Wednesday, December 12, 2018

MAHAKAMA YAAMURU MADINI YA THAMANI YA 2.5/- YATAIFISHWE KUWA MALI YA SERIKALI

Karama Kenyunko,Globu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru madini yenye thamani ya Sh. bilioni 2.5 yataifishwe na kuwa mali ya serikali kwasababu ukwepaji wa kodi ya mrabaha unasababisha Taifa likose mapato.

Pia Mahakama imeamuru wafanyabiashara watatu wa madini wakiwemo raia wawili wa China na mmoja wa India kulipa faini ya Sh.milioni moja kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi miwili kila mmoja.

Wafanyabiashara hao ni Chang Xu, Kai Jiang, Ashok Lavingia na Kampuni ya Sino Africa Collection Ltd waliokuwa wakikabiliwa na mashitaka matano likiwemo la kuwasilisha taarifa za uongo kwa Kamishna wa Madini kwa lengo la kukwepa malipo sahihi ya mirahaba.

Akitoa hukumu hiyo leo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amesema washitakiwa wanatiwa hatiani kwa kukiri kosa na katika kila kosa kila mshitakiwa atatakiwa kulipa Sh. 200,000 na kifungo cha miezi miwili ambapo jumla ni Sh.milioni nne na kifungo cha miezi miwili.Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Jacqueline Nyantori aliiomba Mahakama kutaifisha madini hayo chini ya Sheria ya Madini inayosomwa sambamba na sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya mwaka 2015.

Hata hivyo, Wakili wa Serikali Wankyo Simon, alidai washitakiwa hao ni wakosaji wa kwanza na makosa yao yanagusa masuala ya rasilimali za nchi.Alidai kesi hiyo inalenga ukwepaji kodi ambayo ndio uchumi wa nchi na unategemewa katika vitu vyote vinavyofanyika kwa wananchi wa Tanzania, hivyo wanaomba adhabu kali itolewe kwa washitakiwa kulingana na sheria zilizopo kwa lengo la kutunza rasilimali za madini.

Wakili wa utetezi, John Gamanya na Flora Jacob alidai washitakiwa hao ni wakosaji wa kwanza na ni wafanyabiashara wenye vibali hivyo aliomba mahakama izingatie kuwapunguzia adhabu.Imeelezwa mahakamani hapo kuws katika mashitaka ya kwanza, inadaiwa kati ya Juni Mosi, 2018 na Oktoba 3, mwaka huu maeneo ya jiji la Dar es Salaam, waliratibu na kufadhili biashara iliyofanywa genge haramu kwa lengo la kuchuma faida.

Pia inadaiwa Oktoba 3, mwaka huu maeneo ya Mgahawa wa Penda uliopo barabara ya King's way wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam wakiwa ha leseni ya madini walishindwa kutunza kumbukumbu ya usajili wa madini husika yaliyohifadhiwa.Washitakiwa wakiwa na leseni ya kujihusisha na biashara ya madini walishindwa kuwasilisha kwa Kamishna wa Madini nyaraka halisi ya kuingiza madini mbalimbali waliyoyasajili kwenye kumbukumbu zao ili kuonesha madini ya vito yenye uzito wa gramu 2,849.45 yenye thamani ya Dola za Marekani 385,830.32 waliyokutwa wakiyamiliki.

Katika mashitaka ya nne, washitakiwa walishindwa kuwasilisha nakala halisi ya madini waliyosajili vito vyenye uzito wa gramu 4,531.09 yenye thamani ya Dola za Marekani 735,904.07.Pia inadaiwa washitakiwa waliwasilisha taarifa ya uongo kwa Kamishna wa Madini kuhusu ubora wa madini ya rangi na vito walivyotunza kwa lengo ya kukwepa malipo sahihi ya mrabaha.

No comments: