Thursday, August 16, 2012

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA NANE WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, TAREHE 16 AGOSTI 2012, DODOMA


UTANGULIZI

1.            Mheshimiwa Spika, tarehe 12 Juni, 2012 tulianza Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Nane wa Bunge lako Tukufu na leo tunafikia tamati. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa kwa amani na salama. Mkutano huu ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwasilisha, kujadili na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali ikiwa ni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara, Mikoa na Taasisi mbalimbali.

2.            Mheshimiwa Spika, napenda niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kutumia muda wote wa Mkutano huu kwa ufanisi mkubwa kuchangia hoja zinazolenga katika kujenga na kusaidia Taifa letu. Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa mwamko huo mzuri ambao bila kujali itikadi za Vyama umetoa changamoto kwa Serikali katika kutekeleza malengo tuliyojiwekea ili kuleta maendeleo ya Nchi yetu. Ninawashukuru sana kwa michango yenu.

3.            Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano huu tukiwa hapa Bungeni, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walipata Misiba kwa kupotelewa na Wapendwa wao wakiwemo Wazazi, Ndugu, Jamaa na Marafiki. Nitumie nafasi hii kuwapa pole wote waliofikwa na Misiba hiyo. Lakini kipekee kabisa niruhusu nimtaje na kumpa pole Mheshimiwa Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo kwa kumpoteza Mama yake kutokana na ajali ambayo yeye mwenyewe alihusika na hivyo kupata majeraha makubwa. Aidha, nimpe Pole kwa kumpoteza Baba  yake akiwa bado ana Majonzi ya kumpoteza Mama  yake  katika  kipindi   kifupi.  Tunampa  Pole  Sana. Pamoja na ajali aliyoipata Mheshimiwa Selasini, katika siku chache zilizopita tumeshuhudia Ajali za Barabarani zilizosababisha vifo, majeruhi kwa Abiria wa Magari hayo. Watu wengi wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa. Niungane na Watanzania wote kuwapa pole waliopoteza Ndugu, Jamaa na Marafiki katika Ajali hizo.

4.            Mheshimiwa Spika, vilevile, kama ambavyo wote tunakumbuka kuwa mnamo tarehe 18 Julai 2012 tulipata taarifa ya tukio la kusikitisha kuhusu ajali ya kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Meli hiyo ambayo inamilikiwa na Kampuni ya SEAGUL Transport ilikuwa imebeba Watu 290, wakiwemo Watalii na Raia wa Kigeni 16. Katika ajali hiyo Watu 146 waliokolewa kwa msaada wa Vyombo vya uokoaji na waliobaki 144 wanahofiwa kupoteza Maisha wakiwemo Raia Wawili  wa Kigeni.

5.            Nitumie fursa hii ya mwanzo kabisa kuwapa pole Watanzania wote kwa msiba huo mkubwa ambao ulikumba Taifa letu.  Aidha, kwa uzito wa kipekee nawapa pole Ndugu, Jamaa na Marafiki ambao wamepoteza Wapendwa wao katika ajali hiyo. Kwa wale wote waliopoteza maisha, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu ili azilaze Roho zao mahala Pema Peponi. Amina! Vilevile, tunawaombea wote walionusurika katika ajali hiyo kuweza kurejea katika afya zao za kawaida na hivyo kuendelea na ujenzi wa Taifa.

6.            Aidha, napenda kuwashukuru wote walioshiriki katika uokoaji wa ndugu zetu na hivyo kuokoa maisha yao. Nami niungane na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na Viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa walioifanya kuongoza juhudi za uokoaji, huduma zote walizozitoa kwa Majeruhi na Wafiwa. Vilevile, ninamshukuru Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu kwa kukubali mapendekezo ya  Baraza  la  Usalama  la  Taifa la kuunda Kikosi Maalum cha Uokoaji na Usalama Majini, yaani Coastal Guards. Ni dhahiri kuwa Kikosi hiki kitakuwa na faida kubwa katika Usafiri wa Majini na Usalama wake.

7.            Mheshimiwa Spika, matarajio yetu ni kwamba Tume iliyoundwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuchunguza ajali hiyo itatuwezesha  kujua  mazingira yaliyosababisha ajali  hiyo na kwamba tufanye nini ili kuhakikisha Vyombo hivi vinasimamiwa vizuri katika kuzuia ajali hizo zisitokee tena. Tayari Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua za kuzuia matumizi ya Meli za Kampuni hii ambazo hazitakidhi viwango vya usafirishaji  Abiria. Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza taratibu za kununua Meli Mpya ambayo  itabeba  Abiria 1,000 na  kubeba Magari  Mia  Moja. Inatarajiwa kuwa Ujenzi wa Meli hiyo utachukua takriban Mwaka Mmoja kuanzia sasa.

MJADALA WA BAJETI YA SERIKALI 2012/2013

8.            Mheshimiwa Spika, mjadala wa Bajeti ya Serikali tunaohitimisha leo, ulikuwa na hoja nyingi ambazo Waheshimiwa Wabunge walitaka kupata majibu na ufafanuzi. Yapo maeneo ambayo Waheshimiwa Mawaziri walijibu na kutoa maelezo ya ufafanuzi kwa ukamilifu. Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kazi nzuri waliyoifanya hadi kupitishwa kwa Bajeti za Wizara zao. Ninaelewa kwamba zipo Hoja kadhaa zilizotolewa na Waheshimiwa  Wabunge ambazo  Mawaziri hawakupata muda wa  kuzijibu  na  kutoa  ufafanuzi  wa kina kwa sababu ya muda finyu. Aidha, najua  kwamba  kila Waziri aliahidi kujibu kwa Maandishi hoja ambazo hazikupata nafasi ya kujibiwa wakati wa Majumuisho yake. Napenda nami nitumie muda huu wa kujumuisha Hoja hii siku ya leo kwa kutoa maelezo japo kwa kifupi kwa baadhi ya maeneo.  

MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI YA SERIKALI 2012/2013

9.            Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha kwa mwaka 2012/2013 ni jumla ya Shilingi Trilioni 15.12. Kati ya fedha hizo, Fedha za Matumizi ya Kawaida ni Shilingi Trilioni 10.59  na  Fedha  za Matumizi ya Maendeleo ni Shilingi Trilioni 4.5. Aidha, kati ya Shilingi Trilioni 10.59 za Matumizi ya Kawaida, Shilingi  Trilioni  2.75  ni  za  kulipa  Deni  la Taifa, Shilingi Trilioni 3.78 ni za malipo ya Mishahara na Shilingi  Trilioni  4.06,  sawa  na  Asilimia 26.8 tu ya Bajeti yote  ni  kwa Matumizi  Mengineyo (Other Charges-OC). Bajeti hii imeelekeza Rasilimali Fedha kidogo tulizo nazo katika maeneo machache ya kipaumbele ambayo yatatuwezesha kufungulia fursa za Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini kwa kasi zaidi kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.

10.          Kama mtakavyokumbuka, mwaka jana tarehe 8 Juni 2011 tukiwa hapa Dodoma, Mheshimiwa Rais alizindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi 2025. Mwaka wa Kwanza wa utekelezaji wa Mpango huo, (yaani 2011/2012) ulikuwa wa Mpito (Transition) kabla ya kuanza utekelezaji halisi wa Mipango inayofuata ya Miaka Mitano Mitano ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa hadi 2025. Aidha, Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi alisisitiza kuwa, katika Mfumo wa Upangaji Mipango, ni lazima Serikali ianze kuwekeza katika Vipaumbele vichache vitakavyoleta matokeo (impact) makubwa katika Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini.

11.          Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi walipata fursa ya kushiriki kwenye Uzinduzi wa Mpango huo wa Miaka Mitano uliofanyika hapa Dodoma, St. Gaspar. Aidha, Serikali ilipata fursa ya kuwasilisha Mpango huo Bungeni mwezi Juni 2011 katika Mkutano wa Bunge la Bajeti ya mwaka 2011/2012. Wakati wa mjadala Waheshimiwa Wabunge wengi pia walichangia mawazo na kutoa maoni yao kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/2012 ambayo Serikali imeanza kuyazingatia mwaka huu wa Bajeti ya 2012/2013.

12.          Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kurejea Vipaumbele Vitano vilivyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama ifuatavyo:

·                     Kipaumbele cha Kwanza ni kuwekeza kwenye Sekta za Miundombinu hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya Nishati, Usafirishaji, Maji Safi na Maji Taka, Umwagiliaji na TEHAMA;

·                     Kipaumbele cha Pili ni kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa tafsiri pana ambayo inajumuisha Sekta ya Kilimo cha mazao ya chakula na biashara pamoja na Sekta ya Mifugo, Uvuvi, Ufugaji wa Nyuki na Rasilimali za Misitu. Shabaha Kuu ya kuendeleza Kilimo ni kuleta Mapinduzi ya haraka ya Kilimo yatakayotuwezesha kuongeza uzalishaji na tija ili kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje;

·                     Kipaumbele cha Tatu ni kukuza Maendeleo ya Viwanda, hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa Nchini ili kuwezesha kusindika mazao ya Kilimo, Mifugo, Samaki, Misitu na Mazao ya Ufugaji Nyuki, pamoja na kuongeza thamani ya Madini. Aidha, kuvutia uwekezaji kwenye viwanda vikubwa vya mbolea, saruji na viwanda vya kieletroniki kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kikanda hasa Afrika Mashariki;

·                     Kipaumbele cha Nne ni Maendeleo ya Rasilimali Watu na ujuzi, hasa kukuza Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na kuimarisha huduma za Jamii; na

·                     Kipaumbele cha Tano ni kuendeleza huduma za Utalii, Biashara na Huduma za Fedha ambazo ni muhimu katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.

13.          Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wengi na hasa Kamati ya Uchumi na Fedha kwamba usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa Vipaumbele hivi na nidhamu ya matumizi ya fedha zilizoelekezwa kwenye Vipaumbele vilivyowekwa, itakuwa ndiyo nguzo kuu ya mafanikio ya Ukuaji wa Uchumi wetu, ikiwa ni pamoja na kushirikisha Sekta Binafsi na Wananchi wote kwa ujumla.

14.          Mheshimiwa Spika, vilevile, wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013 baadhi ya Waheshimiwa Wabunge walitoa maoni na ushauri wao kuhusu uwiano wa Bajeti ya Serikali iliyowasilishwa ambayo imezingatia kutenga Asilimia 70 ya fedha za Bajeti kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Asilimia 30 kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo, badala ya mgawanyo wenye uwiano wa Asilimia 65 kwa Asilimia 35 katika matumizi hayo. Pamoja na maoni hayo, tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao walielewa vizuri maelezo ya ufafanuzi yaliyotolewa tarehe 22 Juni 2012 na Waziri wa Fedha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kuhusu Mgawanyo huo wa Bajeti. Kwa ujumla, mgawanyo huo umezingatia hali halisi ya Mapato ya Serikali ikilinganishwa na mahitaji makubwa ya fedha kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Serikali, Mfuko Mkuu wa Serikali na Matumizi Mengineyo ambayo yanajumuisha matumizi kwa ajili ya shughuli zisizoweza kuepukika.

15.          Mheshimiwa Spika, matumizi yasiyoweza kuepukika ni kama vile ununuzi wa Dawa na Vifaa vya Tiba; gharama za uendeshaji wa Shule na Mitihani; uendeshaji wa Shughuli za Bunge; Mahakama na Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na kutoa Ruzuku ya Pembejeo za Kilimo. Matumizi hayo yametengewa jumla ya Shilingi Bilioni 2,032.2, sawa na Asilimia 19.3 ya Matumizi Mengineyo (yaani Other Charges-OC) ya jumla ya Shilingi Trilioni 10.59. Kiasi  kinachobakia cha fedha za Matumizi Mengineyo cha Shilingi Bilioni 1,959.5, sawa na Asilimia 18.6 ndicho pekee kitatumika kwa ajili ya kugharamia shughuli zote za uendeshaji wa Serikali nzima pamoja na kutekeleza kazi muhimu zinazoendelea kama vile, kuendesha Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, Vitambulisho vya Taifa na kukidhi mahitaji ya Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya na shughuli nyingine kama hizo.

16.          Aidha, ni  muhimu Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa sehemu ya fedha za Maendeleo ya Rasilimali Watu na huduma za Jamii ambacho ni Kipaumbele cha Nne cha Mpango wa Maendeleo ya Taifa zimewekwa pia katika Matumizi ya Kawaida. Kiasi  kilichotengwa  katika  Bajeti  kwa  ajili  ya  matumizi hayo ni Shilingi Bilioni 841.4. Fedha hizo zikijumuishwa na Shilingi Trilioni 4.5 zilizotengwa kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo, zinafikia jumla ya Shilingi Trilioni 5.3, sawa na Asilimia 35.5 ya Bajeti yote. Hivyo, uwiano halisi wa Bajeti iliyotengwa kwa Miradi ya Maendeleo ni Asilimia 35.5. Serikali itajitahidi kuzingatia ushauri wa kutenga Bajeti kubwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo kwa kadri Mapato ya Serikali yanavyoongezeka na kubana matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.

17.          Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga vizuri kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2012/2013. Serikali itafanya ukaguzi na ufuatiliaji wa karibu wa Miradi ya Maendeleo na tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa kazi zinazofanyika zinawiana na thamani ya fedha zinazotolewa (Value for Money) kwa Miradi ya Maendeleo. Aidha, Tume ya Mipango imepewa jukumu la kuchambua Mipango Kazi ya Miradi ya Maendeleo na kushauri ipasavyo.

18.          Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba malengo ya ukusanyaji Mapato na Matumizi ya Fedha za Serikali yanazingatia Bajeti iliyoidhishwa na Bunge. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imekubali kuwa kila baada ya robo ya mwaka, Baraza  la  Mawaziri  la  Kazi  litakutana na kujadili mwenendo wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (ya Kodi na yasiyo ya Kodi) pamoja na matumizi ya Serikali katika kipindi hicho. Baraza hilo litajadili Mapato na Matumizi ya kila Wizara, kila Mkoa pamoja na Wakala na Idara za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote za Serikali.

19.          Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Watendaji wote wa Serikali katika ngazi zote kuwa na nidhamu katika matumizi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Matumizi ya Serikali pamoja na kuwajibika ipasavyo katika matumizi ya Bajeti tuliyoipitisha.

KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI NA KUDHIBITI MATUMIZI

20.          Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuimarisha Utendaji kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zinazoongoza Utendaji wa Watumishi wa Serikalini. Ili kutekeleza azma hii kikamilifu, Serikali itatumia uzoefu wa Nchi ya Malaysia ambayo imefanikiwa kuweka mfumo madhubuti wa kupima ufanisi wa Utendaji Kazi wa Viongozi na Watendaji wake kwa kutumia Chombo maalum kinachojulikana kwa jina la PEMANDU. Hatua hiyo, itawezesha Serikali kuimarisha utoaji wa huduma nzuri kwa Wananchi pamoja na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali ikijumuisha Mipango ya Maendeleo.

21.          Mheshimiwa Spika, napenda kusisitiza kwamba, Utendaji Kazi mzuri ni pamoja na matumizi bora ya rasilimali chache tulizonazo, kutoa huduma inayotarajiwa na Watanzania. Sote tunaelewa kwamba, mahitaji ya fedha ni makubwa  sana  kulinganisha  na  uwezo  wetu wa sasa. Hata hivyo, kila  mmoja wetu  akiwajibika ipasavyo na kutumia kwa  uangalifu rasilimali hizo bado tunaweza  kufanya mambo makubwa sana. Ni kwa sababu hiyo Serikali imeendelea kusisitiza  kwamba Bajeti tuliyoipitisha hapa inalenga matumizi yatakayotupatia matokeo makubwa na ya haraka. Tutaendelea kubana matumizi yasiyo na tija kama vile Warsha, Semina na Makongamano, Safari zisizo na lazima Ndani na Nje ya Nchi, ununuzi na matumizi ya magari ya kifahari pamoja na matumizi mengine yasiyo ya lazima.

MAANDALIZI YA MSIMU WA KILIMO 2012/2013 NA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO NA ZANA ZA KILIMO

Mbolea

Mheshimiwa Spika, moja ya maeneo ambayo yalikuwa na hoja nyingi katika Mjadala wa Bunge hili la Bajeti ni suala la Kilimo, hususan maandalizi ya Msimu wa Kilimo, upatikanaji wa Pembejeo na Zana za Kilimo. Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) inalenga kuleta mageuzi ya Sekta ya Kilimo, mkazo  wake  mkuu ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa pembejeo na Zana za Kilimo. Napenda kuwahakikishia Watanzania kwamba, katika msimu wa Kilimo 2012/2013, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu kwa mazao mbalimbali kwa utaratibu wa Vocha. Lengo ni kuongeza upatikanaji wa pembejeo na uelewa wa Wakulima kuhusu matumizi ya mbolea na mbegu bora. Kwenye maeneo ya Nchi yenye ukame, ambayo imethibitishwa na Wataalam kwamba matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao (NPS) inafaa kwa uzalishaji wa Mazao ya Alizeti na Mtama, Vocha za Ruzuku zitatolewa kwa ajili ya mazao hayo. Lengo ni kubadilisha mtazamo hasi kuwa mazao haya hayahitaji mbolea pamoja na kuwapunguzia Wakulima gharama kwa sababu bei ya mbolea ya Minjingu Mazao (NPS) ni nafuu ikilinganishwa na mbolea ya DAP. Vilevile, lengo lingine la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ili kupunguza uagizaji wa Mafuta ya Kula kutoka nje pamoja na kukabiliana na upungufu wa chakula katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nawasihi Wakulima kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao (NPS) kwa sababu bei yake ni nafuu, inatengenezwa hapa Nchini na pia ni rafiki wa mazingira.

Mbegu

22.          Mheshimiwa Spika, mahitaji ya mbegu kwa mwaka ni Tani 60,000, lakini mwaka 2011/2012 Tani 28,770 tu zilizalishwa kutoka katika mashamba ya Wakala wa Mbegu wa Taifa,  Mashamba ya  Magereza  na JKT na Sekta Binafsi. Ili kupunguza tatizo hili, Sekta Binafsi imeruhusiwa kupata Mbegu Mama (Breeder Seeds) kutoka Vituo vya Utafiti ili wazalishe Mbegu za Msingi (Foundation Seeds) zitakazotumika kuzalisha Mbegu zilizothibitishwa (Certified Seeds). Serikali itahakikisha kwamba Mbegu bora zinapatikana kwa wakati ili ziweze kuwafikia Wakulima kabla ya kuanza kwa Msimu wa Kilimo.

Zana za Kilimo

23.          Mheshimiwa Spika, Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilielezea kwa kina jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya Zana Bora za Kilimo ili kuongeza tija na kupunguza Sulubu ya kazi za kutumia Jembe la Mkono. Matumizi ya Matrekta Makubwa na Madogo yaliyoingizwa Nchini na SUMA JKT yameongezeka na hivyo kuongeza eneo linalolimwa kutoka Asilimia 12 mwaka 2010 hadi Asilimia 14 mwaka 2011. Nitumie nafasi hii kuwahimiza Wananchi kwamba Matrekta ya SUMA JKT aina ya Farmtrac 2; Wheel Drive yapatayo 547 bado yapo.  Ninazo taarifa kwamba  Matrekta ya New Holland na Farmtrac 4 Wheel Drive yameisha, lakini bado mahitaji ni makubwa. Serikali inafanya Mpango wa kuagiza Matrekta hayo na tayari kuna Mpango wa kupata Mkopo wa Matrekta 3,000 kupitia Makubaliano kati ya  Serikali ya Tanzania na Serikali ya India. Aidha, bei za Matrekta ya SUMA JKT zimepunguzwa na muda wa marejesho ya Mkopo wa Matrekta hayo kwa Wananchi umeongezwa. Nawasihi Wananchi kujiunga katika Vikundi vya kuwawezesha kukopa Matrekta hayo.

24.          Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tu nilifanya Uzinduzi wa Matrekta 50 ili yakopeshwe kwa Wakulima wa Mkoa wa Ruvuma. Alichokifanya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ni kuchukua jukumu la kuratibu zoezi zima la ukopeshaji wa Matrekta hayo kwa Wakulima katika Mkoa wake. Yeye akawa kama Focal Person wa kukusanya fedha zinazohitajika na kuhakikisha upatikanaji wa Matrekta hayo kwa Wakulima wake. Nitumie mfano huu mzuri kuwaomba Viongozi wote katika ngazi za Mikoa na Wilaya kuweka nguvu za ziada wasaidie katika kufanikisha upatikanaji wa Matrekta hayo katika maeneo yao. Halmashauri zijipange kuhakikisha kwamba fursa iliyotolewa ya kupunguza bei ya Matrekta ya SUMA JKT na fursa ya Asilimia 10 ya malipo ya awali inatumika vizuri. Kipaumbele kiwe kwenye SACCOS, hasa za Vijana.

Hali ya Chakula Nchini

25.          Mheshimiwa Spika, hali ya chakula Nchini ni ya kuridhisha. Takwimu za tathmini ya awali za mwezi Juni 2012 kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na utabiri wa hali ya chakula kwa 2012/2013 zinaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula utafikia Tani 13,572,804 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula yanayokadiriwa kuwa Tani Milioni 11.99. Taifa linatarajia kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 113 na hivyo kuwa na ziada ya Tani Milioni 1.58. Matarajio ni kwamba kwa maeneo yenye kuonesha upungufu wa chakula utaratibu utafanywa wa kupata mahindi toka katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA).

26.          Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ya kuridhisha, tathmini ya mwezi Juni 2012 inaonesha kuwa bado kutakuwepo na uhaba wa chakula katika Mikoa Sita (6) ya Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga na Tabora. Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 2012/2013 Serikali itawezesha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kununua Tani 200,000 za nafaka kutoka kwa Wakulima wa Mikoa iliyozalisha ziada ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma. Aidha, Serikali itahamisha Tani 100,000 za akiba ya Nafaka iliyopo katika Maghala yenye ziada ya chakula kwenda kwenye Maghala ya Mikoa yenye upungufu wa chakula. Zoezi la kuhamisha Mahindi hayo kwenda Dar es Salaam limeanza. Hatua hii pia itatoa nafasi ya kuhifadhi nafaka zitakazonunuliwa Msimu wa Ununuzi wa 2012/2013.

Bajeti ya Kilimo kuwa Asilimia 10

27.          Mheshimiwa Spika, katika Mkutano wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Maputo, Msumbiji mwezi Julai 2003, moja ya makubaliano ya Kikao hicho ni agizo la Nchi zote za Umoja huo kuhakikisha kuwa Bajeti zao za Kilimo zinafikia Asilimia 10 ya Bajeti ya Taifa baada ya kipindi cha miaka Mitano. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, makubaliano hayo tunayatekeleza kwa kadri ya uwezo wetu na fedha zinazotengwa kwa ajili ya Kilimo zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 233.3 mwaka 2005/2006, sawa na Asilimia 5.6 hadi kufikia Shilingi Bilioni 926.2 mwaka 2011/2012, sawa na Asilimia 8. Katika mwaka huu wa fedha 2012/2013, fedha zilizotengwa ni Shilingi Bilioni 1,103.6, sawa na Asilimia 9.0. Ni matumaini yangu kwamba kwa mwelekeo huu tutaweza kufikia Asilimia 10 kama tulivyokubaliana katika Nchi za Umoja wa Afrika muda wowote kuanzia mwaka ujao wa fedha.




MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI

Kuboresha Ufugaji wa Kuku ili Kuondoa Umaskini

28.          Mheshimiwa Spika, ufugaji wa Kuku wa Asili unayo nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa Wananchi waishio Vijijini, kuboresha lishe na kipato chao. Takwimu zinaonesha kuwa Ufugaji wa Kuku wa Asili huchangia Asilimia 94 ya Kuku wote Nchini. Aidha, unachangia Asilimia 80 ya nyama na mayai yanayoliwa Vijijini na Asilimia 20 ya Mijini. Hata hivyo, Sekta hii bado inakabiliwa na changamoto nyingi hususan, vifo vya Kuku vinavyosababishwa na magonjwa hasa ya mdondo (Newcastle Disease).  Changamoto nyingine ni uhaba wa Maafisa Ugani, ukosefu wa taarifa za masoko na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha Miradi endelevu ya Ufugaji Kuku.

29.          Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha ufugaji wa Kuku wa Asili ikiwa ni pamoja na kutengenezwa kwa Chanjo ya Kupunguza Vifo vya Kuku kutokana na Ugonjwa wa Mdondo. Chanjo ya kuzuia Mdondo wa Kuku (Newcastle Disease Vaccine) iligunduliwa Nchini Australia na kufanyiwa majaribio hapa Nchini. Serikali inaagiza mbegu kutoka Australia na kutumia teknolojia hiyo kutengeneza Chanjo hiyo hapa Nchini kupitia Maabara Kuu ya Temeke. Chanjo hii imefanya vizuri sana na katika baadhi ya Vijiji katika Mkoa wa Singida na imepunguza vifo dhidi ya Mdondo wa Kuku kwa Asilimia 96 hadi Asilimia 100.

30.          Mheshimiwa Spika, Shirika la Research Into Use (RIU) linaloongozwa na Timu ya Wataalam ambao ni Vijana wetu waliosoma Chuo Kikuu cha Sokoine, Morogoro wameanzisha Mradi wa  Kuendeleza  Kuku  wa  Asili.  Mradi huu ulizinduliwa Mwezi Machi mwaka huu 2012. Mradi wa RIU, umeonesha kuwa Kuku wa Asili wanaweza kufugwa kibiashara. Mradi huo ambao unatekelezwa katika Mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani umewezesha Wafugaji wa Kuku wa Asili wapatao 3,500 kuongeza idadi ya Kuku wanaofugwa katika Kaya kutoka 5 hadi 10 na kufikia  kati  ya 100 hadi 300. Mafanikio haya yametokana na Wafugaji kuwezeshwa kupata mafunzo, mitaji, masoko na kuwaunganisha na Wadau wengine hususan wauzaji wa Dawa za Tiba ya Kuku.

31.          Kutokana na mafanikio yaliyoonekana katika Mradi huo, Serikali itaendelea kuwasaidia Wananchi na Wafugaji wa Kuku hapa Nchini kuendeleza Ufugaji wa Kuku wa Asili ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo na kuajiri Maafisa Ugani wa kutosha wa Kuku Asili. Vilevile, Serikali itahimiza Mpango wa kuanzisha Mashamba Darasa ya Ufugaji Bora wa Kuku ambao utawezesha  kutoa  elimu  kwa  Wafugaji  wengi  zaidi. Natoa wito kwa Halmashauri za Wilaya kutoa kipaumbele katika kuhamasisha Wananchi kuanza Ufugaji wa Kuku wa Asili ambao umeonesha kuwa na mafanikio na manufaa makubwa ya kuondoa umaskini.

Maendeleo ya Ufugaji Nyuki

32.          Mheshimiwa Spika, kama ambavyo mtakumbuka katika Mikutano kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu nimekuwa nikisisitiza fursa ya kipekee tuliyonayo ya  kufanya Ufugaji Nyuki  ambao  una  faida  kubwa  kiuchumi na katika kuondoa umaskini. Gharama  za Ufugaji  Nyuki ni nafuu sana  ikilinganishwa   na  aina  nyingine yoyote ya Ufugaji. Kutokana na ukweli huo Wananchi wameanza kuhamasika katika maeneo mengi Nchini kuhusu Ufugaji Nyuki. Aidha, Wawekezaji wameanza kuwekeza baada ya kujiridhisha kwamba Ufugaji wa Nyuki katika Nchi yetu una faida na manufaa makubwa.

33.          Mheshimiwa Spika, mwanzoni mwa mwezi Juni 2012 niliweza  kufungua  Kiwanda  kipya  cha kisasa  cha  kuchakata Asali pale Visiga, Kibaha. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuchakata  Tani 10,000 za Asali kwa mwaka. Aidha, vipo pia Viwanda vingine Saba (7) Nchini. Takwimu za mwaka 2011/2012 zinaonesha Uzalishaji wa Asali ulifikia Tani 9,000 zenye thamani  ya  Shilingi  Bilioni  27  na  Nta Tani  600  zenye thamani ya Shilingi Bilioni tatu (3).  Hii ni ishara nzuri ya kwamba Soko la Asali lipo na Asali ni zao muhimu la kuongeza Kipato cha Wananchi. Napenda kutumia nafasi hii tena kuwahimiza Wananchi kutumia fursa hii kwa kuzalisha mazao ya Nyuki kwa wingi, kwani Soko la Asali na Nta lipo tayari.

UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI

34.          Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji, Waheshimiwa Wabunge wengi walionesha kutoridhishwa na hali ya upatikanaji wa Maji katika maeneo mbalimbali Nchini. Maeneo mengi ya Nchini yameendelea kuwa na uhaba wa maji kutokana na uharibifu wa vyanzo vya  maji, ongezeko la watu, ukame unaotokana na athari  za  mabadiliko  ya Tabianchi  na   matumizi  ya  maji yasiyozingatia tija na ufanisi. Aidha, tatizo la Maji limechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii zisizowiana na uwekezaji katika miundombinu ya maji.

35.          Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na Tatizo la Maji Nchini, Serikali inatekeleza Miradi mbalimbali kwa kutumia fedha za ndani na fedha za nje kupitia kwa Wafadhili na Wadau wa Maendeleo. Iko Miradi ya Maji inayoendelea kutekelezwa katika Halmalshauri mbalimbali Nchini kwenye Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Kagera, Katavi, Kigoma na Kilimanjaro. Miradi hiyo iko pia katika Mikoa ya Manyara, Mtwara, Mwanza, Shinyanga na Tabora.

36.          Mheshimiwa Spika, niruhusu nitumie muda mfupi kuelezea Miradi michache inayotekelezwa na Serikali kama njia ya kukabiliana na tatizo hili. Kwa mfano, tarehe 21 Julai 2012 Serikali ya Tanzania imesaini Mkataba na Umoja wa Nchi za Ulaya wenye thamani ya Euro Milioni 51.51 kwa ajili ya Miradi ya Majisafi na Mazingira katika Mikoa ya Lindi, Kigoma, Babati, Mtwara na Rukwa. Aidha, Serikali ya Ujerumani imetenga Euro Milioni 20 kwa ajili ya Mikoa ya Lindi, Kigoma na Rukwa. Majadiliano ya kusaini Mkataba huu na Wafadhili yanaendelea. Halmashauri zimeendelea kutekeleza Miradi ya Maji katika Vijiji 10 ambapo hadi Julai 2012,  Halmashauri  67 zimepata  vibali vya kuanza Ujenzi wa Miundombinu ya Maji. Miradi hii inafadhiliwa chini ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Kiarabu, Serikali za Uholanzi, Ufaransa, Korea Kusini na Ubelgiji. Tayari fedha zimekwishatolewa kwa ajili ya Vijiji ambapo utekelezaji utafanyika kufikia Wastani wa Vijiji Vitano (5) kwa kila Halmashauri.

37.          Mheshimiwa Spika, katika Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria, Serikali ililenga kufikisha maji katika Miji ya Kahama na Shinyanga pamoja na Vijiji vyote vilivyopo kandokando ya Bomba Kuu la kusafirishia Maji umbali usiozidi Km 5. Jumla ya Vijiji 54 vilihusika na kati ya hivyo 39 vilianza kupata huduma ya maji tangu uendeshaji wa Mradi ulipoanza mwezi Februari 2009. Vijiji hivyo vyote vipo katika Mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Katika Awamu ya Pili ya Mradi, Vijiji vyote vilivyopo umbali wa Km 12 kutoka kwenye Bomba Kuu katika Wilaya za Misungwi, Kwimba, Shinyanga na Kahama vitaunganishwa, Vijiji hivyo tayari vimetambuliwa. Tayari Serikali imepeleka kiasi cha Shilingi Milioni 304.5 katika Mradi huu.

38.          Mheshimiwa Spika, Mradi wa ujenzi wa Bwawa la Kawa, katika  Wilaya ya Nkasi  unaendelea  kukamilishwa. Mradi huu unahusu Usanifu wa miundombinu ya usambazaji maji kutoka kwenye Bwawa la Kawa kwenda kwenye Vijiji vya Nkundi, Fyengerezya na Kalundi. Uandaaji wa Makabrasha ya Zabuni kwa ajili ya kupata Mkandarasi wa kujenga miundombinu ya maji umeanza na ujenzi utaanza mara baada ya kupata Mkandarasi. Kiasi cha Shilingi Milioni 300 kimetengwa katika mwaka 2012/2013 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji.
39.           Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2007/2008 hadi 2011/2012, Serikali ilifanya maamuzi ya kutumia Shilingi Milioni 95.9 kwa ajili ya ukarabati wa Bwawa la Mfili na Bomba Kuu la kutoka Mfili hadi kwenye matanki pamoja na upanuzi wa Mtandao wa Maji Safi kwa Mji wa Namanyere. Mwaka 2012/2013 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 2.1 ili kutekeleza hatua za dharura kuupatia Mji huo maji kwa kuboresha huduma ya maji. Aidha, tarehe 23 Septemba 2011 Serikali ilisaini Mkataba na BADEA kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Majisafi kwa Mji wa Orkesumet katika Wilaya ya Simanjiro. Hadi sasa, majina ya Wahandisi Washauri watakaofanya mapitio ya usanifu na kusimamia ujenzi yamepitishwa na Wizara; na BADEA imekwisha idhinisha majina hayo kwa hatua zaidi. Mtaalamu Mshauri anatarajiwa kuanza kazi mwaka 2012/2013.

40.          Mheshimiwa Spika, ni hivi karibuni tu tarehe 22 Julai 2012 Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alizindua Mradi Mkubwa wa Maji Safi katika Jiji la Mbeya uliotekelezwa chini ya Programu ya Regional Centres uliofadhiliwa na Mfuko wa pamoja wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Jumuiya ya Ulaya, na Serikali ya Ujerumani. Kukamilika kwa Mradi huu ambao uligharimu takriban Shilingi Bilioni 80 umeongeza huduma za Maji kutoka Mita za Ujazo 32,000 kwa siku hadi Mita za Ujazo 49,000 kwa siku kwa Wakazi wa Jiji la Mbeya. Lengo ni kufikia Mahitaji ya Jiji hili kwa Asilimia 100 ifikapo mwaka 2017.

41.          Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kwamba Miradi yote ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji Nchini itaendelea kupewa Kipaumbele na Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi hadi yote ikamilike.

Mradi wa Maji wa Ntomoko Wilayani Kondoa

42.          Mheshimiwa Spika, mnamo tarehe 12 Agosti, 2012 nilipata fursa ya kutembelea  mradi wa maji wa Ntomoko  uliopo  Wilayani Kondoa.  Mradi huu ulibuniwa  na Serikali chini ya Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere ili kutoa huduma kwa watu wapatao 23,400 katika Vijiji 17 vilivyoko katika Uwanda kame wa Goima (The Goima Difficult Zone) ambao una tatizo kubwa la kupata maji. Vijiji hivyo haviwezi kupata maji  kupitia visima virefu kutokana na asili ya Tabaka la miamba iliyopo katika Ukanda huo.

43.           Mheshimiwa Spika, Changamoto kubwa zilizopo katika mradi huo, ni pamoja na uchakavu wa Miundombinu na huduma ya maji na ongezeko la mahitaji ya maji linatokana na ongezeko kubwa la Watu ambalo sasa linafikia watu wapatao 55,397. Chanzo cha Maji katika Mradi huu ni Chemchem ya  Ntomoko ambayo ina uwezo wa kuzalisha maji wastani wa lita 689,000 kwa siku. Hata hivyo, kwa sasa mahitaji halisi ya Maji katika Vijiji 17 ni Lita za Ujazo zipatazo 1,464,000 siku. Uchakavu wa Miundombinu ya Mradi umesababisha Vijiji vinavyopata maji kupungua kutoka 17 mwaka 1973 hadi Vijiji Vitano (5) kwa sasa.

44.          Mheshimiwa Spika, ili kuondoa changamoto mbalimbali za Mradi huu, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali itaongeza kiasi cha Shilingi Bilioni 2.3 katika Fedha iliyotengwa kwa Mradi huo na Halmashauri za Wilaya ya Kondoa na Chemba ambazo zimetenga Shilingi Milioni 90. Lengo ni kuhakikisha kuwa Mradi huo unafufuliwa na  kurudisha huduma ya maji kwa Wananchi.  Aidha, Serikali itaendelea na Juhudi za kufufua Miradi ya namna hii ya maji ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata huduma ya maji. Aidha, katika kuhakikisha kuwa chanzo hiki kinalindwa, niliwaelekeza Viongozi wa Wilaya ya Kondoa na Mkoa wa Dodoma kuhakikisha kuwa Wanakijiji cha Mafai ambako ndiko iliko Chemchem ya Ntomoko, wanapata maji kutoka kwenye Chanzo hicho.


USAFIRI  WA  BARABARA  NA  KUKABILIANA  NA MSONGAMANO  WA  MAGARI  MIJINI

45.          Mheshimiwa Spika, wakati wa kujadili Bajeti za Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi, masuala mengi yaliyojitokeza katika mijadala hiyo yalihusu namna ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta Ndogo ya Usafiri wa Barabara.  Changamoto hizo ni pamoja na kutounganika kwa Mtandao wa Barabara na maeneo ya uzalishaji Vijijini pamoja na masoko, msongamano wa magari Mijini na mpangilio usio mzuri wa Miji yetu, uhaba wa fedha za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, uchakavu na uchache wa mitaro ya kuondoa maji ya mvua katika barabara zetu, uhaba wa Watalam na uwezo mdogo wa Makandarasi wa barabara na mfumo dhaifu wa kitaasisi wa kuhudumia barabara za Wilaya na Vijiji.

46.           Mheshimiwa Spika, vilevile, wakati wa kuhitimisha Hoja za Bajeti kuhusu Sekta Ndogo ya Usafiri wa Barabara, Mawaziri wa Sekta hizo walieleza mikakati ya kupunguza changamoto hizo kwa Awamu kwa kuanzia na Bajeti ya mwaka 2012/2013. Barabara zilizopewa kipaumbele katika Bajeti hizo ni zile zenye kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo ya uzalishaji,  kupunguza  msongamano  katika  Miji  hasa  Jiji  la Dar es Salaam,  kuunganisha Nchi yetu na Nchi jirani na kuendelea kutekeleza Programu kuhusu Uwekezaji katika Miundombinu ya Uchukuzi kwa mwaka 2007 hadi 2017. Katika Programu hii, Miradi 16 ya ujenzi wa barabara kuu za lami iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tatu na kuendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nne, ilikamilika kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2005 na 2010. Barabara zilizokamilika katika kipindi hicho zina urefu wa jumla ya Kilometa 1,236.

47.          Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2005 hadi 2012, Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Miradi Mipya 78 ya Ujenzi na Ukarabati wa Barabara zenye urefu wa jumla ya Kilometa 4,176. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 17 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 662.2 imekamilika kwa Asilimia 100 kufikia mwezi Juni 2012  na  mingine  61  ipo  katika  hatua  mbalimbali  za ujenzi. Sambamba na ujenzi unaoendelea katika Miradi hiyo, kuna Miradi mingine 43 iliyobuniwa katika Awamu ya Nne yenye urefu wa jumla ya Kilometa 5,739 ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 16 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 3,817, ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa Usanifu, na Miradi 27 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 1,921 usanifu wake umekamilika na inatafutiwa Makandarasi. Lengo ni kuunganisha kwa awamu Miji Mikuu ya Mikoa yote Nchini kwa barabara za lami ifikapo mwaka 2017/2018.

Kuondoa Msongamano wa Magari katika Jiji la Dar es Salaam

48.          Mheshimiwa Spika, tatizo la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam linaathiri Wananchi wengi. Waheshimiwa Wabunge wengi, hasa wale wa Mkoa wa Dar es Salaam walielezea kwa uchungu tatizo hili. Serikali kupitia Wizara husika imeeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa ili kukabiliana na Msongamano kuwa ni pamoja na kuanzisha Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka, ujenzi wa Barabara za Mzunguko (ring roads), Barabara za Mlisho (feeder roads), Barabara za Juu (flyovers) na kuanzisha huduma za Usafiri wa Reli na vivuko Jijini Dar es Salaam.

Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART)

49.          Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART). Lengo ni kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuwa na Mtandao wa Usafiri wa Mabasi makubwa yatakayopita katika njia Maalum na hivyo kuwahakikishia Wananchi huduma bora za usafiri Jijini. Mradi huo pia utasaidia kupunguza msongamano unaotokana na wingi wa mabasi madogo ya Daladala katika barabara za Jiji.

50.          Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Mwaka 2012/2013 itatumika zaidi katika utekelezaji wa Miradi ya Awamu ya Kwanza na kuanza maandalizi ya Miradi itakayotekelezwa katika Awamu ya Pili na ya Tatu. Awamu ya Kwanza ina Miradi Saba (7) ambayo Mikataba ya Ujenzi ilisainiwa katika vipindi tofauti kuanzia mwezi Mei 2010 hadi mwezi Machi 2012. Miradi yote hii itakamilika katika vipindi tofauti, kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.

Ujenzi wa Barabara Mbalimbali, Madaraja na Barabara za Juu (flyovers)

51.          Mheshimiwa Spika, pamoja na Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi, katika Bajeti Wizara ya ujenzi ya mwaka 2012/2013, Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) unatekeleza Miradi 14 itakayogharimu Shilingi Bilioni 580 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zitakazopunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam. Miradi hiyo inahusu ujenzi wa Barabara Kuu za njia nne, Barabara za Mzunguko (ring roads), Barabara  za  Mlisho (feeder roads)  barabara  ya  kupita  juu  (flyover)  kwenye Makutano ya  TAZARA, Daraja  la  Kigamboni  na  Gati za Vivuko. Miradi hii itakapokamilika itatoa mchango mkubwa katika kupunguza msongamano uliopo hivi sasa.

Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania

52.          Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Julai 2012 nilikagua utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji  wa Miundombinu na Utoaji wa Huduma za Jamii  (Tanzania Strategic Cities Project) unaotekelezwa na Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu (CDA) na Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Mradi huu unatekelezwa pia katika Halmashauri nyingine saba Nchini kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali ya Denmark.

53.           Mheshimiwa Spika, katika ziara hiyo nilibaini kwamba ili Miradi hii itekelezwe kwa kasi iliyokusudiwa, kuna umuhimu mkubwa kwa Wadau wanaoguswa na utekelezaji wakiwemo TANESCO na Mamlaka za Maji, kukutana mara kwa mara ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyoathiri utekelezaji wa Mradi. Halmashauri nyingine ambako Mradi huu unatekelezwa ni Majiji ya Mwanza, Tanga na Mbeya na Arusha  na  Manispaa  za  Kigoma Ujiji  na Mtwara  Mikindani. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa Kilometa 141, ujenzi wa Madampo ya Taka Ngumu, Vituo vya Mabasi na Mitaro ya Maji Machafu. Mradi huu pia unajumuisha kipengele cha kujenga uwezo wa Halmashauri hizo katika usimamizi na uendelezaji Miji, usimamizi na utunzaji mali za Miji, usimamizi wa taka ngumu Mijini na uboreshaji wa Mfumo wa kukusanya mapato ya ndani na upangaji Miji kimkakati. Nitumie fursa hii kuagiza Vikao vya Kamati za Mashauriano za Mikoa husika kujadili taarifa za utekelezaji wa Miradi hii kila vinapokaa ili matatizo yatakayobainika ya kiutekelezaji yaweze kupatiwa ufumbuzi wa pamoja haraka.

54.          Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea na maandalizi ya Mradi mwingine utakaogharimu Dola za Marekani Milioni 255, utakaoanza kutekelezwa mwaka 2013/2014. Mradi huu utahusu uimarishaji wa  Serikali za Mitaa zikiwemo Manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa 11 za Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida, Musoma, Iringa, Bukoba na Lindi  na Miji ya Mpanda, Njombe, Babati, Geita, Korogwe, Bariadi  na Kibaha. Kutekelezwa kwa Miradi hii kutaboresha hali ya Miji yetu pamoja na huduma zitolewazo na hivyo kuondokana na vikwazo vya usafiri na usafirishaji vilivyopo katika Miji hiyo likiwemo suala la kuondoa misongamano ya magari kwa baadhi ya Miji.



UKUSANYAJI WA MAONI KUHUSU KATIBA MPYA

55.           Mheshimiwa Spika, wakati nikiwasilisha Bajeti yangu nilielezea hatua iliyofikiwa katika Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na kwamba Mheshimiwa Rais alikwishateua Tume na tayari Tume hiyo ilianza kazi tarehe 1 Mei, 2012. Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati akiwasilisha Bajeti yake alifafanua kwa kina Muundo na Majukumu ya Tume na utaratibu wa jinsi kazi ya kukusanya Maoni itakavyofanyika.

56.          Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kazi ya kukusanya Maoni inaendelea vizuri. Hadi sasa Wajumbe wa Tume wamekwisha kamilisha kukusanya maoni katika Mikoa minane, ambayo ni Tanga, Pwani, Dodoma, Shinyanga, Kagera, Manyara, Kusini Unguja na Kusini Pemba. Awamu ya Pili inaendelea na Wajumbe hivi sasa wanakusanya maoni katika Mikoa ya Lindi, Morogoro, Mbeya, Ruvuma, Katavi, Kigoma na Mwanza. Nachukua fursa hii kuwapongeza Wananchi kwa kutoa Maoni yao kwa amani na utulivu na bila woga.

57.          Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha kazi za Awamu ya Kwanza, katika Awamu ya Pili, Tume itaandaa utaratibu wa kukusanya maoni ya Wananchi kupitia Mabaraza ya Katiba katika ngazi mbalimbali. Mabaraza hayo yatawashirikisha Wawakilishi kutoka makundi mbalimbali katika Jamii.

58.          Mheshimiwa Spika, ninaelewa zipo changamoto zilizojitokeza kutokana na Jiografia ya Nchi yetu, hususan ukubwa wake hivyo kuwa na uwezekano wa baadhi ya Wananchi wasifikiwe na Tume kwa karibu. Kutokana na changamoto hizo, Tume imeweka taratibu nyingine zitakazowezesha Wananchi kutoa maoni kwa njia ya barua, tovuti na mitandao ya kijamii. Nawashauri Wananchi watumie njia hizo bila kusita ili kuwasilisha maoni yao kwenye Tume. Aidha, tatizo la usambazaji wa Nyaraka kwa wakati nalo linafanyiwa kazi ili nyaraka hizo zisambazwe kwa kasi zaidi.

59.          Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa Wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume pindi watakapofika katika maeneo yao kwa lengo la kupata maoni. Suala la kutoa maoni ni wajibu wetu sote. Katiba nzuri itatokana na maoni ya Wananchi wenyewe. Hii ni fursa pekee kwa Watanzania, hivyo hatuna budi kuitumia kikamilifu.
UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA

60.          Mheshimiwa Spika, tarehe 16 Aprili, 2011 wakati nikihitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge lako Tukufu nilizungumzia hali ya Magonjwa Makuu Nchini. Nilibainisha maradhi makubwa ambayo yamepewa msukumo mkubwa na Serikali katika kuyatokomeza. Magonjwa hayo ni Malaria, Kifua Kikuu, Shinikizo la Damu, Kisukari, Saratani na UKIMWI. Hata hivyo, ilibainika kwamba Magonjwa ya Shinikizo la Damu, Kisukari na Saratani hayajapata msukumo mkubwa unaostahili pamoja na kwamba yamekuwa yakisababisha vifo vingi Nchini. Niruhusu nieleze kwa mara nyingine kwa ufupi kuhusu Ugonjwa wa Saratani, hususan Saratani ya Tezi ya Kibofu cha Mkojo (Prostate Cancer) ambao unawapata Wanaume zaidi.

61.          Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Saratani Duniani (The World Cancer Report) za miaka mbalimbali zinaonesha kuwa Wanaume wawili Duniani wanahitaji kupata matibabu ya Saratani ya Tezi  la Kibofu cha  Mkojo kila dakika tano. Aidha, ukubwa wa tatizo la Ugonjwa huu umekuwa ukiongezeka kwa kasi na sasa unawapata Wanaume wenye umri wa kuanzia Miaka 45 na kuendelea badala ya Miaka 50 ya Awali hivyo, kupanua wigo wa uwezekano wa Watu wengi zaidi kupata ugonjwa huo.  Dalili za Ugonjwa huu katika hatua za mwanzo kabisa ni pamoja na kushindwa kupata haja ndogo vizuri, kupata haja ndogo mara nyingi kuliko kawaida, na kuanza kukojoa damu, au haja ndogo kushindwa kutoka kabisa. Aidha, Vimelea vinapoanza kusambaa, mgonjwa anaanza kupata maumivu ya mgongo, kuvimba miguu, na baadaye figo kushindwa kufanya kazi. Kutokana na hali hiyo, upo umuhimu wa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kuhusu ugonjwa huu na kuhamasisha  Wananchi  waweze  kupima afya  zao  mapema.

62.           Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba Wanaume wote wenye umri unaofika miaka 45 na kuendelea kujenga utamaduni wa kupima afya zao mapema ili kubaini hali ilivyo kuhusu ugonjwa huu wa Saratani ya Tezi la Kibofu cha Mkojo kwa sababu ugonjwa huu unatibika kama ukibainika mapema. Kwa misingi hiyo, napenda kuiagiza Wizara ya Afya kuweka utaratibu maalum wa kuelimisha Wananchi kuhusu  ugonjwa  huu wa Tezi la Kibofu cha Mkojo. 

Bajeti ya Afya kuwa Asilimia 15

63.          Mheshimiwa Spika, katika Mkutano kati ya Mawaziri wa Fedha  na  Mawaziri  wa  Afya wa Afrika ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika  kwa  kushirikiana  na  Shirika la Harmonization  for  Health in Africa (HHA) uliofanyika Nchini Tunisia tarehe 03  hadi 06 Julai 2012, suala kubwa lililojadiliwa lilikuwa  ni kuendelea kusisitiza Serikali  za Nchi za   Afrika   kutenga  fedha   zaidi   kwenye   Sekta  ya   Afya. Lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa, Wananchi wanakuwa na Afya nzuri kwa ukuaji wa uchumi wa Nchi zetu. Mkutano huo ulipendekeza angalau Asilimia 15 ya Bajeti ya Serikali za Nchi za Afrika iende kwenye Sekta ya Afya. Michango mingi iliyotolewa katika Mkutano huo ilithibitisha kwamba, Uchumi wa Nchi za Afrika hauwezi kukua na kuwa endelevu kama Nchi hizi hazina Wananchi wanaopata huduma nzuri za Afya.

64.          Mheshimiwa Spika, licha ya ufinyu wa Bajeti, Serikali imedhamiria kadri ya uwezo wetu kufikia lengo hilo kama ilivyopendekezwa. Fedha zinazotengwa kwa ajili ya Afya zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa maana hiyo, kiasi kilichotengwa kimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 365.8 sawa na Asilimia 8.8 mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Bilioni 1,288.8 sawa na Asilimia 10.0 mwaka 2012/2013. Ni matumaini yangu kwamba, kwa mwelekeo huo Serikali inaamini tutaweza kufikia Asilimia 15 kama tulivyokubaliana katika Mkutano huo. Aidha, ongezeko hilo linaonesha jinsi Serikali ilivyoamua kuwekeza katika Sekta hii muhimu ya Afya kwa manufaa ya Wananchi wake.

AJIRA KWA VIJANA

65.          Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto zinazokabili Taifa letu ni kiwango cha juu cha ukosefu wa Ajira hasa kwa Vijana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla ya Vijana wasio na Ajira hapa Nchini ni Milioni 1.4, sawa na Asilimia 13.4 ya nguvu kazi yote ya Vijana. Kuongezeka kwa kasi kwa ukosefu wa Ajira kwa Vijana kunachangiwa na mambo kadhaa, ikiwemo uwekezaji mdogo wa ndani na nje, kasi ndogo ya ukuaji wa Sekta Binafsi Nchini na ukosefu wa elimu ya ujasiriamali kwa Vijana wengi. Aidha, ukosefu wa Ajira pia unasababishwa na baadhi ya Vijana kuchagua kazi za kuajiriwa, badala ya kujiajiri wenyewe hasa kwenye Sekta zenye fursa kubwa kama vile Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Ufugaji Nyuki.

66.          Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali walipata fursa ya kutoa michango mizuri ya mawazo inayoelezea ukubwa  wa  tatizo  la  Ajira Nchini, na namna ya kulipatia ufumbuzi. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi waliafikiana na Serikali kwamba changamoto ya upatikanaji wa Ajira nyingi kwa Vijana inahitaji ushirikiano wa Wadau wengi. Ni dhahiri kuwa, juhudi za pamoja zinahitajika baina ya Serikali, Sekta Binafsi, Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Taasisi Zisizo za Kiserikali na Jamii kwa ujumla kukabiliana na changamoto hii. Kwa upande wake, Serikali ina wajibu mkubwa wa kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza Uwekezaji na ukuaji wa Sekta Binafsi ili kuongeza fursa nyingi za upatikanaji wa Ajira. Hii ni pamoja na kubuni na kuandaa Sera na Sheria Wezeshi za Uwekezaji, uzalishaji na kufanya biashara. Vilevile, kuhakikisha kwamba kuna miundombinu muhimu ya usafirishaji, umeme wa kutosha, maeneo ya kuwekeza na kuzalisha pamoja na Mfumo bora wa elimu utakaowezesha wahitimu wengi kujiajiri na kushindana katika Soko la Ajira.

67.          Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za kuvutia uwekezaji, Serikali inaimarisha Mifuko mbalimbali ya kuwawezesha Vijana ili waweze kujiajiri wenyewe. Kwa mfano, Mfuko wa Dhamana chini ya Programu ya Taifa ya Kuwezesha Wananchi Kiuchumi, (Maarufu kama Fedha za JK); Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unaosimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mfuko wa Wajasiliamali Wadogo unaosimamiwa na SIDO; na Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) vimeimarishwa na kuwekewa mazingira mazuri ya kuviwezesha kufanya kazi kibiashara na kwa ufanisi. Ni matumaini yangu kwamba tukitumia Mifuko hii vizuri tutaweza kuongeza Ajira kwa Vijana kwa kasi zaidi.  Nasisitiza pia kuwa, ni muhimu kwa vijana wetu na wale wote wanaopata ajira au kujiajiri wenyewe wawe na nidhamu kazini, wafanye kazi kwa weledi na kutumia utaalam wao vizuri.  Tusiwe wepesi kulalamika wakati hatutimizi wajibu wetu kama Waajiriwa.

SENSA YA WATU NA MAKAZI

68.          Mheshimiwa Spika, takriban siku kumi zijazo tutakuwa na Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika kuanzia saa Sita Usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti, 2012 Nchini kote.  Umuhimu wa Sensa hii nimeuelezea katika hotuba zangu za ndani na nje ya Bunge lako Tukufu zikiwemo hotuba za Bajeti kwa miaka mitatu mfululizo. Kwa kutambua umuhimu wake maandalizi yaliyoanza mapema mwaka huu sasa yamekamilika. Kwa vile, Mkutano huu unamalizika siku chache kabla ya kufanyika kwa Sensa hiyo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati Watanzania wote waliojitolea kwa hali na mali wakati wa kipindi chote cha maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi. Tumejitahidi kwa kadri ya uwezo wetu kujiandaa vizuri na sasa siku imewadia. Wito wangu kwa Wananchi wote ni kuendelea kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa na kujitokeza kuhesabiwa kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012 hadi zoezi hilo litakapokamilika.

69.          Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru Viongozi wa Taasisi za Dini ambao kwa pamoja waliona umuhimu wa Sensa na hatimaye kuwahamasisha Waumini wao  kushiriki  katika  zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi.  Niwashukuru kwa kuwasaidia Waumini hao kwa kuwapa maelezo yaliyo sahihi kuhusu  zoezi  zima  la  Sensa. Madhumuni ya Zoezi la Sensa ni kuliwezesha Taifa kupata Takwimu sahihi na za uhakika kuhusu idadi ya Watu ili ziweze kutumika kutunga Sera za Kiuchumi na Kijamii, pamoja na kuwezesha kupanga kwa usahihi, kutekeleza na kutathmini Mipango ya Maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu.

70.          Aidha, napenda kusisitiza tena kwamba Zoezi la Sensa halitakuwa la siku moja tu, bali siku hiyo ya tarehe 26 Agosti, 2012 itakuwa ndiyo siku ya msingi wa kuhesabu Watu waliolala siku hiyo katika Kaya husika. Kazi yenyewe ya kuhesabu Watu itaendelea kwa siku saba hadi tarehe 2 Septemba, 2012. Hivyo, Nawasihi Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wote katika ngazi zote kusimamia zoezi hili na kuendelea kuwahamasisha Wananchi kushiriki kuhesabiwa siku ya Sensa tarehe 26 Agosti 2012.

HITIMISHO

71.          Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hotuba yangu napenda kusisitiza kuwa tumetekeleza wajibu wetu kama Wabunge kwa kutoa michango yetu ndani ya Bunge lako Tukufu. Ni kweli kwamba, tumefanya kazi kubwa inayostahili pongezi. Lakini pia Bunge kama Chombo cha Uwakilishi, linayo majukumu mengine na moja ni kuisimamia Serikali iliyoko Madarakani  itimize  Wajibu wake. Ni wajibu wetu kama Wabunge kuikosoa Serikali ili kuhakikisha kwamba matatizo na kero  mbalimbali za Wananchi yanatatuliwa. Lakini siyo kuikosoa na kuishia hapo tu, bali tuna wajibu wa kuishauri na kuielekeza kwa lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi walio tuchagua.

72.          Mheshimiwa Spika, ili yote hayo yafanyike, ni lazima sisi kama Wabunge tuwe Wasafi na wenye Maadili mbele za Wananchi wetu. Tuhuma za Rushwa zilizojitokeza dhidi ya baadhi ya Wabunge na hivyo kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili, haileti picha nzuri kwa Bunge letu. Ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tutambue dhamana kubwa tuliyonayo kwa Wananchi wetu. Ni vizuri tuienzi dhamana hiyo na kuiheshimu. Hivyo, nawasihi tutumie fursa ya kipindi hiki kilichobaki cha takribani miaka mitatu kuendelea kuimarisha utamaduni wa kushirikiana na kuhakikisha kwamba tunawatumikia Wananchi waliotuchagua kwa bidii zetu zote. 

73.          Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru tena wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu.  Shukrani za pekee ni kwako wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri.  Nawashukuru vilevile Wenyeviti wa Bunge wote kwa msaada mkubwa walioutoa katika kuliongoza Bunge kwenye Mkutano huu. Aidha, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao pamoja na Watumishi wote wa Serikali walioisaidia Serikali kujibu maswali   na   kuwasilisha   Hoja   za  Serikali  hapa  Bungeni. Kipekee namshukuru Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah pamoja na Watumishi wote wa Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha Mkutano huu. Nawashukuru wale wote waliokuwa na jukumu la Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha Mkutano huu unafanyika na kumalizika salama. Napenda pia niwashukuru Madereva wote kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa. Nawashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kuhakikisha kuwa Habari za hapa Bungeni zinawafikia Wananchi. Mwisho, niwashukuru Wananchi wa Dodoma kwa ukarimu wao wa kutupatia huduma zote muhimu na hivyo kukamilisha Mkutano huu wa mafanikio makubwa.

74.          Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi Jumanne, tarehe 30 Oktoba, 2012, litakapokutana saa 3.00 Asubuhi hapa Mjini Dodoma.

75.          Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: