Thursday, December 29, 2011

TAARIFA YA KUFUKUZWA KWA WANAFUNZI WACHACHE VINARA WA UHALIFU KATIKA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Siku za hivi karibuni kumekuwepo taarifa na tahariri kwenye vyombo vya habari kuhusu suala la kufukuzwa kwa wanafunzi wachache vinara wa uhalifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 

Katika taarifa hizo kumekuwa na madai kwamba kabla ya uamuzi wa Baraza la Chuo wa kuwafukuza wanafunzi hao, milango ya mazungumzo na maridhiano kati ya uongozi na wanafunzi ilikuwa imefungwa, na kwamba wanafunzi hao hawakupewa fursa ya kusikilizwa na kujitetea mbele ya vyombo husika vya Chuo. 

Sisi tunadhani madai haya yameandikwa kwenye vyombo vya habari kwa lengo la kupotosha yaliyojiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi uamuzi wa kuwafukuza wanafunzi wachache vinara wa uhalifu kufikiwa na Baraza la Chuo. Taarifa hii inaweka bayana hali halisi kuhusu vitendo vya fujo na uhalifu vilivyofanywa na baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Awali ya yote tungependa kuwakumbusha wadau wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwamba katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mwelekeo miongoni mwa baadhi ya wanafunzi usio wa kawaida na unaotishia ustawi na heshima ya Chuo hiki. 

Kumejitokeza utamaduni hatari wa makundi madogo ya wanafunzi kuvunja taratibu zote za kisheria na za kiuongozi pale kunapokuwa na jambo fulani linalowakera, kwa kutenda vitendo vya kihalifu wazi wazi wakishinikiza matakwa yao yatekelezwe mara moja. 

 Mara nyingi vitendo hivyo vimekuwa vya uhalifu wa jinai. Mwelekeo huu hatari umekuwa ukikua taratibu, na kadiri siku zinavyopita umeanza kuotesha mizizi na kuimarika kama kwamba ni utamaduni unaopaswa kukubalika ili mradi tu unafanyika ndani ya mipaka ya Chuo.

Dalili za kukua kwa utamaduni huu zilianza kuonekana wazi tarehe 22 mwezi Februari mwaka 2008, pale ambapo baadhi ya wanafunzi waliendesha vurugu kubwa wakati wa usiku katika mabweni na maeneo ya huduma ya chakula. 

Katika vurugu hizo, wahusika walivunja milango ya vyumba vya wenzao na kuwatoa nje, waliwamwagia maji baadhi ya wanafunzi wa kike, na kundi mojawapo lilishambulia makazi ya Makamu Mkuu wa Chuo mnamo majira ya saa nne usiku. 

Kwa siku hiyo, lalamiko kubwa la wanafunzi hao lilikuwa ni uhaba wa maji mabwenini. Kwa bahati mbaya, wakati wa vurugu hizo mwanafunzi mmoja alipoteza maisha kwa kutumbukia katika bwawa la kuogelea. Pia kulikuwa na uporaji mali, kupigwa kwa wanafunzi waliokataa kushiriki katika vurugu na uharibifu wa mali za Chuo, wanafunzi na jamii kwa ujumla. 

Mwenendo huo ulikuwa tofauti kabisa na utamaduni uliojengeka Chuoni kwa miaka mingi, ambapo wanafunzi waliendesha harakati zao za kudai haki za msingi na maendeleo ya nchi kwa njia zinazokubalika kisheria na bila kufanya uhalifu au kuingilia uhuru wa wenzao wasiopenda kushiriki katika harakati hizo. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kilijulikana kwa sifa hiyo ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Baraza la Chuo lilistushwa na mwelekeo huo wa kugeuza uhalifu wa jinai kuwa utamaduni unaokubalika chuoni. Hivyo liliunda tume maalum kuchunguza kiini cha mwelekeo huo na kutoa ushauri kwa Chuo. Taarifa ya Tume hiyo, ambayo iliongozwa na Mh. Jaji Emilian Mushi iliwabaini vinara wa vurugu zile na pia kukishauri Chuo kuchukua msimamo thabiti wa kutumia sheria zake ndogo ndogo (By-Laws) kumwadhibu bila kusita mwanachuo yeyote anayevunja sheria na taratibu hizo. 

Baraza la Chuo liliridhia taarifa na mapendekezo ya Tume ya Jaji Mushi, na hivyo kuuagiza uongozi wa Chuo kujenga utamaduni wa kulinda haki na usalama wa wanafunzi walio wengi chuoni kwa kutovumilia vitendo vyovyote vya kihalifu vinavyofanywa na baadhi ya wanafunzi.

Pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa, vitendo vya wanafunzi kufanya uhalifu mkubwa pale wanapokuwa na madai fulani vimeendelea kuongezeka kwa kasi Chuoni. Imekuwa kawaida kwa wanafunzi wachache kutumia fimbo na vurugu kuwalazimisha wenzao walio wengi kutoka madarasani au mabwenini na kujiunga na uhalifu mkubwa wanaouanzisha pale wanapokuwa na madai au malalamiko fulani. 

Itakumbukwa kwamba fujo za aina hii mwanzoni mwa mwaka huu ziliwahi kusababisha mwanafunzi wa kike aliyekuwa mjamzito kupoteza mimba yake baada ya kupigwa kwa fimbo akijaribu kukimbia ili kujiokoa. Pia imekuwa kawaida kwa vikundi vya wanafunzi kuziba lango kuu la kuingilia jengo la Utawala au kupanda ghorofani na kuzingira ofisi za viongozi wa Chuo na kusimamisha kabisa shughuli katika jengo hilo. 

Mara nyingi hayo yametokea wakati Uongozi wa Chuo ukiwa ofisini ukishughulikia tatizo husika kwa kushirikiana na viongozi halali wa wanafunzi. Mara nyingi viongozi wa vurugu hizo wamekuwa wakiitwa ofisini ili kuelimishwa kuhusu kinachoendelea, lakini mara watokapo nje hujiunga tena na wenzao na kuendeleza vurugu, hata kama jambo husika liko katika hatua za mwisho kupatiwa utatuzi. 

Vilevile kumekuwa na matukio mengi ya makundi ya wanafunzi hao kuharibu mali za umma na za watu binafsi katika harakati zao za kuwalazimisha wanafunzi walio wengi wawaunge mkono katika vitendo vya kihalifu.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika vurugu za hivi karibuni. Kama ilivyotangazwa hapo awali, Tarehe 12 na 13 mwezi Desemba, 2011 kikundi kidogo cha wanafunzi kiliendesha vitendo vya uhalifu katika Kampasi Kuu ya Mlimani (Kampasi ya Mwalimu J. K. Nyerere Mlimani). 

 Vitendo hivyo vilisababisha uvunjifu mkubwa wa amani na utulivu, na kuvuruga shughuli za kitaaluma na kiutawala za Chuo. Katika siku hizo mbili, kikundi hicho kiliingia madarasani na kuwatimua wenzao walio wengi madarasani kwa kutumia fimbo, waliwanyanyasa na wakati mwingine kuwamwagia maji wahadhiri waliowakuta wakifundisha, waliziba lango kuu la kuingilia jengo kuu la utawala na kusabisha shughuli ndani ya jengo hilo kusimama, na mara kwa mara waliwazuia wenzao wasiopenda kujihusisha na vurugu hizo wasiingie kwenye magari kwenda hosteli wala wasikae eneo lolote la Chuo na kuendelea kujisomea. 

Jioni ya tarehe 12 kikundi hicho cha vurugu kilifunga lango kuu la kuingilia jengo la utawala hadi saa mbili usiku, na mbaya zaidi, baada ya hapo kilikwenda kafeteria na kuendesha vurugu kubwa. Katika vurugu hizo washiriki waliwapiga wenzao waliokuwa wakila katika kafeteria ya Chuo na kumwaga vyakula vyao, walimwaga uchafu katika chakula kilichokuwa kinasubiri kugawiwa, waliwapiga wafanyakazi wa kafeteria, na waliharibu majokofu ya kafeteria na vifaa vingine.

 Pia waliyashambulia mabasi na magari mengine na kuvuruga kwa muda usafiri katika barabara kuu ipitayo chuoni. Kikundi hicho pia kilitangaza kuipindua serikali halali ya DARUSO, kitendo ambacho kilisababisha kuvunjwa mlango wa chumba cha mmoja wa viongozi wa DARUSO.

Kutokana na vurugu hizo, siku ya Jumanne tarehe 13 Desemba, 2011 wenye mabasi yanayosafirisha wanafunzi kutoka hosteli ya Mabibo kuja kampasi kuu waligoma kutoa huduma hiyo, na hivyo kusababisha wanafunzi wote waishio Mabibo kuja Chuoni asubuhi na kurejea jioni kwa kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 8. 

Pia, kwa kuogopa usalama wao na wa mali zao, waendeshaji wa kafeteria zilizopo Kampasi Kuu waligoma kutoa huduma ya chakula, hivyo kusababisha wanafunzi wengi kushinda na njaa kutwa nzima kwa kukosa sehemu za kupatia huduma ya chakula.

Haya yaliyojiri tarehe 12 na 13 Desemba, 2011 yalikuwa ni mwendelezo wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoanza mwanzoni mwa mwezi Novemba, 2011. Kila mara vitendo hivi vilianzishwa na kikundi kidogo sana cha wanafunzi wanaojiita wanaharakati na hatimaye kupata wafuasi wa kutosha kuvuruga shughuli za Chuo.

 Madai ya wanafunzi walioendesha vurugu hizi yamekuwa yakibadilika kila kukicha. Mwanzoni walidai mikopo kwa ajili ya wanafunzi wote nchini waliochaguliwa kujiunga na elimu ya juu kwa mwaka huu wa masomo na ambao hawakupata mikopo. Baadaye dai kubwa likawa kuachiliwa huru wenzao waliokamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na kuendesha maandamano kinyume cha sheria na kukaidi amri ya Jeshi la Polisi yakutawanyika pasipo shuruti hapo Novemba 14, 2011. 

Katika siku mbili za mwisho madai ya awali yalikuwa kuondolewa adhabu za kinidhamu walizopewa wenzao wachache kwa mujibu wa kanuni na sheria za Chuo, lakini baadaye wakageukia suala la kupatiwa fedha zao za malazi na chakula kwa kipindi cha kuanzia tarehe 10 Desemba, 2011.

 Jambo kubwa lililojitokeza ni kwamba changamoto zote walizolalamikia ama zilikwishatatuliwa na Chuo kwa kushirikiana na uongozi halali wa DARUSO au zilikuwa zinafuatiliwa ili kupatiwa ufumbuzi, na wao walitakiwa wawe wavumilivu na kusubiri marekebisho kwa saa au siku chache tu; jambo ambalo wafanya vurugu hawakuwa tayari kulisikiliza.

Wakati wote huo, wanafunzi waleta vurugu Chuoni hawakuonyesha dalili ya kutaka suluhisho la tatizo lolote lile lipatikane kwa njia ya majadiliano na ufuatiliaji wa kimkakati, bali kwa njia ya vurugu zenye kukiingizia Chuo hasara kubwa ya muda wa masomo na mali.

 Mfano mmoja ni pale uongozi wa DARUSO ulipowasilisha ombi kutaka Uongozi wa Chuo kuingilia kati na kuwasaidia wanafunzi waliowekwa rumande baada ya kufunguliwa mashtaka ya kuendesha maandamo kinyume na taratibu za kisheria na kukataa kutii amri ya Jeshi la Polisi ya kutawanyika pasipo shuruti. 

Wakati wanafunzi wanaojiita wanaharakati wanaanzisha vurugu Chuoni kuhusiana na jambo hilo, Uongozi wa Chuo ukishirikiana na Serikali halali ya DARUSO ulishafikia hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za kuwatoa kwa dhamana wanafunzi waliokuwa rumande, na wengi katika jumuia ya wanafunzi walikuwa wanafahamu hatua hizo zilizokuwa zinachukuliwa kwa ufanisi. 

Hata hivyo, matangazo mengi yaliyokuwa yakieleza utaratibu na hatua ambazo zinachukuliwa, yaliondolewa katika mbao za matangazo ili wanafunzi wengi wasiweze kujua ni nini kinaendelea, na wahisi kuwa uongozi wa Chuo na ule wa DARUSO haukuwa unafanya lolote kutatua matatizo ya wanafunzi. Walioyaondoa matangazo hayo ni washiriki waliokuwa wakiunga mkono vurugu. 

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa taarifa za serikali ya DARUSO zinazoelezea mafanikio yanayofikiwa kwa njia ya mazungumzo na mikakati halali kuondolewa toka mbao za matangazo. Hii inaonyesha kwamba nia kamili ya wanaharakati hao ni kuchochea vurugu Chuoni.

Vilevile, wakati kampeni za kupinga hatua zilizochukuliwa na Baraza la Chuo kuwasimamisha masomo wanafunzi waliokuwa na kesi kwa mujibu wa sheria ndogondogo za Chuo zinafanyika chini chini, Uongozi wa Chuo na Serikali ya DARUSO waliafikiana kuliomba Baraza liwaruhusu wale wanafunzi wote wenye kesi mahakamani waendelee na masomo yao hadi hukumu ya kesi yao itakapotolewa, kwa sharti la kutojihusisha tena na vurugu Chuoni. 

Huku wakijua mafanikio yaliyopatikana katika majadiliano hayo, na wakati Uongozi wa Chuo ukitekeleza makubaliano yao na Serikali ya DARUSO, wanafunzi wale wenye kesi mahakamani waliongeza kasi ya kushiriki wazi wazi katika harakati za kuvuruga masomo na shughuli zingine za Chuo. 

Hayo yalitokea hasa siku ya tarehe 12 Desemba, 2011, siku ambayo wanafunzi waliosimamishwa masomo kutokana na kuwa na kesi mahakamani walirejea Chuoni na kuwa wahutubiaji wakubwa wa kundi la wanafunzi waliolizingira jengo la Utawala. 

Katika hotuba hizo wanafunzi hao waliwahamasisha washiriki wengine kutojali sheria wala taratibu za Chuo, wakisema Mahabusu ya Segerea walikokuwa kabla ya kupata dhamana si lolote. Huo ni uthibitisho mwingine kwamba kundi lililoendesha vurugu, pamoja na wale waliokuwa wanasubiri kwisha kwa kesi zao za mahakamani, halikuwa na lengo la kurejesha utulivu na uendelevu wa masomo Chuoni.

Vurugu zilizotokea tarehe 12 na 13 Desemba zilifikia kiwango cha kitishia kivitendo, usalama wa maisha ya wanafunzi na wafanyakazi wa Chuo, pamoja na mali za umma na za watu binafsi zilizopo katika kampasi ya Mlimani na hosteli ya Mabibo. Baadhi ya wanafunzi ambao hawakushiriki katika vurugu zile walieleza waziwazi hofu na kushangazwa kwao kutokana na kuwaachia waleta vurugu kuendelea na fujo zao hatarishi kwa siku mbili mfululizo bila ya sheria kuchukua mkondo wake. 

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Wakuu wa Vyuo vya Kampasi (Campus Colleges), Shule Kuu, na Kurugenzi za Kitaaluma, ilifanya kikao cha dharura siku ya Jumanne tarehe 13 Desemba, 2011 kujadili hatua za kuchukua ili kuepusha kutokea kwa matatizo makubwa Chuoni. 

Baada ya majadiliano ya kina Kamati ilipendekeza kwamba hatua za kisheria na za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya wanafunzi wote waliokuwa wanaongoza vurugu. Jioni ya siku hiyo hiyo ya tarehe 13 Desemba Baraza la Chuo chini ya Mwenyekiti wake Bw. Peter Ngumbullu na Makamu wake Jaji Joseph Sinde Warioba pia lilifanya kikao cha dharura. 

Katika kikao hicho Baraza lilifanya tathmini yake yenyewe na pia kupitia mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Wakuu wa Koleji, Shule Kuu na Kurugenzi za Kitaaluma na likaelekeza kwamba hatua kali zichukuliwe dhidi ya wanafunzi wote waliokuwa vinara wa vurugu zilizokuwa zikiendelea tangu mwezi Novemba, ikiwa ni pamoja na kuwafukuza Chuo mara moja. 

 Baraza pia lilisisitiza msimamo wake wa awali wa kuuelekeza Uongozi wa Chuo kutokufumbia macho hata kidogo (to have zero tolerance) vitendo vya ukiukwaji wa sheria na taratibu za Chuo.

Maelekezo ya Baraza yalitangazwa kwa wanajumuiya ya Chuo siku hiyo hiyo kupitia mbao za matangazo, na kuanzia tarehe 14 Desemba, 2011 Uongozi wa Chuo ulianza kuyatekeleza. Mara baada ya vinara wa vurugu kuondoka hali ya utulivu ilirejea chuoni, na kuanzia siku hiyo ya Desemba 14 shughuli zote za taaluma zimekuwa zikiendelea kama kawaida.

Kuhusiana na matukio haya, Uongozi wa Chuo ungependa kusisitiza yafuatayo:

Taasisi kubwa kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam haiwezi kuendeshwa kiendelevu bila ya wadau wote kufuata taratibu za kiuendeshaji zilizowekwa.

Kila mwaka wanafunzi kwa ujumla wao huchagua serikali yao ya DARUSO. Lakini tabia iliyoanza kuota mizizi ni ya baadhi ya wanafunzi kuuzuia uongozi wa DARUSO usifanye kazi yake kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizowekwa. Badala yake hushinikiza serikali hiyo ifanye kazi kwa kuvunja taratibu, na isipokubali kufanya hivyo wanafunzi hao huanzisha fujo na vurugu hatarishi kwa usalama wa watu na mali.

Mwenendo ulioanza kuzoeleka wa baadhi ya wanafunzi kutumia vurugu na uhalifu kama ndiyo njia ya kushughulikia mapungufu au kero zinazojitokeza mara kwa mara ni wa hatari siyo tu kwa usalama na maendeleo ya Chuo bali hata katika malezi ya vijana, na kwa hiyo havipaswi kuruhusiwa kuendelea.

Vitendo vya kihalifu vilivyofanywa au kuchochewa na wanafunzi waliofukuzwa Chuo hivi karibuni havilingani na haiba ya taasisi yenye sifa ya kuitwa Chuo Kikuu, ambapo msingi wa malezi ni demokrasia ya majadiliano ya hoja na mikakati ya kiutekelezaji bila kuingilia uhuru wa mtu binafsi au kuhatarisha usalama. Vile vile waliotenda vitendo hivyo hawana sifa ya kuitwa wanafunzi wa Chuo Kikuu ambao matendo yao yanatakiwa kuaksi haiba ya kisomi ya ngazi ya Chuo Kikuu.

Baraza la Chuo lilichukua hatua ya kuwafukuza Chuo vinara wa vurugu za hivi karibuni kwa uchungu mkubwa baada ya njia nyingine zote za kurudisha utulivu Chuoni kushindikana. Njia hizo ni pamoja na mazungumzo na makundi mbalimbali ya wanafunzi, wakiwemo vinara wa vurugu hizo.

Uamuzi wa kuwafukuza Chuo vinara hao ulichukuliwa baada ya uchunguzi wa kina na baada ya kila mmoja wao kuhojiwa na majopo huru ya kinidhamu (Disciplinary Panels). Katika mahojiano yale kila mwanafunzi ambaye hatimaye alifukuzwa Chuo alipata fursa tosha ya kujitetea, lakini maamuzi yalifanywa kutokana na ushahidi ambao watuhumiwa wenyewe walionyeshwa.

Ni vyema kila mdau wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ashiriki kwa kadiri awezavyo kusaidia juhudi zilizoanza za kuhakikisha kwamba vitendo vya kihalifu vinatokomezwa siyo tu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CKD) bali katika taasisi zetu zote za elimu ya juu nchini.

Profesa Yunus D. Mgaya
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Utawala
(Mdhibiti Nidhamu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)

7 comments:

Anonymous said...

Inasikitisha kuona Vijana wa Kitanzania tena watoto wa walalahoi wakikoseshwa elimu kwa sababu tu wameonekana kudai kile kilicho halali chao, ama serikali ikidhani kuwa inakomesha na kuua uwezo wa mtanzania wa kuhoji pale anapoona mambo hayaendi ipasavyo! hii ni taswira mbaya na aibu kubwa kwa Taifa!
serikali na uongozi wa taasisi hizi lazima wajifunze kutoa maamuzi yakinifu, vinginevyo haya wanayoyafanya leo ni sawa na kufunika MOTO na Majivu alaf unapita juu yake ukiwa peku!
Poleni sana Wadanganyika wenzangu! tusichoke kupambana na Sirikali hii iliyojaa Viongozi mafisadi na Mabata bwanyenye!

Anonymous said...

SAAFI SAAANA.NI KWELI CHUO KILIKUWA KINAANZA KUPOTEZA HAIBA YAKE KITAIFA NA KIMA TAIFA KUTOKANA NA VITENDO VYA KIHUNI VYA BAADHI YA WANAFUNZI.KAMA MZAZI NASEMA MSISITE KUCHUKA HATUA KALI KAMA MLIZOCHUKUA,LAKINI BILA KUMUONEA MTU.

Anonymous said...

Hii TANZANIA ya miaka 50 haikufika hapo kwa vurugu, lakini ni bahati mbaya kwamba hiyo ndiyo Democrasia ambayo tunafikiri itachangia maendeleo.
Hii ni hatari hatuwezi kuvumilia huu upuuzi na kama democrasia yenyewe ndiyo hiyo ni heri dictatorship ambayo itatufanya watu tujue kuheshimiana ili tuendelee hata kama ni kwa lazima.

Hayo wasiruhusiwe kurudi kusoma wakatafute njia nyingine kusudi hao wanaowaunga mkono wawasomeshe wanakokujua wao ili waendeleze huo upuuzi.
The Government has to act tough on this hooliganism which is taking roots! Wecant accept this to grow please!

Anonymous said...

Nimemaliza hapo chuo kikuu mwaka 1999 kwa digrii ya kwanza. Nilikaa chini ya Uongozi wa Cyprian Sweke, Maleva Patric na mwisho Kitila Mkumbo. Migomo tulikuwa nayo, lakini hali haikuwa hivyo. Kama hali ya mambo ni kweli kwa maelezo hayo ya chuo ingawa ni ya upande mmoja, sijui upande mwingine, mimi nasikitika sana. Nafanya kazi Serikalini kwa sasa, ila siegemei upande wowote, kwa kweli kukiharibu chuo na mali zake hatukuwahi kufanya wakati wetu. Tulikuwa tunagombana zaidi na Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu wakati ule wa Pius Ng'wandu, Mzee Mkapa , Ndugu Abdalaha Ngololo (ingawa nasikia ameshafariki, kama yuko hai anisamehe)na wengineo. Kwa kweli wadogo zangu acheni kuharibu chuo hicho. Wadogo zenu wangepenga wakikute kizuri kama ninyi tulivyowaachia. Sifurahishwi hata kidogo, nimejisikia vibaya sana. Siwajui kwa majina waliofukuzwa, lakini nawapa pole na kuwa hiyo ni changamoto ya maisha. Wajaribu kuomba tena sehemu nyingine ya elimu ya juu ila wakiwa na mtazamo tofauti hasa katika kuwa na nidhamu. Kwa sasa tayari mimi ni mzazi, nisingependa kuona mwanangu anakuwa msomi wa aina hii ya vurugu. Pia sipendi kuona anarudi nyumbani kwa kufukuzwa chuo kwa sababu ya vurugu. TUDAI HAKI BILA KUHARIBU CHUO WALA MALI ZOZOTE. Niishi hapo.

Anonymous said...

kinachokufanya useme saafi sana ni ujinga wako tu,hii taarifa ni chuo kwa lengo la kuhalalisha uonevu,hlf wewe bila kujua au hata bila kuhitaji kusikia upande wa pili unasema safi saana!!!!!!!!!!

Anonymous said...

Hakuna sheria inayomzuia mtanzania yeyote kudai haki yake na hii ipo kikatiba ibara ya 30. vile vile hakuna sheria inayomruhusu mtanzania yeyote kufanya vitendo vya kihalifu pale anapo dai haki yake. hivyo basi tujifunze watanzania wenzangu kudai haki zetu kwa kufuata taratibu zilizopo pasipo kuvunja amani na utulivu uliopo. inaposhindikana kuna vyombo stahili ambavyo ni mahakama zetu, peleka madai yako na yatatatuliwa kwa haki na usawa. na kipongeza chuo kikuu cha dar es salaam kwa hatua walizochukua kurudisha hali ya amani na utulivu chuoni pia udhibiti huo uendelee hadi tabia hii ikome kabisa watu wajifunze kudai haki kwa njia halali zilizopo kisheria.

Anonymous said...

Vijana ni lazima wajifunze na watambue wanapambana na adui wa aina gani.Kimsingi adhabu iliyotolewa ni kubwa mno.Ni wakati wa kuwa na meza ya mazungumzo bila ya pande yoyote ile kutunishiana misuri.Ninaamini kuna waliofukuzwa ambao hakuwaa na makosa hasa wenye kesi mahakamani.Utetezi lazima ufanywe kwa njia yoyote ile hasa kupitia uongozi wa wanafunzi(DARUSO).Lakini pia inaonekana wanafunzi hawajapata habari hizi kwa undani ingawa nasikia kuna Wanafunzi wenye moyo wa kizalendo wanaandika makala yenye kichwa cha MLIMANILEO kuhabarisha kinachoendelea hapo chuoni.Lakini bado nafikiri wazarendo hao wachache hawatosherzi katika kuhabarisha umma.Napenda kuwapongeza kwa kazi yao nzuri kwani hata mimi nilikuwa mwanafunzi wa hapo lakini niliondoka kabla makala hayo hayajapata nguvu kubwa kama iliyonayo kwa sasa.