Monday, December 3, 2018

MNYETI AWAFAGILIA DC WA KITETO NA SIMANJIRO

MNYETI AWAFAGILIA DC WA KITETO NA SIMANJIRO 

MKUU wa Mkoa wa Manyara Alexander Pastory Mnyeti amewafagilia wakuu wa Wilaya za Kiteto mhandisi Tumaini Magessa na Simanjiro mhandisi Zephania Chaula kuwa ndiyo wakuu wa wilaya bora kwa sasa kwenye mkoa wake, wenye kuchapa kazi na kuhudumia wananchi. 

Mnyeti akizungumza mjini Babati alisema mkuu wa wilaya ya Kiteto mhandisi Tumaini Magessa na mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula, ndiyo wakuu wa wilaya bora kwa sasa mkoani Manyara. 

Alisema anataja majina hayo mawili ya wakuu hao wa wilaya ili iwe changamoto kwa wakuu wengine wa wilaya za mkoa huo wenye wilaya tano, kutekeleza wajibu wao ipasavyo. Alisema wakuu wengine wa wilaya ambao hawajatajwa wasife moyo ila waongeze bidii na juhudi katika kuwatumikia wananchi na kutekeleza wajibu wao ipasavyo. 

Alisema anatangaza majina ya wakuu hao wa wilaya wanaongoza mkoani humo baada ya yeye kushauriana na Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Simon Lulu na Katibu Tawala wa mkoa huo Missaile Mussa, ndipo wakapatikana hao. Alisema mkuu wa wilaya anapaswa kutoa maamuzi kwenye eneo lake la utawala na siyo kupiga simu kwa mkuu wa mkoa kila wakati kuomba msaada ili hali uwezo wa kutoa maamuzi anayo. 

Alisema wameangalia namna wanavyotoa maamuzi yao, utulivu wa wilaya, wanavyowasimamia watumishi wao wa ngazi ya chini na kudhibiti ufujaji wa fedha za miradi ya maendeleo. "Changamoto zenu pambaneni nazo kwani hata mimi napambana na nafasi yangu siyo kila wakati napiga simu kwa mheshimiwa Waziri Mkuu Kasim Majaliwa kuomba msaada ila mkizidiwa itajulikana hapo kweli ni haki," alisema Mnyeti. 

Alisema hata Rais John Magufuli alipotangaza kuwa mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka anaongoza kwa wakuu wa mikoa yeye hakulalamika hivyo na wakuu wa wilaya wengine wasihofie hilo. "Najua mkuu wa wilaya ya Hanang Joseph Mkirikiti atasema ohoo yeye hana mwaka tangu afike Hanang' lakini hata mimi, alipotangazwa wa Simiyu sikusema sina mwaka tangu nije Manyara," alisema Mnyeti. 

Mkuu wa wilaya ya Kiteto, mhandisi Tumaini Magessa alisema baada ya kuwepo utulivu eneo la Emboley Murtangos sasa wanageukia hifadhi ya msitu wa mlima wa simu ili kulinda uhifadhi. 

Mkuu wa wilaya ya Simanjiro mhandisi Zephania Chaula alisema ataendelea kusimamia maendeleo kwenye eneo lake na kuhakikisha wanazidi kupiga hatua nyingine zaidi ya hapo walipo.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto mhandisi Tumaini Magessa ambaye ametangazwa na Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti kuwa ndiyo anaongoza kwa uchapakazi.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Zephania Chaula akisalimiana na wananchi wa eneo lake, mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amesema anashika nafasi ya pili kwa kuchapa kazi. 

No comments: