Saturday, December 7, 2013

Tatizo la Watoto wenye ugonjwa wa vichwa vikubwa na mgongo wazi laongezeka

Afisa Muuguzi msaidizi wa taasisi ya tiba ya mifupa,mishipa ya fahamu na upasuaji wa Ubongo(MOI)katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,akitoa ushauri kwa wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kitengo cha huduma kwa wateja kuhusina na kula vyakula vyenye fuliki acid ya kutosha kama vile mboga za majani,Matunda,Maharage na Viazi,wakati wafanyakazi hao walipofika kutoa msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Tsh Milioni nane(8,000,000)kwa ajili ya watoto wenye ugonjwa wa kichwa vikubwa na mgongo wazi.
Katibu wa chama cha wazazi wa watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na kichwa kikubwa (ASBAHT)Bi.Hidaya Juma (kulia)akielezea jinsi mirija inavyoingizwa kichwani wakati wa matibabu ya watoto wenye matatizo hayo kwa baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kitengo cha huduma kwa wateja wakati wafanyakazi hao walipofika kutoa msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Tsh Milioni nane(8,000,000)kwa ajili ya watoto wenye matatizo ya kichwa vikubwa na mgongo wazi.
Mmoja wa wafanyakazi wa Vodacom Tanzania,kitengo cha huduma kwa wateja akifurahia jambo na mtoto mwenye tatizo la kichwa kikubwa Ibrahim Haji(4)anaetibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,wakati wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kitengo cha huduma kwa wateja walipofika kutoa msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya Tsh Milioni nane(8,000,000)kwa ajili ya watoto wenye matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi.
Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kitengo cha huduma kwa wateja Emmy Njau(kushoto) na kiongozi wa kitengo hicho Geoffrey Wilfred(kulia)wakiwafariji baadhi ya watoto wenye ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,walipofika hospitalini hapo kutoa msaada wa vyakula na viti vya kutembelea vyote vyenye thamani ya Tsh Milioni nane(8,000,000).
Muuguzi Mkuu wa watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,Bi.Haulat Daudi akielezea umuhimu wa vifaa maalumu vinavyotumika wakati wa matibabu kwa watoto wenye ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi mara baada ya kukabidhiwa na Afisa Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa wateja wa Vodacom Tanzania,Bi. Harriet Lwakatare(kushoto)Jumla ya Tsh Milioni nane(8,000,000)zilitumika katika msaada huo.
Mzazi wa mtoto John Winfred wa kwanza toka kushoto aliekaa chini akiwaangalia wafanyakazi wa Vodacom Tanzania kitengo cha huduma kwa wateja Bi.Leah Ntisi na Joseph Msafiri (kulia)wanavyomweka sawa mwanae katika moja ya viti vilivyotolewa msaada vyenye thamani ya Tsh Milioni nane(8,000,000)na wafanyakazi wa kitengo hicho kwa watoto wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wenye ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Baadhi ya wafanyakazi wa Vodacom Tanzania,Kitengo cha huduma kwa wateja wakifarijiana na wazazi wa watoto wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wenye kusumbuliwa na ugonjwa wa kichwa kikubwa na mgongo wazi,wakati wafanyakazi hao walipofika Hospitalini hapo kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya Tsh Milioni nane(8,000,000)mahususi kwa ajili ya watoto hao.

Imeelezwa kuwa tatizo la watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi limekuwa kubwa zaidi tofauti na jamii inavyolichukulia tatizo hilo. Huku ikibainika zaidi kuwa idadi ya watoto wanaozaliwa kwa mwaka na ugonjwa huo ni zaidi ya elfu huku 250 tu ndio wanafika katika taasisi ya tiba ya mifupa, mishipa ya fahamu na upasuaji wa Ubongo (MOI)

Hayo yamebainishwa na Afisa Uhusiano wa Taasisi hiyo Patrick Mvungi wakati akipokea misaada mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania kupitia kampeni ya pamoja na Vodacom inayoendeshwa katika mikoa mbalimbali hapa nchini.

“Tatizo la Ugonjwa wa kichwa kikubwa na uti wa mgongo ni kubwa sana katika nchi yetu na linaongezeka siku hadi siku, na tunapenda kuweka wazi kuwa tatizo hili linasababishwa na wakina mama, kuanzia wanapopata ujauzito hadi kufikia kipindi cha miezi mitatu hapa ndipo tatizo linapotokea, alisema, “Katika kipindi hiki mama asipokuwa anakula chakula chenye lishe (Lishe Bora) na kwenda Kliniki kwa wakati inapelekea kupata upungufu wa madini ya Folic acid.” Alisema Mvungi na kuongeza

“Tunahitaji jamii ituelewe na ndipo tunapo hitaji msaada wa wadau wengine kama Vodacom kutuwezesha kuweza kutoa elimu kwa jamii, kwa mfano hali ilivyo sasa, watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu kwa mwaka inafikia zaidi ya elfu nne (4000) kwa mwaka, lakini watoto tunaowapokea hapa kwa mwaka wanafikia 250 tu. Ni jambo la kusikitisha sana. Alisema Mvungi na kuongeza.

“Idadi ya watoto wanaozaliwa ukilinganisha na tunaowapokea hapa kwetu ni tofauti kabisa, wengi wanakuwa wanaamini tatizo hili linatokana na mambo ya kishirikina na inapelekea watoto wa aina hii kuuwawa wengine wanafichwa na wazazi wao, tunapashwa kuondokana na hali hii ili tuweze kukabiliana na tatizo hili.” Alihitimisha Mvungi.

Akizungumzia juu ya misaada hiyo yenye thamani ya shilingi Milioni nane Afisa Mkuu  wa Kitengo cha huduma kwa wateja wa kampuni ya Vodacom Tanzania Harriet Lwakatare amesema kuwa kampuni yake itaendelea kuunga mkono sehemu muhimu zinazogusa maisha ya jamii kwani wao ndio wanaowaunga mkono kila siku.

“Tunatambua mahitaji muhimu waliyonayo jamii ya Watanzania, hasa watoto hawa wenye ugonjwa huu wa Vichwa vikubwa na mgongo wazi, Tumeguswa sana na maisha ya watoto hawa na tumejisikia faraja kuwasaidia na kuwafariji, tumefarijika kuwa sehemu ya maisha yao,” alisema Lwakatare.

Kwa upande wake moja ya Wazazi wa watoto hao amesema kuwa amefarijika kupokea misaada hiyo, na kuomba jamii iweze kumsaidia aweze kupata ada ya kuendelea kumsomesha mtoto wake.

“Pamoja na tatizo hili alilonalo mtoto wangu ameweza kujitahidi kusoma hadi kufikia darasa la tatu lakini nimeshindwa kumuendeleza kwa sababu ya kukosa ada ya kuendelea kumsomesha naomba kwa mtu yoyote atakae kuwa na  uwezo wa kunisaidia anisidie japo kumsomesha tu.” Alisema Mzee Joseph Kaza, baba wa motto Selemsni Joseph (13) mwenye ugonjwa huo.

WAZIRI MKUU AZIPA NOTISI NEMC, MANISPAA MOROGORO

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametoa mwezi mmoja kwa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) iwe imetoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu matumizi ya maji machafu yanayotokea kwenye viwanda vinne vya ngozi, magunia, nguo na maturubali (canvas).

Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Desemba 7, 2013) mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye kiwanda cha nguo cha 21st Century kilichopo eneo la Kihonda Viwandani nje kidogo ya mji wa Morogoro.

Akizungumza na uongozi wa mkoa, wilaya, kiwanda hicho pamoja na NEMC  ya mara baada ya kutembelea eneo ambalo limeathirika na maji yanayotiririka kutoka kwenye viwanda hivyo, Waziri Mkuu alisema tatizo lililopo linachangiwa na kutokuwepo kwa mtu au taasisi maalum ya kusimamia mabwawa ya mfumo wa majitaka (waste management ponds).

“Viwanda hivi vilibinafsishwa lakini mfumo wa usafishaji majitaka haukubinafsishwa... NEMC iishauri Serikali nini kinapaswa kifanyike. Ifanye utafiti kuhusu matumizi ya majitaka yanayotoka kwenye viwanda hivi na ilete uchambuzi huo Serikalini,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye alitembelea eneo la Kihonda Mbuyuni katika kata ya Mafisi ambako maji hayo yanaingia korongoni na kuelekea mto Ngerengere, alishuhudia mifereja ya maji machafu yenye harufu kali na rangi mchanganyiko ya kijani na bluu ikitiririka katikati ya nyumba za watu.

“Hatuwezi kuendelea na hali hii ya kutiririsha maji kwenye makazi ya watu, ni bomu litakalolipuka hivi karibuni. Kuna watoto wanacheza katika maeneo yale wanaweza kunywa au kunawa yale maji, kuna mifugo inapita, inaweza kunywa yale maji, ni hatari kwa kila mmoja wetu,” alisisitiza.

Aliitaka NEMC iangalie uwezekano wa kumpatia mtu binafsi aendeshe mfumo huo hata kama itabidi asimamiwe na Halmashauri lakini kinachotakiwa ni kupatikana kwa mtu mwenye uwezo wa kuendesha mfumo huo kwa utaalamu. Aliipa NEMC miezi miwili ili iwe imekamilisha utafiti wake pamoja na kuangalia uwezekano wa kumpata mtaalamu wa kuifanya kazi hiyo.

Alitoa pia mwezi mmoja kwa Manispaa ya Morogoro kuwa imetafuta eneo jipya na kubwa zaidi kwa ajili ya kumwaga takataka kwani dampo lililopo katika kata hiyo linachangia uchafuzi wa mazingira na kuleta kero kwa wananchi.

“Wakati ule dampo linaletwa huku ilikuwa ni sahihi kwa sababu huku kulikuwa ni nje ya mji lakini kwa sasa siyo sahihi. Nimemwambia Meya akae na watu wake wafikirie kujenga dampo jingine la kisasa... watafute eneo kubwa na kuwe na mifumo ya kisasa,” alisema.

Kuhusu matumizi ya kuni katika kiwanda hicho, Waziri Mkuu alisema hakubaliani kabisa na matumizi ya kuni kwa sababu yanachangia uharibifu mkubwa wa mazingira. Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho, uendelee na mpango wake mpya wa kutumia makaa ya mawe au hata kuangalia mpango wa kutumia umeme utakaotokana na gesi.

“Najua kuna gharama katika kubadilisha mfumo wa boilers zenu lakini matumizi ya tani 50 za magogo kwa siku hapana! Tani 50 nazilinganisha na magunia 500 ya mahindi, sasa kwa miezi sita au kwa mwaka mmoja, mtatumia kuni kiasi gani? Si Morogoro nzima itateketea? Alihoji Waziri Mkuu.

Akijitetea kuhusu suala hilo, mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji alisema moto unaotokana na makaa ya mawe hauna nguvu ya kutosha kuzalisha mvuke wa kuzalisha umeme wa kuendeshea mitambo ya kiwanda hicho. “Tumeomba kwa mwaka mmoja tu tupewe ruhusa ya kuchanganya makaa ya mawe na vipande vya miti hadi tutakapopata boilers mpya,” alisema.

Waziri Mkuu alimweleza Bw. Dewji asubiri majibu ya maombi yake kutoka NEMC ambako maombi hayo yalipelekwa lakini pia akawaonya viongozi wa NEMC kuwa makini wakati wanapitia maombi hayo ili waweze kuwa na mbinu za kubainisha kama kweli vitatumika vipande vya miti au watarudia utaratibu wao wa zamani wa kutumia magogo lakini wanayakata katika vipande vidogo vidogo.

Hata hivyo, katika kikao hicho Meya wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Amiri Nondo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Said Amanzi walielezea kutoridhishwa kwao na uhusiano uliopo baina ya uongozi wa kiwanda hicho na mamlaka zilizopo wakidai kufungiwa mageti na kutotekelezwa kwa maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.

Waziri Mkuu alimtaka mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji ajenge mahusiano mazuri na uongozi wa mkoa kwa sababu viwanda vyake viko katika mkoa huo na hivyo hana budi kuzingatia maslahi ya wakazi wa Morogoro kwanza. “Wao ni viongozi wa mkoa lakini pia ni wawakilishi wa wananchi, kwa hiyo wanawajibika kwa wananchi, linapotokea jambo wao ndiyo wataulizwa na wananchi,” alisisitiza.

MKE WA RAIS MAMA SALMA KIKWETE AKIFUNGA RASMI MKUTANO WA MAWAZIRI WA NCHI ZA MASHARIKI NA KUSINI MWA AFRIKA KUHUSU ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA VIJANA

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Rais Mstaafu wa Botswana na Mjumbe wa High Level Group Dr. Festus Mogae wakati wa kikao cha Mawaziri wa Elimu na Afya kutoka nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika unaofanyika Cape Town nchini Afrika Kusini tarehe 7.12.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiwa pamoja na viongozi waandamizi waliohudhuria mkutano wa High Level Group hukom Cape Town wakisimama kwa dakika moja kwa ajili ya kumkumbuka hayati Rais Nelson Mandela. Kutoka kushoto ni Bwana Enver Surty, Waziri wa Elimu ya Msingi wa Afrika Kusini, Dr. Festus Mogae, Rais Mstaafu wa Botswana, Mama Salma, Bwana Luiz Loures, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, UNAIDS, Dr. Julitha Onabanjo, Naibu Mkurugenzi Mkuu, UNFPA, Bwana Qian Tang, Naibu Mkurugenzi Mkuu-Elimu- UNESCO, Bwana Geeta Rao Gupta, Naibu Mkurugenzi Mtendaji, UNICEF.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dr. Hussein Mwinyi akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa High Level Group unaofanyika huko Cape Town kuzungumzia elimu ya afya ya uzazi na ukimwi kwa vijana katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mawaziri wa Elimu na Afya kutoka nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wakiapa kwa niaba ya nchi zao kutekeleza majukumu waliyopitisha kwenye kikao cha High Level Group, kuhusiana na elimu ya afya ya uzazi ( comprehensive sexuality education and sexual and reproductive health services) mwishoni mwa kikao cha siku mbili kilichofanyika huko Cape Town.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipiga picha na Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS, Bwana Michel Sidibe wakionyesha umuhimu wa dhana nzima ya mkutano wa High Level Group ( YOUNG PEOPLE TODAY, TIME TO ACT NOW) kuhusiana na masuala ya elimu ya afya ya uzazi kwa vjijana katika nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa Mawaziri kutoka nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika kuhusu elimu ya afya ya uzazi kwa vijana wa nchi hizo. Mkutano huo wa siku mbili unafanyika nchini Afrika Kusini katika Mji wa Cape Town tarehe 6-7.12.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akipongezwa na Dr. Julitha Onabanjo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNFPA kwa hotuba aliyoitoa wakati wa kufunga mkutano wa siku mbili wa Mawaziri wa Elimu na Afya kutoka katika Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika huko Cape Town.
Baadhi ya washiriki wa mkutano waqkisikiliza hotuba ya ufungaji iliyokuwa ikitolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete huko Cape Town nchini Afrika Kusini tarehe 7.12.2013.
Baadhi ya washiriki wa mkutano waqkisikiliza hotuba ya ufungaji iliyokuwa ikitolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete huko Cape Town nchini Afrika Kusini tarehe 7.12.2013.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akitoka kwenye ukumbi wa mkutano baada ya kuufunga rasmi huku akisindikizwa na washiriki baada ya kutoa hotuba (BEYOND THE COMMITMENT) iliyosisimua wajumbe wa mkutano huo.PICHA NA JOHN LUKUWI

Makamu wa Rais wa Shirika la Microsoft akutana na Balozi Seif Ali Idd

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikiongoza kikao cha pamoja kati ya Uongozi wa Shirika la Microsoft na Watendaji wa Mawasiliano, Sayansi na Elimu ya Juu wa SMT Na SMZ kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo ndani ya jengo la Bunge Mjini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Shirika la Microsoft lenye Makao Makuu yake Mjini Seattle Nchini Marekani Bw. David Tennenhouse wa tatu kutoka kulia aliyevaa miwani akielezea mipango itakayofanywa na shirika lake kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { Costec }.Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.

Shirika la Kimataifa la Mitandao ya Mawasiliano la Microsoft  linakusudia kuendesha mradi maalum  na Tanzania wa kuwasaidia wanafunzi wa Vyuo Vikuu Nchini Tanzania  { Broard Band } katika masomo yao kupitia mfumo wa kisasa wa mtandao wa Internet.

Mfumo huo mpya utamuwezesha kila mwanafunzi wa chuo Kikuu kufikia hatua ya kuwa na Laptop yake itakayoambatana na vifaa vyake vikijumuisha pia huduma za mtandao wa Internet ili kumrahisishia masomo yake.

Makamu wa Rais wa Shirika la  Microsoft lenye Makao Makuu yake Mjini Seattle Nchini Marekani Bw. David Tennenhouse alieleza hayo katika kikao cha pamoja kati ya Uongozi wa Shirika lake na Watendaji wa Taasisi za Sayansi, Mawasiliano ya Elimu ya juu Bara na Zanzibar kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya waziri Mkuu iliyopo ndani ya Jengo la Bunge Mjini Dodoma.

Kikao hicho kilichokuwa chini ya mwenyekiti wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kimekuja kufuatia  ziara yake aliyoifanya katika Mji wa Seattle Nchini Marekani wiki chache iliyopita ambapo Uongozi wa Microsoft uliahidi kufika Tanzania kwa mazungumzo zaidi ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Bwana David Tennenhouse aliwaeleza wajumbe wa kikao hicho kwamba Microsoft tayari imeshatiliana saini Mkataba na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { Costec } kwa ajili ya kuendesha mradi huo wa Braord Band.

Alifahamisha kwamba awamu ya kwanza ya mpango huo maalum  inaanzia kwa wanafunzi wa chuo kikuu cha Dar es salaam na baadaye kuendelea na vyuo vyengine vikuu vya Tanzania.

Kwa  Zanzibar mpango huo utajumuisha vyuo vikuu vya SUZA, Tunguu, Chukwani vikiwemo pia chuo cha Ufunsi Mbweni, Chuo cha Elimu ya Afya Mbweni, Chuo cha Uongozi wa Fedha Chwaka pamoja na Chuo cha Kiislamu Mazizini.

Makamu wa Rais wa Shirika hilo la Microsoft alieleza kwamba makubaliano yao mengine ya msingi na  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania { Costec } yanahusisha pia mradi wa kusaidia walimu kufundisha mitaala ya Kompyuta { T 21 }.

Akitoa shukrani zake kwa Shirika hilo la Microsoft Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza uongozi wa Taasisi hiyo kwa hatua iliyochukuwa katika kipindi kifupi mara tu baada ya ziara yake ya hivi karibuni Nchini Marekani ambapo pia alipata nafasi ya kutembelea Ofisi za Shirika hilo Mjini Seattle.

Balozi Seif alisema Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia washirika wa maendeleo zimekuwa zikifanya jitihada za kuwajengea mazingira bora ya kitaaluma wanafunzi wake kupitia mfumo mpya wa mawasliano ili wawe na uwezo kamili wa kuhimili mabadiliko ya teknolojia yaliyopo hivi sasa Duniani.

Katika Kikao hicho watendaji wa Taasisi za Mawasiliano, sayansi na Elimu ya Juu ya SMT na SMZ wameuomba uongozi wa shirika hilo la Microsoft  kusaidia uanzishwaji wa kituo cha utengenezaji wa mawasiliano { IT Park } pamoja na ulinzi kwenye mitandao kwa ajili ya kuwaepusha  watoto na wanafunzi kuingia katika mmong’onyoko wa maadili.

Katika Kikao hichowatendaji wa Taasisi za Mawasilino, Sayansi na Elimu ya juu Tanzania Barana na Zanzibar wameuomba Uongozi wa shirika hilo la Microsoft kusaidia uanzishwaji wa kituo cha utengenezaji wa mawasiliano{ IT Park } pamoja na ulinzi kwenye mitandao kwa ajili ya kuwaepusha watoto na wanafunzi kuingia katika mmong’onyoko wa maadili.

Pia waliomba huduma za misaada na taaluma kwenye E Government, mpango maalum wa ulinzi wa Mkongo wa Taifa pamoja na mradi wa kukusanya vijana kuwashajiisha ili waweze kujiendeleza zaidi kimaisha.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kazi Ulimwenguni { ILO } Bwana Guy Ryder hapo Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumao yao Balozi Seif  aliushauri  Uongozi wa Shirika hilo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika harakati zake za kujikwamua katika vikwazo vya kiuchumi  likiwemo tatizo la  ajira kwa watoto.

Alisema kazi kubwa iliyopo hivi sasa ni kuwajengea mazingira bora ya  kitaaluma watoto pamoja na kundi la Vijana kwa lengo la kukabiliana vyema na fursa za ajira ambazo nyingi  zinazohitaji kiwango kikubwa cha elimu hupatikana katika Taasisi, Jumuiya na Mashirika Binafsi.

“ Zipo fursa nyingi za ajira hasa katika taasisi, jumuiya na mashirika binafsi lakini mara nyingi kinachojitokeza kwa vijana walio wengi hapa nchini ni kuwa na ufinyu wa taalamu “ Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Kazi la Kimataifa { ILO } Bwana Guy Ryder alisema  mataifa mengi duniani yakiwemo pia yale yaliyoendelea bado yanakabiliwa na changa moto kubwa za ajira hasa kwa Vijana.

Bwana Ryder alisema changamoto hiyo inasababishwa na ukosefu wa taaluma kwa Vijana hao jambo ambalo shirika lake litajitahidi kuona  taaluma hiyo inawafikia wahusika hao ili wawe za uwezo wa kujiajiri wenyewe badala ya kutegemea ajira za Serikali.

Mkurugenzi huyo wa Shirika la Kimataifa la Kazi  ulimwenguni { ILO } aliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa  Tanzania na ile ya  Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mzuri inayotoa kwa shirika hilo hasa katika kukabiliana na ajira za watoto.

Bwana Guy Ryder alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Shirika hilo litaendelea kusaidia Serikali hizo katika kuona watoto wanaotumikishwa katika kazi mbali mbali wanaachana nazo ili baadaye warejee  maskulini.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Shirika la Kimataifa la Kazi Ulimwneguni { ILO } alikuwepo Nchini Tanzzania kwa ziara ya siku Nne kutembelea na kuona Programu na miradi inayosimamiwa pamoja na kufadhiliwa na shirika hilo.                                                                                                           

Othman Khamis  Ame              

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar                                                        
7/12/2013.

WATANZANIA WAASWA KUHESHIMU HAKI ZA MTOTO

DSC_0960
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania (THBUB), Jaji Mstaafu Amir Manento akizungumza na waandishi wa habari wakati mdahalo wa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu kuelekea maadhimisho ya siku hiyo ambayo hufanyika tarehe 10 mwezi Disemba kila mwaka.
DSC_0885
Meza Kuu kati kati ni msimamizi (moderator) Dkt Khoti Kamanga toka UDSM, kushoto kwake ni Bw, Godfrey Mulisa toka UN, kushoto mwisho ni Mwakilishi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Bw, Harold Sungusia na kulia kwa msimamizi ni Francis Nzuki kutoka Tume ya Sheria na Haki za Binadamu na Utawala Bora na mwisho kulia ni Bi, Felistas Mushi toka Wizara ya Sheria na Katiba.

Na Damas Makangale

WAZAZI na Walezi wameaswa kuacha mara moja tabia ya kwenda na watoto katika sherehe na harusi mbalimbali za kwa sababu ni kosa la Jinai kwa mujibu wa sheria na Haki za Mtoto.

Akizungumza kwenye mdahalo wa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ambao huadhimisha kila tarehe 10 mwezi Disemba kila mwaka, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania, Jaji Mstaafu Amir Manento amesema kwa mujibu wa sheria na Haki za Mtoto wazazi au walezi hawaruhusi kwenda na watoto katika sherehe za usiku.

“wazazi na walezi na watu wa kawaida wanamazoea ya kwenda na watoto kwenye sherehe za harusi na majumba ya starehe lakini kwa mujibu wa sheria na haki za mtoto na marekebisho yake ya 2009 ni uvunjifu wa sheria na haki za mtoto,” amesema Jaji Manento.


Amesema kuwa Tanzania iliridhia tamko rasmi la Haki za Binadamu ili pamoja na mambo mengine kulinda Uhuru na Haki za Binadamu pamoja na haki ya kuishi.

“Tarehe 10 Disemba imeainishwa kuwa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Kuainishwa siku ya Kimataifa ya Haki za binadamu kunakumbusha juhudi kubwa zilizofanywa kwa lengo la kuwafanya watu waheshimu Haki za Binadamu kote duniani,” alisisitiza.

Jaji Manento amesema suala la kuheshimiwa haki za binadamu lilipewa kipaumbele cha kwanza wakati wawakilishi wa nchi mbalimbali walipokuwa wakibuni Hati ya Umoja wa Mataifa.

Aliongeza kuwa Januari mwaka 1947 iliundwa kamati ya haki za binadamu na hati ya kamisheni hiyo ilipasishwa katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Disemba 1948.
Jaji manento amesema kuwa kwa msingi huo siku hiyo ya tarehe 10 Disemba ilitambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu duniani kote.
DSC_0930
Mwakilishi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Bw. Harold Sungusia akiwasilisha mada yake kuhusu historia na chimbuko la Haki za Binadamu katika bara la Afrika tangu enzi za miaka 1200 kwenye nchi ya Mali (Mali Empire).

Amesema kuwa imepita zaidi ya miongo sita sasa tangu kutolewa Azimio la Haki za Binadamu ambalo linakusanya thamani za pamoja kwa ajili ya kuondoa ubaguzi, kueneza uhuru na kupambana na dhuluma dhidi ya binadamu duniani.

Alilisitiza kwamba hapana shaka kuwa kutetea haki za binadamu kwa ajili ya kutimiza lengo hilo ni kazi yenye thamani kubwa. Hata hivyo aliongeza kadhia hiyo inayumbishwa na nchi za Magharibi ambazo zinatumia haki za binadamu na ripoti zinazotolewa na taasisi za haki za binadamu kama nyenzo na fimbo ya kisiasa kwa baadhi ya nchi zinazoendelea.

Kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ni “mafanikio na changamoto katika kuhamasisha na kulinda Haki za Binadamu Tanzania” .
DSC_1003
Juu na chini ni Baadhi ya vijana wa shule za sekondari mbalimbali na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
DSC_0972
Mjumbe kutoka Tume ya Sheria na Haki za Binadamu na Utawala bora Bw, Francis Nzuki (wa pili kulia) akizungumzia uzoefu wake katika kuhamasisha Haki za binadamu katika Magereza nchini Tanzania hasa kwa Wafungwa.
DSC_0989
Mwakilishi kutoka Wizara ya Sheria na Katiba, Bi.Felistas Mushi akiwasilisha mada kuhusu kwanini kuna mpango mkakati wa serikali katika kutekeleza Haki za Binadamu nchini Tanzania.
DSC_1052
Mtaalamu wa mambo ya Utawala bora , Grainne Kilcullen kutoka UNDP akiwahamasisha vijana waliohudhuria mdahalo huo kuwa mstari wa mbele katika kusimamia Haki za Binadamu na kuwaelimisha jamii inayowazunguka kuzitambua Haki zao za msingi.
DSC_1061
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini Tanzania, Jaji Mstaafu Amir Manento (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Huduma za sheria wa Tume ya Sheria na Haki za Binadamu na Utawala bora, Bw. Nabor Assey ( wa pili lulia), Mtaalamu wa mambo ya Utawala bora , Grainne Kilcullen kutoka UNDP na Afisa Habari wa Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Habari (UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikizungumziwa kwenye mdahalo huo.
DSC_1025
Pichani Juu na chini ni baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakitoa maoni na kuchangia mada mbalimbali zilizokuwa zikijadiliwa kwenye mdahalo huo.
DSC_1029
DSC_1043
Wanafunzi mbalimbali wakipata maelezo kutoka kwa Investigation Officer wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Bi. Getrude Alex (kushoto) juu ya machapisho mbalimbali yanayotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora nchini.
DSC_1067
Afisa Habari wa Kitengo cha Umoja wa Mataifa cha Habari (UNIC), Bi. Usia Nkhoma Ledama akitoa neno la shukrani kwa wote walioshiriki mdahalo huo.

Friday, December 6, 2013

Shindano la Mama Shujaa wa Chakula Mtandaoni lafikia tamati

Ezeline Mujila


 Balozi wa Grow Masoud Kipanya (kati) Eluka na Bonda Boy (kulia) wakifurahia matokeo.
 Bi Anna Maembe Katibu Mkuu Wizara Ya Maendeleo  Ya Jamii Jinsia Na Watoto akkiasema machache

Mdau Bill Marwa na Marc Wegerif kutoka Oxfam.
 Gloria Kidulile

Khadija Mwanamboka, Balozi Wa Kampeni Ya Grow akifafanua jambo.
 Mkamiti Mgawe Afisa Mradi Haki za Kiuchum  kutoka Oxfam akiongea
 Mshindi wa shindano la Mama Shujaa wa chakula mtandaoni Neema Urasa Kivugo kutoka Kibaya Kiteto akifurahia na kushangiliwa baada ya kutangazwa matokeo

Mshindi Neema Urasa akipongezwa  na Shamim Mwasha
 Mwakilishi Kutoka TAWLAE akifurahia haki kutendeka
 Neema Urasa kabla ya kutangazwa mshindi
Wageni  waalikwa

Mama Kikwete aitaka jamii ya Afrika ya Mashariki na Kusini kuwalea watoto wa kike kama watoto wao waliowazaa

Na Anna Nkinda,  Cape Town.
Jamii imetakiwa kushirikiana kwa pamoja  na kuchukua hatua za karibu kwa kuwalea  watoto wa  kike kama watoto wao wa  kuwazaa huku wakiwapa nafasi kama watoto wa kiume, kuwapatia elimu, kuwaheshimu na  kuwalinda jambo ambalo litawafanya wafanikiwe katika maisha yao.

Wito huo umetolewa leo  na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano wa kamati maalum ya viongozi wanaoshughulikia huduma na elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kutoka nchi za Jumuia ya Afrika ya Mashariki (EAC) na Jumuia ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Kikanda kwa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) unaofanyika katika Hoteli ya The Westin iliyopo mjini Cape Town  nchini Afrika ya Kusini.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema tafiti  zinaonyesha Duniani kote zaidi ya wasichana milioni 58 wameolewa wakiwa na  umri wa chini ya miaka 18 kati ya hao milioni 15 wanaumri wa kati ya miaka 10 hadi 14 huku wengi wao wakiwa wameolewa kinyume na matakwa yao na kushuhudia unyanyasaji wa  kijinsia,  uelewa mdogo wa haki zao na kutopata elimu ya afya ya uzazi.

“Idadi ya watoto wa kike wanaomaliza elimu ya msingi imeongezeka na kuwazidi watoto wa kiume ingawa idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya Sekondari ni ndogo ukilinganisha na watoto wa kiume katika nchi nyingi za Afrika”, alisema Mama Kikwete.

Kwa upande wa maambukizi mapya ya Virusi vya  Ukimwi Mama Kikwete alisema asilimia 42 ya watu wanaopata maambukizi ni vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24, katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara vijana ni asilimia 80.


Mama Kikwete alisema, “Nchini Tanzania tafiti zilizofanyika zimeonyesha kuwa watoto wa kike wengi wanajihusisha  na mahusiano ya kimapenzi mapema kwa asilimi 13 ambao wanafanya  mapenzi kabla ya umri wa miaka 15 na kwa upande wa watoto wa kiume ni asilimia saba matokeo yake ni upatikanaji wa mimba za utotoni.

Msichana  mmoja kati ya wasichana  wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 ni mjamzito  au ameshazaa. Idadi hii ni kubwa katika nchi nyingi za Afrika inasikitisha kwani  kubeba mimba katika umri mdogo kunaweza kusababisha kifo cha mama mjamzito  pamoja na mtoto wakati wa kujifungua”.

Akifungua mkutano huo wa siku mbili Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS)  Prof. Sheila Tlou alisema wajumbe wa kamati hiyo wanatakiwa kuhakikisha maazimio waliyokubaliana yanapitishwa na kufanyiwa kazi  katika nchi husika ili vijana waweze kupata elimu ya afya ya uzazi.

Prof. Tlou alisema, “Tutahakikisha kuwa rasilimali za kutosha zinapatikana ikiwa ni pamoja na kutafuta fedha kutoka kwa wafadhili mbalimbali hii ni kuhakikisha kuwa maadhimio haya yanafanikiwa kwani vijana ni   viongozi wa leo wanaohitaji kupata huduma ikiwa ni pamoja na elimu ili waweze kujiepusha na mazingira ambayo yatawapelekea kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi”.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa EAC Jesca Eriyo alisema mwaka mmoja uliopita wakuu wa nchi za Afrika ya Mashariki walikubaliana kuhakikisha wanaimarisha  utolewaji wa elimu ya afya ya uzazi katika nchi zao na hivyo kuwa rahisi kwa nchi hizo kufanyika kazi maazimio hayo.
“Vijana wanamaswali mengi kuhusu afya ya uzazi na inafika wakati  hawajui wa kumuuliza hivyo basi elimu ya uzazi ifundishwe kwao kwani kutokana na mila za kiafrika  ni vigumu kwa mzazi kuongea na mtoto wake kuhusu afya ya uzazi”, alisema Eriyo.
Alimalizia kwa kusema kuwa vijana wanatakiwa kujua hali ya afya zao ikiwa ni pamoja na kupima kama wamepata maambukizi ya Virusi vya  Ukimwi na kujiepusha na wababa na wamama (mafataki) ambao wanaweza kuwarubuni na kuwaharibia maisha yao jambo ambalo litasababisha  kupatikana kwa kizazi kizuri hapo baadaye.

Kamati hiyo imekutana kwa mara ya pili kwa ajili ya kupitia rasimu ya maazimio ya kuhakikisha kuwa vijana wote katika nchi zilizopo ukanda wa Afrika ya Mashariki na Kusini wanapata elimu kuhusiana na afya ya uzazi na ujinsia jambo ambalo litawasaidia  kufahamu zaidi  ugonjwa Ukimwi kwamara ya kwanza ilikutana mwezi wa nane nchini Botswana.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kusainiwa  na  mawaziri wa Afya na Elimu kutoka nchi 21 za Afrika Mashariki na Kusini ambayo inatakuwa ni sehemu ya utekelezaji kwa nchi kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa vita dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na magonjwa ya zinaa unaotarajiwa kufanyika   hivi karibuni mjini humo.

Balozi seif ali iddi atembelea hoteli yenye chumba ndani ya Bahari katika Hoteli ya Manta Resort iliyoko Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Na Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar 
Mradi mpya wa ujenzi wa Chumba cha chini ya Bahari uliofanywa na Hoteli ya Manta Resort iliyopo katika Kijiji cha Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba umeiweka Zanzibar katika ramani mpya ya Dunia katika harakati za kuimarisha sekta ya Utalii unaobeba nafasi kubwa ya Uchumi katika Mataifa mengi Ulimwenguni. 
Chumba hicho cha chini ya Bahari kilichopo Makangale ambacho ni cha pekee Barani Afrika kimeiwezesha Zanzibar kuwa ya tatu kwa kuwa na mradi kama huo Duniani ikitanguliwa na Nchi za Puerto Riko,Sweden, Kisiwa cha Fiji na ikifuatiwa na Dubai. 
Mradi huo ulioko katika Matengenezo unatarajiwa kuwa na vyumba takriban 220. Jengo hilo lenye huduma kamili anazostahiki kuzipata mwanadamu ni pamoja na chumba cha kulala,huduma za maji safi,Choo, umeme, sehemu ya Mapumziko, na eneo maalum la juu kwa ajili ya kuotea jua. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ambae ndiye aliyeweka Nanga ya Msingi ya mradi huo wa Makangale Miezi 12 iliyopita Tarehe 25/12/2012 akakizindua tena rasmi chumba cha mradi huo kilichoko umbali wa mita Nne chini ya Bahari. 
Uzinduzi huo uliojumuisha mamia ya Wananchi wa Kijiji cha Makangale pamoja na majirani zake ulishuhudiwa pia na Viongozi kadhaa wa Serikali, vyama vya Siasa pamoja na watendaji wa Sekta ya Utalii wakiongozwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake Mh. Bihidndi Hamad. 
Akizungumza mara baada ya kuuzindua Mradi huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kwamba uwepo wa mradi huo wa chumba cha chini ya Bahari ni kielelezo muhimu kitakachokuwa kivutio kwa wageni katika harakati za kukuza utalii hapa Zanzibar.
 Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale kwa kuamua kuwekeza mradi huo wa kipekee Barani Afrika ambao utaleta maendeleo makubwa katika Sekta ya Utalii. “ Nimeshuhudia uzuri wa chumba hichi ambapo yapo mazingira mazuri ya mapumziko na kulala, samaki wa kuvutia. 
Natarajia wakaazi wanaonguuka eneo hilo watashirikiana vyema na uongozi wa Hoteli hiyo katika kukilinda chumba hicho kinachotarajiwa kuongeza ushawishi kwa watalii kutembelea Zanzibar “. Alisisitiza Balozi Seif. 
 Alielezea matumaini yake kwamba Uongozi wa Hoteli ya Manta Resort Makangale utaendelea kutoa huduma bora na za uhakika ili kuongeza idadi ya wageni na watalii kutembelea Pemba. Katika kuunga mkono jitihada hizo za wawekezaji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwapa mashirikiano ya karibu wawekezaji wa sekta hiyo ili waendeshe shughuli zao kwa ufanisi mkubwa. 
“ Sisi Viongozi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Rais, Makamu wa Kwanza wa Rais na mimi mwenyewe tunapofanya ziara nje ya nchi hutumia fursa ya kuwabembeleza wawekezaji kuwa kuwekeza Nchini mwetu hasa katika sekta ya utalii na Viwanda. 
Bahati nzuri wanatuitikia na wanakuja na ndio maana leo Zanzibar ina vitega uchumi vingi vya sekta ya utalii na mfano hai ni huu mradi wa chumba cha chini ya Bahari hapa Makangale “. Alifafanua Balozi Seif. 
Alifahamisha kwamba pamoja na maendeleo ya ujenzi wa miradi ya uwekezaji katika sekta ya utalii lakini bado Serikali pamoja na Wananchi wanahitaji kuendelea kuwa na matumaini ya kuongezeka kwa idadi ya watalii hali ambayo itasaidia kuongeza mapato ya Taifa. 
Hata hivyo Balozi Seif alitahadharisha kwamba watalii na wageni hao hawataingia nchini iwapo jamii haitojikita katika kuendeleza amani na utulivu ndani ya maeneo yao hasa sehemu zenye vitega uchumi hivyo. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wananchi hawanabudi kupania kuiweka nchi katika hali hiyo ya amani na usalama ili wageni hao washawishike kupenda kuendelea kutembelea Nchini na kuishi bila ya wasi wasi. 
“ Tuwe wanyenyekevu kwa wageni wetu, tuwaonyeshe bashasha za Kizanzibari kama ilivyo tabia na desturi yetu, tusiwabughudhi wakiwa ufukweni au katika matembezi yao. Tunataka wafurahie ukaazi wao katika visiwa vyetu vya karafuu na Viungo “. Alieleza Balozi Seif. 
Mapema Meneja Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu kwa Nini “ alisema utafiti wa mradi huo ulifanyika kwa karibu miaka sita ambapo wataalamu wa kimazingira na mambo ya bahari walilazimika kupima mwenendo wa maji ya bahari ya eneo hilo ili kuwa na uhaika wa kuanzisha mradi huo. 
Bwana Methew Saus alisema mazingira ya Kisiwa cha Pemba yamepelekea kuanzishwa kwa mradi huo wa majaribio wa chumna cha chini ya Bahari uliogharimu zaidi ya Dola za Kimarekani Laki Tano { U$ 500,000 } sawa na fedha za Kitanzania Milioni Mia 758,000,000/-. 
Meneja huyo wa Hoteli ya Manta Resort ya Makangale ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Wizara inayosimamia Sekta ya Utalii kwa ushirikiano iliyompa kuweza kufanikisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar. 
Akimkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk alisema mradi huo kwa kiasi kikubwa umeanza kuitangaza vyema Zanzibar katika sekta ya utalii wa Daraja la juu duniani. 
Waziri Mbarouk aliwaasa wananchi na hasa wavuvi wanayoizunguuka hoteli hiyo kujiepusha na uvuvi pembezoni mwa mradi huo jambo ambalo litaondoa sifa na mazingira halisi ya kuwepo kwa samaki wanaokizunguuka chumba hicho. 
Alikemea tabia iliyoanza kujichomoza ya baadhi ya wavuvi wa maeneo hayo ya kuvua kwa kutumia nyavu ndogo nje ya chumba hicho kwani inaweza kumvunja moyo muwekezaji huyo ambae ameshajitolea kusaidia maendeleo ya Vijiji jirani na Hoteli hiyo. 
Mradi wa mwanzo wa ujenzi wa vyumba vya chini ya Maji Jules Undersea Lodge umeanza Nchini Puerto Rica mwaka 1970, Utter In Vasteras Sweden Mwaka 2000, Poseidon Undersea Resort Fiji na Mwengine Crescent Hydropolis unaendelea kujengwa Nchini Dubai.
Balozi Seif akiwa pembezoni mwa dirisha ndani ya  chumba cha chini ya Bahari akiangalia samaki na mazingira yake mara baada ya kuuzindua mradi huo hapo Manta Resort Hoteli Makangale.
Balozi Seif akiangalia ngazi ya kutokea juu ya chumba cha chini ya Bahari katika Hoteli ya Manta Resort Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba kwenye sherehe za uzinduzi wa chumba hicho ikiwa ni muendelezo wa sherehe za kutimia miaka 50 ya mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Meneja  Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus  kwa kukamilisha ujenzi wa chumba cha chini ya Bahari kwenye hoteli yake iliyopo Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba huku Waziri wa Habari Mh. Marouk akifurahia kitendo hicho.
Kitanda na mandhari halisi na nzuri iliyomo ndani ya chumba cha chini ya Bahari katika hoteli ya Manta Resort Makangale Kaskazini Pemba mradi uliozinduliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar balozi Seif.
Sehemu ya choo katika chumba cha chini ya Bahari kilichopo kwenye Hoteli ya Manta Resort  huko Makangale Pemba.
Meneja  Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus Maarufu “ Babu kwa Nini “akitoa maelezo ya hatua zilizochukuliwa kukamilisha ujenzi wa chumba cha chini ya Bahari katika Hoteli ya Manta Resort iliyoko Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba.Kushoto ya Balozi Seif ni Mkewe Mama Asha Suleiman Iddi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Said Ali Mbarouk na Naibu wake Mh. Bihindi Hamad.
Meneja  Mkuu wa Hoteli ya Manta Resort Bwana Methew Saus akionyesha eneo la juu la chumba cha chini ya bahari ambapo mgeni atapata fursa ya kupunga upepo pamoja na kuota jua.
Mandhari nzuri ya Hoteli ya Manta Resort ya Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba eneo ambalo kipo chumba cha chini ya Bahari.