WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametoa mwezi mmoja kwa Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) iwe imetoa mapendekezo kwa Serikali kuhusu matumizi ya maji machafu yanayotokea kwenye viwanda vinne vya ngozi, magunia, nguo na maturubali (canvas).
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumamosi, Desemba 7, 2013) mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kwenye kiwanda cha nguo cha 21st Century kilichopo eneo la Kihonda Viwandani nje kidogo ya mji wa Morogoro.
Akizungumza na uongozi wa mkoa, wilaya, kiwanda hicho pamoja na NEMC ya mara baada ya kutembelea eneo ambalo limeathirika na maji yanayotiririka kutoka kwenye viwanda hivyo, Waziri Mkuu alisema tatizo lililopo linachangiwa na kutokuwepo kwa mtu au taasisi maalum ya kusimamia mabwawa ya mfumo wa majitaka (waste management ponds).
“Viwanda hivi vilibinafsishwa lakini mfumo wa usafishaji majitaka haukubinafsishwa... NEMC iishauri Serikali nini kinapaswa kifanyike. Ifanye utafiti kuhusu matumizi ya majitaka yanayotoka kwenye viwanda hivi na ilete uchambuzi huo Serikalini,” alisema.
Waziri Mkuu ambaye alitembelea eneo la Kihonda Mbuyuni katika kata ya Mafisi ambako maji hayo yanaingia korongoni na kuelekea mto Ngerengere, alishuhudia mifereja ya maji machafu yenye harufu kali na rangi mchanganyiko ya kijani na bluu ikitiririka katikati ya nyumba za watu.
“Hatuwezi kuendelea na hali hii ya kutiririsha maji kwenye makazi ya watu, ni bomu litakalolipuka hivi karibuni. Kuna watoto wanacheza katika maeneo yale wanaweza kunywa au kunawa yale maji, kuna mifugo inapita, inaweza kunywa yale maji, ni hatari kwa kila mmoja wetu,” alisisitiza.
Aliitaka NEMC iangalie uwezekano wa kumpatia mtu binafsi aendeshe mfumo huo hata kama itabidi asimamiwe na Halmashauri lakini kinachotakiwa ni kupatikana kwa mtu mwenye uwezo wa kuendesha mfumo huo kwa utaalamu. Aliipa NEMC miezi miwili ili iwe imekamilisha utafiti wake pamoja na kuangalia uwezekano wa kumpata mtaalamu wa kuifanya kazi hiyo.
Alitoa pia mwezi mmoja kwa Manispaa ya Morogoro kuwa imetafuta eneo jipya na kubwa zaidi kwa ajili ya kumwaga takataka kwani dampo lililopo katika kata hiyo linachangia uchafuzi wa mazingira na kuleta kero kwa wananchi.
“Wakati ule dampo linaletwa huku ilikuwa ni sahihi kwa sababu huku kulikuwa ni nje ya mji lakini kwa sasa siyo sahihi. Nimemwambia Meya akae na watu wake wafikirie kujenga dampo jingine la kisasa... watafute eneo kubwa na kuwe na mifumo ya kisasa,” alisema.
Kuhusu matumizi ya kuni katika kiwanda hicho, Waziri Mkuu alisema hakubaliani kabisa na matumizi ya kuni kwa sababu yanachangia uharibifu mkubwa wa mazingira. Aliutaka uongozi wa kiwanda hicho, uendelee na mpango wake mpya wa kutumia makaa ya mawe au hata kuangalia mpango wa kutumia umeme utakaotokana na gesi.
“Najua kuna gharama katika kubadilisha mfumo wa boilers zenu lakini matumizi ya tani 50 za magogo kwa siku hapana! Tani 50 nazilinganisha na magunia 500 ya mahindi, sasa kwa miezi sita au kwa mwaka mmoja, mtatumia kuni kiasi gani? Si Morogoro nzima itateketea? Alihoji Waziri Mkuu.
Akijitetea kuhusu suala hilo, mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji alisema moto unaotokana na makaa ya mawe hauna nguvu ya kutosha kuzalisha mvuke wa kuzalisha umeme wa kuendeshea mitambo ya kiwanda hicho. “Tumeomba kwa mwaka mmoja tu tupewe ruhusa ya kuchanganya makaa ya mawe na vipande vya miti hadi tutakapopata boilers mpya,” alisema.
Waziri Mkuu alimweleza Bw. Dewji asubiri majibu ya maombi yake kutoka NEMC ambako maombi hayo yalipelekwa lakini pia akawaonya viongozi wa NEMC kuwa makini wakati wanapitia maombi hayo ili waweze kuwa na mbinu za kubainisha kama kweli vitatumika vipande vya miti au watarudia utaratibu wao wa zamani wa kutumia magogo lakini wanayakata katika vipande vidogo vidogo.
Hata hivyo, katika kikao hicho Meya wa Manispaa ya Morogoro, Bw. Amiri Nondo na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Bw. Said Amanzi walielezea kutoridhishwa kwao na uhusiano uliopo baina ya uongozi wa kiwanda hicho na mamlaka zilizopo wakidai kufungiwa mageti na kutotekelezwa kwa maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.
Waziri Mkuu alimtaka mmiliki wa kiwanda hicho, Bw. Gulam Dewji ajenge mahusiano mazuri na uongozi wa mkoa kwa sababu viwanda vyake viko katika mkoa huo na hivyo hana budi kuzingatia maslahi ya wakazi wa Morogoro kwanza. “Wao ni viongozi wa mkoa lakini pia ni wawakilishi wa wananchi, kwa hiyo wanawajibika kwa wananchi, linapotokea jambo wao ndiyo wataulizwa na wananchi,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment