Thursday, September 5, 2013

SEHEMU YA PILI YA MAHOJIANO YA MWANDISHI WA KISWAHILI- PROF. SAID A MOHAMMED

 Na Freddy Macha
 Kwa wasomaji wapya. Mwandishi Said A Mohammed keshaandika zaidi ya vitabu thelathini ikiwemo michezo ya kuigiza (tamthiliya), riwaya, mashairi na vitabu ya watoto. Riwaya yake maarufu, Asali Chungu, ilichapwa mara ya kwanza, 1976. Mwandishi aliyetopea, Adam Shafi, aliwahi kusema katika mahojiano na mhadhiri wa Kiswahili Ujerumani, Lutz Diegner, kwamba Asali Chungu ni miongoni mwa hazina kuu za Kiswahili na hupenda sana, kukisoma... Endelea... Riwaya zako tatu zimepishana miaka 36. Je kwanini, muda mrefu toka Utengano hadi Nyuso? Asali Chungu (1977), Utengano(1980) na Nyuso za Mwanamke (2010), Mhanga Nafsi Yangu (2012). Vile vile dhamira kuu inamwangalia mwanamke kwa macho na hisia za kumtetea. Mwandishi mwingine Mwafrika anayesimama upande wa kina mama (hasa vitabu vyake vya mwanzo) ni Msomali - Nuruddin Farah. Je, kwanini wanaume muwatetee wanawake? Kwani hawawezi kuandika wenyewe? Nyuso za Mwanamke 
Mwandishi Said Ahmed Mohammmed Kuandika riwaya au kazi yoyote ya fasihi kunahitaji wakati, utulivu na wiitisho wa ndani wa nafsi ya mwandishi. Huwezi tu kujilazimisha kufululiza. Kisha nadhani vita vya wanawake ni vita vya wanaume pia kama ilivyo kwamba vita vya wanaume ni vita vya wanawake. Kwa hali hii hakuna suala la kwa nini? Kwa bahati mbaya waandishi wanaume wachache tu ndio wenye msimamo wa ukombozi wa wanawake katika fasihi ya Kiswahili. Ama suala la wanawake kutoandika wenyewe wapo wachache katika fasihi ya Kiswahili wanaoandika hata kwamba hawajitetei. Jambo hili linashikamana na historia ya wanawake katika jamii zetu. Wanawake popote pale wamekuwa katika historia ya ukandamizwaji, je kwa nini tusiwatetee?.

Sauti unayotumia kuelezea kisa chako katika Nyuso za Mwanamke ni tofauti na Utengano na Asali Chungu. Mtindo wa Nyuso ni wa “ki-maelezo” zaidi kuliko kutumia wahusika kama Semeni, Zuberi na Dude (Asali Chungu) na Maimuna, Maksudi na Shoka (Utengano). Je kwanini ukaamua kufanya hivyo? Pubishers Longhorn Nairobi 
Wachapishaji wake mwanafasihi Said Mohammed wenye makao makuu Nairobi na ofisi mbalimbali Afrika Mashariki. Mwandishi Said A Mohammed Kila kazi ya fasihi katika utanzu wake ni kama mtoto ambaye amezaliwa na mama na babake. Hawezi mtoto mmoja awe sawa na mtoto mwengine wa tumbo moja. Huu ni ukweli pia katika uandishi wa kubuni. Lakini sidhani kwamba simulizi yangu katika Nyuso za Mwanamke ni simulizi ya kueleza tu, yaani “telling or descriptive”, bali kwa sehemu kubwa ni ya kuonyesha “showing” kupitia wahausika wangu. Na kwa upande mwingine haiwezakani riwaya kuisimulia kwa mtindo mmoja bali kwa mshikamano wa mitindo miwili. “Nyuso..” imechukua muda mrefu sana kumshika msomaji kuliko vile visa vya mwanzo.Hadi ukurasa wa 44 ndipo kisa kinapoanza kujitokeza kwamba chamhusu mtu na mzazi wake. Mwandishi ana uhuru wa kuchagua mtindo wa kuelezea riwaya yake. Je kwanini ukachagua mtindo huu wa mafumbo mafumbo na kuchelewesha habari na maudhui? Je kadri mwandishi unavyoendelea kukomaa unashawishika kufanya majaribio ya ki fani? Na je, umepata “matokeo” au mrejesho nyuma gani kutoka kwa wasomaji wako kuhusiana na kisa hiki? Mwandishi Said A Mohammed Kama kweli wasomaji wote wanahisi kuchelewa kwa hadithi ya Nyuso za si hakika. Labda inaweza kuwa riwaya hii ina katika matapo (layers) mengi. Isitoshe, mhusika mkuu Nana ana tatizo la kuzungumza ndani ya nafsi yake na kuzungumza mwenyewe kwa mwenyewe, kwa hivyo mwanzo hakuna mgongano wa wahusika ambao unatazamiwa kumchangamsha msomaji. Nana ana tatizo linalomfanya aelezee yeye nani na kwa nini ametengana na mamake, jambo ambalo ni msingi mkubwa wa hadithi hii. Lakini hata magwiji wa riwaya wanazungumziwa kuwepo “purple colours” na uchangamfu katika kazi zao – yote mawili. Utengano S Mohammed 
  “Utengano” na “Nyuso” zina mlolongo wa maneno mapya au “magumu” ya Kiswahili. Huu ni mtindo mzuri sana wa kuendeleza lugha yetu.Si waandishi wengi wanaotupa “sherehe” kama hii. Labda tutegemee kwamba “Asali” ikichapishwa tena pia iwekewe “sherehe” , maana ina maneno mengi “magumu”? Mwandishi Said A Mohammed Kwanza niseme kwamba Kiswahili kina utajiri mwingi lakini waandishi wachache wanasahau hivyo au hawataki kusikia wenzao wanavyosema na wanavyoandika. Pili, wazo lako nalikubali kwa ukamilifu. Sherehe-2 
  Visa vyako huchimba undani wa wahusika kuonyesha maisha magumu lakini hapo hapo kutekenya ndoto njema na fikra za wanadamu. Ukurasa 118 (Asali) tunaonyeshwa Dude alipopata ahueni baada ya kufarijiwa na mke wa Zuberi. Mwandishi unasema: “Ata! Dude hataki tena kufa; anataka aishi.Ni nani asiyetaka kuishi?” Utengano hali kadhalika.Bi Kocho anaonyesha ari ya kike akiongea na Farashuu (uk 61): “Sifi kwa ufukara, nikafa kwa kuteswa na mtu. Wakati wa kuogopa umekwisha. Hata kama Maksuudi angalikuwa Mzungu.” Na “Nyuso” hali kadhalika (uk 39): “Nilihisi kwamba haki ya kuwa huru ni haki yangu ya kwanza ya msingi.” Je, lengo na msimamo wako mwandishi kuonyesha jazba ya wanadamu na kwamba ushindi ni kheri yetu kuliko fikra za kushindwa na kukata tamaa na maisha? Au imetokea tu? Mwandishi Said A Mohammed Unajua kutaka tusitake, kila mwandishi ana msimamo na falsafa yake. Mimi siwezi kuwafanya wahusika wangu wakate tamaa. Bila ya tamaa binadamu hawezi kujikomboa. Ukweli ni kwamba bado tunatawaliwa na tena vibaya vibaya. Asali Chungu 
Riwaya hizi tatu zimeelezewa ndani ya maisha ya Visiwani peke yake. Lakini mwandishi umetembea na kuishi mazingira mengine mfano Kenya, Tanzania Bara na Ulaya. Kwanini huangalii huko pia kama ulivyofanya katika hadithi yako fupi “Tazamana Na Mauti” (Damu Nyeusi) inayoangalia maisha ya London? Mwandishi Said A Mohammed Hadithi mara nyingi huja na kuendana na mandhari (setting) yake. Baada ya kukaa nje ya Zanzibar na Tanzania nimepata uzoefu wa nje, kwa hivyo soma kazi kama Baba Alipofufuka, Dunia Yao, Mhanga Nafsi Yangu n.k, utaona kwamba nimefaidikia kimaudhui na kimandhari yanayokamatana katika uwili mmoja. Si kazi zangu zote ni za nyumabani tu. Kifani una lugha ya kipekee inayochora mandhari, wahusika, hisia, mazingira. Mifano iko mingi sana – ila tuchague michache ndani ya “Utengano” na “Asali” zinavyochambua mazingira ya maskini- kilabuni (Utengano, uk 138-143 ) ambapo wanawake wawili – Maimuna na Kijakazi wanavyogombana. Hapa umeshika taji la kukionyesha Kiswahili kilivyo kitamu: “Kijakazi mwenye tabia ya uso wa samaki usiosikia viungo”; “Shoka alitia pamba masikioni”; “Nani anayeshtua watu akitupiwa mbwa hamtaki”; “Kijakazi alijitazama akajiona kapwaya kweli”; “Alikua shetani na aliweza kummeza yeyote.” Na kadhalika. “Asali Chungu,” inayachora maisha ya wananchi kwa undani. Kama wakati Semeni akijipamba. Uk 42 : “Baadaye alikunja miguu yake akaanza kuisinga kwa baki ya mafuta yaliyoroa mikononi mwake. Akarejesha zana zake chumbani na kurudi kukaa kwenye kiti cha marimba pale pale kwenye baraza. Alikua kakaa kwenye kile kiti, kinyume mbele, kajivuta nyuma na kukimwaya kiuno chake upande wa ukutani. Kifua na mikono ikalalia kiegemeo cha kiti, kichwa chake kimeelemea kwenye mikono yake aliyoipachika pamoja; akawa anamwangalia Pili aliyejitia hajamwona, anamfundika kijakazi mkia wa mwisho.” Je, una nini la kuwafundisha waandishi wachanga wanaokua sasa hivi namna ya kuyasifia na kuyapamba na kuyachora vizuri mazingira wanayoyaandika. Waandishi wengi vijana leo wanaandika michezo ya sinema, wanaandika tenzi za rapu (Bongo Flava) wanaandika hadithi fupi fupi. Ila mara nyingi hawajaonyesha mazingira kitaswira. Nini siri wanayoikosa? Ukiacha kipaji yaani. Mwandishi Said A Mohammed Kwanza wakipende Kiswahili, pili, wakisikilize na tatu wakisome kutokana na wale wanaokipenda Kiswahili. Wakubali kuiga, maana wigo si mbaya iwapo utatumika kwa kufunguka tu. Tuangalia mambo mawili pia yanayohusu lugha. Kwanza tueleze vipi ukaunda misemo mizito kwa maneno machache. Yanatoka wapi? Mfano: Nyuso (Sura 7; uk 70); “Maiti kasoro nukta.” Asali (Sura 11; uk 143) : “Ulimwengu ni mchafu. Je, yeye mlimwengu awe vipi?” Asali (Sura 8; uk 101) “Mungu haombwi; hutoa.” Utengano (Sura 10; uk 118 ) : “Bora nusu ya shari kuliko shari kamili.” Pili, tusaidie tafsiri ya maneno na misemo ya visiwani ambayo haieleweki kwa baadhi ya wasomaji wa bara: “Sherehe za wana kindakindaki” (Asali, Sura 12; uk 159) “Kuruka adi-mfundo” (Asali, Sura 8; uk 111) Je ni “andasa” au “andis”? (Asali, Sura 4; uk 50) “Hapendi, hataki, hajali wala habali” – (Utengano, Sura 1; uk3) “Mkareti” (Utengano, Sura 2; uk 20) Mwandishi Said A Mohammed Nafikiri misemo na maneno hayo hapo juu yanatokana na upeo wangu wa kubuni na ukwasi wa lugha nilioupata katika utamaduni wangu. Ndio ule utamu wa lugha ulioutaja hapo juu. Mwandishi lazima awe mweledi na mwepese wa kutumia maneno na misemo yenye kuvutia na kushangaza. Mbali na hayo mwandishi lazima asikilize watu wanavyosema katika jamii husika na utamaduni wake unaotoa nafasi ya kuunda misemo na kauli za mvutio. Kindakindaki ni mtoto wa mtu mkubwa kama vile mfalme. Adimfundo ni aina ya mchezo wa kuruka vyumba vilivyochorwa ardhini. Neno andasa ni nomino na andis(i) ni kitenzi. Hapendi, hataki, hajali wala habali ni kauli ya msisitizo wa kutopenda. Mkareti ni aina ya mmea wenye mbegu ngumu kama mawe na pia unazungukwa na miba. Said A Mohammed 
Profesa Said A Mohammed, alistahafu kazi ya kufundisha Kiswahili vyuo vikuu mbalimbali duniani, mwaka jana. Soma sehemu ya kwanza ya mahojiano hapa: http://www.kitoto.wordpress.com

No comments: