Wednesday, December 5, 2018

WATOTO 52 NA WATU WAZIMA WAWILI WENYE MATATIZO YA MOYO YA KUZALIWA NAYO WAFANYIWA UPASUAJI KAMBI MAALUM

Wagonjwa 54 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo wamefanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua na bila kufungua kifua katika kambi maalum ya matibabu inayofanyika katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Matibabu hayo yanafanywa na madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kushirikiana na madaktari wa mradi wa Little Heart wa nchini Saud Arabia ambao ni moja ya mradi wa Afya ulioko ndani ya Taasisi ya Msaada ya Muntada yenye makao makuu yake mjini London nchini Uingereza.

Upasuaji huo umefanyika kwa watoto 52 na watu wazima wawili wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu na valvu .

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salam Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto kutoka JKCI Godwin Sharau alisema kwa upande wa upasuaji wa kufungua kifua wamefanya upasuaji kwa watoto 19 kwa kurekebisha valvu, kuziba matundu, kurekebisha mishipa ya moyo ambayo imekaa vibaya na kurekebisha mfumo wa uzungukaji wa damu katika moyo.

Dkt. Sharau alisema watoto waliowafanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na wengine wameshatoka katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) na kupelekwa wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu ikiwa ni pamoja na kuanza mazoezi.

Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto Godfrey Mbawala alisema wamefanya upasuaji wa bila kufungua kifua kupitia tundu dogo linalotobolewa katika mshiba mkubwa wa damu uliopo kwenye paja kwa wagonjwa 35 kati ya hawa watoto 33 na watu wazima wawili.

Dkt. Mbawala alisema watu wazima waliowafanyia upasuaji wanaumri wa miaka 31 lakini matatizo ya moyo waliyokuwa nayo ni ya kuzaliwa nayo ambapo mmoja mshipa wake mkubwa wa moyo ulikuwa umebana na kushindwa kupitisha damu vizuri na mmoja alikuwa na tundu ambalo wameliziba.

“Tunaendelea na matibabu kwa wagonjwa, hadi sasa kwa mgonjwa tuliyemfanyia upasuaji mwenye umri mdogo ni miezi sita na umri mkubwa ni miaka 31. Ninawasihi wazazi wenye watoto wenye matataizo ya moyo wasikate tama kwani magonjwa ya moyo yanatibika”, alisema Dkt. Mbawala.

Naye Abubakari Matitu mwenye umri wa miaka 31 ambaye ni mkazi wa Kisarawe alisema alianza kuhisi kuwa na matatizo mwaka 2015 akiwa na umri wa miaka 28 akaamua kwenda kufanyiwa vipimo na mara baada ya kufanyiwa vipimo aligundulika kuwa na tatizo la tundu katika moyo na mshipa mkubwa wa damu unaotoa damu kwenye moyo na kupeleka mwilini haukuwa unapitisha damu vizuri.

“Nilianza kliniki katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete mwaka 2015, mwezi huu siku ya Ijumaa nililazwa na kufanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua siku ya Jumatatu. Namshukuru Mungu baada ya kufanyiwa upasuaji najisikia hali ya tofauti ukilinganisha na nilivyokuwa mwanzo”.

“Ninawashauri watanzania wenzangu wakipata matatatizo wafanye utaratibu wa kufikia katika hospitali kubwa kwa ajili ya kupatiwa huduma. Mimi nimetibiwa, kabla ya matibabu niliambiwa damu ilikuwa inashuka kwa tabu katika miguu baada ya matibabu ninasikia kabisa damu inashuka miguuni”, alisema Matitu ambaye kitaaluma ni Afisa Muuguzi.

Jumla ya watoto 80 wanatarajiwa kutibiwa katika kambi hiyo ya siku nane iliyoanza tarehe moja na itamalizika tarehe nane mwezi huu .

No comments: