Tuesday, February 8, 2011

HOTUBA YA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA, PROFESA JOHN NKOMA, WAKATI WA UZINDUZI RASMI WA JENGO LA MAKAO MAKUU YA TCRA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA


MHESHIMIWA MGENI RASMI, DAKTA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

MHESHIMIWA PROF. MAKAME MBARAWA, WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

WAHESHIMIWA MAWAZIRI NA MANAIBU MAWAZIRI,

WAHESHIMIWA MAKATIBU WAKUU NA MANAIBU MAKATIBU WAKUU,

WAHESHIMIWA MABALOZI MLIOPO,

MHESHIMIWA JUDGE MSTAAFU BUXTON CHIPETA, MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI YA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA,

WAJUMBE WA BODI NA MENEJIMENTI YA MAMLAKA YA MAWASILIANO,

WAJUMBE WA KAMATI YA MAUDHUI YA MAMLAKA YA MAWASILIANO,

WAHESHIMIWA WAGENI WAALIKWA,

WAANDISHI WA HABARI,

MABIBI NA MABWANA,

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Awali ya yote, napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, kukushukuru wewe Mh. Rais kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kushirikiana nasi katika shughuli hii muhimu ya uzinduzi wa jengo letu jipya la Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini, liitwalo “Mawasiliano Towers”.

Tunafahamu wingi wa kazi zako na ugumu wa ratiba yako ya kazi na majukumu ya kitaifa ulionayo. Kushiriki kwako katika hafla hii, kumetufariji mno kwani ni kielelezo thabiti cha imani yako kwetu na kuthamini tukio hili muhimu katika historia ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (Tanzania Communications Regulatory Authority – TCRA) ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003. Mamlaka ilichukua majukumu yaliyokuwa yakisimamiwa na zilizokuwa Tume ya Mawasiliano Tanzania (Tanzania Communications Commission – TCC) na Tume ya Utangazaji Tanzania (Tanzania Broadcasting Commission – TBC). Kuunganishwa kwa taasisi hizo mbili kulitokana na uamuzi wa serikali ili kwenda sambamba na maendeleo ya kiteknolojia katika sekta ya mawasiliano. Mamlaka hii inahusika na udhibiti wa simu, utangazaji, posta na teknolojia za elektroniki, na kwa ujumla matumizi ya simu, televisheni, radio na kompyuta ikiwemo intaneti.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Wajibu na MAJUKUMU ya TCRA ni kama yafuatavyo:

· kukuza ushindani katika utoaji wa huduma za sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini;

· kulinda maslahi ya watumiaji huduma za habari na mawasiliano nchini;

· kuweka mazingira yatakayosaidia watoa huduma waweze kunufaika na uwekezaji ;

· kuhakikisha kuwa huduma zinawafikia watumiaji wote wakiwemo wa kipato cha chini, walio vijijini na wasiojiweza; kuelimisha umma ili uelewe vema huduma zinazotolewa katika sekta;

· Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na 12 ya 2003;

· Kutoa leseni na pia kufuta inapobidi kwa kuzingatia maelekezo ya Sheria ya Sekta inayohusika;

· Kuweka vigezo na kusimamia utoaji wa huduma za mawasiliano, Posta na Utangazaji ;

· Kusimamia utendaji wa watoa huduma katika sekta ikiwa ni pamoja na viwango vya uwekezaji; gharama za huduma; ubora wa utoaji na usambazaji wa huduma, n.k.;

· Kusuluhisha migogoro na malalamiko ndani ya sekta;

· Kutunga sheria ndogo na kanuni zitakazorahisisha utekelezaji wa Sheria ya Mamlaka pamoja na zile za sekta;

· Kushirikiana na wadhibiti wa mawasiliano katika nchi nyingine ili kuboresha utoaji huduma nchini;

· Kuzingatia mikataba iliyowekwa baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali nyingine au Mashirika ya Kimataifa;

· Kutelekeza majukumu mengine itakayopangiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

SERA, SHERIA, KANUNI NA MFUMO WA LESENI

Sekta ya Mawasiliano imekuwa haraka sana na mojawapo ya sababu ya maendeleo hayo ni kuwepo kwa sera, sheria, kanuni na mfumo mzuri wa utoaji leseni.

SERA (COMMUNICATION POLICIES)

  • Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya simu ya mwaka 1997 (National Telecommunications Policy of 1997)
  • Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2003 (National ICT Policy of 2003)
  • Sera ya Taifa ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 (National Information and broadcasting Policy of 2003)
  • Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003 (National Postal policy of 2003)

SHERIA (COMMUNICATIONS LEGISLATIONS)

  • Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na.12 ya mwaka 2003 (Tanzania Communications Regulatory Authority Act No 12 of 2003)

  • Sheria ya Mfuko wa Mawasialiano ya mwaka 2006 (Universal Communications Service Access Fund Act of 2006)

  • Sheria ya mawasiliano ya elektroniki na posta ya mwaka 2010 (Electronic and Postal Communications Act (EPOCA) of 2010) ambayo ilipitishwa na Bunge Januari 2010 na kufuta sheria mbili: Sheria ya Utangazaji Na. 6 ya Mwaka 1993 (Tanzania Broadcasting Services Act No 6 of 1993) na Sheria ya Mawasiliano Tanzania Na. 18 ya mwaka 1993 (Tanzania Communications Act No 18 of 1993)

KANUNI (COMMUNICATIONS REGULATIONS)

Kwa hivi sasa kanuni zinazotumika ni za mwaka 2005. Ili kwenda na wakati, na kufuatana na sheria mpya ya EPOCA, mchakato unaendelea ili kutengeneza kanuni mpya za mwaka huu 2011. Wadau wote wa sekta watahusishwa. Kanuni hizi mpya zitazingatia maendeleo kwenye sekta. Kanuni za mwaka 2005 ni hizi zifuatazo:

1. The Tanzania Communications (Broadband Service) Regulations 2005

2. The Tanzania Communications (Consumer Protection) Regulations 2005

3. The Tanzania Broadcasting Services (Content ) Regulations 2005

4. The Tanzania Communications (Licensing) Regulations 2005

5. The Tanzania Communications (Importation and Distribution) Regulations 2005

6. The Tanzania Communications (Installations and Maintenance) Regulations 2005

7. The Tanzania Communications (Interconnection) Regulations 2005

8. The Tanzania Communications (Telecommunication Numbering and Electronic address) Regulations 2005

9. The Tanzania Postal Regulations 2005

10. The Tanzania Communications (RadioCommunications and Frequency Spectrum ) Regulations 2005

11. The Tanzania Communications (Tariff) Regulations 2005

12. The Tanzania Communications (Type Approval of Electronic Communications Equipment) Regulations 2005

13. The Tanzania Communications (Quality of Service) Regulations 2005

14. The Tanzania Communications (Access and Facilities) Regulations 2005

MFUMO WA LESENI (CONVERGED LICENSING FRAMEWORK)

Tarehe 23 Februari, 2005, Mamlaka ilianzisha mfumo mpya wa utoaji leseni unaozingatia muingiliano wa teknolojia unaojulikana kama “ Converged Licensing Framework” (CLF). Leseni zinazotolewa katika mfumo huu hazifungamani na aina ya teknolojia inayotumika (Technology Neutral) wala aina ya huduma inayotolewa (Service Neutral). Zipo aina nne za leseni zinazotolewa katika mfumo huu mpya ambazo ni:

  • Leseni ya kujenga miundo mbinu ya mawasiliano (Network Facilities License (NFL))
  • Leseni ya kutoa huduma za mawasiliano (Network Services License (NSL))
  • Leseni za matumizi ya kutoa huduma za mawasiliano (Applications Service License (ASL))
  • Leseni ya Utangazaji (Contents Services License (CSL))

Kuna masoko manne: Kimataifa (International), kitaifa (National), kimkoa (Regional) na kiwilaya (District).

Aina nyingine ya leseni zinazotolewa ni

  • Leseni kwa ajili ya utoajiwa huduma za posta kwa Uma (Public Postal License)
  • Leseni kwa ajili ya utoaji wa huduma za nyaraka na vipeto kwa njia ya haraka (Courier Services License)
  • Leseni kwa ajili ya kutumia ya masafa ( Frequency user License)
  • Leseni kwa ajili ya kufunga na kutengeneza mitambo ya mawasiliano (Installation and Maintenance License)
  • Leseni kwa ajili ya kuagiza na kusambaza vifaa vya mawasiliano (Importationand and distribution License)
  • Leseni kwa ajili ya kuruhusu matumizi ya kifaa cha mawasiliano (Type approval )
  • Leseni kwa ajili ya kuruhusu matumizi ya Namba ( Numbering Resources)

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

MAFANIKIO:

1. Mfumo wa leseni wa mwingiliano wa teknolojia (Converged Licensing Framework”) ulioanzishwa mwaka 2005 umekuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya mawasliano. Kwa mfano leseni ya miundombunu, siyo tu tumeona maendeleo katika mitandao ya simu za mkononi, lakini vilevile tumeona kwa mara ya kwanza mitandao ya mkongo baharini “Submarine cables” ikifika kwenye pwani, kwa mfano “Seacom” ambayo uliizindua 2009, na “EASSY cable” ambayo ilizinduliwa 2010. Tumeona maendeleo mengi kwenye leseni ya matumizi (Application Service License) katika matumizi ya intanet, kutuma pesa kwa simu (M-Pesa ya Vodacom, Zap ya Airtel, Tigo-Pesa ya Tigo, Z-Pesa ya Zantel, Mobipawa ya E-fulusi). Kwa sasa ni rahisi kutulia simu ya mkononi kulipia bili za maji, umeme, DSTV nk.

2. Maendeleo ya Sekta ya Mawasiliano ya Simu Nchini

Sekta ya mawasiliano imekuwa kwa kasi sana katika kipindi kifupi. Katika miaka ya 1990 kulikuwa na kampuni moja tu ya simu. Mwaka 2000 kulikuwa na kampuni nne (4) za mitandao ya simu, na mwaka 2011 ziko 9 ambazo ni Vodacom, Airtel, Tigo, Zantel, TTCL, Benson Informatics, Sasatel, Seacom, na Six Telecoms. Kampuni zizotoa huduma (Application Service Licenses) zilikuwa 11 mwaka 2000, zikawa 23 mwaka 2005, na kufikia 68 mwaka 2010. Laini za simu zimeongezeka toka 284 109 mwaka 2000, na kuwa milioni 3.2 mwaka 2005, kufikia milioni 20.5 mwaka 2010.

3. Kufungua ofisi za kanda za TCRA

Mamlaka imefungua ofisi sita za kanda kwa lengo la kuwafikia wananchi kwa urahisi, kupnguza gharama za kufuata huduma makao makuu, na pia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma. Ofisi hizi zipo Zanzibar, Dodoma, Arusha, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam.

4. Usimamizi wa Masafa ya Mawasiliano.

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekuwa ikutumia kwa ufanisi mitambo sita ya kisasa, pamoja na minne iliyonunuliwa mwaka 2006 ili kujiimarisha na kujiongezea uwezo wake wa kupanga na kuthibiti matumizi ya masafa nchini. Hivi sasa ofisi za Kanda ya Mamlaka ina mitambo (mobile frequency monitoring station) inayotumika kusimamia masafa. Kuwepo kwa mitambo hiyo kumepunguza muda wa kuchunguza na kumpangia muombaji masafa na kutambua kwa urahisi watumiaji haramu wa masafa na kuelewa mahali walipo; na kuzuia muingiliano (harmful interference) baina ya watumiaji wa masafa hivyo kuongeza ubora wa mawasiliano nchini.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi;

5. Usimamizi wa Namba za Simu na Uboreshaji wa Matumizi ya Namba za Dharura

Usimamizi wa namba za mawasiliano pia umekuwa na mafanikio. Namba za simu ni moja kati ya rasilimali adimu za taifa inayotambulisha watumiaji wa simu na kuwezesha maunganisho ya simu za wateja ndani na nje ya nchi katika mitandao mbalimbali. Mamlaka imesimamia kikamilifu utekelezaji wa Mpango wa Namba wa Taifa (National Telecommunication Numbering Plan) uliopitishwa mwaka 2005/06 ili kukidhi ongezeko la wateja wa simu za mkononi. Hadi kufikia Novemba 2006 makampuni yote yalikuwa yametekeleza agizo lililowataka kubadilisha namba za mitandao yao.

Hali kadhalika, ili kuwezesha wananchi kutumia namba za dharura kikamilifu, kama 111 na 112, Mamlaka ilitenga jumla ya Shs.522 milioni kwa ajili ya kusaidia Jeshi la Polisi kujenga kituo cha kisasa cha mawasiliano ya dharura (Emergency Call Centre) kinachosimamiwa na Jeshi hilo ili kuhudumia wananchi watakaofikwa na matatizo mbali mbali. Kituo hicho kimekamilika na kina mitambo ya kisasa yenye uwezo wa kupokea simu na kutunza kumbukumbu ya simu zilizoingia hata kama haikupokelewa na kutoa taarifa ya matatizo yaliyojitokeza. Mamlaka pia ilighaamia mafunzo ya maafisa 45 wa polisi ili kuweza kutumia vifaa hivyo na kituo hiki tayari kimekabidhiwa kwa Jeshi la Polisi. Ni rai yetu kuwa kituo hicho kitatumiwa kikamilifu kwa manufaa ya wananchi wote.

6. Usimamizi wa Ubora wa Vifaa vya Mawasiliano (Standards and Type Approval)

Usimamizi wa ubora vya vifaa vya mawasiliano ni eneo jingine ambalo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania inajukumu kwa mujibu wa sheria kusimamia ubora wa vifaa vya mawasiliano vinavyoaingizwa nchini na kuunganishwa na mtandao wa taifa kwa ajili ya mawasiliano mbali mbali. Lengo la kuthibiti uingizaji na usambazaji wa vifaa na vyombo vya mawasiliano ya simu na redio nchini ni kuilinda mitandao na watumiaji wa vifaa kwa kuhakikisha kuwa vifaa/vyombo husika vinakidhi viwango vilivyowekwa kitaifa na kimataifa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

7. Kusimamia gharama za muingiliano kati ya Makampuni ya simu nchini (Interconnection Rates).

Mheshimiwa Mgeni Rasmi, gharama hizi kimsingi ni changamoto kubwa kwa nchi zingine lakini hapa Tanzania, TCRA imefanikiwa kusimamia suala hili na kuweka viwango ambavyo hutumika na makampuni ya simu. Kabla ya mwaka 2002, viwango hivi vilikuwa ni senti 25 za kimarekani, na zilpunguzwa toka mwaka 2004. Mwaka 2008 Januari gharama hizi ziliwekwa katika kiwango cha senti 7.83 za kimarekani, mwaka 2009 senti 7.65 za kimarekani, mwaka 2010 senti 7.49 za kimarekani na mwaka huu toka Januari 1 senti 7.32 za kimarekani, ambazo ni sawa na Sh 103 za kitanzania. Kuwekwa kwa viwango hivi kumesababisha kupungua kwa gharama za simu kila mwaka.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

8. Mpango Kabambe (Strategic Plan)

Mamlaka ilitengeneza mpango kabambe (Strategic Plan) kwa kipindi cha 2006/7 hadi 2010/11. Mpango huu uliweka bayana dira, dhima na vipaumbele katika kazi za Mamlaka na utekelezaji wake hatua kwa hatua.

Mpango huu ni moja ya sababu za mafanikio ya udhibiti wa sekta hii na njia inayoihakikishia Mamlaka kuwa shughuli zake mwaka hadi mwaka zinafuata utaratibu na kukidhi mahitaji ya sekta na hivyo kuweza kuisimamia sekta ya mawasiliano kwa ufanisi. Hivi sasa tuko katika mkakati wa kutengeneza tena mpango kabambe mpya wa 2011/12 hadi 2015/16 ambao uko katika hatua za mwisho kukamilika.

9. Uimarishaji Habari na Matumizi ya Wavuti (Internet) na Anwani Pepe zenye Kuiwakilisha Tanzania (.tz ccTLD)

Mamlaka inaendelea kuimarisha utumiaji wa intaneti ili kuhamasisha watanzania kuwa sehemu ya “Jamii habari” (information society), yaani kuwa na mfumo wa maisha ambao jamii ina fursa, haki na uwezo wa kuwasiliana, kujifunza, kupashana habari bila vikwazo kupitia “Internet”. Hivi sasa kwa mujibu wa takwimu za utafiti uliofanywa na Mamlaka ya mawasiliano kuna watumiaji wa intaneti (wavuti) wapatao milioni 4.8.

Mwaka 2008 Mamlaka ilichukua hatua za makusudi na kuanzisha kituo maalum Tanzania National Information Centre (tzNIC) kwa ajili ya kusajili majina ya mitandao na anwani pepe zinazotumia jina la nchi yetu (.tz ccTLD). Matumizi ya kituo hicho yataboresha huduma hiyo na kukuza utaifa wetu.

Hali kadhalika, Mamlaka ikishirikiana na jumuiya ya watoa huduma ya intaneti (TISPA – Tanzania Internet service Providers Association) imenunua swichi za intaneti (IXPs – Internet Exchange Points) zilizowekwa kwenye miji ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Dodoma, na baadae Mbeya. Madhumini ya kuwekwa kwa swichi hizi ni kuwafanya watumia huduma za internet na hususani e-mail kuwasiliana kwa urahisi zaidi bila kulazimika e-mail zao kwenda katika mitambo nje ya nchi, na hivyo kupunguza gharama na kuongeza kasi ya intaneti.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

10. Zoezi la Usajili wa Laini za Simu

Kuanzia tarehe 1julai 2009, mamlaka ilisimamia zoezi la usajili wa laini za simu. Kusidi la zoezi hili ni pamoja na kuwalinda wateja, kuhakikisha huduma za ziada katika huduma za simu za mkononi zinakuwa salama kwa mfano huduma za kibenki kwa kutumia simu na huduma za kulipia Ankara za huduma mbalimbali. Hali kadhalika, ilikusudiwa makampuni ya simu yaweze kuwafahamu wateja wake.

Zoezi hili limeenda vizuri na takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80% ya laini za simu zimesajiliwa tayari, yaani laini milioni 16.5 kati ya laini 20.5 zilizopo sokoni zimesajiliwa. Haya ni mafanikio makubwa kwa nchi. Nitumie nafasi hii kuyapongeza makampuni ya simu kwa ushirikiano walioonesha katika utekelezaji wa zoezi hili. Hali kadhalika, niwapongeze watanzania waliojitokeza kwa wingi na kuitikia wito wa kusajili laini zao za simu na kuwasihi wale ambao bado hawajafanya hivyo, waharakishe na kutekeleza agizo hili kwani kwa mujibu wa sheria, ni kosa la jinai kuwa na laini ambayo haijasajiliwa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

11. Sekta ya Utangazaji

Mamlaka inadhibiti sekta ya utangazaji, ambalo limeonesha mafanikio makubwa sana miaka ya karibuni. Vyombo vya Utangazaji, vikiwa ni sehemu ya Mawasiliano kwa umma ni muhimu sana kwa maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.

Tangu kufunguliwa kwa Sekta (liberalization) ya Utangazi nchini kwa wawekezaji binafsi mwaka 1993, kumekuwepo na ukuaji wa kasi kutoka radio moja tu (Radio Tanzania) hadi Radio 57 na vituo vya televisheni 29 hadi sasa. Maombi mbali mbali ya leseni za utangazaji yako katika hatua mbali mbali za mchakato wa kutoa leseni hizo kwa mujibu wa sheria.

Mamlaka inasimamia mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa utangazaji kutoka analojia (analogue) kwenda dijitali (digital). Mabadiliko haya yaliridhiwa na wanachama wa shirika la Mawasiliano ya Kimataifa (International Telecommunications Union – ITU) katika mkutano wao uliofanyika mjini Geneva – Uswisi June 2006. Tanzania ni mwanachama wa ITU. Mkutano huo ndio uliofikia makubaliano na kuweka taratibu ambazo zinapaswa kufuatwa na nchi zote wanachama ikiwa ni pamoja na kuanza kwa kipindi cha mpito cha urushaji wa matangazo ya digital. Mabadiliko hayo yanatakiwa yawe yamekamilika ifikapo 2015. Tanzania pamoja na nchi zingine za Afrika mashariki tumekubaliana tuwe tumekamilisha zoezi hili ifikapo 2012. Hivi sasa kuna makampuni matatu ambayo yamepewa leseni ya miondombinu (Network Facility License) ili kuwa “Multiplex Operator”. Katika mfumo wa digitali, makampuni mengine yatapewa leseni ya “utangazaji” (Content Service License).

Uhamaji huu una gharama zake, ikiwemo gharama za vin’gamuzi (decoder) kwa ajili ya kunasia matangazo ambapo gharama yake inategemewa kufikia karibu dola za kimarekani 50. Tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kuwasaidia wananchi kwa kuwaondolea kodi ili wasikose huduma za utangazaji hapo itakapozimwa mitambo ya analojia inayotumika kwa sasa.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

12. Huduma za Posta na Simbo za Posta (Post Code).

Maendeleo ya sekta ya posta ni pamoja na ukuaji wa sekta kwa kuongeza ushindani, hususan kwenye usambazaji wa vifurushi. Mamlaka imepanga leseni tano kwa ajili ya utoaji wa huduma za nyaraka na vipeto kwa njia ya haraka (Courier Services License).

Moja kati ya hatua zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mawasiliano katika utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Posta (2003) ni kuibua mradi wa kuanzisha anwani mpya za kitaifa (Postcode), ambao una mfumo wa kutumia tarakimu tano (Five Digits Numerical System). Mradi huu ulizinduliwa rasmi na Mh. Makamu wa Rais mwezi Januari 2010 mjini Arusha. Mradi huu unanuia kuandaa anwani ambazo zitawezesha barua na vipeto kufikishwa kwenye makazi au ofisini ya mteja ili kumpunguzia mhusika muda anaopoteza kufuata barua posta. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano na wadau wote muhimu. Manufaa ya mfumo huu mpya wa anwani yatakuwa si kwa posta tu bali kwa jamii nzima. Utaboresha kazi za taasisi nyingine muhimu ikiwemo Polisi, Zimamoto, Mamlaka ya Mapato, Hospitali (Ambulance services), Biashara (Registration) na Uhamiaji. Vile vile utarahisha utekelezaji wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano kwa kuwezesha bidhaa zinazonunuliwa kwa njia ya mtandao (e-commerce).

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

13. Ushirikiano wa Kimataifa katika mawasiliano

Moja kati ya majukumu ya Mamlaka ya Mawasiliano yaliyoainishwa kwenye Sheria iliyoianzisha ni pamoja na kulipia michango kwa niaba ya serikali, kushiriki kwenye taasisi za mawasiliano za kimataifa. Mamlaka imekuwa iikilipia michango hiyo kila mwaka na kuifanya Tanzania kufaidika na huduma zitolewazo na taasisi hizo. Taasisi za kimataifa zinazohusika kwa sasa ni pamoja na Umoja wa simu Duniani (International Telecommunication Union (ITU); Umoja wa Posta Duniani (Universal Postal Union, UPU); Umoja wa simu wa jumuia ya madola (Commonwealth Telecommunications Organisation (CTO)), Commonwealth Broadcasting Association (CBA). Kwa upande wa kontinenti la Afrika, kuna Umoja wa simu Africa (African Telecommunications Union (ATU)), Umoja wa Posta Afrika (Pan African Postal Union (PAPU)); Umoja wa Wadhibiti wa Mawasiliano Kusini mwa Afrika (CRASA), Chama cha Watangazaji Kusini mwa Afrika (SABA), Umoja wa Taasisi za Mawasiliano Afrika Mashariki (East African Communication Organisation (EACO)), na taaasisi zinginezo.

14. Mawasiliano Towers.

Kwa muda mrefu sasa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ilikusudia kuwa na ofisi zake za kutosheleza wafanyakazi kutoa huduma wakiwa mahali pamoja, badala ya sehemu mbili, yaani ofisi zetu zilizokuwa Upanga na Mikocheni. Jitihada zilifanyika kwa muda mrefu ili kuhakikisha kuwa azma hii inafikiwa mapema ili kuwa na ofisi nzuri zenye miundombinu mahiri ya kutekeleza majukumu ya Mamlaka hii, ikizingatiwa kukua kwa haraka kwa teknolojia katika sekta ya mawasiliano.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Kama ulivyoona wakati wa ukaguzi wa jengo hili, Idara zote za Mamlaka ziko mahala pamoja tofauti na ilivyokuwa awali ambapo zilikuwa katika majengo mawili, sehemu tofauti. Hali hiyo ilipunguza jitihada za kutoa huduma kwa ufanisi kama inavyokusudiwa. Gharama za jengo hili ni shilingi za kitanzania 39, 454, 028, 936.00. Jengo hili limejengwa na kampuni ya China Railway Jianchang Engineering (T) Co. Ltd (CRJE) kama kontrakta mkubwa, na makontrakta wadogo wa huduma, na Mshauri Mtaalamu (Consultant) ni Archplan International Inc. Hili jengo lina gorofa kumi na nne, na kwa hivi sasa ofisi zote zinatumika, ikiwa pamoja na maofisi ya TCRA, na taasisi za umma na makampuni. Vile vile, Mamlaka ina mpango wa kuanzisha “Communication Museum” katika jingo hili. Hii “museum” itaweka kumbukumbu kuhifadhi historia ya mawasiliano hapa nchini.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

CHANGAMOTO

1. Gharama za huduma za mawasiliano

Pamoja na mafanikio mazuri katika sekta ya mawasiliano, kumekuwepo na changamoto mbalimbali, kwa mfano gharama za huduma za mawasiliano ya simu na “Interneti” ingawa zimeshuka, zimebakia kuwa juu ikilinganishwa na kipato cha mwananchi. Hii kwa kiasi kikubwa imeendelea kusababishwa na kutokuwepo kwa miundo-mbinu na huduma zingine zinazohitajika katika urahisishaji wa kutoa huduma za mawasiliano.

2. Kuunganisha Mawasiliano vijinini

Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ni mhimili wa maendeleo ya taifa na ulimwengu kwa ujumla, mijini na vijijini. Kwa kuwa lengo kubwa la serikali ni kuwawezesha wananchi kupata Habari (universal access) na kuwa kwa njia hiyo wanachi walio wengi hawataachwa nyuma katika maendeleo ndani ya karne hii ya utandawazi, serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano itaendelea kuhakikisha kuwa rasilimali adimu zikiwemo masafa na namba za simu zinatumika kwa makini (efficiently and effectively) ili kukidhi mahitaji ya taifa na kuharakisha maendeleo. Mamlaka itandelea kuchangia katika mfuko wa mawasiliano.

3. Ujenzi wa mkongo wa mawasiliano kupitia kwenye miundombinu

Ujenzi wa mkongo wa mawasiliano (Optical fibre) unategemea upatikanaji wa vibali vya kujenga kwenye miundombinu mingine (Right of way) kama kwenye barabara, reli, njia za umeme. Mkongo wa Taifa utakapokamilika, inategemewa utapunguza kwa kiasi kikubwa huduma za mawasiliano nchini.

4. Wizi wa Simu za Mkononi na miundombinu ya mawasiliano

Kwa kipindi kirefu watumiaji na watoa huduma katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wameendelea kupata hasara, kutokana na wizi wa simu za mikononi na makampuni yanapata hasara kubwa kutokana na kuibiwa kwa miundo mbinu ya mawasiliano katika maeneo mbambali nchini.

Ili kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa wizi wa simu za mkononi Mamlaka kwa kushirikiana na watoa huduma na wadhibiti wa mawasiliano Afrika Mashariki wamekubaliana kwamba kila kampuni iweke vifaa vya kutunza kumbukumbu ya simu zote zinazounganishwa na mtao wake ili wizi utokeapo wasaidie kufunga simu hiyo isiweze kuunganishwa na mtandao mwingine endapo ituzwa kwa mteja mwingine. Hili linakwenda sambamba na zoezi la uandikishaji wa laini za simu za mkononi.

5. Usalama katika Mtandao (Cybersecurity)

Changamoto ya usalama katika mtandao wa intaneti ni jambo la kimataifa na Tanzania kama sehemu ya jumuia ya kimataifa, haina budi kujiandaa kukabiliana nayo. Mamlaka imekuwa inajitahidi kushiriki katika mafunzo na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hii. Aidha sheria mpya ya mawasiliano ya elektroniki na posta (EPOCA) imeainisha njia mbalimbali za kukabiliana na tatizo hili kisheria.

6. Matumizi ya Intaneti kwa maendeleo

Matumizi ya Intaneti mazuri yanaweza kuchangia katika maendeleo ya nchi katika maeneo kama Serikali Mtandao (e-Government), elimu mtandao (e-Education), afya mtandao (e-health), biashara mtandao (e-commerce) na kadhalika. Kuwepo kwa mkongo wa mawasiliano kutapelekea changamoto ya wananchi kuwa na ujuzi wa kutumia intanet kwa maendeleo.

7. Uharibifu wa Mazingira

Tokea huduma ya simu za mikononi na huduma ya kulipia kabla “Prepaid Services” zianze hapa nchini, kumekuwa na uchafufuzi mkubwa wa mazingira kwa kutupa ovyo karatasi za vocha za muda wa maongezi kila wanapomaliza kuzitumia. Aidha, betri na hata simu mbovu zimekuwa zikitupwa bila utaratibu wa kulinda mazingira. Mamlaka kwa kushirikiani na wadau mbalimbali wa Mazingira pamoja na makampuni ya simu wameweka mikakakati mbalimbali kukabiliana na tatizo hili ikiwa ni pamoja na mfumo wa kuweka fedha kwa njia ya electroniki.

8. Maudhui

Maudhui katika sekta ya Mawasiliano ni changamoto ingine ambayo hatuna budi kukabiliana nayo ili kulinda maadili ya taifa letu. Mamlaka ina kamati ya maudhui ambayo inafuatilia kwa ufanisi changamoto zinazotokana na swala hili. Majukumu ya Kamati ni pamoja na kumshauri Waziri wa Utangazaji juu ya masuala ya kisera; kusimamia maudhui; kushughulikia malalamiko ya watumiaji na watoa huduma.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi,

Hitimisho

Baada ya maneno haya, kwa heshima na taadhima, naomba nimkaribishe Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania aseme machache na kumuomba Mh. Waziri akukaribishe kutuzindulia jengo hili la “Mawasiliano Towers”.

Asante sana.

No comments: