamoja
na Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2012/2013
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Wizara ya Fedha mwaka
2011/2012 fungu Namba 50 wizara ilitenga shilingi bilioni 659 kwa
ajili ya miradi ya maendeleo na fedha zilizotumika hadi kufikia Juni
2012 ni shilingi bilino 402.7 ambapo fedha za ndani zikiwa shilingi
bilioni 78.65 sawa na asilimia 11.9 ya bajeti ya maendeleo hivyo
kutegemea fedha za nje katika kutekeleza miradi ya maendeleo
kwa asilimia 88.1. Kambi Rasmi ya Upinzani, pamoja na Seriliali
kutokubali kutumia mapato ya ndani zaidi katika kugharimia miradi
ya maendeleo, I azidi kushauri serikali kuwa na Makati wa dhati wa
muda mrefu wa kuachana na utaratibu wa kutegemea misaada ya
nje. Mkakati huo ulenge kuiongezea mapato kwa kutumia mbinu
mbalimbali za kodi.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya 2012/2013 serikali imetenga
shilingi bilioni 546.51 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo
Page 31
31
ambayo ni pungufu kwa asilimia 18 ya bajeti ya mwaka 2011/2012
ambapo serikali ilitenga shilingi bilioni 659. Katika bajeti ya 2012/2013
ni asilimia 19.3 tu ya fedha za ndani ndizo zimeelekezwa kwenye
miradi ya maendeleo na asilimia 80.7 ya makadirio ni fedha za nje
ikiwa ni mikopo ya kibiashara na misaada. Kambi Rasmi ya Upinzani
inahoji: ni maendeleo yapi ambayo serikali inadhamiria kwa
kutenga fedha ya maendeleo ambayo ni pungufu kwa asilimia 18
ya bajeti ya mwaka jana?
Hitimisho
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani Bungeni inasisitiza umuhimu
wa kuisimamia vema Wizara ya Fedha katika kusimamia uchumi wa
nchi. Tuna imani kwamba Waziri wa Fedha ndugu William Mgimwa
na Manaibu wake Mhe. Janeth Mbene na Mhe. Saada Mkuya
Salum wataweza kukabili changamoto tulizoainisha katika hotuba
yetu na kufanyia kazi mapendekezo ambayo tumeyatoa. Tumeona
dalili za Wizara hii na hasa Waziri na Manaibu wake kusikiliza katika
masuala ya Kikodi hivyo, tuna imani kwamba wataendelea kusikiliza.
Kambi Rasmi ya Upinzani haitasita kutoa ushirikiano kwa lengo la
kuleta maendeleo katika nchi yetu. Hata hivyo, tutakosoa kwa
nguvu zetu zote na kuchukua hatua za kiuwajibikaji dhidi ya njama
zozote za kudhoofisha maendeleo ya Taifa na watu wake. Siku zote
tutasimama upande wa wanyonge na kuwasemea wasio na sauti,
Page 32
32
Watanzania milioni 30 wanaoishi vijijini na kwenye dimbwi la
Umasikini (The Bottom 30M).
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi
Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
……………………………………
Kabwe Zuberi Zitto (Mb)
Waziri Kivuli-Wizara ya Fedha
12.08.2012
KIAMBATANISHO A.
Sheria mbalimbali kuhusiana na fedha haramu
i. the establishment of the Permanent Commission of Inquiry, or
Ombudsman, 1966;
ii. the Foreign Exchange Control Act 1966;
iii. the Anti-Corruption Act 1971;
iv. the establishment of an anti-corruption squad in 1975;
v. the Economic Sabotage Act 1983;
vi. the Economic and Organised Crime Act 1984;
vii. the Proceeds of Crime Act 1991;
viii.the Leadership Code (Declaration of Assets) Act 1995;
ix. the appointment of the Presidential Commission of Inquiry into Corruption,
1996;
x. the BOT Circular to Banking and Non-banking Financial Institutions, No. 8
of 2000, on Money Laundering.

xi. the Drugs and Illicit Traffic of Drugs Act 1995;
xii. the Arms and Ammunition Act 1991;
xiii.the Mutual Assistance in Criminal Matters Act 1991; and
xiv.
the Tanzania Intelligence and Security Act 1998.
xv. The anti-money laundering Act, 2007
xvi.
the anti-money laundering (amendment) act, 2012

1 comment:

Anonymous said...

Kabwe chukua nchi bwana wananchi tule bata