Sunday, November 13, 2016

Serikali haitatoa Vibali vya kununua Jasi/Makaa ya Mawe Nje ya nchi- Prof. Muhongo

Shughuli ya uchimbaji na upakiaji wa makaa ya mawe ikifanyika katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka uliopo  kata ya Ruanda mkoani Ruvuma. Mgodi huo una mashapo ya makaa ya  mawe tani milioni 400.
Na Teresia Mhagama

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameendelea kusisitiza  kuwa Serikali haitatoa vibali kwa Viwanda nchini kununua madini ya Jasi na Makaa ya Mawe  nje ya nchi wakati Tanzania ina mashapo ya kutosha kukidhi mahitaji wa viwanda hivyo.
Aliyaeleza hayo wakati alipofanya ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini ya makaa ya mawe katika mgodi wa Ngaka unaomilikiwa na kampuni ya TANCOAL  katika Kata ya Ruanda mkoani Ruvuma. 30
Katika ziara hiyo Profesa Muhongo aliambatana na watendaji mbalimbali kutoka viwanda vya simenti vinavyotumia makaa hayo ya mawe, Chama cha Wamiliki wa Malori (TATOA), Wazalishaji wa Makaa ya Mawe, Watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na viongozi kutoka  Mkoa wa Ruvuma, wilaya ya Mbinga na Songea.
“Baadhi viwanda vya simenti vimelalamika kuwa kuna upungufu wa makaa ya mawe, ndio maana wadau wote tuko hapa ili kuhakiki je ni kweli kuna upungufu wa makaa ya mawe au la,” alisema Profesa Muhongo.
Akijibu suala la upungufu wa makaa wa mawe, Meneja wa TANCOAL, David Kamenya alisema kuwa katika mgodi huo wa Ngaka, Makaa ya mawe yapo ya kutosha na kuna mashapo Tani milioni 400 ambazo uchimbaji wake utafanyika kwa muda wa miaka 40.
Aliongeza kuwa Mgodi huo pia una vifaa vya kutosha vya kuchimba madini hayo ili kuweza kukidhi mahitaji ya wateja na kwa siku wanaweza kuzalisha makaa ya mawe tani 1200 hadi 1500 kulingana na mahitaji wanayopata ila kampuni ina uwezo  wa kuzalisha hadi tani 3000 siku.
Kuhusu ubora wa makaa ya mawe, TANCOAL ilieleza kuwa makaa hayo yana ubora unaotakiwa sawa na makaa ya mawe ambayo viwanda mbalimbali nchini vimekuwa vikiagiza kutoka Afrika Kusini.
Katika ziara hiyo kampuni za simenti za Tanga, Rhino na Lake zilikiri kuwa kuna mashapo ya kutosha ya makaa ya mawe lakini changamoto iliyopo ni uwepo wa magari ya kutosha na yanayofaa kusafirisha makaa hayo.
Kuhusu Changamoto hiyo Profesa Muhongo alimtaka Mwenyekiti wa TATOA pamoja na wanachama wake wenye magari yenye uwezo wa kusafirisha makaa hayo,  kukutana na watendaji wa viwanda vya Simenti, tarehe 15 Novemba, 2016 jijini Dar es Salaam ili wenye viwanda hao wakague magari hayo na kuweza kufanya maamuzi ya kuingia mikataba ya kutumia magari husika.
Aidha, Profesa Muhongo  alisema kuwa,  lazima kuwe na mikataba  kati ya TANCOAL na viwanda vinavyohitaji makaa hayo ya mawe na endapo kampuni ya TANCOAL itashindwa kuzalisha makaa ya mawe ya kutosha,  kampuni hiyo ndiyo itakayobeba lawama ya kushindwa kutekeleza mkataba wa kazi husika.
“Hivyo hapa tumeshahitimisha kuwa makaa ya mawe yapo ya kutosha, hivyo mtu asithubutu kuomba kibali cha kuagiza madini haya nje ya nchi, narudia uamuzi wa Serikali ni kwamba,  ruhusa haitatolewa kabisa, mtatumia makaa yanayozalishwa hapa Tanzania,” alisema Profesa Muhongo.
Akitoa uamuzi wa Serikali wa kuzuia uagizaji wa madini hayo nje ya nchi mwezi Agosti mwaka huu, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa Hazina ya madini ya Jasi nchini ni zaidi ya Tani 300,000 na kuna tani zaidi ya milioni 5 za makaa ya  mawe ambazo zinatosheleza mahitaji ya nchi.

No comments: