Monday, December 12, 2011

SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU WA TANZANIA BARA ZAFANA MUSCAT, OMAN

Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Oman,Mheshimiwa Abdallah Kilima Akitoa salaam za maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara
Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Oman,Mheshimiwa Abdallah Kilima na wageni rasmi wakikata keki ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.

Ubalozi wa Tanzania mjini Muscat, Oman chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Kaimu Balozi Abdallah Abasi Kilima, uliandaa hafla mbili zilizofana sana za kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania bara .

Sherehe ya kwanza ilifanyika tarehe 7 Disemba 2011katika ukumbi wa Jibrin kwenye hotel ya kitalii ya Intercontinental Muscat.

Mgeni rasmi katika sherehe hii alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Oman Mtukufu Sayyed Mohammed bin Salim Al Said , aliyefuatana na maafisa wengine waandamizi toka Wizara ya Mambo ya Nje, Oman ambao ni Mheshimiwa Balozi Salim bin Mohammed Al Riyami,Mkurugenzi Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa,Mheshimiwa Balozi Mohamed bin Ahmed Al Kiyumi , Mkurugenzi Idara ya Afrika , Wizara ya Mambo ya Nje.

Sherehe hii pia ilihudhuriwa na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao nchini Oman , wananchi wa Oman , wafanyabiashara , watanzania waishio Oman , pamoja na waomani wenye asili ya Tanzania.

Katika hotuba yake Mheshimiwa Kaimu Balozi Abdalah Kilima alisifu juhudi za serikali za Tanzania na Oman katika kukuza uhusiano bina ya nchi mbili ambao ni wa kihistoria, aliieleza kuwa uhusiano wa Tanzania na Oman ni wa namna ya pekee kwa kuwa Oman ni nchi pekee iliyo nje ya bara la Afrika ambayo wananchi wake wana uhusiano wa kidamu na kiutamaduni unaothibitishwa na matumizi ya Kiswahili kwa wananchi wengi wa oman, vigezo hivi ni chachu katika kuimarisha uhusiano baina ya Oman na Tanzania, uhusiano ambao unazidi kuimarika kadri siku zinavyoenda.

Mheshimiwa Balozi na mgeni Rasmi walikata keki ikiwa ni ishara kuitakia mema Tanzania na Oman.

Katika maadhimisho hayo Ubalozi ulitoa tuzo kwa makampuni kadhaa ikiwa ni ishara ya kutambua na kuenzi mchango wa makampuni hayo katika kufanikisha shughuli mbalimbali za ubalozi, makampuni haya ni Ajib Trading LLC, Kenya Airways, Safeway LLC na MB Holdings.

Sherehe ya pili ilifanyika tarehe 9 Disemba 2011 katika hoteli ya Ramee Dreams Resort ambayo ilihudhuriwa na watanzania na marafiki wa Tanzania wanaoishi nchini Oman, Mheshimiwa Kaimu Balozi aliwakumbusha wa Tanzania kuwa Tanzania imethubutu, imeweza na inazidi kusonga mbele na kuwa wahudhuriaji wote ni mashahidi wa hilo kwa kuwa wengi mafanikio yao yametokana na kuthubutu na kuweza kwa serikali katika maeneo mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Katika sherehe hii, Ubalozi ulitoa tuzo kwa uongozi wa hoteli ya Ramee Dreams Resort kwa kutambua na kuheshimu mchango wa hoteli hii katika kukuza, kutangaza na kuendeleza muziki na utamaduni wa Tanzania, Ubalozi pia ulitoa tuzo kwa kikundi cha wasanii cha BAWA kwa kufanikisha sherehe hizi za miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania baraSherehe zote mbili zilichangamshwa na burudani ya wasanii mahiri toka kikundi cha Bagamoyo Women Artists au maarufu kama BAWA kutoka pwani ya Bagamoyo

No comments: