Thursday, December 13, 2018

WABANGUAJI KOROSHO WAMPA KONGOLE RAIS MAGUFULI


Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, akisisitiza jambo kwenye kikao na wawakilishi wa Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania(UWWKT) kilichofanyika kwenye hoteli ya Lindi Sea View. Pembeni ya Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi, mhehsimiwa Shaibu Ndemanga, Mkurugenzi Mkuu wa SIDO Profesa Sylvester Mpanduji na kulia ni Mwenyekiti wa UWWKT Tumpale Magehema 
Baadhi ya wanachama wa Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania (UWWKT) wakimisikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mhandisi Stella Manyanya. Umoja huo wa wabanguaji wadogo wa korosho umeonesha nia ya kubangua korosho iliyonunuliwa na serikali. 
Mwenyekiti wa Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania (UWWKT) Bi. Tumpale Magehema akisoma risala mbele ya Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mhandisi Stella Manyanya alipofanya kikao na baadhi ya wanachama wa umoja huo mjini Lindi. 
Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, mhandisi Stella Manyanya(katikati walioketi) kwenye picha ya pamoja na wawakilishi wa wanachama wa Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania (UWWKT). Wengine walioketi kuanzia kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa SIDO, Profesa Sylvester Mpanduji, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga, Mwenyekiti UWWKT Tumpale Magehema na Mkurugenzi Mtendaji wa ANSAF, Audax Rukonge.

…………………………..

Na Mwandishi Wetu

Uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kununua korosho za wakulima na kuzibangua nchini umepongezwa na Umoja wa Wabanguaji Wadogo wa Korosho Tanzania (UWWKT).

Akisoma risala mbele ya Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Stella Manyanya, Mwenyekiti wa umoja huo Bi. Tumpale Magehema amesema uamuzi wa Rais Magufuli una nia ya kuwapa ajira wanachama wake wapatao 2881, jambo ambalo ni la kupongezwa.

Licha ya kutoa ajira Bi. Tumpale ameueleza uamuzi huo wa kijasiri uliofanywa na Rais Magufuli utaongeza ari ya kufanya kazi na kuchochea ukuaji wa uchumi hasa kwenye mikoa inayolima korosho kwa wingi.

Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Katibu wa umoja huo Bw. Audax Mkongi, alimueleza mhandisi Manyaya kuwa umoja huo ni asasi mwamvuli ya kitaifa ya wabanguaji wadogo yenye jumla ya vikundi 183 kutoka wilaya tisa za mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Morogoro. Baadhi ya wilaya hizo ni Ulanga, Tandahimba, Kisarawe, Liwale na Ruangwa.

Kwenye taarifa yake Bw. Mkongi amesema tangu umoja huo uanzishwe mwaka 2015 umefanikiwa kumiliki mashine za kubangua korosho ghafi kwa kutumia mkono 117, mashine za kutumia miguu 317, mashine za kuchemshia (boiler) 23, mashine za kupanga madaraja 12, mashine za kukaushia (oven) 12, na za kufungashia 14 zenye uwezo wa kubangua korosho ghafi kg 25,370 kwa siku.

Kwa upande wake mgeni rasmi kwenye hafla hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Lindi Sea View, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya ameupongeza umoja huo kwa ari na nia ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano ya uchumi wa viwanda.

Licha ya kuupongeza umoja huo, mhandisi Manyanya pia amewahakikishia ushirikiano kutoka wizara yake na kwa kuanza serikali inaandaa utaratibu wa kuutumia ili kuingia nao mikataba ya kubangua korosho iliyonunuliwa na serikali msimu huu.

Wakati huo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), Profesa Sylvester Mpanduji amesema taasisi yake itaendelea kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele pamoja na wadau wengine wa korosho kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati ili kuongeza thamani na ubora wa zao hilo ambalo linaongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni.

No comments: