Tuesday, January 11, 2011

TAARIFA YA MATATIZO YANAYOWAKABILI WAFANYAKAZI WANATAALUMA WA CHUO KIKUU CHA DODOMA

Utangulizi

Tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) mwaka 2007 kumekuwa na maendeleo makubwa ya miundo mbinu mbalimbali hasa majengo na barabara. Chuo kimepanuka kwa kiwango cha kuridhisha na hii ni hatua ya kupongezwa na mpenda maendeleo yeyote.

Sanjari na ujenzi wa miundo mbinu kutokana na kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi watumishi wa fani mbalimbali wamekuwa wakiajiriwa tangu kuanzishwa kwa chuo. Katiba ya Chuo (University Charter) imeweka wafanyakazi katika makundi makuu mawili. Moja ni kundi lenye wafanyakazi wanataaluma ambao pamoja na mambo mengine kazi yao kubwa ni ufundishaji, utafiti na ushauri; na pili ni kundi la wafanyakazi wa upande wa utawala. Hata hivyo chuo kinakua kwa haraka sana na hivyo kuhitaji idadi ya wafanyakazi iendanayo na kasi ya ukuaji wa chuo.

Matatizo ya Wafanyakazi Wanataaluma UDOM

Pamoja na jitihada nzuri ya kuajiri wafanyakazi ili kukidhi mahitaji ya chuo, kumekuwapo matatizo mbalimbali yanayowakabili wafanyakazi katika Chuo Kikuu cha Dodoma. Matatizo makubwa yanaegemea katika swala la malipo ya stahili mbalimbali pamoja na mishahara kama inavyoelekezwa katika nyaraka mbalimbali za serikali. Mkutano wa 4 wa UDOMASA umeainisha matatizo hayo ni kama yafuatavyo:

Mosi, wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma hawajapata mishahara mipya tangu kutangazwa kwa ongezeko la asilimia 20-30 mwezi Julai 2010 kupitia Waraka wa Msajili wa Hazina namba 4, wa mwaka 2010 uliotolewa 3 Agosti 2010. Ushahidi toka Hazina umeonesha kwamba mishahara mipya ililipwa mwezi Novemba 2010 kwa vyuo vikuu vyote vya umma ikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma. Mkutano umeazimia kwamba fedha hizo za mishahara ambayo menejimenti ya UDOM imekata kupitia mishahara mipya ya Hazina zilipwe kwa wahusika mara moja wakati mkutano wa wanataaluma unaendelea.

Pili, Hazina imekuwa ikilipa mishahara ya juu katika ngazi husika lakini menejimenti ya UDOM inapunguza kwa visingizio mbalimbali. Kwa mfano, mfanyakazi mwenye Check No 11818320 (PUTS 15), Hazina mwezi Novemba na December ilimlipa 2,269,890/=, Chuo kilimlipa 1,605,310/= jambo linaloashiria udanganyifu. Payroll ya Hazina inaonesha kuwa fedha inayotoka hazina ni tofauti na fedha anayolipwa mwanataaluma hapa UDOM. Wanataaluma wana wasiwasi kuwa tabia hii ya kupunguza mishahara imekuwa ikiendelea kwa muda sasa. Hivyo, mkutano umeazimia kuwa fedha zote ambayo menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma imekuwa ikikata zilipwe.

Tatu, upunguzwaji wa mishahara inayotoka Hazina kimsingi umeathiri uchangiaji wetu katika mifuko ya hifadhi ya jamii (NSSF, LAPF, PPF, PSPF n.k.), pamoja na michango yetu katika vyama vya wafanyakazi kama vile RAAWU. Hali hii ya upunguzwaji mishahara pia umeathiri uchangiaji wa mwajiri katika mifuko ya hifadhi ya jamii kama inavyotakiwa na sheria husika. Mfano mfanyakazi anayelipwa 853,300/= badala ya 1,248,070/= kama ilivyo katika payroll ya hazina anachangia LAPF kiasi cha 42,665/= (asilimia 5) kwa mwezi badala ya 62,403.3/= kwa mwezi. Pia uchangiaji wa mwajiri unapungua hali ambayo itaathiri mafao ya uzeeni. Mkutano umeazimia kuwa kiasi chochote ambacho kilipunjwa katika mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na vyama vya wafanyakazi ilipwe mara moja wakati wanataaluma wanaendelea na mkutano wao.

Nne, Chuo Kikuu cha Dodoma kimekuwa kikitoa salary slips zake badala ya kutoa salary slips zinazotka Hazina. Aidha menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma imedai kuwa Hazina haitoi salary slips. Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na uongozi wa UDOMASA umeonesha kuwa salary slips zimekuwa zikichukuliwa kutoka hazina na maafisa wa UDOM. Madai ya menejimenti ya UDOM kuwa hazina haitoi salary slips yanaashiria mbinu inayotumiwa kupunja mishahara ya wafanyakazi inayotoka Hazina. Mkutano umeazimia kuwa kila mfanyakazi apatiwe salary slips zake tangu Hazina waanze kutoa.

Tano, fedha za kujikimu wakati wa kuanza ajira pamoja na usafirishaji wa mizigo wakati wa kuja kuanza kazi hatujalipwa. Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma imeripotiwa mwaka 2008 ikisema kuwa zaidi ya asilimia 95 ya wafanyakazi wa taasisi hii hawakustahili kulipwa fedha za kujikimu. Mazungumzo ya hivi karibuni yamepelekea menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma kukubali kuwa fedha za kujikimu ni stahili ya mfanyakazi yeyote anapoanza kazi, ingawa wamesema kinagaubaga kuwa haitaweza kulipa stahili hizo kwa sasa kwa kisingizio kuwa ni fedha nyingi sana. Mkutano umeazimia kuwa Chuo Kikuu cha Dodoma kilipe stahili hizi kwa wafanyakazi wote. Zoezi hili la malipo ya fedha ya kujikimu lifanyike mara moja wakati wanataaluma wakiendelea na mkutano wao.

Sita, katika kikao cha tarehe 29 Desemba, 2010 kati ya menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma na viongozi wa UDOMASA iliripotiwa na menejimenti ya chuo kuwa wafanyakazi 409 hawajasajiliwa katika payroll ya Hazina. Aidha menejimenti imeshindwa kutoa sababu za msingi kwa tatizo hili licha ya kuwa wafanyakazi hao wameshafanya kazi kwa miezi kadhaa sasa. Mkurugenzi wa Rasilimaili Watu katika Chuo hiki alitoa sababu zisizoweza kuaminika kuwa Hazina ndiyo yenye matatizo. Aidha, uongozi wa UDOMASA imeuliza swala hili Hazina lakini lawama zilirudishwa menejimenti ya UDOM. Hali hii ya kutoingizwa wafanyakazi katika Payroll ya Hazina, pamoja na mambo mengine unapelekea wafanyakazi wa UDOM kuishi kwa mashaka makubwa kwa kuwa menejimenti ya UDOM imekuwa ikitenda kazi zake si kwa kuzingatia kanuni bali kwa vitisho. Mkutano umetoa umeazimia kuwa wafanyakazi wote ambao mpaka sasa walikuwa hawajaingizwa kwenye payroll ya Hazina wawe wameingizwa ifikapo mwisho wa mwezi Januari, 2011. Aidha, ofisi iliyohusika na uzembe huu ndani au nje ya menejimenti ya UDOM iwajibike.

Saba, Chuo Kikuu cha Dodoma kimeandaa Sera ya Mazishi ambayo inafanya mwajiri kukwepa wajibu wake wa kisheria. Menejimenti ya UDOM kwa miezi kadhaa sasa imekuwa ikikata 3,000/= kwa wafanyakazi kila mwezi bila idhini ya waajiriwa. Na uwajibikaji wa fedha haupo wazi. Hali hii inaashiria kuwa menejimenti ya chuo inafanya kazi nje ya kanuni na sheria zinazosimamia makato ya fedha. Mkutano umeazimia kuwa chuo kisimamishe ukataji huo na timu huru iundwe na isimamie fedha hizo, wakati wadau wakifanya mchakato wa kuijadili upya kuhakikisha inakidhi mahitaji yao, na mwajiri hakwepi jukumu lake.

Nane, lingine ni kutokuwepo kwa samani katika ofisi za wanataaluma na wengine hawana ofisi kabisa. Tatizo hili la samani na vitendea kazi vingine limefanya mazingira ya kazi kuwa magumu mno kwa utendaji wa wanataaluma kama vile ufundishaji na pia wanafunzi wameathirika kwa kuwa wanawakosa walimu wao maofisini. Vitendea kazi kama vile kompyuta na printer zipo katika baadhi ya ofisi ya wakuu wa idara pekee. Pia ukubwa wa madarasa unaadhiri utendaji wa walimu kwa kuwa baadhi ya madarasa yana idadi kubwa ya wanafunzi (mfano zaidi ya 1200 katika ukumbi mmoja). Mkutano umeazimia kuwa wanataaluma wote wapatiwe ofisi zenye samani (meza, viti, makabati, dustbin n.k), pamoja na vitendea kazi vingine kama kompyuta, projector ili kuweza kurahisisha mazingira ya kazi.

Juhudi zilizofanywa na UDOMASA kutatua matatizo tajwa

Matatizo yaliyoanishwa hapo juu ni ya msingi na yamekuwepo tangu kuanzishwa kwa chuo mwaka 2007. Jumuiya ya wanatalaamu (UDOMASA) imefanya juhudi mbalimbali bila mafanikio. Juhudi hizo ni kama ifuatavyo

Tarehe 17 Novemba, 2008 ulifanyika mkutano mkuu wa kwanza wa UDOMASA kwa ajili ya kujadili mambo ya msingi likiwemo suala la fedha za kujikimu. Jambo hili lilijadiliwa tena katika mkutano mkuu wa pili tarehe 18 Novemba, 2008. Pamoja na juhudi za uongozi wa UDOMASA kuongea na menejimenti ya chuo walijibiwa kuwa asilimia kubwa ya waajiriwa UDOM hawastahili fedha za kujikimu. Hali hii ilipelekea wanataaluma kugoma kufanya kazi, na baadaye wanataaluma watatu kusimamishwa kazi kwa kisingizio cha kuchochea mgomo huo. Waliosimamishwa kazi ni pamoja na Dr Kisanga, Titus Mpemba, na Rajab Chipila. Kutokana na kusimamishwa kwa wanataaluma hao umoja wao uliyumbishwa au kusambaratishwa kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja hadi hali ya umoja ilipofufuka mwishoni mwa mwaka jana, 2010 baada ya uongozi wa kwanza wa UDOMASA kumaliza muda wake kufuatia uchaguzi uliofanyika tarehe 19 Oktoba, 2010.

Tarehe 10 Novemba, 2010 uongozi mpya UDOMASA ulikwenda kuonana na menejimenti ya UDOM kwa ajili ya utambulisho lakini menejimenti ikawakataa kwa kisingizio kuwa hawakuwa na sifa za wanataaluma. Hata hivyo viongozi wapya wa UDOMASA waliiambia menejimenti ya UDOM kuwa wapo tayari kuachia ngazi iwapo menejimenti itatoa barua kueleza kutowatambua na kuthibitisha si wanataaluma, jambo ambalo halikutekelezwa. Siku chache baadaye mwenyekiti mpya wa UDOMASA, Paul Loisulie, alipokea barua kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo ambayo ilishauri kuwa viongozi wapya wa UDOMASA wanatakiwa kutumia muda mwingi ili kujiendeleza kimasomo na si kujiingiza katika siasa za UDOMASA. Barua hii ambayo kimsingi haikurejea kauli ya Makamu Mkuu wa Chuo ya kuwa viongozi wapya wa UDOMASA hawakuwa na sifa zinazotakiwa ilitafsiriwa na wana UDOMASA kuwa ni dhamira ya chuo kudhoofisha umoja wa wanataaluma hapa chuoni.

Baada ya muda si mrefu uongozi mpya wa UDOMASA uliomba kibali cha mkutano mkuu kutoka kwa DVC-PFA na kukubaliwa. Hivyo mkutano mkuu wa tatu ukafanyika tarehe 4 Desemba 2010 ambao pamoja ulijadili fedha za kujikimu, mishahara mipya kama inavyoelekezwa na waraka wa Hazina namba 4, 2010, na sera ya mazishi. Mkutano uliamua kuwa viongozi wa UDOMASA wafanye uchunguzi wa kinachoendelea kwa masuala ya fedha ya kujikimu na mishahara mipya.

Ufuatiliaji ulifanyika kwa kwenda Ofisi ya Utumishi wa Umma; Hazina; na Wizara ya Elimu. Hazina ilikiri kuwa mishahara mipya ilishapelekwa katika vyuo vikuu vyote kikiwamo Chuo Kikuu cha Dodoma. Aidha, Hazina iliongeza kuwa fedha ya kujikimu inatakiwa kulipwa kupitia Other Charges (OC) ya taasisi husika, kwa hiyo UDOM pia ilitakiwa kulipa fedha ya kujikimu kupitia OC.

Viongozi wa UDOMASA walipokwenda Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma waliambiwa kuwa ofisi hiyo inahusika na sera na kwamba masuala ya taasisi za umma yanashughulikiwa na Msajili wa Hazina. Wakaahidi kuwa wangetafuta utaratibu wa kuzungumza na Hazina. Jitihada za kuonana na Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu hazikuzaa matunda kwa kuwa wahusika hawakuwepo.

Baada ya kurudi kutoka katika ofisi za juu, uongozi wa UDOMASA ulifanya jitihada kuonana na Msaidizi wa Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala) na Mkurugenzi wa rasilimali watu UDOM ambao walidai kuwa mishahara mipya imeletwa lakini ilikuwa na makosa makubwa. Pia walikiri kuwa fedha ya kujikimu zinatakiwa kutoka ndani ya chuo (OC) lakini ikadaiwa kuwa fedha hazitoshi kulipa wafanyakazi kwa kuwa ni wengi sana kwa sasa.

Tarehe 29 Desemba, 2010 uongozi wa UDOMASA ulikutana na menejimenti ya UDOM ambapo taarifa ya mishahara kuanzia 2007 hadi Novemba 2010 ilisomwa na Mkurugenzi wa rasilimali watu. Pia iliripotiwa kuwa wafanyakazi 409 hawakuwapo katika payroll ya hazina. Menejimenti ya chuo ilitoa lawama kwa hazina kwa matatizo yanayohusiana na mishahara, fedha ya kujikimu pamoja na wafanyakazi 409 kutokuwapo katika orodha ya hazina. Hivyo, baada ya majadiliano kikao kiliunda timu ya watu watano (Mkurugenzi rasilimali watu, Msarifu, Wawakilishi wawili wa UDOMASA, na mwakilishi mmoja wa RAAWU) ili kuweza kufuatilia matatizo hayo. Pia ilikubaliwa kuwa fomu ziletwe ili ziweze kujazwa na wafanyakazi ambao hawapo katika payroll ya hazina ili timu iweze kwenda nazo wiki ifuatayo. Aidha, ilikubaliwa pia Makamu Mkuu wa Chuo asionane na wafanyakazi kwa ajili ya kutakiana heri ya mwaka mpya mpaka hapo timu itaporudi kutoka Dar es Salaam.

Kinyume na makubaliano, Mkurugenzi rasilimali watu pamoja na Msarifu walikwenda Dar es Salaam siku iliyofuata hali ambayo iliwapa taabu viongozi wa UDOMASA pamoja na wafanyakazi kwa ujumla. Kutokana na hili viongozi wa UDOMASA walikwenda kumuuliza Naibu wa Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala) kuhusu safari ya ghafla ya watu waliotakiwa kuwa katika timu ya kufuatilia matatizo, lakini alieleza kuwa safari ile ilikuwa ya mambo ya bajeti. Tuliamini kimsingi, bila ushahidi wowote.

Mwenyekiti na Katibu wa UDOMASA pamoja na Mwenyekiti wa RAAWU tawi la UDOM waliweza kuondoka tarehe 4, Januari 2011 kwenda Dar es Salaam kuungana na Msarifu na Mkurugenzi rasilimali watu kwa ajili ya kutatua matatizo yanayowakabili wafanyakazi kama ilivyokubaliwa katika kikao cha tarehe 29 Desemba, 2011.

Wakati tunaendelea kusubiri majibu kutoka timu iliyokwenda Dar es Salaam tuliona matangazo yaliyobandikwa katika mbao mbalimbali za matangazo yakidai kuwa Makamu Mkuu wa Chuo alitaka kuongea na wafanyakazi tarehe 6 Januari, 2011 saa nane mchana. Mkutano huu wa Makamu Mkuu wa Chuo na wafanyakazi ulikwenda kinyume na makubaliano ya kikao cha tarehe 29 Desemba, 2010. Hivyo, Makamu Mkuu wa Chuo alipomaliza kutoa taarifa katika mkutano wake na wafanyakazi, Makamu Mwenyekiti wa UDOMASA alimtaka ajibu madai ya msingi ya wafanyakazi (fedha za kujikimu, mishahara mipya) kwa kuwa alifanya mkutano kinyume na makubaliano. Aidha, Makamu Mkuu wa Chuo pia alitakiwa kueleza habari zilizozagaa kuwa chuo kililetewa mishahara mipya kuanzia Novemba, 2010 lakini chuo hakikuwa tayari kulipa kama ilivyoletwa kutoka hazina. Makamu Mkuu wa Chuo hakuweza kujibu. Aidha, katika mkutano wa Makamu Mkuu wa Chuo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Mipango, Fedha na Utawala) alieleza kuwa amepokea barua ikimshauri kuanza kupunguza deni la fedha ya kujikimu kupitia OC.

Tarehe 8 Januari, 2011 wanataaluma walifanya mkutano mkuu wa nne ikiwa pamoja na mambo mengine kupokea taarifa ya maswala muhimu ya stahili za wafanyakazi. Baada ya kujadiliana kuanzia saa nane mchana hadi saa 12 jioni mkutano uliahirishwa kwa masharti ya kuendelea siku ya Jumatatu ya tarehe 10 Januari, 2011.

Hitimisho

Kwa kuwa uongozi wa UDOMASA umefanya jitihada za kufuatilia utatuzi wa matatizo haya yanayohusiana na fedha katika Hazina; Wizara ya Elimu; na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na kuonekana kuwa matatizo yapo hapa ndani ya chuo; na kuwa menejimenti ya UDOM mpaka wanataaluma wanakwenda kwenye mkutano haikuwa tayari kushughulikia matatizo haya, Mkutano Mkuu wa nne wa UDOMASA wa tarehe 8 Januari, 2011 uliamua umwombe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete aingilie kati suala hili. Pia wanataaluma wameamua kuendelea kufanya mikutano mpaka hapo matatizo yatakapopatiwa ufumbuzi.

Paul Loisulie,

Mwenyekiti

UDOMASA.

University of Dodoma Academic Staff Association

University of Dodoma, Chimwaga Complex, P.O. Box 259,Udom, Cell +255 755 210310,

+ 255 784 855444,+ 255 712 792561, Email: khamismkanachi@yahoo.com


No comments: