Monday, December 3, 2018

MKUTANO WA WADAU WA MAENDELEO ,MAAFISA WA SERIKALI NA MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII-TASAF WAANZA JIJINI DAR ES SALAAM.

Na. Estom Sanga-DSM 

Mkutano wa siku tano utakaojadili utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF umeanza jijini Dar es salaam baada ya kukamilika kwa ziara katika maeneo ya utekelezaji wa Mpango huo katika mkoa wa Mwanza na kisiwa cha Unguja. 

Mkutano huo unaowashirikisha Wadau wa Maendeleo wanaochangia utekelezaji wa Mpango huo,Maafisa wa Serikali kuu na baadhi ya halmashauri na Wafanyakazi wa TASAF hufanyika kila baada ya miezi sita kwa kutembelea maeneo ya utekelezaji wa Mpango na kuona mfanikio na changamoto za utekelezaji kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi. 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema kazi kubwa iliyoko mbele ya Mfuko huo,Wataalamu, Wadau wa Maendeleo ni kuhakikisha kuwa maelekezo ya Serikali ya kuweka utaratibu mzuri wa kuwashirikisha walengwa katika kufanyakazi kupitia Mpango wa Ajira ya Muda unazingatiwa kwa ukamilifu. 

Bwana Mwamanga amesema licha ya mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Mpango huo unaojumuisha takribani Kaya za Walengwa zipatazo Milioni Moja na Laki Moja , bado kuwa idadi kubwa ya Wananchi walioko nje ya Mpango ambao wamekuwa wakiomba kujumuishwa ili nao pia waweze kunufaika na sera hiyo ya serikali ya kupambana na umaskini.

Amesema katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Mpango huo inayotarajiwa kuanza mapema mwakani, suala la kushirikisha Walengwa hasa wenye uwezo wa kufanya kazi za maendeleo litapewa uzito mkubwa . 

Taarifa ya Utekelezaji kutoka TASAF makao makuu na baadhi ya Maeneo ya Utekelezaji wa Shughuli za Mpango inayonyesha kuweko kwa mafanikio makubwa kwa Walengwa kuanza kuboresha maisha yao kwa kutumia huduma za Mpango hususani katika nyanja za Elimu, Afya,Makazi na shughuli za uzalishaji mali kama ufugaji wa kuku, mbuzi na ng’ombe ambazo zimewaongezea kipato ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kujumuishwa kwenye Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akimkaribisha Kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Bw. Mohamed Muderis (aliyeketi) kuzungumza kwenye mkutano wa Wadau wa Maendeleo,Maafisa wa Serikali na TASAF jijini Dar es salaam.


Kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia, Bw. Mohamed Muderis (aliyesimama) akizungumza na Wadau wa Maendeleo, Maafisa wa Serikali na TASAF (hawapo pichani) mwanzoni mwa mkutano unaojadili utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini jijini DSM.


Picha ya chini na juu ni baadhi ya Wadau wa Maendeleo , Maafisa wa Serikali na TASAF wakiwa kwenye mkutano unaojadili utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulioanza leo jijini DSM.Mtaalamu wa Habari na Mawasiliano wa TASAF,Bi. Zuhura Mdungi (mbele) akiwa katika mkutano wa Wadau wa Maendeleo na Maafisa wa Serikali na TASAF ambapo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulioanza leo jijini Dar es salaam.

No comments: