Mtaalam kutoka kiwanda cha kuzalisha saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, Victor Kamuhabwa (wa kwanza kulia mbele) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa pili kushoto mbele) namna mfumo wa uendeshaji wa mitambo unavyofanya kazi kwenye ziara ya Naibu Waziri Nyongo kwenye kiwanda hicho tarehe 13 Desemba, 2018.
Mtaalam kutoka kiwanda cha kutengeneza vyombo vya ibada kwa kutumia madini ya mawe kinachomilikiwa na Shirika la Benedictine Abbey katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Mhandisi Kassari Viater (kulia mbele) akielezea namna mashine ya kukata mawe makubwa inavyofanya kazi kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati mbele) kwenye ziara ya Naibu Waziri Nyongo kwenye kiwanda hicho.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia Omari (kulia) akibadilishana mawazo na Mhandisi Migodi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Aidan Gumbo Mhando (kushoto) kwenye ziara hiyo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiangalia zawadi aliyokabidhiwa na mmoja wa watendaji wa kiwanda cha kutengeneza vyombo vya ibada kwa kutumia madini ya mawe kinachomilikiwa na Shirika la Benedictine Abbey katika Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Paulo Gembe (hayupo pichani) mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika kiwanda hicho. Kushoto ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Ephrahim Mushi na kulia ni Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi, Sophia Omari.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mtwara na Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi mara baada ya kumalizika kwa ziara.
Na Greyson Mwase, Lindi
Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa Nchini wametakiwa kuongeza ubunifu kwenye ukusanyaji wa mapato ili kuweza kufikia lengo lililowekwa na Serikali hivyo Sekta ya Madini kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 13 Desemba, 2018 na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo kwenye kikao chake na watumishi wa Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Lindi iliyopo Wilayani Nachingwea mkoani Lindi ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku mbili kwenye mkoa huo, yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini pamoja na kutatua kero mbalimbali.
Naibu Waziri Nyongo aliyekuwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Mhango alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inakuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa sekta nyingine kutokana na makusanyo ya kodi mbalimbali za madini.
“Ninawaagiza maafisa madini wakazi kuhakikisha wanafikia lengo lililowekwa na Serikali kwenye ukusanyaji wa kodi mbalimbali zitokanazo na Sekta ya Madini kwa kuwa wabunifu, na tupo tayari kusaidia pale itakapowezekana,” alisema Naibu Waziri Nyongo. Katika hatua nyingine, Nyongo aliwataka maafisa madini kujiridhisha na maeneo yanayoombewa leseni kabla ya kutoa leseni ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza kati ya wamiliki wa leseni na wananchi wanaozunguka maeneo ya uchimbaji.
Wakati huohuo akizungumza mara baada ya kuhitimisha ziara yake kwenye kiwanda cha uzalishaji wa saruji cha Dangote kilichopo mkoani Mtwara, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwenye sekta ya madini na kusisitiza kuwa Serikali ipo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji ili waweze kuzalisha zaidi na Serikali kupata mapato yake stahiki.
Aidha, Naibu Waziri alifanya ziara katika machimbo ya kokoto yanayomilikiwa na kampuni za Drumax Construction na Said Seff na kiwanda cha kutengeneza vyombo vya ibada kwa kutumia madini ya mawe kinachomilikiwa na Shirika la Benedictine Abbey katika Wilaya ya Masasi na kuwahakikishia watendaji wake kuwa Serikali imejipanga katika kutatua changamoto zinazowakabili ili uwekezaji wao uwe na manufaa, hivyo kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
No comments:
Post a Comment