HAPPY NEW YEAR
Monday, January 1, 2018
JK AUKARIBISHA MWAKA MPYA 2018 NA WANANCHI WA MSOGA, MKOANI PWANI USIKU HUU
Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mkewe Mama Salma Kikwete wakiwa pamoja na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgallu, sambamba na wananchi wa mji wa Msoga Mkoani Pwani kusherehekea kuukaribisha mwaka mpya wa 2018 katika hafla iliyoandaliwa na Dkt. Kikwete kijijini kwake Msoga, usiku huu.
Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiangalia fataki angani wakati wa sherehe ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2018, iliyofanyika usiku huu kijijini kwake Msoga, Mkoani Pwani.
Mbunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete (aliyemshika mtoto) alikuwa ni mmoja wa wakazi wa mji wa Msoga waliojumuika nyumbani kwa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kulikofanyika hafla ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2018.
Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akipeana mkono wa heri ya mwaka mpya na baadhi ya wageni waliofika kijijini kwake hapo.
Msanii wa Muziki wa Singeli, Msaga Sumu akitumbuiza mbela ya maelfu ya wananchi wa Msoga katika sherehe ya kuukaribisha mwaka mpya 2018, iliyofanyika Nyumbani wa Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete, Msoga Mkoani pwani.
Burudani ya Ngoma ya Asili.
Burudani ya Utamaduni wa Kimaasai.
Sunday, December 31, 2017
SALAMU ZA MWAKA MPYA KUTOKA KWA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA Dkt. Faustine Ndugulile
SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA AFYA.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya 2018. Hii ni neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia kwani kuna wengi walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni nyote kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa huduma za afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu na uadilifu licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wa kila siku. Nami nawatia shime na hamasa ili muendelee na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua kuwa Sera yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi pamoja na yale ya Taifa. Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha na kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara yangu. Jambo hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la minong’ono, manung’uniko na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya baadhi ya watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au miiko ya kazi zao na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo yatakayoweza kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya kupitia Watoa Huduma za Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo linatokea.
- Wanataaluma wa Afya:
Nawakumbusha Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi, Wakunga, Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya ya Kinywa na Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na Wafiziotherapia, kwamba taaluma hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza yamejengwa katika misingi ya kuaminiwa (Trust) na Jamii, na kwamba kuaminiwa huko ndio kiini cha heshima ya taaluma hizi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma kutekeleza majukumu yake akiongozwa na msingi huu mkuu, pamoja na misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI, UAMINIFU, USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha, naendelea kuwakumbusha kuwa, utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama. Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika utekelezaji wa wajibu wenu kama wanataaluma ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote wanaokuja mbele yenu kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa siku zote mnao wajibu wa kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa kuzingatia Sheria nyingine za nchi, Kanuni, Sera, pamoja na Miongozo iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko ya Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha, nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya Afya kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma wote walio chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi (Professionalism) pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na kuchukua hatua stahiki za nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana wajibu wa kuhakikisha kuwa Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao kwa misingi hii iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi iharibiwe na wakorofi wachache miongoni mwenu.
- Mabaraza ya Taaluma
Natumia fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya Wizara yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria zinazosimamia Wanataaluma wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu na ujuzi unaokubalika, na atambulike kwa kupewa usajili na leseni ya kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona kuwa jamii inapata huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika. Hivyo, Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.
- Wanajamii
Napenda kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya zilizo salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na zinazozingatia heshima na utu wa binadamu. Pia, mnayo haki ya kupata taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri au tiba kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa misingi ya Sheria za Nchi. Kati ya vitendo visivyo kubalika ni pamoja na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi, dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya, uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya ya simu za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.
Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
- Wanataaluma na Watoa Huduma,
- Kila Mwanataaluma na mtoa huduma anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
- Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa kazi ipasavyo.
- Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.
- Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au malalamiko.
- Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).
- Mabaraza ya Taaluma
Kila Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika Wilaya, Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu dhidi ya wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na anuani za barua pepe (e-mails).
- Wanajamii kwa ujumla:
- Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
- Nawasihi wanajamii wote kutoa taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
- Uongozi wa kituo husika,
- Mganga Mkuu wa Wilaya,
- Mganga Mkuu wa Mkoa,
- Ofisa wa TAKUKURU,
- Baraza la Taaluma Husika,
- Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
- Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
- Kiongozi yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.
Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.
Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO.
31/12/2017.
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) MKOA WA SINGIDA CHAZINDUA KAMPENI ZA UCHAGUZI MDOGO
Baadhi ya wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida kaskazini wakiwa kwenye viwanja vya mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mtinko,singida vijijini juzi.
Baadhi ya wanachama wa CCM waliohudhuria mkutano wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Singida kaskazini wakiwa kwenye viwanja vya mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Mtinko,singida vijijini juzi.
Naibu katibu Mkuu wa CCM Tanzania bara,Rodrick Mpogolo akizindua kampeni za uchaguzi mdogo wa CCM katika jimbo la Singida kaskazini zilizofanyika juzi katika Kijiji cha Mtinko,singida vijijini.
Mgombea wa kiti cha ubunge wa jimbo la Singida kaskazini,Justine Monko akiwa tayari amepokea ilani ya chama kwa ajili ya kutekeleza yaliyoainishwa ndani ya ilani hiyo.(Picha zote Na Jumbe Ismailly)
Na,Jumbe Ismailly SINGIDA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida kimezindua kampeni zake za uchaguzi mdogo katika jimbo la Singida Kaskazini na kusisitiza juu ya kudumisha amani,utulivu na mshikamano uliopo hapa nchini.
Akizindua kampeni hizo zilizofanyika katika Kijiji cha Mtinko,Singida Vijijini,kwa niaba ya Katibu mkuu wa CCM taifa,Naibu katibu mkuu wa CCM,Tanzania bara,Rodrick Mpogolo alisema idadi kubwa ya wananchi wameendelea kukichagua chama cha mapinduzi kutokana na kuwa na mipango mizuri ya maendeleo.
Alizitaja sababu zingine kuwa ni chama chenye historian a pia kina awamu tano za uongozi na kwamba ni chama kilichokomaa na endapo kitakabidhiwa nchi au ukikabidhi madaraka,watakuwa na uhakika kwamba madaraka hayo yameshikwa na watu waliokomaa.
Kwa mujibu wa Naibu katibu mkuu huyo wakati wote CCM imekuwa ikishughulikia kero za watu na kwa hivi sasa inayo matumaini makubwa ya kubadilisha maendeleo ya nchi na kwamba hivi sasa rais wan chi amekwisha hamisha makao makuu ya serikali yake Mkoani Dodoma,jirani kabisa na Mkoa wa Singida.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida,Dk.Rehema Nchimbi pamoja na kuwashawishi wananchi wa jimbo la Singida kaskazini kumchagua mgombe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini hakusita pia kutaja utekelezaji unaofanya na serikali ya chama hicho kwa hivi sasa.
Dk.Nchimbi ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa Mkoa wa Singida aliweka bayana kwamba mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya pili nay a tatu umeshaanza na tayari zaidi ya shilingi bilioni 71.3 zinatarajiwa kutumika kusambaza nishati hiyo katika vijiji vyote.
“Kwa hivyo nawaombeni wananchi wa jimbo la Singida kaskazini mchagueni mgombea wa CCM kwani mkimleta mtu mwingine haijui ataanza kwanza kujifunzafunza atatuchelewesha,kwa hiyo mleteni Monko ili aendeleze utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)”alisisitiza Dk.Nchimbi.
Akimkaribisha Naibu Katibu Mkuu wa CCM,Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida,Juma Hassani Kilimba alisema kutokana na wingi wa wananchi waliohudhuria mkutano huo wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo,unadhihirisha wazi kwamba wao tayari kumchagua mgombea huyo wa CCM ifikapo jan,13,mwaka ujao.
Hata hivyo Kilimba alisisitiza huku akijinasibu kwamba chama hicho hakina wasiwasi juu ya kushinda katika uchaguzi huo mdogo kutokana na serikali ya chama hicho kujishusha kwa wananchi wa ngazi za chini.Naye mgombea wa chama hicho Justine Monko kwa upande wake amewahakikishia wakazi wa jimbo hilo kwamba hataweza kuwaangusha endapo watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao kwa kumchagua kwa kura za kutosha na za kishindo na hatasita kuwatumikia kwa weledi wa hali ya juu.
“Namshukuru sana Rais wetu Dk.John Pombe Magufuli kwa kuniteua kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Liwale,kanipa nafasi hiyo nimejifunza mengi sana pamoja na namna bora ya kuwatumikia wananchi”alisisitiza Monko.
Subscribe to:
Posts (Atom)




































