Friday, December 9, 2016

RAIS DKT JOHN POMBE MAGUFULI ATOA MSAMAHA KWA WAFUNGWA 5,678 KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA 55 YA UHURU WA TANZANIA BARA

Katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe  9 Disemba, 2016 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i)           Wafungwa wote wamepunguziwa moja ya sita (1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2 (i-xx).

(ii)         Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, KIFUA KIKUU (TB) na SARATANI (CANCER) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii)       Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi ambao umri huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv)        Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v)          Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability) ambao ulemavu huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2.      Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i)              Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.
(ii)            Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.
(iii)          Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv)          Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v)            Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.

(vi)          Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery).

(vii)        Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (firearms, ammunitions and explosives).

(viii)      Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix)          Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x)            Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi)          Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

(xii)        Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

(xiii)      Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv)       Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv)         Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi)       Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii)      Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na  usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili (Poachers).

(xviii)   Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya        wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix)       Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

(xx)      Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 9/10/2016.

3.      Wafungwa wapatao 5,678 watafaidika na msamaha huu baada ya kupunguziwa 1/6 ya vifungo vyao ambapo 1,340 wataachiliwa huru na wafungwa 4,338 watanufaika na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki. Ni mategemeo ya Serikali kwamba watakaoachiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Imesainiwa na;
Meja Jenerali  Projest  Rwegasira
KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
9/12/2016

No comments: