Tuesday, December 12, 2017

NEC yawajibu UKAWA

Na Mwandishi Maalum
MKURUGENZI wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani alisema chama cha siasa kutangaza kugomea kushiriki uchaguzi hakuwezi kuifanya tume ihahirishe uchaguzi kwani tume haiko kumshawishi mtu au chama kushiriki uchaguzi.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ramadhani alisema chama kushiriki uchaguzi ni jambo la hiyari na tume ya uchaguzi iko pale kwa ajili  ya kuweka na kutengeza mazingira yatakayofanya vyama vya siasa kushirki uchaguzi.

Alisema iwapo kuna chama kitaamua kutoshiriki uchaguzi, chama kitakachoshiriki hata kama ni mmoja mgombea wake atapita bila kupingwa.  Alisistiza kuwa hakuna sehemu yoyote ya katiba na sheria ya uchaguzi inayotamka kwamba chama kisiposhiriki uchaguzi basi uchaguzi unaahirishwa. 

“Ila ikitokea vyama vikasusa vyote kushiriki kwenye uchaguzi hapo ndipo unaweza kuahirishwa kwa kuwa hakutakuwa na mgombea,”alifafanua mkurugenzi wakati alipokuwa anazungumza na baadhi ya waandishi wa habari ambao walitaka kupata ufafanuzi wa tume kuhusu tamko lililotolewea na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe.

Hivyo ameviasa vyama vya siasa vinavyotishia kutoshiriki kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu na kata sita kufuata mifumo ya kisheria ya kushughulikia malalamiko ya uchaguzi.

Aliitaja mifumo hiyo kuwa ni kuwasilisha malalamiko kwenye kamati ya maadili wakati wa kampeni,  wakati wa kuanza kupiga kura wakala akiwa na malalamiko anajaza fomu namba 14 na fomu namba 16 wakati upigaji kura unapoeendelea  na kama mgombea hakuridhikai anaruhusiwa kwenda mahakamani.

Juzi Mbowe  alitishia kuwa vyama vinavyounda umoja wa katiba (UKAWA) havitashiriki uchaguzi iwapo changamoto mbalimbali zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata 43 zisipofanyiwa kazi na NEC.

Akizungumzia hoja hiyo Ramadhani alisema kwamba katika orodha ya vyama vilivyopo NEC, Ukawa sio moja ya vyama vya siasa na akaongeza kuwa kushiriki kwenye uchaguzi ni hiyari ya chama cha siasa.

“Niwasihi vyama vya siasa watumie mifumo iliyopo ya kawaida ya kuwasilisha malalamiko yao, kwenye kamati za maadili, kujaza fomu namba 14 kabla ya kura kuanza kupigwa, fomu 16 wakati kura zinapigwa na kuwasilisha malalamiko mahakamani baada ya kura kuhesabiwa,”alisema Kailima.

Aliseima hiyo ndio mifumo iliyowekwa kisheria katika kushughulikia changamoto za  uchaguzi zinapojitokeza, “Je hiyo mifumo wanayotaka wao ni ipi?  Kama kama kuna mgombea hakuridhika mahakama zipo aende maana wamepewa siku 30 za kufungua kesi.”

Alisema NEC haiwezi kuahirisha uchaguzi kwani sheria inatamka kuwa uchaguzi unaweza kuahirishwa iwapo tu kuna mgombea amefariki, kutokuwepo mgombea, zikitokea ghasia na fujo au wagombea wakifungana kwa kura.

“Je kuna mgombea amefariki? Haya mambo yote manne hayajatokea, sasa tutaahirishaje uchaguzi? Alihoji Ramadhani na akavitaka vyama vya siasa kutumia mifumo iliyopo kuwasilisha malalamiko yao

Akizungumzia kuhusu jimbo la Longido ambalo Mbowe alidai kuwa shauri la uchaguzi bado liko mahakamani na kwamba wameiandikia NEC kuhusu suala hilo na hawajajibiwa barua yao, Ramadhani alisema madai hayo sio ya kweli kwani barua zote walizoandikiwa wamezijibu.

Alisema jimbo hilo liko wazi kwa kuwa mahakama ndio imeiandikia NEC kuitaarifu kumalizika kwa kesi iliyokuwepo mahakamani. Alisema kwamba NEC itasimamisha uchaguzi wa jimbo hilo iwapo tu wataambiwa na mahakama kusimamisha mchakato huo.

“Nimesikitishwa na kauli kwamba eti wametuandikia barua sisi tume ya kusimamisha uchaguzi wa Longido eti hatujawajibu, tulipata barua kutoka kwa ole Nangole (Onesmo) tukamjibu, tukapata barua kwa wakili wa Ole Nangole nikamjibu, tukapata barua kutoka kwa katibu wa Chadema tukamjibu na nikaongea naye kwenye simu, sasa aleo wanaposema kwamba hatujawajibu kwa kweli kauli hiyo imenisikitisha sana,”alisema Ramadhani.

No comments: