Sunday, October 9, 2016

SHEREHE ZA MWENGE WA UHURU ZILIVYOFANA WILAYANI KISHAPU

Habari na Picha na Robert Hokororo
Mwenge wa Uhuru umewasili na kupokelewa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ukitokea Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.
Uliwasili majira ya saa 2 asubuhi katika Kijiji ya Bubiki ambapo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alimkabidhi mwenzake wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba kabla ya kuanza mbio zake kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Ukiwa wilayani humo ulizindua miradi 11 yenye thamani ya sh. bilioni 1.6 ikiwemo ule wa maji kutoka Ziwa Victoria mkoani mwanza unaotarajiwa kuanza kuwanufaisha wakazi wa Kishapu hivi karibuni.
Mara baada ya kuwasili wilayani humo mbio za Mwenge wa Uhuru zikiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo na viongozi mbalimbali ulianza mbio zake kuelekea katika mradi wa kwanza wa vyumba vipya vya madarasa na matundu ya vyoo.
Katika mradi huo Kiongozi wa mbio hizo kitaifa, George Jackson Mbijima alikagua na kufungua mradi huo kabla ya msafara huo kuelekea katika miradi mingine ikiwemo Klabu ya Wapinga Rushwa Shule ya Sekondari Mipa.
Pia mradi wa ufugaji nyuki katika eneo la Mipa ulizinduliwa ambapo utakuwa kichocheo cha maendeleo kwa wafugaji nyuki na maendeleo mazima ya zao la asali katika wilaya.
Msafara wa Mwenge ulifika Kijiji cha Dulisi na ambapo jiwe la msingi liliwekwa katika zahanati inayoendelea kujengwa ambayo kukamilika kwake kuitasaidia kusogeza huduma kwa wakazi wake na wa maeneo ya jirani.
Mradi mwingine ni jengo la kisasa la ofisi ya kata Mwadui Lohumbo lenye ofisi mbalimbali zikiwemo ya mtendaji, kata, kijiji, maofisa ugani na watumishi wengine wa halmashauri ngazi ya kata.
Mbali ya miradi hiyo pia mawe ya msingi yaliwekwa katika kituo cha polisi kilichopo stendi mpya ya mabasi kilichopo mjini Mhunze wilayani humo pamoja daraja jipya la magari na wapiti kwa miguu.
Miradi yote hiyo miwili itakuwa kichocheo kwa uchumi na huduma bora kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Mwenge huo ulikesha katika viwanja maarufu vya Shirecu vilivyopo mjini humo kwa burudani mbalimbali hadi asubuhi ambapo msafara ulianza kuelekea Kijiji cha Wigelekeo Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Taraba alimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ili ambaye aliukabidhi Mkoa wa Simiyu kupitia kwa Mkuu wake, Anthony Mtaka.

Mwaka huu kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kinafanyika mkoani Simiyu ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Josph Magufuli.
 Mwenge wa Uhuru ukikimbizwa katika maeneo mbalimbali mara baada ya kuwasili wilayani Kishapu.
 Viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba wakisubiri kukabidhiwa Mwenge wa Uhuru wilayani humo katika Kijiji cha Bubiki.
 Kikundi cha ngoma cha Makirikiri kikionresha manjonjo yake katika ufunguzi wa mradi wa stendi kuu ya mabasi na kituo cha polisi eneo la Mhunze wilayani Kishapu wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru.
 Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza wakati wa kuupokea mradi wa maji ya Ziwa Victoria katika eneo la Mwadui lohumbo wakati Mwenge wa Uhuru ulipopita na kuuzindua.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Stephen Magoiga akicheza kwa furaha kuhamasisha wanafunzi waliofika kuulaki Mwenge wa Uhuru mara baada ya kuwasili wilayani humo.
 Sehemu ya umati wa wananchi waliojitokeza kuulaki Mwenge wa Uhuru mara baada ya kuwasili wilayani Kishapu ukitokea wilayani Shinyanga.
 Sehemu ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wakiselebuka kuonesha furaha yao ya kuukaribisha Mwenge wa Uhuru kiwilaya.
 Sehemu ya maelefu ya wananchi wakifuatilia matukio mbalimbali wakati wa sherehe za Mwenge kiwilaya zilizofanyikika katika viwanja vya Shirecu mjini Mhunze ambako kulifanyika mkesha uliochagizwa na burudani mbalimbali.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba akizungumza na maelfu ya wananchi walishiriki katika sherehe za Mwenge wa Uhuru viwanja vya Shirecu ambako ulikesha. Pia Taraba alitoa zawadi ya ng’ombe kwa timu ya soka Watumishi FC iliyoshinda katika mashindano maalumu kuelekea Mwenge wa Uhuru.

No comments: