Monday, December 17, 2018

Shule za Jumuia ya Wazazi (CCM) kufundisha ufugaji nyuki

Na Joseph Zablon

Jumuia ya Wazazi (CCM), imeanza kutekeleza mpango wa kutoa elimu ya ufugaji nyuki kibiashara kwa wanafunzi wa shule zote zinazomilikiwa na jumuia hiyo na kwa wananchi wa wilaya zote nchini kwa lengo la kujiimarisha kiuchumi na pia kutoa ajira kwa vijana mara baada ya kuhitimu masomo yao ya sekondari

Akizungumza na waandishi wa habari kufuatia ziara ya hivi karibuni ya kukagua utekelezaji wa mpango huo, Mwenyekiti wa Jumuia hiyo, Dk Edmund Mndolwa alisema ufugaji nyuki licha ya kuwezesha upatikanaji wa asali lakini pia kuna mazao mengi yanayotokana na wadudu hao.

“Tutalenga kwanza kwenye asali ingawa kuna mazao mengi na yenye thamani kubwa kuliko asali” alisema na kuongeza kuwa ameziagiza shule zote 55 za sekondari za wazazi nchi nzima kuhakikisha hadi Aprili 2019 mazao ya kwanza au kabla ya hapo” alisema mwenyekiti huyo.

Alisema anawapongeza viongozi na watendaji wa shule hizo kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwani utakuwa na mchango mkubwa katika kuitoa ajira kla vijana,jamii, pato la ndani la Taifa,  upatikanaji wa fedha za kigeni, huanzishwaji wa viwanda vidogo na kupunguza umaskini kwa jamii.

Alisema mpango huo ambao ulibuniwa na yeye mwenyewe, ukakubaliwa na kamati ndogo ya baraza, kisha ukapitishwa na Baraza Kuu la Jumuia ya Wazazi Taifa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kuziendesha shule hizo na kuziimarisha kiuchumi tofauti na ilivyokuwa awali.

“Tunatekeleza mpango mkakati tuliojiwekea wa kuhakikisha pamoja na mambo mengine shule zinakuwa na ongezeko la wanafunzi katika muhula mpya wa masomo 2019 na pia kupata fedha za ziada kwa ajili ya kulipa madeni ya shule hizo za Wazazi” alisema Dk Mndolwa.

Alisema katika ziara yake ya ukagua uhai wa jumuia katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Manyara na Arusha hivi karibuni, alisema ameridhishwa na mipango ya utekelezaji wa mradi huo na alibainisha kuwa tayari kuna walimu wakufunzi ambao wamepata mafunzo ya ufugaji nyuki.

Dk Mndolwa alisema walimu hao ambao waliteuliwa walimu wakuu wa shule za jumuia hiyo, walipata mafunzo yao mkoani Singida na wanatarajiwa kuwa chachu kwa wenzao na wanafunzi kwa ujumla wake na mafunzo hayo ya ufugaji nyuki yatakuwa yakitolewa katika shule hizo kwa wakati usioingiliana na wa masomo ya kawaida.

Pia Dk Mndolwa alibainisha kuwepo kwa changamoto za upatikanaji wa mbao kwa ajili ya utengenezaji wa mizinga hususan wilaya za mjini na kuwataka viongozi na watendaji kuichukulia kama fursa kwa kutafuta ufumbuzi kwa kuwashirikisha viongozi wa serikali. 
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wazazi (CCM) Taifa, Dk Edmund Mndolwa (kulia), akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari na wajumbe wa Baraza Kuu la Jumuia hiyo jijini Dar es Salaam, kuhusiana na kuanza kutekeleza kwa mradi wa mafunzo ya ufugaji nyuki mashuleni kwa shule zinazomilikiwa na jumuia hiyo. Picha na Joseph Zablon.No comments: