Thursday, July 2, 2015

HOTUBA YA MHESHIMIWA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA UFUNGUZI WA KIWANDA CHA KUZALISHA VIUADUDU VYA KUULIA VILUWILUWI VYA MBU WANAOENEZA MALARIA KILICHOPO KATIKA ENEO LA VIWANDA LA TAMCOKIBAHA, PWANI TAREHE 2 JULAI, 2015

 Mheshimiwa Hailemariam Desalegm, Waziri Mkuu wa Ethiopia;
Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu;
Mheshimiwa Dkt. Abdala Kigoda, Waziri wa Viwanda na Biashara;
Mheshimiwa Dkt. Kebwe Stephen Kebwe, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii;
Ndugu Lobani Gutieres Ravelo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa  Kampuni ya LABIOFAM, Cuba;
Ndugu Joyce Phumaphi, Katibu Mtendaji wa ALMA;
Mheshimiwa Lorge Luis Lopez Tarmo, Balozi wa Cuba nchini Tanzania;
Mheshimiwa Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani;
Waheshimiwa Mabalozi wa Nchi za Nje na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa;
Wageni Waalikwa;
Wanahabari;
Mabibi na Mabwana;
          Ni furaha iliyoje kwangu kuwepo hapa leo, kushuhudia  uzinduzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Viuadudu vya Kuua Viluwiluwi wa Mbu.  Furaha yangu inaongezeka zaidi kwa kuwepo ugeni mkubwa wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Mheshimiwa Hailemariam Desalegn. Yeye ndiye Mwenyekiti wa Umoja wa Viongozi wa Afrika walio mstari wa mbele katika Mapambano Dhidi ya Malaria katika Bara la Afrika (ALMA). Kwa niaba ya Watanzania wenzangu wote namshukuru sana mgeni wetu kwa kutenga muda wake na kusafiri kutoka Ethiopia kuungana nasi siku ya leo. Ujio wako unaweka uzito mkubwa kwenye azma yetu hii ya kutokomeza Malaria katika Bara letu.
          Pamoja nasi, napenda pia kuwakaribisha watu wafuatao; kwanza, Ndugu Alfred Romberto Corta, Rais wa Kampuni ya LABIOFAM ya Cuba waliotuuzia teknolojia ya kutengeneza dawa hizo. Wa pili, ni Bibi Joy Pumaphi, Katibu Mtendaji wa ALMA. Mwisho, ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu wageni wote wengine waliopo hapa leo.
Chimbuko la Kiwanda
Wageni waalikwa;
          Chimbuko la ujenzi wa kiwanda hiki ni ziara yangu niliyoifanya nchini Cuba mwezi Desemba, 2009. Katika ziara ile, mwenyeji wangu Rais Raul Castro alinipangia ratiba ya kutembelea Kiwanda cha LABIOFAM kinachomilikiwa na Serikali ya Cuba na kinachozalisha dawa za viluwiluwi vya mbu wanaosababisha malaria.  Baada ya kuvutiwa na maelezo na teknolojia ile na kuhakikishiwa kuwa haina athari kwa mazingira na afya ya binadamu niliagiza mambo mawili yafanyike. Kwanza, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iagize dawa hizo kutoka Cuba zitumike nchini; na Pili, Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lianzishe ushirikiano na Kampuni ya LABIOFAM kwa lengo la kujenga kiwanda cha aina hiyo hapa nchini.
Shukurani kwa Serikali ya Cuba
Mabibi na Mabwana;
          Shukrani zangu za pekee zimuendee Mheshimiwa Raul Castro, Rais wa Jamhuri ya Kisoshalist ya Cuba, na rafiki mkubwa wa Tanzania, kwa kukubali kutuuzia teknolojia hii. Wenzetu wa Cuba wametufaa sana kwani “hawajatupa tu samaki, bali wametupa ndoano ya kuvua samaki”.  Wangeliweza kabisa kwa tamaa kukataa kutuuzia teknolojia na  ujuzi wao na kutaka kutuuzia dawa.  Pamoja na kuwa wao si nchi tajiri hawakufanya hivyo. Wameshirikiana nasi katika ujenzi na kukubali kutupa wataaalam ambao watabakia nchini kwa miaka mitano kufundisha watu wetu na kutusaidia kwa masuala ya kiufundi na kitaalam.  Tunaye pamoja nasi kiongozi na Mhandisi Mkuu aliyesimamia ujenzi huu Ndugu Alfredo R. Drespo Dorta ambaye amesafiri toka Cuba kuja kushuhudia ufunguzi wa kiwanda hiki. Huu ndio urafiki wa kweli na udugu.  Nakuomba Mheshimiwa Balozi wa Cuba unifikishie shukrani zangu za dhati na za Watanzania wenzangu kwa Rais Raul Castro na kwa ndugu zetu wananchi wa Cuba.
Vita Dhidi ya Malaria
Mabibi na Mabwana;
          Leo tunapiga hatua kubwa na ya aina yake katika vita yetu dhidi ya malaria hapa nchini na katika Bara la Afrika hasa nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.   Katika Ripoti ya Malaria Duniani ya mwaka 2014 iliyotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) inakadiriwa kuwa, mwaka 2013, malaria ilisababisha vifo vya watu 584,000. Kati ya vifo hivyo asilimia 90 vilitokea barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara. Bahati mbaya sana waathirika wakubwa walikuwa ni wanawake na watoto chini ya umri wa miaka 5.  Inakadiriwa pia kwamba malaria inazigharimu nchi wastani wa asilimia 40 ya fedha zao za bajeti ya afya na kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa baadhi ya nchi za Afrika kwa asilimia 1.3. 
Kinachosikitisha zaidi ni ule ukweli kwamba, upo uhusiano mkubwa kati ya malaria na umasikini.  Bahati nzuri ugonjwa huu unazuilika na kutibika maana uliwahi kuwa tishio kubwa duniani lakini  leo ni tishio zaidi  Afrika. uzoefu wa nchi nyingine duniani waliofanikiwa kuzuia na kutokomeza. Unatupa matumaini kuwa na sisi tukiiga mifano yao tunaweza kuwa kama wao. Kuwekeza katika kiwanda cha aina hii kutatuwezesha kutokomeza malaria.
Hali ya Malaria Nchini
Mabibi na Mabwana;
          Tangu mwanzoni mwa uongozi wangu kupambana na malaria tuliupa kipaumbele cha juu. Ndicho chanzo cha wagonjwa wengi na vifo vingi nchini. Tumekuwa tunafanya mambo makuu matatu katika kupambana na malaria; kwanza, kutumia dawa mseto kutibu wagonjwa wa malaria. Pili,  kuhamasisha matumizi ya vyandarua vilivyopuliziwa dawa na tatu, kupulizia dawa inayoua mbu ndani ya nyumba. Kwa kufanya hivyo tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa kupunguza  wagonjwa na vifo vitokanavyo na malaria. Kiwango cha maambukizi nacho kimepungua kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka 2012. Vifo vitokanavyo na malaria kwa uzazi vimekupungua kutoka 41 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2004 hadi 12 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2014.  Idadi ya wagonjwa chini ya miaka 5 imepungua kutoka wagonjwa milioni 5,372,569 mwaka 2004 hadi wagonjwa milioni 3,486,326 mwaka 2014 na vifo vya watoto wa miaka 5 kwenda chini vimepungua kutoka 7,907 mwaka 2004 hadi 4,008 mwaka 2014.  Kwa ujumla idadi ya wagonjwa wote imepungua kwa asilimia 51 na vifo kwa asilimia 71 kati ya 2004 na 2014.
          Kwa upande wa matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa, Serikali imesambaza vyandarua 26,371,329 nchi nzima, yaani vyandarua viwili kwa kaya, kwa watoto wa umri wa chini ya miaka 5 na kina mama wajawazito.  Matokeo yake, idadi ya matumizi ya vyandarua vilivyotiwa dawa imeongezeka kutoka asilimia 23 mwaka 2004 hadi asilimia 92 mwaka 2012.  Kwa upande wa wajawazito kutoka asilimia 27 mwaka 2004 hadi asilimia 75. mwaka 2014.  Kwa upande wa watoto wa miaka 5, idadi imeongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2004 hadi asilimia 72 mwaka 2014.
          Mafanikio zaidi makubwa na ya kujivunia yamepatikana Zanzibar. Kiwango cha maambukizi ya malaria kimeshuka na kufikia asilimia 0.2 hivi sasa. Pamoja na kufanya yale mambo matatu ndugu zetu wa Zanzibar walipulizia  na kuua viluwiluwi vya mbu waenezao malaria.  Kama imewezekana Zanzibar inatufanya tuamini kuwa itawezekana na huku Bara pamoja na ukubwa wa eneo na wingi wa watu.  Ni kwa sababu hiyo, tulichukulia uwekezaji huu wa kiwanda cha kuzalisha viuatilifu kuwa uwekezaji wa kimkakati katika vita dhidi ya malaria.  Kwa kuwa sasa dawa hizi zitakuwa zikizalishwa nchini kwa wingi na gharama nafuu, jukumu letu sasa ni kuanzisha kampeni nchi nzima ya kupulizia maeneo yote ili kuua viluwiluwi vya mbu pale wanapozaliwa. Sasa tunatangaza vita si tu na mbu bali na viluwiluwi vyake.
Maelekezo Mahsusi
Mabibi na Mabwana;
          Natoa pongezi kwa Bodi ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa kusimamia vizuri ujenzi wa kiwanda hiki.  Jukumu kubwa na lililo  mbele yenu sasa ni kuhakikisha kiwanda hiki kinazalisha na kujiendesha kibiashara.  Hatutarajii kiwanda hiki kiijiendeshe kwa hasara maana biashara yenyewe ni ya uhakika ndani na nje ya nchi yetu.  Kama nilivyokwishasema hapo awali, Tanzania ni mwanachama, tena mwanachama mwanzilishi wa Umoja wa Marais wa Afrika walio katika Mapambano Dhidi ya Malaria (ALMA).  Umoja huu una nchi 49 Sote kwa pamoja, tunayo dhamira ya kuondokana na malaria katika nchi zetu na tumejiwekea malengo. Uwepo hapa wa Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Ethiopia ni ushahidi huo. Shirikianeni na Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa  Kimataifa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutangaza  bidhaa za kiwanda hiki. Tafuteni masoko barani Afrika, maana, kutokomeza malaria hakutegemei mafanikio katika nchi yetu tu, bali pia na kwa nchi nyingine katika Bara letu.
          Naelekeza pia ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kukitumia kiwanda hiki katika mipango yake ya kutokomeza malaria katika Halmashauri zetu.  Halmashauri zihamasishe watu wetu na kaya zilizo kwenye maneo yao ya utawala kutumia dawa zinazozalishwa na kiwanda hiki.  Angalieni namna bora ya kuwezesha hilo kufanyika.  Kwa kupulizia dawa hizi na kutokomeza viluwiluwi wa mbu kutang’oa mzizi wa fitina unaosababisha maambukizi na vifo vya malaria.
Hitimisho
Mabibi na Mabwana;
          Kama nilivyosema awali, leo ni siku ya furaha sana kwangu kwa kukamilika kiwanda hiki na kupata fursa ya kushuhudia ufunguzi wake. Mafanikio tuliyoyapata katika kutibu malaria ni makubwa na ya kutia moyo.  Hata hivyo, mafanikio hayo yasingekuwa endelelevu iwapo tusingeongeza nguvu na mkazo katika kukinga na kuzuia maambukizi.  Kiwanda hiki tunachokifungua leo kitaimarisha uwezo wetu wa kukinga na kuzuia maambukizi ya malaria.  Wahenga wamesema daima “kinga ni bora kuliko tiba”.  Sasa tuna uhakika kuwa mapambano yetu dhidi ya malaria tumeyafikisha mahali pazuri.  Nafurahi kuona leo tunatamka kwa vitendo kuwa “Malaria Haikubaliki”.  Sasa natangaza kuwa kiwanda cha Kuzalisha Viuadudu vya Viluwiluwi vya Mbu kijulikanacho kama Tanzania Biotech Products Limited kimefunguliwa rasmi.

                    Asanteni  kwa kunisikiliza!

No comments: