Wednesday, November 28, 2018

UPELELEZI KESI YA UHUJUMU UCHUMI WAFANYAKAZI WA NEMC BADO HAUJAKAMILIKA


Na Karama Kenyunko blogu ya jamii

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeelezwa kuwa, upelelezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili wafanyakazi watano wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) bado haujakamilika. 

Wakili wa Serikali, Jenipher Massue aamedai hayo leo Novemba 28.2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando wakati kai hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa, 

"Mheshimiwa kesi leo imekuja kwa ajili ya kutajwa upelezi bado haujakamilika tu naomba tarehe ya kutajwa" amedai wakili Massue.
Hakimu Mmbando ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 12, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. 

Katika kesi hiyo wafanyakazi hao wanakabiliwa na mashtaka sita ya uhujumu uchumi likiwamo la kughushi saini ya Waziri wa nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira,Januari Makamba katika vyeti vya tathmini ya uharibifu wa Mazingira.

Washtakiwa hao ni Ofisa wa Mazingira NEMC,Deusdith Katwale(38) na Mtaalam wa IT, Luciana Lawi(33) wote wakazi wa ubungo Msewe, Katibu Muhasi wa NEMC (Sekretari), Edna Lutanjuka (51) Mkazi wa Mbezi Beach St Gasper, Msaidizi wa ofisa Mwaruka Mwaruka (42) naOfisa mazingira Nemc, Lilian Laizer (27) wote Wa kazi wa Ukonga Mombasa na Ofisa mazingira wa Nemc, Magori Wambura (38) mkazi wa Bombambili. 

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka sita ikiwamo la kula njama, mawili ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara ya Sh.Milioni 160




Kwa pamoja washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Septemba 27, 2016 na April Mosi,2018 jijini Dar es Salaam walikula njama ya kutenda kosa la kughushi.

Katika shtaka la pili washtakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 17,2017 Dar es Salaam kwa udanganyifu walighushi cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 wakijaribu kuonesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati wakijua si kweli.

Washtakiwa hao, katika shtaka la tatu wanadaiwa kuwa Oktoba,2017 Dar es Salaam kwa nia ovu walighushi saini ya Januari Makamba ambaye ni Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira katika cheti cha tathmini ya uharibifu wa Mazingira chenye usajili namba EC/ EIA/3366 wakijaribu kuonesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati wakati wakijua si kweli.

Katika shtaka la nne, mshtakiwa Edna anadaiwa kuwa Oktoba 2017 katika ofisi za NEMC Makao Makuu Dar es Salaam kwa kujua alitoa cheti cha kughushi cha tathmini ya uharibifu wa mazingira chenye namba ya usajili EC/EIA/3366 cha oktoba 17,2017 kwa Deogratius Chacha, akijaribu kuonyesha kuwa cheti hicho ni halali na kwamba kimetolewa na NEMC wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la tano, washtakiwa hao wote wanadaiwa kuwa kati ya Septemba 27 na Aprili 6 ,2018 walijipatia kwa njia ya udanganyifu Sh. Milioni 160 toka kwa PMM Estate (2001) Ltd kwa madai kuwa wangeweza kufanya tathimini ya uharibifu wa mazingira na kumpatia cheti ambacho kinatolewa na NEMC kitendo ambacho si kweli.

Katika shtaka la sita washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Septemba27, 2016 na Aprili 6,2018 Dar es Salaam waliisababishia NEMC hasara ya Sh.Milioni 160.


No comments: