Thursday, October 19, 2017

NSSF IMEKUWA MFANO WA KUIGWA KATIKA NYANJA ZA KIUCHUMI NA KIJAMII

Waziri wa kazi, ajira, sera, bunge, vijana na wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amelipongeza Shirika la NSSF kwa kuwa mfano wa kuigwa katika nyanja za kiuchumi na kijamii. Waziri mkuu aliyasema hayo katika mkutano wa wadau wa NSSF unaoendelea katika Kituo cha kimataifa cha mikutano AICC, Arusha

Waziri wa kazi pia alipongeza NSSF kwa kuandaa mkutano wa wadau unaofanyika hapa jijini Arusha, alisema mkutano huo siyo muhimu kwa NSSF na wadau tu bali pia kwa maendeleo na ustawi wa Taifa letu. Pia alifurahi kupata  nafasi ya kufuatilia utendaji wa NSSF pamoja na kuona moja kwa moja kutoka kwa wadau wa NSSF.
Pia aliwapongeza  wadau wa NSSF kwa kuitikia wito wake wa kuja kushiriki ili kupata taarifa za utekelezaji wa maazimio waliyokubaliana mwaka jana, taarifa za utendaji na kuchangia mawazo yatakayoleta tija ya kulijenga Shirika. Aidha, aliwapongeza Wageni mbalimbali katika mkutano huo ambao ni pamoja na Mhe. Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Ndg. Eric Shitindi, Mkurugenzi Mkuu wa SSRA na Wakurugenzi wa Mifuko mingine ya Pensheni.

Vile vile Waziri wa kazi alitoa pongezi kubwa kwa namna ambavyo NSSF  ilivyojitolea katika kutekeleza jukumu la kukuza Uchumi wa Viwanda  kwani alisema Ujenzi wa Taifa si jukumu la Serikali Kuu peke yake bali ni la kila Mtanzania mmoja mmoja, taasisi na makampuni, na ndio maana NSSF pamoja na kuwa na jukumu la hifadhi ya jamii kwa mujibu ya sheria yake husika, imeona haja ya kupanua wigo wa uwekezaji wake na kuelekea katika viwanda jambo ambalo litaongeza ajira, kuongeza uzalishaji, na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla. 
 Waziri Mhagama alitoa  mfano katika uwekezaji wa NSSF  katika kukuza viwanda tumeshuhudia uwezekano wa kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania kutoka na uwekezaji ilioufanya katika viwanda mbali mbali. Nichukue fursa hii kuipongeza NSSF kwa kutoa mkopo wa shilingi bilioni 3.1 kwa lengo la kuongeza uzalishaji katika kiwanda cha madawa kilichopo Kibaha chini ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC). Katika kiwanda hiki ambapo ajira 100 zimezalishwa. Uzalishaji wa viuadudu ulianza Mwezi Desemba 2016 na mpaka sasa kiwanda kimezalisha jumla ya lita 327,400 ambazo ziliuzwa katika masoko ya ndani na nje.

Shirika lilitoa Mkopo kwa ajili ya upanuzi wa Kiwanda cha Chaki kilicho chini ya Usimamizi wa Halmashauri ya Maswa, Mkoani Simiyu mnamo mwezi June, 2017. Mkopo huu kwa ujumla utaongeza uzalishaji wa chaki kutokea vipande 432,000 vya chaki nyeupe (sawa na  Katoni 180) kwa siku hadi vipande milioni 4.8 vya chaki nyeupe na za rangi (sawa na Katoni 2,000) kwa siku. Ongezeko la uzalishaji huu wa chaki utasaidia kuendeleza Sera ya Serikali ya “Elimu Bila Malipo” kwani itasaidia kupunguza mahitaji makubwa ya chaki katika shule za awali na msingi. Jumla ya Ajira 100 za moja kwa moja zinatarajiwa kutokana na uwekezaji huu.
 Pia aliwapongeza NSSF kwa kushirikiana na PPF, na Jeshi la Magereza kupitia Kampuni ya Mkulazi, wamewekeza katika Mradi mkubwa wa shamba la miwa na Kiwanda cha Sukari kilichopo Mbigiri ambapo tayari hatua za upandaji miwa zimeanza nami nikiwa miongoni mwa watu waliopata fursa ya kupanda miwa ya

mwanzo kabisa. Kiwanda hiki Cha Mbigiri kitakapokamilika kinatarajiwa kuzalisha tani 50,000 za sukari kwa mwaka. Mpaka sasa mradi huu umezalisha ajira 300 za moja kwa moja na pia kupitia mpango wake wa wakulima wa nje katika eneo la Dakawa, imeweza kuandikisha jumla ya wakulima 1,500 wanaotegemewa kuanza kilimo cha miwa kuanzia mwezi Novemba, 2017 ambao watalima heka 15,297.

No comments: