Sunday, December 2, 2018

KAIMU MTENDAJI MKUU AITAKA TEMESA TANGA KUONGEZA UZALISHAJI


Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle kulia akitoa maagizo wakati akikagua gari ya kubeba mitambo mbalimbali (low bed truck) katika karakana ya TEMESA mkoa wa Tanga wakati wa ziara yake mkoani humo kukagua utendaji kazi na kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi wa wakala huo. Kushoto ni Kaimu Meneja Mhandisi Mhangaiko Ngoroma.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akikagua Propela ya kivuko cha MV. PANGANI II ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa katika yadi ya Songoro, kivuko hicho kinatarajiwa kuungana na kivuko cha MV. TANGA kutoa huduma katika eneo la Pangani na Bweni katika eneo la mto Pangani mara baada ya kukamilika kwa matengenezo yake. Nyuma yake ni Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir.
vuko cha MV. TANGA kinachotoa huduma katika mto Pangani, kati ya Pangani na Bweni wilayani Pangani mkoani Tanga kikielea majini wakati kikiendelea kutoa huduma ya kuvusha abiria na magari.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle wa pili kushoto akisisita umuhimu wa kuzingatia usalama wa vivuko kwa wafanyakazi wa kivuko hicho wakati wote wanapotoa huduma hiyo katika kivuko cha MV TANGA kinachotoa huduma katika mto Pangani, kati ya Pangani na Bweni wilayani Pangani mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya kukagua usalama wa vivuko.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle katikati (aliyevaa koti) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi na mabaharia wa kivuko cha MV TANGA kinachotoa huduma katika mto Pangani, kati ya Pangani na Bweni wilayani Pangani mkoani Tanga mara baada ya kumaliza kikao na wafanyakazi hao. PICHA ZOTE NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO (TEMESA)



………………………………

ALFRED MGWENO (TEMESA TANGA)

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme TEMESA Mhandisi Japhet Y. Maselle, amehitimisha ziara yake mkoani Tanga kwa kuwataka watendaji na viongozi wa Wakala mkoani humo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili kuinua mapato ya kituo hicho.

Akizungumza na wafanyakazi wa TEMESA Tanga pamoja na mafundi wa karakana mara baada ya kuwasili mkoani humo, mhandisi Maselle aliwasisitizia suala la ubunifu hasa katika upande wa karakana ambapo aliwataka kuiga mfano kutoka mkoa wa Singida ambao uzalishaji wake umeongezeka kwa kipindi cha hivi karibuni kutokana na kubuni njia mbalimbali ili kuongeza pato lake ikiwemo kuepuka kupeleka kazi ndogo ndogo za ufundi katika karakana teule. 

Vilevile alipata pia fursa ya kusikiliza changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika utendaji kazi wao pamoja na kukagua baadhi ya mitambo iliyopo katika karakana hiyo. Changamoto kubwa iliyoonekana ilikuwa ni uchakavu wa mitambo ambapo Mhandisi Maselle alisema kuwa ni vyema sasa Wakala ukaanza utaratibu wa kununua mitambo mipya ili kuongeza ufanisi zaidi upande wa Ukodishaji mitambo.

Mhandisi Maselle pia alitembelea kivuko cha MV. TANGA ambacho kinatoa huduma ya kuvusha abiria kati ya Pangani na Bweni katika mto Pangani mkoani Tanga ambapo alikagua hali ya usalama wa kivuko hicho na kuendelea kusisitiza suala hilo kupewa kipaumbele kikubwa wakati wote wa uvushaji, ‘’hakikisheni mnatoa mafunzo ya usalama walau mara mbili kwa wiki maana wanaovuka hapa kila siku asilimia kubwa ni wakazi wa hapa hapa’’, alisema Mhandisi Maselle.

Aidha Kaimu Mtendaji Mkuu, aliwapongeza kwa kuzingatia suala la nidhamu kwa viongozi wao lakini pia kusifia muonekano wa mabaharia wa kivuko hicho ambao walikua wamevalia sare zao zinazoweza kuwatambulisha kiurahisi kwa abiria na kuweza kupatiwa msaada pindi wanapohitaji.

Pamoja na kusikiliza kero, changamoto na maoni yao, Kaimu Mtendaji Mkuu alipata pia wasaa wa kukagua kivuko cha MV. PANGANI II (kilichokuwa awali kinaitwa MV. UTETE kilichohamishwa kutoka Utete wilaya ya Rufiji mkoani Pwani) ambacho kinafanyiwa ukarabati mkubwa na Kampuni ya Kizalendo ya Songoro Marine Boatyard ya jijini Mwanza, kivuko hicho kinatarajiwa kuungana na kivuko cha MV. TANGA kutoa huduma eneo hilo mara tu ukarabati wake utakapokamilika.

No comments: