Friday, December 7, 2018

TRA YAWATAKA MAWAKALA FORODHA KUHAKIKISHA NAMBA ZAO ZA UTAMBULISHO WA MLIPAKODI (TIN)

Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA) imewataka Mawakala wa Forodha wote kuhakakisha wanafanya uhakiki wa namba zao za Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na kuisaidia mamlaka hiyo kukusanya mapato mengi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishna wa Kodi za Ndani wa mamlaka hiyo, Abdul Zuberi katika Semina iliyowakutanisha na makampuni ya mawakala wa forodha iliyojadili masuala mbalimbali ya kodi na ushuru wa forodha.

Amesema kuwa mawakala hao wanatakiwa kuhakiki TIN zao kutokana na kuwepo mkanganyiko kuwa na zaidi TIN hali inayowapa shida ya kutambua idadi ya mawakala wanaotakiwa kulipa kodi.“ Kuna watu wana TIN zaidi ya moja wanazitumia bila kufanyiwa uhakiki na wengine wanazifanyia udanganyifu inatupa tabu kuwatamabua hivyo ni vema mkazifanyia uhakiki,” amesema.

Amebainisha kuwa TRA mawakala watakaobainika kutumia TIN zaidi ya moja bila kuzifanyia uhakiki watachukuliwa hatua za kisheria.Amesisitiza kuwa mawakala wa forodha watakaofanya uhakiki wa TIN zao watapatiwa cheti cha utambulisho ili kuondokana usumbufu wakati wa kuwakagua.

Ameongeza kuwa mawakala wanatakiwa kuwasilisha taarifa sahihi za mapato yao kwa mwaka pamoja kulipa Kodi ya Ongezeko la Mapato (VAT).

Amefafanua kuwa mamlaka hiyo itatoa kwa mawakala jinsi ya kutambua Mashine za Kielektroniki feki (Efd) na kwamba kufanya kutawasaidia kuwaepusha kukumbwa na mkono wa sheria na faini.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFA) ambaye pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam,Frank Kamugisha ameiomba mamalaka hiyo kujenga utaratibu wa kukutana nao kuzungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili ili ziweze kutafutiwa ufumbuzi. 

Kamugisha amesema anaamini mambo yaliyojadiliwa yatafanyiwa kazi ili kuondoa sintofahamu kati yao na TRA kwenye masuala ya kodi na forodha. 
Pia amesema chama hicho kitayapa umuhimu yale yote walioelekezwa ili kujenga uchumi wa nchi kwa kuisaidia mamlaka hiyo kukusanya kodi.

No comments: