Saturday, December 1, 2018

DKT ABBASI AWAUNGANISHA 'LIVE' MAAFISA HABARI WA TAASISI ZA UMMA KUFAFANUA KERO ZA WANANCHI*

SERIKALI ya Awamu ya Tano imeendelea kutumia ubunifu katika kuwahudumia wananchi ikiwemo kujibu na kufafanua kero zao papo kwa papo.

Katika hatua isiyokuwa ya kawaida, Msemaji Mkuu wa Serikali leo akiwa ziarani mkoani Morogoro alilazimika kuwapigia simu baadhi ya watendaji wa Serikali akiwa moja kwa moja studio za Redio Abood FM na ATV ili wajibu kero za sekta zao.

Afisa wa kwanza kukumbana na "kibano" hicho alikuwa Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Bw. Paschal Shelutete ambaye alipigiwa kwa mstukizo na kuunganishwa moja kwa moja studio ili ajibu swali la mwananchi aliyelalamikia tembo kutoka hifadhi mbalimbali kuvamia mashamba ya wananchi na kuharibu mazao.

Bw. Shelutete akionekana kulijua vyema eneo lake alifafanua kuwa kutokana na changamoto hiyo Tanapa na Mamlaka nyingine za Serikali kama Idara ya Wanyamapori zimekuwa na programu za kuwaelimisha wananchi wanaokaa karibu na hifadhi na mapori ya akiba.

"Tunaendelea kuwaelimisha wananchi wahakikishe wanatoa taarifa hizi kila wanapowaona wanyama wa porini wanarandaranda katika maeneo yao ili mamlaka zichukue hatua stahiki," alifafanua akitoa maelekezo ya hatua za kufuatwa.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Mawasiliano katika Shirika la Reli Tanzania (TRC), Jamila Mbarouk naye alipokurupushwa na kuunganishwa studio moja kwa moja kwa njia ya simu alifafanua vyema swali la mwananchi aliyetaka kujua utaratibu wa fidia kwa watakaoguswa na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Bi. Jamila aliwahakikishia wananchi wote nchini ambao wataguswa na ujenzi unaoendelea sasa kuwa watalipwa kwa mujibu wa sheria na hakuna atakayeonewa na wale ambao hawajapokea malipo taratibu zinakamilishwa.Hata hivyo alifafanua kuwa wale waliojenga ndani ya hifadhi ya reli hawatahusika kulipwa ila wataombwa kupisha ujenzi huo ili uendelee kwa kasi kwa manufaa ya watanzania wote.

Dkt. Abbasi alisisitiza kuwa watendaji wa umma kwa sasa wanapaswa kujua kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Haki ya Kupata Taarifa na Sheria ya Huduma za Habari wanapaswa wakati wowote kutoa habari na ufafanuzi muhimu kwa umma isipokuwa tu kwa masuala yaliyozuiwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha alisisitiza kuwa viongozi wa umma wakiwemo maafisa habari wanapaswa kutangaza utekelezaji wa ahadi za Serikali kwa kujua kinachoendelea wakati wote ili wananchi wasiwe na shida au kupata mkanganyiko usio wa lazima.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kipindi hicho Dkt. Abbasi alisema Rais Dkt. Magufuli amedhamiria kuondoa kero za watanzania hivyo kila mtendaji wa Serikali lazima ashiriki katika safari hiyo na awe tayari kuzitatua kero zilizoko ktk eneo lake kwa haraka.

"Kwa kuwa nimebaini wananchi yako maeneo mengi wameielewa ajenda ya Mhe Rais lakini yapo maeneo machache wanatakiwa kupata ufafanuzi zaidi kuanzia sasa viongozi wa ngazi zote wajiandae popote tulipo na wao popote walipo tutawapigia simu wafafanue na kujibu kero za wananchi.Utaratibu huu utaendelea kwa kustukiza hivi hivi," alisema Dkt. Abbasi.

No comments: