Friday, December 14, 2018

UJENZI BARABARA BARIADI HADI MASWA MKOANI SIMIYU WASHIKA KASI

Maafisa wa Serikali kutoka Wizara ya Maji, Wizara ya Ujenzi, miundombinu na Mawasiliano, wakiongozwa na Wizara ya Fedha na Mipango, wakipata maelezo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Bariadi hadi Maswa, (km50) wakati wa ziara ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani Simiyu, ili kujua mafanikio, changamoto na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.
Mchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Jordan Matonya, akitaka kupata ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Bariadi hadi Maswa, mkoani Simiyu, yenye urefu wa km 50, kutoka kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara mkoani humo, Mhandisi Mohamedi Athumani (Hayuko pichani).

……………………..

Na Benny Mwaipaja, WFM, Simiyu

UJENZI wa barabara yenye urefu wa kilometa 50 kati ya mji wa Bariadi na Maswa mkoani Simiyu kwa kiwango cha lami, inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 88, unaendelea kwa kasi ambapo hivi sasa umefikia asilimia 34.

Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini-TANROADS, mkoa wa Simiyu, Mhandisi Mohamedi Athumani, ameiambia timu ya maafisa wa Serikali inayoongozwa na Wizara ya Fedha na Mipango, inayofuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo mkoani humo kwamba mradi huo utakapo kamilika mwezi Oktoba mwakani, utafungua fursa za kibiashara na kiuchumi kwenye mkoa huo na mikoa jirani ya Mwanza, Shinyanga, Singida na nchi jirani ya Kenya.

Amesema kuwa kazi zilizofanywa na mkandarasi anayejenga barabara hiyo, Kampuni ya CHICO ya China, ni kuanza kwa ujenzi wa madaraja makubwa mawili ya Simiyu na Banhya na uinuaji wa tuta la barabara maeneo mbalimbli ya mradi.

“Kuna madaraja mengine madogo madogo (Pipe culverts 57) pamoja na makalvati madogo (Box culverts 12), kwenye kipande hiki cha Barabara chenye urefu wa kilometa 50 na mkandarasi, Kampuni ya CHICO inafanyakazi vizuri na tuna imani kwamba ujenzi wa barabara hii utakamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2019 kama mkataba unavyoonesha” alifafanua Mhandisi Athumani.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri Mkazi wa mradi huo, Mhandisi Swalihi Kazuvi amesema kuwa barabara ya Mwigumbi-Maswa-Bariadi na Lamadi, inayojengwa kwa kiwango cha lami, yenye urefu wa kilometa 172, itakapokamilika, italeta chachu ya maendeleo yanayopitiwa na barabara hiyo.

“Kipande cha barabara ya lami kutoka Mwigumbi mpaka Maswa na kile cha Bariadi hadi Lamadi vimekamilika kwa hiyo kipande kilichobaki ni hiki (Bariadi-Maswa), ndio maana unaona magari yanayopita barabara hii ni mengi licha ya kwamba kipande hiki cha kilometa 50 hakijakamilika, madereva wanaona afadhali wapite huku kwenda Musoma kuliko kupitia njia ya Mwanza” aliongeza Mhandisi Swalihi Kazuvi

Lengo la ziara hiyo ya maafisa wa Serikali ni kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezawa katika Mkoa huo ili kujua mafanikio, changamoto na mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.

No comments: