Sunday, December 9, 2018

TRA YAIBUKA MSHINDI WA JUMLA UANDAAJI VITABU VYA HESABU

Na Veronica Kazimoto ,Dar es Salaam 

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeibuka mshindi wa jumla katika tuzo za uandaaji wa hesabu bora mwaka 2017 zinazotolewa kila mwaka na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA). 

Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika mwishoni mwa wiki katika Kituo cha Mikutano cha NBAA Bunju jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Kamishna Mkuu wa TRA Charles Kichere, amewaasa wahasibu nchini kuwasaidia wateja wao kuandaa vitabu vya mahesabu kwa kufuata viwango vya kimataifa ili kuepuka kufanya marekebisho ya vitabu hivyo na kupotea kwa kodi. 

Amesema taasisi nyingi zimekuwa hazijui kuandaa vitabu vya mahesabu na wakati mwingine hulipua katika kuviandaa ambapo matokeo yake vimekuwa vikikataliwa na kutakiwa kurudia mahesabu hayo hali ambayo inafanya kazi hiyo kuwa ngumu na wakati mwingine inaleta mashaka. 

Kichere amesema siri ya ushindi wao ni ushirikiano mzuri walionao kama mamlaka ikiwa ni pamoja na kutoa muda wa ziada wa kazi ili kuweza kukidhi viwango vya kimataifa na kama taasisi ya kukusanya mapato lazima ifanye hivyo. 

“Tumefurahi kupata tuzo hii inayoonyesha kuwa, tunatengeneza mahesabu yetu kwa kufuata taratibu na viwango vya kitaifa katika uandaji wa vitabu vinavyohusiana na fedha. Tumekuwa na ushirikiano mzuri na wahasibu wetu ambao mara zote wamejitolea muda wao ili kukidhi vigezo hivi vya kimataifa,” amesema Kichere. 

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji ambaye alikuwa mgeni rasmi katika utoaji wa tuzo hizo, aliwaambia wahasibu kuwa, imani yake ni kwamba, siku tatu walizokutana wamezitumia vizuri kwa kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu kwa undani. 

Amesema kuwa amefurahishwa na namba ya wahudhuriaji wa mkutano huo wa wahasibu ambayo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka jambo ambalo limewawezesha kujadili kwa undani changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji wa kazi zao. 

Kabla ya ushindi huo wa jumla, TRA ilipata ushindi wa kwanza katika kipengele ya kushindanisha Taasisi za Serikali ambapo Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) lilikuwa la pili na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) ilikuwa ya tatu.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji akimkabidhi Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere tuzo ya uandaaji wa vitabu vya hesabu kwa kuzingatia taratibu na kanuni za mahesabu katika Taasisi za Serikali zinazotumia Mfumo wa Uhasibu wa IPSAS ambapo TRA imeibuka mshindi wa jumla. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki. 
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (wa tatu kulia) akiwa ameshikilia tuzo ya uandaaji wa vitabu vya hesabu kwa kuzingatia taratibu na kanuni za mahesabu katika Taasisi za Serikali zinazotumia Mfumo wa Uhasibu wa IPSAS ambapo TRA imeibuka mshindi wa jumla. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha cha Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere (wa tatu kulia) akiangalia kwa makini tuzo ya uandaaji wa vitabu vya hesabu kwa kuzingatia taratibu na kanuni za mahesabu katika Taasisi za Serikali zinazotumia Mfumo wa Uhasibu wa IPSAS ambapo TRA imeibuka mshindi wa jumla. Hafla ya utoaji wa tuzo hizo ilifanyika katika Kituo cha Mikutano cha cha Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) jijini Dar es Salaam mwishoni wa wiki.

No comments: