Monday, July 23, 2012

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA UZINDUZI WA MRADI WA MAJI SAFI NAUSAFI WA MAZINGIRA JIJINI MBEYA, 22 JULAI, 2012


Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya;
Mheshimiwa Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe;
Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe;
Waheshimiwa Wabunge;
Wakuu wa Wilaya;
Ndugu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji;
Mheshimiwa Andris Piebalgs, Kamishna wa Maendeleo wa
       Jumuiya ya Umoja wa Ulaya,
Mheshimiwa Klaus Peter Brandes, Balozi wa
      Serikali ya Ujerumani nchini Tanzania;
Mheshimiwa Philberto Cerian Sebugondi, Balozi wa
    Umoja wa Ulaya;
Waheshimiwa Viongozi wa Chama cha Mapinduzi na wa  Vyama vya Siasa Walioopo Hapa;
Viongozi wa Serikali;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana leo hapa katika Jiji la Mbeya. Nampongeza Mkuu wa Mkoa na wananchi wote wa Mbeya kwa mapokezi mazuri waliyonipatia. Asanteni sana. Aidha namshukuru Waziri wa Maji kwa kunipa heshima kubwa ya kunialika nije kuungana na wananchi wa Mbeya katika uzinduzi wa mradi mkubwa wa Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Jiji la Mbeya.
Ndugu wananchi;
Mradi huu ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa Jiji hili la Mbeya na vitongoji vyake. Kukamilika kwa mradi huu ni kutimia kwa ahadi yangu na ya Ilani ya CCM tangu kipindi changu cha kwanza na hiki cha pili.  Ni mradi ambao utahudumia wananchi wapatao 381,000 na una uwezo wa kuhudumia watu 490,000, idadi ambayo mji huu utaifikia mwaka 2017.  Kupitia mradi huu, mahitaji ya maji safi kwa Jiji la Mbeya yametoshelezwa kwa asilimia 100 na itakuwa hivyo hadi mwaka 2017.  Naomba Wizara ianze sasa kazi ya kutafuta namna ya kuongeza maji baada ya mwaka huo.  Mwaka 2017 si mbali ni miaka mitano tu ijayo.
  Nafurahi pia kuwa, matayarisho ya mipango ya kuipatia maji miji ya Vwawa, Tunduma, Mlowo, Mbalizi, Kyela, Tukuyu, Itumba, Lujewa na Kasumulo imekamilika.  Kilichobaki ni kupata fedha za kuitekeleza.  Tutasaidiana na Wizara kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Maji.
Hakuna mwenye shaka kuhusu manufaa ya mradi huu kwani sote tunafahamu kuwa maji ni uhai na Jiji letu la Mbeya limekuwa linakabiliwa na tatizo la upungufu wa maji. Upatikanaji wa maji safi na salama katika Jiji la Mbeya sasa utakuwa ni wa uhakika.  Inawafanya wakazi wa Mbeya kupunguza muda ambao walikuwa wanaupoteza kutafuta maji. Ndugu zetu sasa hususan akina mama, watapata muda wa kutosha kufanya shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato chao. Wanafunzi nao watapata muda wa ziada wa kujisomea  masomo yao na watoto watakuwa na muda mwingi wa kucheza badala ya kuhangaika umbali mrefu kutafuta maji.  Aidha, usafi wa miili yao utakuwa na uhakika.  Kupatikana kwa maji safi na salama kutasaidia kuboresha afya za wakazi wa Mbeya.
Magonjwa ya milipuko kama vile kipindupindu, kuhara, minyoo na magonjwa mengine yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama yatapungua sana na inawezekana yakatoweka kabisa. 
Ndugu Wananchi;
Natoa wito kwa wana–Mbeya Mjini kutumia fursa hii kuunganishwa kwenye huduma ya maji safi na salama. Kwa wale walio karibu na mtandao wa maji taka, wachukue hatua za kuunganishwa kwenye huduma ya uondoaji wa majitaka.  Kufanya hivyo kutasaidia kuimarisha usafi wa mazingira na kuboresha afya zenu.  Pamoja na hayo nawaomba wananchi wa Mbeya Mjini na taasisi zilizopo hapa mkumbuke kulipa bili za maji kwa wakati. Fedha hizo zinahitajika sana ili kuhakikisha kuwa huduma hii ya majisafi na uondoaji majitaka inakuwa endelevu. Msipofanya hivyo, Mamlaka zinazohusika zitashindwa kutoa huduma hii  na manufaa yote ya mradi yanayokusudiwa yatayeyuka.  
Ndugu wananchi;
Mradi huu wa maji safi na usafi wa mazingira umegharimu  shilingi bilioni 79.5. Serikali yetu imechangia shilingi bilioni 29.1, Umoja wa Ulaya umetoa shilingi bilioni 36.9 na Serikali ya Ujerumani imetoa shilingi bilioni 13.5.  Mradi huu wa Mbeya ni miongoni mwa miradi kadhaa ya majisafi na usafi wa mazingira hapa nchini ambayo imefadhiliwa na Umoja wa Ulaya. Miradi mingine iliyokamilika ni ile ya Jiji la Mwanza, Manispaa ya Songea na Manispaa ya Iringa. Miradi mingine inayoendelea kutekelezwa hivi sasa kwa ufadhili wa marafiki zetu hawa ni ile  ya miji ya Mtwara, Babati, Musoma na Bukoba.  Kwa mujibu wa fedha walizotupatia jana, miradi ya maji safi na usafi wa mazingira ya miji ya Lindi, Kigoma na Sumbawanga itatekelezwa na matatizo ya maji katika miji hiyo kuwa historia kama ilivyo kwa Mbeya.
Ndugu Wananchi;
Washirika wetu hawa ni watu wema sana.  Wameonesha moyo wa ukarimu na upendo wa hali ya juu kwa nchi yetu na watu wake. Wametoa mchango mkubwa wa kuiwezesha Serikali yetu kuendelea kutekeleza dhamira yake adhimu ya kuinua hali ya maisha ya Watanzania. Hivyo, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali na kwa niaba yenu wenzangu,  kuwashukuru marafiki zetu hawa.  Kwa namna ya pekee Umoja  wa Ulaya kupitia kwa Rais wake Mheshimiwa Jose Manuel Barroso na Kamishna wa Maendeleo, Mheshimiwa Andris Piebalgs.  Hivyo hivyo natoa shukrani kwa Serikali na watu wa Ujerumani kupitia kwa Mheshimiwa Klaus Peter Brandes, Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania.  Tunawashukuru kwa kuunga mkono jitihada za Serikali yetu na wananchi wa Tanzania za kuboresha maisha yao.  Marafiki zetu hawa wawili wamekuwa wanatusaidia katika mipango yetu mingi ya maendeleo licha ya hii ya maji.  Asanteni sana kwa uwezeshaji huo usio kifani.
Ndugu wananchi;
Ni muhimu mkaelewa kuwa wakati Serikali inafanya jitihada hizi kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anapata huduma ya maji safi na salama, na ninyi wananchi mnao wajibu wa kuhakikisha kwamba maji yanatumika ipasavyo na ikibidi kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Tuache tabia ya kutumia maji hovyo kwani hii ni rasilimali adimu sana inayohitaji kutunzwa vizuri tena kwa uangalifu mkubwa.  Pia, nawaomba mlinde vyanzo vya maji na hususan chanzo cha maji haya visiharibiwe ili mjihakikishie upatikanaji wa maji ulio endelevu.  Tusipofanya hivyo baada ya muda si mrefu maji yatapungua na hata kukauka kabisa na kuwafanya watu kurudia kenye tatizo la zamani la upungufu au kukosa maji. 
Naomba mamlaka husika na wananchi kuhakikisha kwamba chanzo cha maji kiko salama wakati wote.  Katu msiwape nafasi watu waovu kukiharibu.  Vilevile, mnalo jukumu la kulinda na kuhifadhi miundombinu ya maji safi na maji taka dhidi ya hujuma zinazoweza kufanywa na watu wasiopenda maendeleo.  Waswahili wanayo misemo miwili:  “Kitunze kikutunze” na “Kitunze Kidumu”  Zingatieni maneno ya hekima ya misemo hii.  Bila ya hivyo,  kazi yote hii itakuwa haina maana.  Sherehe hii itageuka kuwa mchezo wa kuigiza.  Hakikisheni watu watakaoharibu mabomba, valvu, vitekeo vya maji na vyanzo vya maji wanakamatwa na kupelekwa kwenye vyombo vya sheria.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wetu Serikalini, tutaendelea kutoa kipaumbele cha hali ya juu katika kuendeleza sekta ya maji nchini. Juhudi zetu hazitakoma kwa vile tunafahamu umuhimu wa maji kwa maendeleo ya taifa. Tutahakikisha kuwa wananchi wengi wa Tanzania wanafikiwa mapema iwezekanavyo na huduma ya maji safi na salama, tena kwa bei nafuu. Kama imewezekana kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Mbeya na kwenye miji na maeneo mengine nchini tutaweza.  Tutaendelea kutekeleza Sera ya Maji na Programu ya Maji kwa mijini na vijijini.  Naamini inawezekana kabisa kuongeza huduma hiyo kwenye maeneo ambayo hivi sasa haipo au haitoshelezi mahitaji. Kinachohitajika ni ushirikiano kutoka kwa wadau wetu wote wakiwemo wananchi, washirika wa maendeleo, vyama visivyo vya kiserikali na vya kijamii, na uongozi wa Serikali katika ngazi zote.  Napenda kusisitiza kuwa dhamana kubwa kwenu wananchi ni kutoa mchango unaostahili katika ujenzi na matumizi ya miradi.  Pia, tunalo jukumu kubwa la kutunza miradi hii na vyanzo vya maji. Tukifanya hayo tutajihakikishia kuwepo kwa rasilimali ya maji kwa miaka mingi ijayo na kwa kiwango cha kutosha.
Napenda kumpongeza Waziri wa Maji na timu yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuendeleza na kutekeleza mipango ya kitaifa ya kuimarisha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya mijini na vijijini. Ili kuongeza ufanisi wa kutekeleza mipango yenu, nawashauri mshirikiane kwa karibu zaidi na uongozi wa mikoa na wilaya zote nchini. Pia, washirikisheni wananchi wote wa maeneo husika katika kuibuni, kuitekeleza, kuisimamia na kuitunza miradi ya maji. Ushirikishwaji ni jambo jema kwani unawafanya wanachi, ambao ndio wadau wakuu, wawe sehemu ya mradi.
Ndugu wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu, naomba nitumie fursa hii kukumbusha mambo mawili ya msingi.  La kwanza ni zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika nchini kote tarehe 26 Agosti, 2012.  Sensa ambayo hufanyika kila baada ya miaka kumi, ni muhimu sana kwa kupanga mipango ya maendeleo ya nchi yetu. Inasaidia kufanya uamuzi wa uhakika katika kupanga na kutekeleza vyema  mipango ya maendeleo ya kiuchumi na huduma za jamii.  Kwa maana hiyo basi, nawaomba mjitokeze kwa wingi siku hiyo ili mkahesabiwe.  Tafadhali toeni ushirikiano unaostahili kwa mawakala wa Sensa watakapoanza kufanya kazi yao. Tukumbuke, Sensa ni kwa ajili ya maendeleo ya taifa letu. 
Nafahamu kuwepo madai ya baadhi ya watu kutaka swali la watu kuwa dini gani liingizwe.  Swali hilo halipo sasa na wala halijawahi kuwepo kwa nia njema kabisa.  Nia ya sensa ni kujua idadi ya watu kwa maeneo yao, marika na jinsia zao ili kuwezesha kupanga mipango ya maendeleo na huduma za jamii.  Hatupangi mipango yetu ya maendeleo kwa misingi ya dini au rangi za watu bali kwa kuzingatia maeneo na shughuli, mambo ambayo hunufaisha watu wa dini zote.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine linahusu mchakato wa kuandika  Katiba mpya ya nchi yetu. Kama mnavyofahamu, wajumbe wa Tume ya Katiba tayari wameanza  kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi.  Maoni ya wananchi ndiyo yatakayoleta Katiba ambayo itakuwa yenye manufaa kwa Watanzania wote.  Hivyo basi, nawaomba mjitokeze kwa wingi  wakati Tume hiyo itakapofika kwenye maeneo yenu kukusanya maoni yenu. Nawaomba mtumie nafasi hiyo ya kihistoria vizuri. Nendeni mkatoe  maoni yenu kwa utulivu. Nawahakikishia kuwa maoni yenu yataheshimiwa bila kujali itikadi za siasa, umri, rangi au kabila. Maoni yote yatakayotolewa yatapewa uzito na alama sawa.
Ndugu wananchi;
Mwisho, napenda kuwashukuru tena ndugu zetu wa Umoja wa Ulaya na Serikali ya Ujerumani kwa kuwezesha utekelezaji wa mradi huu. Vilevile ninawashukuru watendaji wote wa Wizara ya Maji, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka na wananchi wote kwa ujumla kwa ushirikiano wenu mzuri uliofanikisha utekelezaji wa mradi niliozindua leo. Utunzeni ili na wenyewe uwatunze. Nawaomba mzingatie uhifadhi wa mazingira ili vyanzo vya maji viendelee kuwa salama. Sote tukumbuke kuwa  Majisafi na Salama kwa Afya Bora.  
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments: