Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amegundua ujanja unaofanywa na baadhi ya wananchi wa Moshi mkoani Kilimanjaro wa kutochukua hati miliki za ardhi kwa lengo la kukwepa kulipa kodi ya ardhi.
Kufuatia hali hiyo Lukuvi ameagiza takriban hati 5,000 ambazo hazijachukuliwa katika Wilaya hiyo kuchukuliwa na wahusika na watakaoshindwa kuzichukua watafikishwa mahakamani kwa kosa la kukwepa kulipa kodi. Katika Manispaa ya Moshi Jumla ya viwanja 15,000 vimepimwa na kati ya hivyo ni hati 10,168 tu ndizo wamiliki wake wamejitokeza kuzichukua.
Aidha, Waziri Lukuvi amemuagiza Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi katika wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro kuhakikisha ifikapo februari mwaka ujao (2019) anasitisha kesi za migogoro ya ardhi na kuanza kujikita katika kusikiliza kesi za wamiliki wa ardhi wasiolipa kodi ya ardhi ili kuiwezesha serikali kupata mapato.
‘’Wote wasiolipa kodi iwe waliokuwa na hati ama wasio na hati lakini wanaishi katika maeneo ya mijini yaliyopangwa ikifika februari 2019 watafikishwa mahakamani na tutahakikisha wanadaiwa kuanzia kipindi walichomilikishwa na wakishindwa nyumba zao zitapigwa mnada’’ alisema Lukuvi
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo zaidi ya 150 waliojitokeza kuwasilisha kero zao za ardhi kwa Waziri Lukuvi katika program maalum ya Funguka kwa Waziri leo (jana), alisema katika ziara yake wilayani Moshi amebaini kuna hati zipatazo 5000 huku baadhi yake zikiwa na zaidi ya miaka 18 hazijachukuliwa na wahusika ambapo kwa mujibu wa Lukuvi wengi wao hawataki kuzichukua kwa kuogopa kulipa kodi ya ardhi.
Alisema, ulipaji kodi ya ardhi siyo hiari na mtu yoyote anayeishi katika eneo la mjini aelewe kuwa anaishi kwenye eneo lilipangwa na lazima aishi kwa masharti ya mipango miji ya mamlaka husika na kusisistiza kuwa mtu huyo lazima awe na hati na namna yoyote ya kukwepa kulipa kodi ni sawa na kosa la uhujumu uchumi.
Lukuvi amezitaka manispaa za miji kuhakikisha wananchi wanaishi kwa sheria za mipango miji na kuepuka kuishi wanavyotaka wao na kuwataka wananchi kuacha kuishi kwa mazoea.
Lukuvi ameshangazwa na baadhi ya watendaji wa ardhi katika wilaya ya Moshi kwa kushindwa kushughulikia kero za wananchi kwa wakati jambo alilolieleza kuwa linasababisha wananchi kushindwa kupatiwa hati kwa wakai huku baadhi ya watendaji wakishindwa kujibu hata barua ambazo baadhi yake zipo za tangu miaka ya tisini,
Wengi wa wananchi waliojitokeza kuwasilisha kero zao katika mkutano na Waziri Lukuvi walilalamikia kuchukuliwa maeneo yao huku mamlaka husika zikishindwa kuwatatulia kero zao kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa na kulazimika kuwasilisha malalamiko yao kwa waziri mwenye dhamana ya ardhi.
Mmoja wa wakazi wa Moshi Iddy Mkwazu alisifu hatua iliyochukuliwa na Waziri Lukuvi kukutana na wananchi wa wilaya ya Moshi kwa lengo la kutatua kero ya migogoro ya ardhi na kueleza kuwa katika muda wote wa ufahamu wake hajawahi kuona kikao cha aina hiyo na kubainisha kuwa hatua hiyo inaweza isiwafurahishe baadhi ya watu lakini ina faida kubwa kwa wananchi walio wengi.
No comments:
Post a Comment