Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe jana akipata maelezo ya ujenzi wa Jengo la mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kutoka kwa Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Unetec ya Dubai, Geofrey Asulumenye (aliyenyoosha mkono. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema.
Baadhi ya vyumba katika jengo la mizigo la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza ambalo linaendelea kujengwa, jana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe alitembelea na kuridhika na maendeleo ya ujenzi.
Mhandisi Simon Makoye (mwenye kofia ngumu), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe (katikati), mchoro wa eneo linapojengwa rada, jana alipotembelea na kukagua maendeleo ya miradi inayoendelea kwenye Kiwanja cha Ndege cha Mwanza.
Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Unetec ya Dubai, Geofrey Asulumenye (kushoto) akimpa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe maelezo mbalimbali ya ujenzi wa Jengo la kuongozea ndege la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza wakati alipofanya ziara jana.
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri (MAB) YA Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Prof. Ninatubu Lema (kulia), akiongozana na Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Marwa Rubilya wakiambatana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe aliyetembelea kukagua maendeleo ya miradi kwenye kiwanja cha Ndege cha Mwanza. PICHA ZOTE KWA HISANI YA TAA
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
WACHORAJI wa jengo jipya la abiria la Kiwanja cha Ndege cha Mwanza, wametakiwa kuharakisha ili serikali itangaze zabuni ujenzi uanze haraka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe amesema jana mkoani hapa alipokuwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miundombinu ya kiwanja hicho ambayo ipo kwenye maboresho makubwa.
Mhe. Kamwelwe amesema kukamilika kwa michoro hiyo ya jengo la kisasa kutasaidia serikali kupitia wasimamizi wa ujenzi huo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), kutangaza zabuni na kupatikana kwa mkandarasi atakayejenga jengo hilo.
“Kiwanja cha ndege kinashughuli nyingi na jengo la abiria ni kityu muhimu sana, hivyo ninaharakisha hao wachoraji wajitahidi kufanya haraka ili kukamilisha michoro hiyo,” amesisitiza Mhe. Waziri.
Hatahivyo, amesema ameridhishwa na mradi wa ujenzi wa jengo la mizigo ambalo lipo mita chache kutoka eneo la abiria, ambapo ndege za mizigo zimejengewa maegesho yake rasmi tofauti na awali zilikuwa zikishusha upande wa ndege za abiria.
Halikadhalika ametembelea jengo la kisasa la kuongozea ndege, ambalo nalo limekamilika kwa asilimia 90 na kuridhishwa na utendaji wa Mhandisi Mkazi, Godfrey Asulumenye wa Kampuni ya Unetec ya Dubai, pamoja na eneo linapojengwa rada.
“Nimeridhika kuna maendeleo kwa kiasi kikubwa tofauti na nilivyopita awali, sasa kuna tofauti maboresho yamekamilika kwa asilimia kubwa na imebaki sehemu za kumalizia tu, ninaimani kwa kiasi kikubwa mkandarasi huyu atakamilisha kwa wakati na kuboresha zaidi sehemu ambazo wanaona hazijakaa sawa kabla ya kukabidhi,” Mhe. Kamwelwe.
Mhandisi Asulumenye amesema maboresho hayo yamehusisha ujenzi wa jengo la mizigo, jengo la kuongozea ndege, Kituo cha umeme, urefushaji wa barabara ya kutua na kuruka kwa ndege kwa mita 700 na ikikamilika itakuwa na urefu wa Km4.
Maboresho mengine kwa mujibu wa Mhandisi ni pamoja na uwekaji wat aa za kuomgozea ndege (AGL), mifereji mikubwa ya kupitisha maji ya mvua, maegesho ya ndege, mifumo ya maji taka na matenki ya maji safi.
Kiwanja cha Ndege cha Mwanza kwa sasa ni daraja la 4C kinauwezo wa kuhudumia ndege za abiria 300 na maboresho yakikamilika kitapanda na kuwa daraja la 4D. Takwimu zinaonesha kinahudumia abiria 500,000 kwa mwaka ila matarajio ni kufikia abiria milioni mbili (2) baada ya maboresho kukamilika.
No comments:
Post a Comment