Wednesday, January 2, 2019

NHIF YAKUTANA NA VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA TUNDURU

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF)mkoa wa Ruvuma,umekutana na wanachama na viongozi wa vyama viwili vya msingi vya ushirika vinavyojihusisha na kilimo cha zao la korosho katika wilaya ya Tunduru.

Lengo ni kuhamasisha wanachama na viongozi wa vyama hivyo kujiunga na mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kwa ajili ya kupata huduma za matibabu pindi wanapoumwa kwa kuwa shughuli za kilimo zinahitaji mtu mwenye afya njema ambayo itamruhusu kuendelea na majukumu yake katika kipindi cha msimu wa kilimo.

Wanachama hao ni kutoka vyama vya Naluwale na Mumsasichema kata ya Muhwesi ambayo ni maarufu kwa uzalishaji mkubwa wa korosho wilayani hapa.Akizungumza na Wanachama hao kaimu Meneja wa mfuko huo Antony Mgima alisema, mpango huo unalenga kutoa huduma kwa mwanachi mmoja kwa gharama ya shilingi 78,600 ambapo mwanachama atapata fursa ya kuhudumiwa kuanzia ngazi ya zahanati,kituo cha Afya na Hospitali zote Nchini.

Alisema, mpango huu wa sasa utasaidia sana kila mmoja kunufaika nao tofauti na hapo awali ambapo ni watumishi wa umma pekee yao ambayo walikuwa na sifa ya kuwepo katika mpango wa huduma za matibabu.

Kwa mujibu wake, mwanachama wa NHIF ana hiari ya kumlipia fedha kama michango kwa mtu yoyote ambaye anaona anastahili kuwemo katika mpango hasa ikizingatia kuwa, kwa sasa mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeboresha sana huduma zake .

Mkuu wa wilaya ya Tunduru Juma Homera,ameitaka NHIF kuhakikisha wanawashirikisha viongozi wa vijiji na kata katika kuhamasisha wananchi wengi zaidi ili nao waweze kujiunga na mfuko huo badala ya kulenga wanachama na viongozi wa vyama vya ushirika.

Alisema, hatua hiyo itasaidia sana kupata wananachi wengi kwani tabia ya wananchi wanataka kusikia kauli za viongozi wao wa serikali na sio vyama vya msingi kwa sababu baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wanalalamikiwa sana kutokana na kuwaibia wakulima ambao ni wanachama wao.

“ni vema sasa mkaenda mbalki zaidi kufanya mikutano na wananchi wengine katika vijiji vyetu hasa kipindi hiki ambacho minada ya korosho inatarajia kuanza,ni lazima sisi sote tuwe na mkakati wa pamoja kutangaza huduma zinazotolewa na NHIF badala ya kuelekeza nguvu kubwa kwa wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika”alisema Homera.

Hata hivyo, amewataka wakulima ambao ni wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika kuchangamkia fursa ya kujiunga na NHIF kwa ajili ya kupata huduma ya matibabu hasa kwa kutambua kuwa,watu wenye Afya njema watakuwa na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shgughuli za uzalishaji mali.

Alisema, kutokana na changamoto kubwa ya matibabu kwa baadhi ya maeneo hapa Nchini,mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeamua kuisaidia serikali katika kukabiliana na tatizo hilo na kuhaidi kuwa,serikali ya wilaya na NHIF kwa pamoja itahakikisha inapita viijini ili kuhamasisha watu wengi kujiunga na mfuko huo.

Baadhi ya wanachama wa vyama hivyo Hussen Namkuhule na Ali Mbemba wameuomba mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuongeza idadi ya wategemezi ambao wataingizwa katika utaratibu wa uanachama na kupata matibabu badala ya kuwa na ukomo.

No comments: