Sunday, November 25, 2018

UKATILI WA KIJINSIA NI KANSA MPYA NCHINI: DKT NDUGULILE



Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza na wana Shirika la KWIECO lilichopo Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro linaloshughulisha na utoaji wa masaada wa kisheria kwa wahanga waliofanyiwa vitendo vya ukatili wa Kijinsia.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia moja ya bidhaa zinazotengenzwa na wanachama wa Shirika la Floresta Tanzania lililopo Marangu Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya kukagua kazi zinazofanywa na wanawake wajasiriamali mkoani humo
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akiangalia mua uliokuzwa vizuri kwa njia za kiasili bila kutumia mbolea za kisasa unaolimwa na wanawake wajasiriamali wa Umoja wa Vicoba Marangu (UVIMA) uliopo Mkoa wa Kilimanjaro wakati wa ziara ya kukagua kazi zinazofanywa na wanawake wajasiriamali mkoani humo
Wanakikundi kutoka Shirika la Floresta na kutoka Umoja wa Vicoba Marangu (UVIMA) wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo Pichani) wakati akizungumza nao mara baada ya kukagua shughuli wanazofanya
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akikagua taarifa katika kitabu kilichopo chumba cha Polisi katika Kituo cha kutoa Huduma za pamoja ( ONE STOP CENTRE) katika Hospitali ya Wilaya ya Hai. Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW



Na Mwandishi Wetu Moshi

Imesemekana kuwa vitendo vya Ukatili wa kijinsia kwa miaka hivi karibuni vimezidi kukithiri na kuathiri wanawake na Watoto nchini nahivyo kufikia hatua ya kufananishwa na ugonjwa wa Kansa.

Hayo yamebainishwa wakati wa Ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile alipotembelea Shirika lisilo la Kiserikali la Kilimanjaro Women Information Exchange Community Organization (KWIECO) na kujionea shughuli za huduma za kisheria zinazotolewa kwa wahanga wa Ukatili wa Kijinsia katika Mkoa wa Kilimanjaro.

Naibu Waziri Ndugulile amesema vitendo vya Ukatili wa Kijinsia vimekuwa vinaongezeka sana na kwa mwaka 2017 vitendo 41,000 viliripotiwa na kati ya hivyo vitendo 13,000 vilifanywa dhidi ya watoto. “Kwa idadi ya vitendo hivi vya kikatili ingekuwa kwa ujambazi hali ingekuwa mbaya yani ukatili wa kijinsia ndio Kansa mpya nchini” alisisitiza Dkt. Ndugulile

Dkt. Ndugulile amewataka Wataalam wa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii kutoka ofisini na kwenda kwa wananchi kusikikiza kero na kutatua changamoto zao ili kuwapa chachu ya kuboresha maendeleo na ustawi wao. Amesisitiza kuwa Serikali imeamua kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuanzisha Mpango Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watotokwa kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2021/2022 ili kuondokana kabisa na vitendo hivyo dhalili.

Pia Naibu Waziri Ndugulile ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kushirikiana na Serikali katika kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto. Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kilimanjaro Women Information Exchange Community Organization (KWIECO) Bi. Elizabeth Maro Minde amesema Shirika lake limejikita katika kusaidia wahanga wa vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto na wamewasaidia wahanga hao na kufanikiwa kupata haki zao.

“Vitendo hivyo vinafanywa na watu wa karibu na familia yake kama Baba, Mama, mjomba na majirani na hivyo kusababisha kuwepo kwa changamoto katika upatikanaji wa ushahidi stahiki kwa pande zote mbili.” alisisitiza Bi. Elizabeth

Naibu Waziri Ndugulile yupo mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tatu kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Afya na Maendeleo ya Jamii katika mkoa wa Kilimajaro.

No comments: